Kitabu cha Biblia Namba 57—Filemoni
Mwandikaji: Paulo
Mahali Kilipoandikiwa: Rumi
Uandikaji Ulikamilishwa: c. (karibu) 60-61 W.K.
1. Ni nini baadhi ya hali za barua kwa Filemoni?
BARUA hii ya Paulo yenye busara na upendo sana ni ya upendezi mkubwa kwa Wakristo leo. Si kwamba tu ndio waraka mfupi kabisa uliohifadhiwa kutoka mikononi mwa “mtume wa watu wa Mataifa” lakini katika Biblia nzima ni Yohana wa Pili na wa Tatu tu ndizo zenye habari chache zaidi. Pia, hii tu ndiyo barua “ya faragha” ya Paulo, kwa kuwa haikuelekezwa kirasmi kwa kundi fulani au kwa mwangalizi fulani mwenye madaraka, bali ilielekezwa kwa mtu binafsi na ilishughulikia tatizo moja tu maalumu ambalo Paulo alitaka kuzungumza na ndugu huyu Mkristo, Filemoni ambaye yaonekana alikuwa mwenye mali, aliyeishi katika jiji la Firigia la Kolosai, katikati kabisa ya Asia Ndogo.—Rum. 11:13.
2. Barua hii iliandikwa kwenye hali gani ya msingi na kwa kusudi gani?
2 Kusudi la barua hii lafunuliwa wazi: Wakati wa kifungo chake cha kwanza gerezani katika Rumi (59-61 W.K.), Paulo alikuwa na uhuru mkubwa wa kuhubiri Ufalme wa Mungu. Miongoni mwa wale waliosikiliza kuhubiri kwake alikuwamo Onesimo, mtumwa mtoro wa nyumbani mwa Filemoni, rafiki ya Paulo. Tokeo ni kwamba, Onesimo akawa Mkristo, na kwa kukubaliana na Onesimo, Paulo aliamua kumrudisha yeye kwa Filemoni. Pia wakati huu ndipo Paulo aliandika barua kwa makundi katika Efeso na Kolosai. Katika barua hizi mbili, alitoa shauri jema kwa watumwa Wakristo na wenye watumwa juu ya jinsi ya kujiendesha wenyewe ifaavyo katika uhusiano huu. (Efe. 6:5-9; Kol. 3:22–4:1) Hata hivyo, kuongezea hayo, Paulo akatunga barua kwa Filemoni ambamo yeye binafsi alisihi kwa ajili ya Onesimo. Ilikuwa barua iliyoandikwa kwa mkono wake mwenyewe—jambo lisilo kawaida ya Paulo. (Flm. 19) Uandikaji huo wa kibinafsi uliongezea sana uzito wa kusihi kwake.
3. Yaelekea sana barua kwa Filemoni iliandikwa lini, nayo ilipelekwaje?
3 Yaelekea kabisa kwamba barua hii iliandikwa karibu 60-61 W.K., kwa maana yaonekana Paulo alikuwa amehubiri katika Rumi muda mrefu utoshao kufanya waongofu. Pia, kwa sababu katika mstari 22 yeye aonyesha tumaini la kuachiliwa, twaweza kukata shauri kwamba barua hii iliandikwa baada ya muda fulani wa yeye kufungwa gerezani kupita. Yaonekana kwamba barua hizi tatu, moja kwa Filemoni na zile kwa makundi katika Efeso na Kolosai, zilipelekwa na Tikiko na Onesimo.—Efe. 6:21, 22; Kol. 4:7-9.
4. Ni nini kinachothibitisha ni nani mwenye kuandika na uasilia wa Filemoni?
4 Kwamba Paulo alikuwa ndiye mwandikaji wa Filemoni yaonekana wazi kutokana na mstari wa kwanza, ambamo yeye atajwa kwa jina. Alitambuliwa kuwa hivyo na Origen na Tertullian.a Uasilia wa kitabu hiki waungwa mkono pia na kuorodheshwa kwacho, pamoja na nyaraka nyingine za Paulo, katika Muratorian Fragment cha karne ya pili W.K.
YALIYOMO KATIKA FILEMONI
5. (a) Barua yafunguka kwa salamu na pongezi gani? (b) Paulo amwambia Filemoni nini juu ya Onesimo mtumwa wake?
5 Onesimo katumwa arudie bwana-mkubwa wake akiwa “zaidi ya mtumwa” (Mist. 1-25). Paulo apeleka salamu za uchangamfu kwa Filemoni, kwa Afia “dada yetu” (NW), kwa Arkipo, “askari mwenzetu,” na kwa kundi katika nyumba ya Filemoni. Ampongeza Filemoni (ambaye jina lake lamaanisha “Mwenye Kupenda”) kwa sababu ya upendo na imani alivyo navyo kuelekea Bwana Yesu na watakatifu. Ripoti za upendo wa Filemoni zimemletea Paulo shangwe na faraja kubwa. Paulo, mwanamume mwenye umri mkubwa na mfungwa, sasa ajieleza kwa uhuru mkubwa wa uneni kuhusu Onesimo “mtoto” wake, ambaye alipata ‘kumzaa’ akiwa katika vifungo vya gereza. Onesimo (ambaye jina lake lamaanisha “Mwenye Kuleta Faida”) alikuwa hapo kwanza amekuwa mtu asiyefaa kitu kwa Filemoni, lakini sasa ni mwenye mafaa kwa wote wawili Filemoni na Paulo.—Mist. 2, 10.
6. Ni kutendewa kwa aina gani ambako Paulo apendekeza kwa ajili ya Onesimo, naye atoa sababu kwa njia gani yenye busara?
6 Mtume angependa kubaki na Onesimo ili amhudumie gerezani, lakini hangefanya hivyo bila ruhusa ya Filemoni. Kwa hiyo anamtuma arudi, “na sasa yeye si mtumwa tu, ila ni bora zaidi ya mtumwa: yeye ni ndugu yetu mpenzi.” Paulo aomba kwamba Onesimo apokewe kwa fadhili, jinsi ile ile ambavyo Paulo mwenyewe angepokewa. Ikiwa Onesimo amemkosea Filemoni, acha hilo lidaiwe kwenye hesabu ya Paulo, kwa maana, Paulo amwambia Filemoni, hata “Wewe unalo deni kwangu.” (Mist. 16, 19, HNWW) Paulo atumaini kwamba huenda karibuni aachiliwe na kwamba huenda akamtembelea Filemoni, naye amalizia kwa salamu.
KWA NINI NI CHENYE MAFAA
7. Kwa habari ya Onesimo, Paulo alifuatiliaje sana wito wake wa juu akiwa mtume?
7 Kama inavyoonyeshwa na barua hii, Paulo hakuwa akihubiri “gospeli ya kijamii,” akijaribu kuondosha mfumo wa mambo uliopo na mashirika yao, kama vile utumwa. Yeye hata hakujikatia kauli ya kuweka huru watumwa Wakristo, bali, badala yake, alipeleka mtumwa aliyekuwa ametoroka Onesimo kwenye safari iliyomchukua kilometa zaidi ya 1,400 kutoka Rumi mpaka Kolosai, kwenda kwa bwana-mkubwa wake Filemoni. Kwa hiyo Paulo alishikilia sana wito wake wa juu akiwa mtume, akifuatilia sana utume wake wa kimungu wa “ufalme wa Mungu . . . na kuyafundisha mambo ya Bwana Yesu Kristo.”—Mdo. 28:31; Flm. 8, 9.
8. Ni matumizi gani yenye kutumika ya kanuni za Kikristo yanayotolewa kielezi na Filemoni?
8 Barua kwa Filemoni ni yenye kufunua kwa kuwa yaonyesha upendo na umoja uliokuwako miongoni mwa Wakristo wa karne ya kwanza. Katika hiyo twajifunza kwamba Wakristo wa mapema waliitana “ndugu” na “dada.” (Flm. 2, 20, NW) Zaidi ya hayo, yafunua kwa Wakristo leo matumizi yenye kutumika ya kanuni za Kikristo miongoni mwa ndugu Wakristo. Kwa upande wa Paulo, twaona wonyesho wa upendo wa kidugu, staha kwa ajili ya mahusiano ya kiraia na kwa ajili ya mali ya mtu na mwenzake, busara yenye matokeo, na unyenyekevu wa kusifika. Badala ya kujaribu kumlazimisha Filemoni amsamehe Onesimo kwa kutumia mamlaka aliyokuwa nayo akiwa mwangalizi mwenye kuongoza katika kundi la Kikristo, Paulo alimsihi kwa unyenyekevu kwa msingi wa upendo wa Kikristo na urafiki wake wa kibinafsi. Waangalizi leo waweza kufaidika na busara ambayo Paulo alimfikia Filemoni kwayo.
9. Kwa kutekeleza ombi la Paulo, ni kitangulizi gani kizuri ambacho Filemoni angeweka chenye kupendeza Wakristo leo?
9 Bila shaka Paulo alitazamia Filemoni atekeleze ombi lake, na kwa Filemoni kufanya hivyo kungekuwa ni matumizi yenye kutumika wa aliyosema Yesu katika Mathayo 6:14 na aliyosema Paulo katika Waefeso 4:32. Wakristo leo pia waweza kutazamiwa wawe wenye fadhili na wenye kusamehe ndugu aliyekosa. Ikiwa Filemoni angeweza kusamehe mtumwa aliyekuwa mali yake na akiwa huru kisheria kutenda vibaya kama alivyopenda, Wakristo leo wapaswa kuweza kusamehe ndugu aliyekosa—hili likiwa ni takwa lisilo gumu sana.
10. Utendaji wa roho ya Yehova ukoje wazi katika barua kwa Filemoni?
10 Utendaji wa roho ya Yehova waonekana wazi sana katika barua hii kwa Filemoni. Wadhihirishwa katika njia ya kiufundi ambayo kwayo Paulo alishughulikia tatizo lenye kuudhi upesi. Waonyeshwa wazi katika hisia-mwenzi, shauku nyororo, na tegemeo katika Mkristo mwenzi ambazo Paulo aonyesha. Waonyeshwa na uhakika wa kwamba barua kwa Filemoni, kama Maandiko mengineyo, yafundisha kanuni za Kikristo, yatia moyo umoja wa Kikristo, na kukuza upendo na imani ambazo ni tele miongoni mwa “watakatifu,” wanaotumainia Ufalme wa Mungu na ambao katika mwenendo wao fadhili za upendo za Yehova zaonyeshwa.—Mst. 5.
[Maelezo ya Chini]
a The International Standard Bible Encyclopedia, kilichohaririwa na G. W. Bromiley, Buku 3, 1986, ukurasa 831.