Sura Ya Tano
Imani Yao Ilishinda Jaribu Kali
1. Watu wengi huhisije juu ya kujitoa kwa Mungu na kwa nchi yao?
JE, WAPASWA kujitoa kwa Mungu au kwa nchi unayoishi? Wengi wangejibu kwa kusema, ‘Mimi huheshimu Mungu na nchi. Mimi humwabudu Mungu kulingana na kanuni za dini yangu; na wakati uleule, mimi huwa mwaminifu kwa nchi yangu.’
2. Mfalme wa Babiloni alikuwaje kiongozi wa kidini na vilevile wa kisiasa?
2 Leo, huenda tofauti kati ya ujitoaji wa kidini na uzalendo isionekane wazi, lakini katika Babiloni la kale tofauti hiyo haikuwepo. Kwa kweli, mambo ya serikali na mambo matakatifu yalichanganyikana sana hivi kwamba wakati mwingine hayangeweza kutofautishwa. “Katika Babiloni la kale,” aandika Profesa Charles F. Pfeiffer, “mfalme alikuwa Kuhani wa Cheo cha Juu na mtawala pia. Alitoa dhabihu na kuamua maisha ya kidini ya raia zake.”
3. Ni nini kinachoonyesha kwamba Nebukadreza alikuwa mtu wa kidini kwelikweli?
3 Mfikirie Mfalme Nebukadreza. Jina lake mwenyewe lamaanisha “Ee Nebo, Mlinde Mrithi!” Nebo alikuwa mungu wa Babiloni wa hekima na kilimo. Nebukadreza alikuwa mtu wa kidini kwelikweli. Kama ilivyotaarifiwa mapema, alijenga na kurembesha mahekalu ya miungu kadhaa ya Babiloni naye alijitoa hasa kwa Marduki, ambaye alimsifia ushindi wake mbalimbali wa kijeshi.a Pia yaonekana kwamba Nebukadreza alitegemea sana uaguzi akipanga mambo yake ya kivita.—Ezekieli 21:18-23.
4. Fafanua roho ya kidini ya Babiloni.
4 Kwa kweli, mambo ya kidini yalienea kotekote Babiloni. Jiji hilo lilikuwa na mahekalu zaidi ya 50, ambamo miungu mingi ya kiume na ya kike iliabudiwa, kutia ndani ule utatu wa Anu (mungu wa anga), Enlil (mungu wa dunia, hewa, na dhoruba), na Ea (mungu aliyetawala maji). Utatu mwingine ulikuwa wa Sin (mungu-mwezi), Shamash (mungu-jua), na Ishtar (mungu wa kike wa uwezo wa kuzaa). Mizungu, uchawi, na unajimu zilitumiwa sana katika ibada ya Babiloni.
5. Wayahudi waliokuwa uhamishoni walikabili ugumu gani uliotokezwa na mazingira ya kidini ya Babiloni?
5 Kuishi miongoni mwa watu walioabudu miungu mingi kulifanya mambo yawe magumu kwa Wayahudi waliokuwa uhamishoni. Karne kadhaa mapema, Musa alikuwa amewaonya Waisraeli kwamba kungekuwa na matokeo mabaya ikiwa wangemwasi Mpaji-Sheria Mkuu Kuliko Wote. Musa aliwaambia hivi: “BWANA atakupeleka wewe, na mfalme wako utakayemweka juu yako, kwa taifa usilolijua wewe wala baba zako; nawe huko utatumikia miungu mingine ya miti na mawe.”—Kumbukumbu la Torati 28:15, 36.
6. Kwa nini kuishi Babiloni kulitokeza ugumu wa pekee kwa Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria?
6 Wayahudi walijikuta katika hali iyo hiyo. Kuwa wenye uaminifu-maadili kwa Yehova kungekuwa jambo gumu, hasa kwa Danieli, Hanania, Mishaeli, na Azaria. Vijana hao wanne Waebrania walikuwa wameteuliwa kipekee ili wafundishwe mambo yanayohusu utumishi wa serikali. (Danieli 1:3-5) Kumbuka kwamba hata walikuwa wamepewa majina ya Kibabiloni—Belteshaza, Shadraka, Meshaki, na Abednego—yamkini ili kuwachochea wajipatanishe na mazingira yao mapya.b Kwa kuwa wanaume hao walikuwa na vyeo mashuhuri, ingeonekana waziwazi ikiwa wangekataa hata kidogo kuabudu miungu ya nchi hiyo—hata kungeonwa kuwa uhaini.
SANAMU YA DHAHABU YATOKEZA TISHO
7. (a) Fafanua sanamu iliyosimamishwa na Nebukadreza. (b) Kusudi la sanamu hiyo lilikuwa nini?
7 Yaonekana kwamba Nebukadreza alisimamisha sanamu ya dhahabu kwenye uwanda wa Dura akijaribu kuimarisha muungano wa milki yake. Sanamu hiyo ilikuwa na kimo cha dhiraa 60 (meta 27) na upana wa dhiraa 6 (meta 2.7).c Watu fulani huamini kwamba sanamu hiyo ilikuwa nguzo tu, au mnara mrefu wenye pande mraba zilizochongoka juu. Yawezekana kwamba ilikuwa na jukwaa lenye kimo cha juu sana ambalo lilikuwa na sanamu kubwa sana yenye umbo la kibinadamu, ambayo huenda ilimwakilisha Nebukadreza mwenyewe au mungu Nebo. Vyovyote vile, nguzo hiyo ndefu iliwakilisha Milki ya Babiloni. Kwa hiyo, ilipaswa kuonekana na kustahiwa.—Danieli 3:1.
8. (a) Ni nani walioalikwa kuhudhuria kuzinduliwa kwa sanamu hiyo, na wote waliohudhuria walipaswa kufanya nini? (b) Hukumu ya kukataa kuinamia sanamu hiyo ilikuwa nini?
8 Basi, Nebukadreza akapanga kuwe na sherehe ya kuizindua. Alikusanya maamiri, manaibu, maliwali, makadhi, watunza-hazina, mawaziri, mawakili, na wakuu wa wilaya zake zote. Mbiu ikapigwa: “Enyi watu wa kabila zote, na taifa, na lugha, mmeamriwa hivi, wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, lazima kuanguka na kuiabudu sanamu ya dhahabu, mfalme Nebukadreza aliyoisimamisha. Na kila mtu asiyeanguka na kuabudu atatupwa saa iyo hiyo katika tanuru ya moto uwakao.”—Danieli 3:2-6.
9. Yaonekana kuinamia sanamu ambayo Nebukadreza alikuwa amesimamisha kulimaanisha nini?
9 Watu fulani huamini kwamba Nebukadreza alipangia sherehe hiyo akijaribu kuwalazimisha Wayahudi waridhiane ibada yao kwa Yehova. Huenda haikuwa hivyo, kwa kuwa yaonekana kwamba maofisa wa serikali tu ndio walioalikwa kuhudhuria tukio hilo. Kwa hiyo, Wayahudi pekee ambao wangekuwapo ni wale tu waliokuwa na vyeo fulani katika serikali. Basi, yaonekana kwamba kuinamia sanamu hiyo kulikuwa sherehe iliyokusudiwa kutia nguvu muungano wa wenye kutawala. Msomi John F. Walvoord ataarifu hivi: “Kwa upande mmoja, wonyesho huo wa maofisa ulikuwa udhihirisho wenye kuridhisha wa nguvu za milki ya Nebukadreza na kwa upande mwingine ulikuwa wa maana ili kuabudu miungu ambayo kwa maoni yao ilikuwa imewawezesha kupata ushindi mbalimbali.”
WATUMISHI WA YEHOVA WAKATAA KURIDHIANA
10. Kwa nini haingekuwa vigumu kwa wasio Wayahudi kutii amri ya Nebukadreza?
10 Ingawa wengi wa watu waliokusanyika waliabudu miungu mbalimbali ya kibinafsi, hawangeona ugumu wowote wa kuabudu sanamu ya Nebukadreza iliyokuwa mbele yao. “Wote walikuwa wamezoea kuabudu sanamu, na kuabudu mungu mmoja hakukuwazuia wasisujudie mungu mwingine,” akaeleza msomi mmoja wa Biblia. Aliendelea kusema hivi: “Jambo hilo lilipatana na maoni yaliyokuwako wakati huo ya waabudu-sanamu ya kwamba kuna miungu mingi . . . na kwamba si kosa kusujudia miungu ya watu wengine au nchi nyingine.”
11. Kwa nini Shadraka, Meshaki, na Abednego walikataa kuinamia sanamu?
11 Hata hivyo, lilikuwa jambo tofauti kwa Wayahudi. Walikuwa wameamriwa hivi na Mungu wao, Yehova: “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu.” (Kutoka 20:4, 5) Kwa hiyo, muziki ulipoanza na wale waliokusanyika walipoisujudia sanamu, vijana watatu Waebrania—Shadraka, Meshaki, na Abednego—waliendelea kusimama.—Danieli 3:7.
12. Wakaldayo fulani waliwashtaki Waebrania hao watatu juu ya nini, na kwa nini?
12 Kukataa kwa maofisa hao watatu Waebrania kuabudu sanamu hiyo kuliwaghadhibisha Wakaldayo fulani. Mara moja, wakamwendea mfalme “wakaleta mashitaka juu ya Wayahudi.”d Hawakutaka kujua sababu. Wakitaka Waebrania hao wahukumiwe kwa sababu ya kutokuwa waaminifu-washikamanifu na kwa sababu ya uhaini, washtaki hao walisema hivi: “Wako Wayahudi kadha wa kadha uliowaweka juu ya mambo ya wilaya ya Babeli, yaani, Shadraka, na Meshaki, na Abednego; watu hawa, Ee mfalme, hawakukujali wewe; hawaitumikii miungu yako, wala kuiabudu ile sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”—Danieli 3:8-12.
13, 14. Mwenendo wa Shadraka, Meshaki, na Abednego ulimfanya Nebukadreza atendeje?
13 Lazima Nebukadreza awe alitamauka kama nini kwa sababu Waebrania hao watatu hawakutii amri yake! Kwa wazi hakuwa amefanikiwa kugeuza Shadraka, Meshaki, na Abednego wawe watetezi waaminifu-washikamanifu wa Milki ya Babiloni. Je, hakuwa amewaelimisha katika hekima ya Wakaldayo? Kwani, hata alikuwa amebadili majina yao! Lakini ikiwa Nebukadreza alifikiri kwamba elimu nyingi ingewafundisha njia mpya ya kuabudu au kwamba kubadili majina yao kungebadili nyutu zao, alikuwa amekosea sana. Shadraka, Meshaki, na Abednego walidumu wakiwa watumishi waaminifu-washikamanifu kwa Yehova.
14 Mfalme Nebukadreza akaghadhibika. Mara moja, akamwita Shadraka, Meshaki, na Abednego. Akauliza: “Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, je! ni kwa makusudi hata hammtumikii mungu wangu wala kuisujudia sanamu ya dhahabu niliyoisimamisha?” Huenda Nebukadreza alisema maneno hayo akiwa ameshangaa asiweze kuamini. Ni lazima awe alifikiri, ‘Wanaume watatu wenye akili timamu wangewezaje kupuuza amri hiyo ya moja kwa moja—ambayo kutoitii kungetokeza adhabu kali?’—Danieli 3:13, 14.
15, 16. Nebukadreza aliwapa Waebrania hao watatu fursa gani?
15 Nebukadreza alinuia kuwapa Waebrania hao watatu fursa nyingine. “Basi sasa, kama mkiwa tayari,” akasema, “wakati mtakapoisikia sauti ya panda, na filimbi, na kinubi, na zeze, na santuri, na zomari, na namna zote za ngoma, kuanguka na kuisujudia sanamu niliyoisimamisha, ni vema; bali msipoisujudia, mtatupwa saa iyo hiyo katika tanuru iwakayo moto; naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na m[i]kono yangu?”—Danieli 3:15.
16 Yaonekana, somo la sanamu ya ndoto (iliyorekodiwa katika Danieli sura ya 2) halikuwa limebadili moyo na akili ya Nebukadreza daima. Huenda tayari alikuwa amesahau taarifa yake mwenyewe aliyomwambia Danieli: “Mungu wenu ndiye Mungu wa miungu, na Bwana wa wafalme.” (Danieli 2:47) Sasa ilionekana kama Nebukadreza alikuwa akishindana na Yehova, akisema kwamba hata Yehova hangeweza kuwaokoa Waebrania kutoka katika hukumu ambayo wangepata.
17. Shadraka, Meshaki, na Abednego walisemaje baada ya kusikia toleo la mfalme?
17 Shadraka, Meshaki, na Abednego hawakuhitaji kufikiria tena jambo hilo. Walijibu mara moja wakisema: “Ee Nebukadreza, hamna haja kukujibu katika neno hili. Kama ni hivyo, Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto; naye atatuokoa na mkono wako, Ee mfalme. Bali kama si hivyo, ujue, Ee mfalme, ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”—Danieli 3:16-18.
WATUPWA NDANI YA TANURU YENYE MOTO!
18, 19. Ni nini kilichotukia Waebrania hao watatu walipotupwa kwenye tanuru yenye moto?
18 Nebukadreza mwenye ghadhabu akaamuru kwamba watumishi wake waipashe moto tanuru, mara saba zaidi ya kawaida. Kisha akaamuru “baadhi ya watu mashujaa wa jeshi lake” kuwafunga Shadraka, Meshaki, na Abednego na kuwatupa kwenye “tanuru iliyokuwa ikiwaka moto.” Walitekeleza maagizo ya mfalme, wakawatupa Waebrania hao watatu motoni, wakiwa wamefungwa na wakiwa na mavazi yao—huenda ili wachomeke haraka zaidi. Hata hivyo, mashujaa wa Nebukadreza wenyewe ndio waliouawa na miali ya moto.—Danieli 3:19-22.
19 Lakini jambo la ajabu lilikuwa likitukia. Ingawa Shadraka, Meshaki, na Abednego walikuwa katikati ya tanuru yenye moto, miali haikuwa ikiwachoma. Nebukadreza alipigwa na butaa kama nini! Walikuwa wametupwa kwenye moto mkali, wakiwa wamefungwa kwa nguvu, lakini bado walikuwa hai. Hata walikuwa wakitembea-tembea tu motoni! Lakini Nebukadreza aliona kitu kingine. “Je! hatukutupa watu watatu, hali wamefungwa, katikati ya moto?” akauliza mawaziri wake wa makao ya kifalme. “Kweli, Ee mfalme,” wakajibu. “Tazama,” Nebukadreza akapaaza sauti, “mimi naona watu wanne, nao wamefunguliwa, wanatembea katikati ya moto hali hawana dhara; na sura yake yule wa nne ni mfano wa mwana wa miungu.”—Danieli 3:23-25.
20, 21. (a) Nebukadreza aliona nini juu ya Shadraka, Meshaki, na Abednego walipotoka kwenye tanuru? (b) Nebukadreza alilazimika kukiri nini?
20 Nebukadreza akaukaribia mlango wa tanuru yenye moto. “Enyi Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watumishi wa Mungu Aliye juu,” akawaita kwa sauti, “tokeni, mje huku.” Waebrania hao watatu wakatoka motoni. Haikosi watu wote waliojionea muujiza huo—kutia ndani maamiri, manaibu, maliwali, na mawaziri—waliduwaa. Kwani, ilikuwa kana kwamba vijana hao watatu hata hawakuwa wameingia kamwe ndani ya tanuru! Hawakuwa na harufu ya moto, na hakuna hata unywele wa vichwa vyao uliokuwa umechomeka.—Danieli 3:26, 27.
21 Sasa Mfalme Nebukadreza alilazimika kukiri kwamba Yehova ndiye Mungu Aliye Juu. “Na ahimidiwe Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego,” akatangaza, “aliyemtuma malaika wake, akawaokoa watumishi wake waliomtumaini, wakaligeuza neno la mfalme, na kujitoa miili yao ili wasimtumikie mungu mwingine, wala kumwabudu, ila Mungu wao wenyewe.” Kisha mfalme akaongezea onyo hili kali: “Basi mimi naweka amri ya kuwa kila kabila ya watu, na kila taifa, na kila lugha, watakaonena neno lo lote lisilopasa juu ya huyo Mungu wa Shadraka, na Meshaki, na Abednego, watakatwa vipande vipande, na nyumba zao zitafanywa jaa; kwa kuwa hakuna Mungu mwingine awezaye kuokoa namna hii.” Basi, Waebrania hao watatu wakapendelewa tena na mfalme, ‘wakakuzwa katika wilaya ya Babeli.’—Danieli 3:28-30.
IMANI NA JARIBU KALI LEO
22. Watumishi wa Yehova wa leo hukabili hali gani zinazofanana na zile za Shadraka, Meshaki, na Abednego?
22 Leo, waabudu wa Yehova hukabili hali kama zile zilizowakabili Shadraka, Meshaki, na Abednego. Ni kweli kwamba huenda watu wa Mungu wasiwe uhamishoni kihalisi. Hata hivyo, Yesu alisema kwamba wafuasi wake wangekuwa “si sehemu ya ulimwengu.” (Yohana 17:14) Wao ni “wageni” kwa kuwa hawakubali desturi, mitazamo, na mazoea yanayowazunguka ambayo si ya Kimaandiko. Kama mtume Paulo alivyoandika, Wakristo wanapaswa “[kukoma] kufanyizwa kulingana na mtindo wa mfumo huu wa mambo.”—Waroma 12:2.
23. Waebrania hao watatu walionyeshaje kwamba walikuwa imara, na Wakristo leo wanaweza kuigaje kielelezo chao?
23 Waebrania hao watatu walikataa kufanyizwa kulingana na mfumo wa Babiloni. Hata mafundisho mengi ya hekima ya Wakaldayo hayakuwafanya wayumbeyumbe. Majadiliano hayangeweza kuubadili msimamo wao, nao walikuwa waaminifu kwa Yehova. Wakristo leo wanahitaji kuwa imara hivyohivyo. Hawapaswi kuaibika kwa kuwa wanatofautiana na walimwengu. Kwa kweli, “ulimwengu unapitilia mbali na ndivyo na tamaa yao.” (1 Yohana 2:17) Kwa hiyo, kujipatanisha na mfumo huu wa mambo ulio mahututi ni upumbavu na ubatili.
24. Msimamo wa Wakristo wa kweli walinganaje na ule wa Waebrania watatu?
24 Wakristo wanahitaji kujilinda dhidi ya aina zote za ibada ya sanamu, kutia ndani zile ambazo si wazi.e (1 Yohana 5:21) Shadraka, Meshaki, na Abednego walisimama mbele ya sanamu ya dhahabu kwa utii na staha, lakini walitambua kwamba kuiinamia si wonyesho tu wa staha. Kulikuwa ibada, na kuiabudu kungetokeza hasira ya kisasi ya Yehova. (Kumbukumbu la Torati 5:8-10) John F. Walvoord aandika hivi: “Kihalisi huko kulikuwa kusalimu bendera, ingawa, kwa sababu uaminifu-mshikamanifu kwa dini na kwa taifa ulikuwa kama kitu kimoja, huenda kukawa kulihusisha mambo ya kidini.” Leo, Wakristo wa kweli huchukua msimamo thabiti kama huo dhidi ya ibada ya sanamu.
25. Umejifunza nini kutokana na kisa halisi cha Shadraka, Meshaki, na Abednego?
25 Simulizi la Biblia juu ya Shadraka, Meshaki, na Abednego ni kielelezo halisi kwa wote ambao wameazimia kujitoa kwa Yehova peke yake. Yaonekana kwamba mtume Paulo aliposema juu ya wengi waliodhihirisha imani, kutia na wale ambao “wa[li]zima kani ya moto,” alikuwa akiwarejezea Waebrania hao watatu. (Waebrania 11:33, 34) Yehova atawathawabisha wote wanaoiga imani hiyo. Waebrania hao watatu walikombolewa kutoka katika tanuru iwakayo moto, lakini twaweza kuwa na uhakika kwamba atawafufua watu wote walio waaminifu-washikamanifu wapotezao maisha yao wakishika uaminifu-maadili naye atawabariki kwa kuwapa uhai udumuo milele. Vyovyote vile, Yehova “huwalinda nafsi zao watauwa wake, na kuwaokoa na mkono wa wasio haki.”—Zaburi 97:10.
[Maelezo ya Chini]
a Watu fulani huamini kwamba Marduki, aliyeonwa kuwa mwanzilishi wa Milki ya Babiloni, huwakilisha Nimrodi aliyefanywa kuwa mungu. Hata hivyo, hakuna uhakika wa jambo hilo.
b Jina “Belteshaza” lamaanisha “Linda Uhai wa Mfalme.” Huenda “Shadraka” lamaanisha “Amri ya Aku,” mungu-mwezi wa Sumeria. “Meshaki” yamkini larejezea mungu wa Sumeria, nalo “Abednego” lamaanisha “Mtumishi wa Nego,” au Nebo.
c Kwa sababu sanamu hiyo ilikuwa kubwa sana, wasomi fulani wa Biblia huamini kwamba ilitengenezwa kwa mbao kisha ikafunikwa kwa dhahabu.
d Usemi wa Kiaramu unaotafsiriwa “-leta mashitaka” wamaanisha ‘kula vipande’ vya mtu—kana kwamba kumtafuna kwa kumchongea.
e Kwa kielelezo, Biblia huonyesha kwamba ulafi na tamaa zahusiana na ibada ya sanamu.—Wafilipi 3:18, 19; Wakolosai 3:5.
UMEFAHAMU NINI?
• Kwa nini Shadraka, Meshaki, na Abednego walikataa kuinamia sanamu iliyosimamishwa na Nebukadreza?
• Msimamo wa Waebrania hao watatu ulimfanya Nebukadreza atendeje?
• Yehova aliwathawabishaje Waebrania hao watatu kwa sababu ya imani yao?
• Umejifunza nini kwa kusikiliza kisa halisi cha Shadraka, Meshaki, na Abednego?
[Picha katika ukurasa wa 68]
[Picha katika ukurasa wa 70]
1. Mnara wa hekalu (“ziggurat”) huko Babiloni
2. Hekalu la Marduki
3. Bamba la shaba linaloonyesha mungu Marduki (kushoto) na mungu Nebo (kulia) wakiwa wamesimama juu ya majoka
4. Picha ya Nebukadreza, aliyejulikana sana kwa sababu ya ujenzi wake
[Picha katika ukurasa wa 76]
[Picha katika ukurasa wa 78]