Mungu Huonaje Ibada ya Jumuiya ya Wakristo?
“SI KILA mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni,” akasema Yesu Kristo, “bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni. Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya . . . kwa jina lako . . . miujiza mingi? Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”—Mathayo 7:21-23.
Kupitia Neno lake takatifu, Biblia Takatifu, Mungu ameonyesha wazi mapenzi yake ni nini. Je, makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yanafanya mapenzi ya Mungu? Au, wao ni wale ambao Yesu aliwaita ‘watendao maovu’?
Umwagaji wa Damu
Kwenye usiku kabla ya kifo cha Bwana-Mkubwa wake, karibu Petro aanzishe vita yenye silaha dhidi ya kikundi cha askari-jeshi kilichotumwa kumkamata Yesu. (Yohana 18:3, 10) Lakini Yesu alirudisha utulivu akamwonya Petro hivi: “Wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga.” (Mathayo 26:52) Onyo hilo la wazi linarudiwa kwenye Ufunuo 13:10. Je, makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yamelitii? Au wao hushiriki katika lawama la vita vinavyoendelea katika sehemu mbalimbali za dunia?
Wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, mamia ya maelfu ya Waserbia na Wakroatia waliuawa kimakusudi katika jina la dini. “Katika Kroatia,” yaripoti The New Encyclopædia Britannica, “utawala wa huko wa kifashisti ulianza kutekeleza sera ya ‘utakasaji wa kijamii’ uliopita hata mazoea ya Nazi. . . . Ilitangazwa kwamba thuluthi moja ya idadi ya Waserbia ingefukuzwa kutoka nchini, thuluthi moja ingegeuzwa imani kwenye Ukatoliki wa Kiroma, na thuluthi moja ingeangamizwa. . . . Kushirikiana kwa sehemu kwa makasisi Wakatoliki katika mazoea haya kuliharibu vibaya sana mahusiano ya kanisa na serikali baada ya vita hiyo.” Idadi zisizohesabika za watu zililazimishwa kugeuka imani kuwa Wakatoliki au zife; maelfu mengine hata hayakupewa chaguo. Vijiji vizima-vizima—wanaume, wanawake, na watoto—vililazimishwa kuingia ndani ya makanisa yao ya Othodoksi na kuuawa. Namna gani majeshi yenye kupinga ya Ukomunisti? Je, yalikuwa na utegemezo wa kidini pia?
“Baadhi ya makasisi walishiriki vitani kwenye upande wa majeshi ya uasi,” charipoti kitabu History of Yugoslavia. “Majeshi ya Wanamgambo yalikuja hata kutia ndani makasisi kutoka makanisa ya Othodoksi ya Kiserbia na Katoliki ya Kiroma,” chataarifu kitabu Yugoslavia and the New Communism. Tofauti za kidini huendelea kuchochea vita katika nchi za Balkani.
Na namna gani Rwanda? Katibu mkuu wa Catholic Institute for International Relations, Ian Linden, alikiri ifuatavyo katika jarida The Month: “Uchunguzi uliofanywa na African Rights [shirika la kupigania haki za Waafrika] katika London huandaa kielelezo kimoja au viwili vya viongozi wenyeji Wakatoliki, Waanglikana, na Wabaptisti wanaolaumiwa kwa kupuuza au kutenda katika mauaji ya wanamgambo. . . . Hakuna shaka lolote kwamba idadi kubwa za Wakristo mashuhuri katika parishi walihusika katika mauaji.” Kwa kuhuzunisha, mapigano kati ya wale waitwao Wakristo isivyofaa huendelea kukumba Afrika ya kati.
Uasherati na Uzinzi
Kulingana na Neno la Mungu, ngono ina mahali pamoja tu penye kuheshimika, na mahali hapo ni katika kifungo cha ndoa. “Ndoa na iheshimiwe na watu wote,” yataarifu Biblia, “na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.” (Waebrania 13:4) Je, viongozi wa makanisa wanaunga mkono fundisho hili la Mungu?
Katika 1989 Kanisa Anglikana katika Australia lilitoa hati rasmi juu ya ngono iliyodokeza kwamba ngono kabla ya ndoa si kosa ikiwa wenzi wana uwajibikaji kamili wao kwa wao. Majuzi zaidi, kiongozi wa Kanisa Anglikana katika Scotland alitaarifu hivi: “Kanisa halipasi kulaumu mahusiano ya kizinzi kuwa yenye dhambi na mabaya. Ni lazima Kanisa likubali kwamba uzinzi husababishwa na hali yetu tuliyorithi.”
Katika Afrika Kusini makasisi kadhaa wamesema kwa ujasiri kwa kuunga mkono ugoni-jinsia-moja. Kwa kielelezo, katika 1990 gazeti la Afrika Kusini You lilimnukuu mhudumu mashuhuri wa Anglikana akisema: “Andiko halimfungi mtu daima. . . . Naamini kwamba kutakuwa na mabadiliko katika mtazamo na sera ya kanisa kuelekea wagoni-jinsia-moja.”—Tofautisha na Warumi 1:26, 27.
Kulingana na 1994 Britannica Book of the Year, ngono imekuwa suala kubwa katika makanisa ya Marekani, hasa mambo kama vile “kuwekwa rasmi kuwa wahudumu kwa wale wanaojulikana kuwa wagoni-jinsia-moja wa kiume na wa kike, uelewevu wa kidini wa haki za wagoni-jinsia-moja, kubariki kwa ‘ndoa za wagoni-jinsia-moja,’ na kuhalalishwa au kulaumiwa kwa mitindo-maisha inayohusianishwa na ugoni-jinsia-moja.” Mafarakano ya dini mashuhuri yaliyo mengi huvumilia makasisi wanaoshindania uhuru mkubwa zaidi wa kingono. Kulingana na 1995 Britannica Book of the Year, maaskofu 55 wa Kiepiskopali walitia sahihi mkataa “wakihakikisha kukubaliwa kwa kuagizwa-rasmi kwa wagoni-jinsia-moja na kwa zoea hilo.”
Makasisi fulani huunga mkono ugoni-jinsia-moja, wakidai kwamba Yesu hakuupinga kamwe. Lakini ndivyo ilivyo kweli? Yesu Kristo alitangaza kwamba Neno la Mungu ni kweli. (Yohana 17:17) Hilo lamaanisha kwamba yeye alikubali maoni ya Mungu juu ya ugoni-jinsia-moja kama yafafanuliwavyo kwenye Mambo ya Walawi 18:22, ambalo lasomwa hivi: “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo.” Isitoshe, Yesu aliorodhesha uasherati na uzinzi miongoni mwa mambo “yote yaliyo maovu [ambayo] yatoka ndani, nayo yamtia mtu unajisi.” (Marko 7:21-23) Neno la Kigiriki uasherati ni neno lenye kutia ndani mambo mengi zaidi kuliko uzinzi. Hilo hufafanua namna zote za mahusiano ya kingono ya nje ya ndoa iliyohalali kisheria, kutia ndani ugoni-jinsia-moja. (Yuda 7) Yesu Kristo aliwaonya pia wafuasi wake wasimvumilie yeyote anayedai kuwa mwalimu Mkristo anayepunguza uzito wa uasherati.—Ufunuo 1:1; 2:14, 20.
Viongozi wa kidini wanaposhindania kuwekwa rasmi kwa wagoni-jinsia-moja wa kiume na wa kike, hilo huwaathirije washiriki wa makanisa yao, hasa vijana? Je, si kichocheo cha kujaribu ngono nje ya ndoa? Tofauti na hilo, Neno la Mungu lawahimiza Wakristo ‘wakimbie uasherati.’ (1 Wakorintho 6:18, NW) Mwamini mwenzetu akitumbukia katika dhambi hiyo, msaada wenye upendo unatolewa kwa nia ya kumrudisha mtu huyo kwenye kibali cha Mungu. (Yakobo 5:16, 19, 20) Namna gani msaada huo ukikataliwa? Biblia hutaarifu kwamba isipokuwa watu hao watubu, “hawataurithi ufalme wa Mungu.”—1 Wakorintho 6:9, 10.
‘Kuwazuia Watu Wasioe’
Kwa sababu ya “kuenea kwa uasherati” (NW), Biblia husema kwamba “ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa.” (1 Wakorintho 7:2, 9) Licha ya shauri hili lenye hekima, wengi miongoni mwa makasisi wanatakwa kubaki waseja, yaani, bila kuoa. “Nadhiri ya useja haivunjwi,” aeleza Nino Lo Bello katika kitabu chake The Vatican Papers, “kasisi, mtawa wa kiume, au mtawa wa kike akishiriki katika mahusiano ya kingono. . . . Msamaha kwa ajili ya mahusiano ya kingono waweza kupatikana kwa kuungama kwa haki katika chumba cha kuungamia, ilhali ndoa ya kasisi yeyote haitatambuliwa na Kanisa hata kidogo.” Je, fundisho hilo limetokeza matunda mema au mabaya?—Mathayo 7:15-19.
Bila shaka, makasisi wengi huishi maisha safi kiadili, lakini sivyo ilivyo na walio wengi sana. Kulingana na 1992 Britannica Book of the Year, “Kanisa Katoliki ya Kiroma liliripotiwa kuwa lililipa dola milioni 300 ili kumaliza kesi za makasisi kutenda vibaya kingono.” Baadaye, chapa ya 1994 ilisema hivi: “Kifo cha makasisi kadhaa kutokana na UKIMWI kilifunua kuwapo kwa makasisi wagoni-jinsia-moja na maoni ya kwamba kulikuwa na idadi kubwa sana ya . . . wagoni-jinsia-moja waliovutwa kwenye ukasisi.” Si ajabu kwamba Biblia hutaarifu kwamba ‘kuwazuia watu wasioe’ ni ‘fundisho la mashetani.’ (1 Timotheo 4:1-3) “Kwa maoni ya wanahistoria fulani,” aandika Peter de Rosa katika kitabu chake Vicars of Christ, “[useja wa makasisi] labda umeharibu maadili zaidi kuliko mpango wowote mwingine katika Magharibi, kutia ndani umalaya. . . . [Huo] umekuwa kwa sehemu kubwa dosari kwenye jina la Ukristo. . . . Sikuzote useja wa kulazimishwa umeongoza kwenye unafiki miongoni mwa makasisi. . . . Kasisi aweza kuanguka mara elfu lakini anakatazwa na kanuni hata kuoa mara moja.”
Baada ya kufikiria maoni ya Mungu kuhusu ibada ya Baali, si vigumu kutambua jinsi ambavyo ni lazima awe anaona makanisa yaliyogawanyika ya Jumuiya ya Wakristo. Kitabu cha mwisho cha Biblia huchanganya namna zote za ibada bandia chini ya jina “[“Babiloni Mkubwa,” NW] mama wa makahaba na machukizo ya nchi.” “Ndani yake,” Biblia huongeza, “ilionekana damu ya manabii, na ya watakatifu, na ya wale wote waliouawa juu ya nchi.”—Ufunuo 17:5; 18:24.
Kwa hiyo, Mungu ahimiza wote wanaotaka kuwa waabudu wake wa kweli: “Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake, wala msipokee mapigo yake. . . . Mapigo yake yatakuja katika siku moja, mauti, na huzuni, na njaa, naye atateketezwa kabisa kwa moto. Kwa maana Bwana Mungu aliyemhukumu ni mwenye nguvu.”—Ufunuo 18:4, 8.
Swali sasa latokea: Baada ya kutoka dini bandia, mtu aende wapi? Ni namna gani ya ibada inayokubalika kwa Mungu?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]
Ibada ya Sanamu
Ibada ya Baali ilihusisha utumizi wa sanamu. Waisraeli walijaribu kuchanganya ibada ya Yehova na ile ya Baali. Hata walileta sanamu katika hekalu la Yehova. Maoni ya Mungu kuhusu ibada ya sanamu yalionyeshwa wazi alipoleta uharibifu juu ya Yerusalemu na hekalu lalo.
Mengi ya makanisa ya Jumuiya ya Wakristo yamejaa sanamu, ziwe ni kwa namna ya msalaba, picha, au sanamu za Mariamu. Isitoshe, waenda-kanisani wengi wanafundishwa kuinama, kupiga magoti, au kufanya alama ya msalaba mbele ya mifano hii. Kinyume na hilo, Wakristo wa kweli wanaamriwa ‘waikimbie ibada ya sanamu.’ (1 Wakorintho 10:14) Wao hawajaribu kumwabudu Mungu kwa msaada wa vitu vinavyoonekana.—Yohana 4:24.
[Hisani]
Musée du Louvre, Paris
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
“Kiongozi wa Kanisa Apaswa Kuwa Bila Kosa”
MANENO hayo yanatoka katika Tito 1:7, kulingana na Today’s English Version. Biblia King James Version yasomwa hivi: “Ni lazima askofu awe bila lawama.” Neno “askofu” latokana na neno la Kigiriki linalomaanisha “mwangalizi.” Hivyo wanaume wanaowekwa rasmi kuongoza katika kutaniko la Kikristo la kweli lazima waishi kupatana na viwango vya msingi vya Biblia. Wakikosa kufanya hivyo, ni lazima waondolewe kutoka cheo chao cha uangalizi, kwa kuwa wao si “vielelezo [tena] kwa lile kundi.” (1 Petro 5:2, 3) Takwa hili linachukuliwa kwa uzito kadiri gani na makanisa ya Jumuiya ya Wakristo?
Katika kitabu chake I Care About Your Marriage, Dakt. Everett Worthington arejezea uchunguzi wa mapadre 100 katika jimbo la Virginia, Marekani. Zaidi ya asilimia 40 walikiri kuwa wameshiriki katika namna fulani ya mwenendo wenye kuamsha-ashiki pamoja na mtu fulani ambaye hakuwa mwenzi wao wa ndoa. Idadi kubwa yao ilikuwa imefanya uzinzi.
“Muda wote wa mwongo uliopita,” laonelea Christianity Today, “kanisa limefadhaishwa kwa kurudia-rudia na funuo za mwenendo usio wa adili wa baadhi ya viongozi walo wenye kuheshimiwa sana.” Makala “Kwa Nini Mapadre Wazinzi Hawapaswi Kurudishwa” ilipinga zoea la kawaida katika Jumuiya ya Wakristo la kuwarudisha haraka viongozi wa kanisa kwenye vyeo vyao vya awali baada ya “kushtakiwa kwa sababu ya dhambi ya kingono.”