-
Sehemu 23: 1945 kuendelea—Wakati wa Kufanya Hesabu U KaribuAmkeni!—1990 | Novemba 8
-
-
Sasa, katika kizazi chetu, milki nzima ya ulimwengu ya dini bandia yaelekeana uso kwa uso na msiba. Kwa mara nyingine ‘majeshi yenye kupiga kambi’ yanajitayarisha kufikiliza hukumu ya kimungu. Kama vile majeshi ya Kiroma ya karne ya kwanza yaliyopangwa kwa kusudi la kudumisha Pax Romana (Amani ya Kiroma), majeshi yenye kupiga kambi leo ni chombo cha kutunza amani pia. Unabii wa Biblia waonyesha kwamba vikosi vya kijeshi miongoni mwa mataifa yaliyo washirika wa UM yatakuwa chombo cha Yehova katika kufanya hesabu mwishowe pamoja na Yerusalemu wa ki-siku-hizi, Jumuiya ya Wakristo, na pia sehemu nyingine yote ya Babuloni Mkubwa.—Ufunuo 17:7, 16.
Hilo litatukia lini? Wathesalonike wa Kwanza 5:3 hujibu hivi: “Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.”
“Mweneo Mkubwa wa Amani”
Wakati wa 1988 aliyekuwa waziri wa serikali United States, George Schultz, alisema kwamba “amani inabubujika kila mahali.” Mstadi mmoja wa sera za mambo ya nchi za kigeni alisema juu ya “mweneo mkubwa wa amani.” Gazeti la kila juma Die Zeit la Kijeremani lenye sifa liliuliza hivi: “Je! ingeweza kuwa kwamba, katika karne yenye maangamizo mengi sana, mwongo wayo wa mwisho ungeweza kuwa ndiyo alama ya mwisho ya uharibifu na mwanzo wa enzi ya marekebisho yenye amani?” Na gazeti Time lilisema hivi: “Amani inatisha katika Iran-Iraq, Kampuchea, Afghanistan, Afrika ya upande wa kusini na hata Amerika ya Kati.”
Mwaka 1989 ulikuwa umejawa pia na maongezi ya amani. Katika Februari gazeti la Kijeremani Süddeutsche Zeitung lilitoa tahariri hii: “Kuanzia karibu 1985 tumekuwa tukiishi katika kipindi ambamo yale mataifa [mawili] yenye nguvu nyingi yamefanya mengi zaidi badala ya kuficha kucha zao. . . . Leo ni sehemu chache duniani ambako mataifa hayo mawili yenye nguvu nyingi hayasogeleani karibu. . . . Kwa vyovyote, dalili hazijapata kamwe kuwa nzuri hivyo, pande zote mbili hazijapata kuchukua mambo kwa uzito hivyo, na hatua nyingi sana kadiri hiyo kuchukuliwa wakati ule ule mmoja kuelekea upande ufaao.”
Hivi majuzi tu kama miaka sita iliyopita, mambo hayakuonekana kuwa maangavu sana. Mwandishi wa habari Roy Larson alisema kwamba “muda wote wa 1983 viongozi wa kidini kuzunguka ulimwengu walipaaza sauti ya ‘amani, amani,’ lakini hakukuwa na amani.” Je! matukio ya ulimwengu yenye kushangaza tangu wakati huo ni utimizo wa 1 Wathesalonike 5:3? Hatuwezi kusema. Hata hivyo, ni wazi kwamba leo “amani na usalama” yakaribia kutimia kuliko wakati uliotangulia.
Viongozi wa Kidini Wanafanya Kazi kwa Bidii—Kwa Ajili ya Nini?
Kama vile Larson aonyeshavyo, viongozi wa kidini hawakukaa tu bila utendaji wa kufuatia amani. Akiendelea na mkadirio wake wa 1983, yeye ataja “safari ya amani” ya kwenda Amerika ya Kati na visiwa vya Karibbea ambayo John Paul 2 alifunga. Pia wakati wa mwaka huo, Mkutano wa Kitaifa wa Maaskofu Wakatoliki United States ulichagua kufuata barua ya kiuchungaji yenye kichwa “Tatizo la Kupata Amani.” Muda mfupi baada ya hapo, wawakilishi wa makanisa zaidi ya 300 kutoka nchi 100 walikutana kwenye Kusanyiko Kuu la sita la Baraza la Makanisa Ulimwenguni na yakakubali azimio kama hilo. Waevanjeli wengi Waprotestanti walihusika pia katika kile ambacho Larson alikiita “mshughulikio wa amani katika tufe lote.”
Wakati wa kuanzishwa kwalo katika 1948 na kwenye mkutano walo wa 1966, Baraza la Makanisa Ulimwenguni lilisema wazi dhidi ya utumizi wa silaha za uangamivu za ki-siku-hizi. Kwa hiyo, makasisi na wanatheolojia wengi wamechukua silaha ili kutafuta amani, wanaume kama mwanatheolojia Mprotestanti wa Ujeremani Helmut Gollwitzer. Mapema kidogo mwaka uliopita, katika pindi ya mwaka wa 80 wa siku ya kuzaliwa kwake, yeye alisifiwa na kichapo cha kila juma cha Kiswisi kuwa “mwanatheolojia mwenye kuhusika kisiasa, mwenye kujitahidi sikuzote kutafuta amani,” ambaye “kwa njia ya fundisho na bidii yake ya kutimiza wajibu wa kisiasa amevuta kwa uthabiti wanatheolojia wengi na pia harakati ya amani ndani ya kanisa.”
Hivyo, haishangazi kwamba Babuloni Mkubwa aliunga mkono kwa bidii ule Mwaka wa Amani ya Kitaifa wa 1986, ambao shirika la Umoja wa Mataifa lilikusudia uwe hivyo, mkataba walo ukilitaka “kudumisha amani na usalama wa kimataifa.” Wakati wa mwaka huo, papa Mkatoliki, Askofu mkuu Mwanglikana wa Canterbury, na viongozi wengine wa kidini 700, kutia na watu wenye kudai kuwa Wakristo, Wabuddha, Wahindu, Waislamu, waabudu-maumbile wa Kiafrika, Waamerika wenyeji (Wahindi), Wayahudi, Wasiki (Wakalasinga), Wazoroasta, Washinto, na Wajain, walikutana pamoja kule Assisi, karibu na Roma, ili kusali kwa ajili ya amani.
Katika Januari 1989, Sunday Telegraph la Sydney, Australia, liliandika kwamba washiriki wa “imani ya Kibuddha, ya Kikristo, ya Kihindu, ya Kiyahudi, ya Kiislamu, ya Kisiki, ya Kiyunitaria, ya Kibaha’i, ya Kikonfyushasi, ya Kijain, ya Kishinto, ya Kitao, ya Raja Yoga na ya Kizoroasta” walikuwa wamekutana katika Melbourne kwa ajili ya kusanyiko la tano la Mkutano wa Ulimwengu Kuhusu Dini na Amani. La maana kuangalia, wale “wajumbe zaidi ya 600 kutoka nchi kama 85 . . . walikiri kwamba misukosuko yenye kusababishwa na tofauti za kidini ilitumiwa vibaya kwa muda mrefu kuwa kimoja cha visababishi vikubwa vya vita.”
Mhusiko wa kidini katika utafutaji wa amani wathibitisha aliyosema Dag Hammarskjöld, aliyekuwa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa: “Shirika [UM] na makanisa husimama bega kwa bega kuwa washirikiani katika jitihada za wanadamu wote wenye nia njema, bila kujali wana itikadi gani au namna gani ya ibada, ili kuleta amani duniani.”
Ingawa hivyo, miendo ya kuteta kwa Babuloni Mkubwa, maandamano yake ya peupe, na namna nyingine zisizoonekana wazi zaidi za kujiingiza kwa dini katika mambo ya kisiasa zitaongoza kwenye uangamivu wake.a Tayari yamesababisha mzozano mwingi, kama vile alivyokiri hivi majuzi Albert Nolan, mtawa mmoja Mdominika wa kutoka Afrika Kusini: “Njia pekee yenye matokeo ya kupata amani kupatana na mapenzi ya Mungu ni kuingia katika pigano. . . . Ili kuweza kupunguza silaha, mahitilafiano na serikali karibu hayawezi kuepukwa.”
Acheni Babuloni Mkubwa aendelee kupaaza sauti ya kutaka amani. Acheni papa aendelee kutoa baraka yake ya kimapokeo ya Urbi et orbi (kwa jiji [Roma] na ulimwengu) wakati wa Krismasi na Ista. Acheni aendelee kudhania—kama alivyofanya katika Mei mwaka juzi—kwamba upungufu wa sasa wa mivuto ya kisiasa ni jibu la Mungu kwa sala “za Kikristo.” Kusema-sema maneno ya amani na kujitwalia baraka ya Mungu bila haki hakuwezi kumwondolea Babuloni Mkubwa matendo yake ya zamani ya umwagaji damu. Hayo humtia chapa ya kuwa ndiye kizuizi kikubwa zaidi ambacho kimepata kuwako cha amani kati ya wanadamu, na pia kati ya wanadamu na Mungu. Kwa njia iliyo au isiyo ya moja kwa moja, kila tatizo la ainabinadamu laweza kufuatiliwa lionekane kwamba yeye ndiye chanzo chalo!
Lo, ni jambo la kinyume kama nini kwamba dini bandia huendelea kujitahidi, pamoja na UM, kuleta “amani na usalama” ule ule utakaokuwa utangulizi wa uharibifu wayo! Mwisho wa dini bandia utatetea uhaki wa Mungu wa dini ya kweli, ambaye asema: “Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.”—Wagalatia 6:7.
-
-
Utafutaji wa Amani na UsalamaAmkeni!—1990 | Novemba 8
-
-
Utafutaji wa Amani na Usalama
Watu walio wengi wana tamaa ya kiasili ya amani na utulivu, lakini tamaa hiyo imevurugwa muda wa sehemu kubwa ya historia ya kibinadamu. Hata hivyo, miaka ya majuzi kumekuwako matimizo ya kustaajabisha katika jitihada ya binadamu kutafuta amani, kama ionyeshavyo orodha inayofuata.
1985: (Oktoba) Umoja wa Mataifa waadhimisha mwaka wa 40 wa siku ya kuzaliwa kwao na yapiga mbiu 1986 uwe Mwaka wa Amani ya Kimataifa.
(Novemba) Mkutano wa mataifa makubwa ulio wa kwanza katika muda wa miaka sita Gorbachev na Reagan wakutanapo; Reagan asema juu ya “mwanzo mpya kabisa.”
1986: (Januari) Gorbachev atoa wito wa kupiga marufuku silaha zote za nyukilia kufikia mwaka 2000.
(Septemba) Mkutano Juu ya Hatua za Kusitawisha Uhakika na Usalama na Kuondoa Silaha Katika Ulaya (mataifa 35, kutia na United States, Kanada, Urusi, na Ulaya yote isipokuwa Albania) watia sahihi mkataba wa kupunguza hatari ya kutokea vita ya kiaksidenti.
(Oktoba) Mkutano kati ya Reagan na Gorbachev katika Iceland wakosa kutimilika, ingawa Gorbachev asema walikuwa kwenye ukingo wa kufanya “maamuzi makubwa, yenye kufanyiza historia.”
1987: (Januari) Mwongozo wa glasnost (kusema wazi) waonekana kuwa ukielekeza kwenye enzi mpya katika Urusi.
(Machi) Ziara ya kwanza ya waziri mkuu Mwingereza kwenda Mosko katika muda wa miaka 12.
(Desemba) Gorbachev na Reagan watia sahihi mapatano ya INF (Intermediate-range Nuclear Forces [Makombora ya Nyukilia ya Masafa ya Kati]) ili kukomesha makombora ya nyukilia ya masafa ya kati.
1988: (Machi) Nikaragua na wapambani wenye kupinga Ukomunisti watia sahihi mapatano ya kukomesha vita, wakianza masikilizano ya kufikia suluhisho la daima.
(Aprili) Urusi yatangaza kuondoa vikosi kutoka Afghanistan kufikia Februari 1989; Ethiopia na Somalia zakubaliana kumaliza pigano.
(Mei) Vietnam yatangaza kuondoa askari 50,000 katika Kampuchea kabla ya mwisho wa mwaka, na waliosalia kufikia 1990.
(Juni) Waziri Mkuu wa Australia Bob Hawke asema hivi juu ya mkutano kati ya Gorbachev na Reagan katika Moscow: “Kwa mara ya kwanza katika kipindi kizima cha baada ya vita, kuna ishara halisi za kuibuka kwa ulimwengu uwezao kuishi kwa kujengana katika amani.”
(Julai) Iran yatangaza kupokewa kwa azimio la UM lenye wito wa kukomesha pigano katika vita ya miaka minane baina ya Iran na Iraq.
(Agosti) United States yakubali kulipa haki za UM ambazo zilikuwa zimezuiliwa, mwendo uliokwisha chukuliwa na Warusi, hivyo wakisaidia kumaliza tataniko la kifedha la UM na kulipatia tena msimamo.
(Septemba) Vikosi vya magaidi wa Morocco na Polisario vyapokea mpango wa UM kumaliza miaka 13 ya vita katika Sahara ya Magharibi.
(Oktoba) Vikosi vya kutunza amani vya UM vyatuzwa Tuzo la Nobeli la Amani; Libya na Chad zamaliza rasmi hali ya vita yenye kuwako kwa muda mrefu.
(Desemba) Kwenye UM, Gorbachev atangaza hatua kubwa ya upande mmoja ya kupunguza vikosi vya Urusi katika muda wa miaka miwili na kuondolewa kwa vikosi vifaru Czechoslovakia, Hungari, na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Ujeremani; Afrika Kusini, Namibia, na Kyuba zaafikiana kutekeleza azimio la UM siku ya Aprili 1, 1989, zikitoa uhuru wa Namibia na kumaliza miaka 22 ya vita; nusu ya askari 50,000 Wakyuba katika Angola kuondolewa kufikia Novemba 1, na waliosalia kufikia Julai 1, 1991; United States yakubali kuongea na Shirika la Ukombozi wa Palestina baada ya Yasser Arafat kuhakikishia kabisa haki ya Israeli “kuwako katika amani na usalama.”
1989: (Januari) Mataifa 149 yenye kuhudhuria Mkutano wa Paris Kuhusu Silaha za Kikemikali zatoa wito hatua ya haraka sana ichukuliwe kupiga marufuku usitawishaji, utengenezaji, uwekaji akiba, na utumiaji wa silaha za kikemikali.
(Februari) Costa Rica, Honduras, El Salvador, Nikaragua, na Guatemala zatia sahihi mwafaka wa kuhifadhi amani katika Amerika ya Kati; kikundi kilicho kikubwa zaidi cha uasi Kolombia, FARC (Majeshi Yenye Silaha ya Mapinduzi Kolombia), chatangaza kukomesha pigano, kikitokeza matumaini ya kwamba miaka 35 ya vita vya magaidi huenda yakaribia kuja kwenye ukomo.
(Machi) Mawaziri wa nchi za kigeni kutoka mataifa 35 waanza maongezi katika Vienna juu ya CFE (Masikilizano Kuhusu Majeshi Yenye Silaha za Kawaida Katika Ulaya), yakikusudiwa kupunguza majeshi katika Ulaya.
(Aprili) Vietnam yatangaza kuondoa kabisa askari katika Kampuchea kufikia Septemba 30.
(Mei) Hungari yaanza kuondoa kizuizi chayo cha seng’enge ya miaka 40 katika mpaka wa Austria; kwenye mkutano wa kwanza wa viongozi Warusi na Wachina katika muda wa miaka zaidi ya 30, Warusi watangaza kupunguzwa kwa majeshi ya Esia; Warusi waanza hatua ya upande mmoja kuondoa askari wao na silaha katika Ulaya ya Mashariki.
(Juni) Wito wa Bush wa kupunguza sana askari, vifaru, mizinga, na ndege za vita katika Ulaya kufikia 1992 waongoza gazetihabari kusema hivi: “Kwa kweli huenda hiyo ikafungua mlango wa mipunguzo ya silaha iliyo mikubwa zaidi tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu 2.”
(Agosti) Mataifa matano ya Amerika ya Kati yaafikiana juu ya mpango wa kumaliza vitendo vya uhasama katika Nikaragua.
-