Fashoni—Mtindo wa Kale wa Kigiriki
NA MLETA HABARI WA AMKENI! KATIKA UGIRIKI
KWA NINI waandikaji Wakristo Paulo na Petro walihitaji kutoa shauri hususa kuhusu mavazi ya kike katika karne ya kwanza? Kwa kielelezo, Paulo aliandika hivi: “Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani.” (1 Timotheo 2:9) Vilevile, Petro aliona uhitaji wa kusema kuhusu “kusuka nywele kwa nje,” “kuvalia madoido ya dhahabu,” na “kuvalia mavazi ya nje.”—1 Petro 3:3, NW.
Walikuwa wakiandikia Wakristo waliokuwa wakiishi chini ya uvutano wa utamaduni wa Kiyunani, ambao ulitoka moja kwa moja kwenye ustaarabu wa kale wa Kigiriki. Je, kulikuwa na kitu chochote kama fashoni katika Ugiriki wa kale? Wengi wanapofikiria juu ya Mgiriki asili wa kale, huenda wakamwazia akivalia ile khi·tonʹ, yenye mweneo mkubwa au joho—vazi lililo kama gauni—licha ya hali ya kuwa kiume au kike, kipindi cha wakati, au mahali pa kuzaliwa pa mwenye kuivaa.a Je, maoni hayo ni sawa? La!
Jinsi Vazi la Juu Lilivyofanyizwa na Kuvaliwa
Kuchunguza kwa ukaribu sanamu, michoro ya kiserami, na maandishi ya kale kwafunua kwamba mavazi ya kale ya Kigiriki yalikuwa zaidi ya kuwa tu majoho marefu meupe. Mitindo, nguo, rangi, na bombwe, na vilevile virembesho, vilikuwa vya aina tofauti. Wanawake hasa walitumia vifaa tofauti vya kiubuni ili kurembesha sura zao.
Wasomaji wa utenzi uitwao Odyssey wa mtunga-shairi wa kale wa Kigiriki Homer, unaloelezea kuzunguka-zunguka miaka kumi kwa shujaa wa kihadithi Odysseus, huenda wakakumbuka kwamba huku akimngojea arudi nyumbani, Penelope, mkeye shujaa huyo, aliendelea kufuma na kufumua kipande kilekile cha nguo kwa miaka yote hiyo. Homer afanya marejezo zaidi kwa mavazi, ikimaanisha kwamba kutokeza mavazi kulikuwa moja ya madaraka makuu ya kinyumbani ya mwanamke tangu nyakati za kale.
Baada ya kitambaa kuwa kimefumwa, kilikatwa ili kutengeneza khi·tonʹ—vazi lililo kama shati, la kitani, na baadaye nyakati nyingine la sufu—lililofanyiza msingi wa mavazi ya kiume na ya kike. Katika nyakati za Kikale (yapata 630 hadi 480 K.W.K.), khi·tonʹ ya wanawake (iliyokuwa ikiitwa e·sthesʹ wakati huo) ilikuwa kipande cha kitambaa chenye upana wa mwanamke na urefu ulio mara mbili urefu wa mikono yake. (Linganisha Yohana 19:23; Matendo 10:30, The Kingdom Interlinear.) Khi·tonʹ ilikazwa kwa vifungo, ambavyo mwanzoni vilitengenezwa kwa mifupa ya miguu ya wanyama wadogo na baadaye kwa chuma. Ilikuwa wazi pande zote mbili, ikishikanishwa pamoja kwa ukanda kiunoni na hivyo ikileta sura ya mavazi mawili tofauti.
Baadaye katika karne ya sita K.W.K. khi·tonʹ ya Ionia ilionekana ikiwa kama vazi badala ya kanzu fupi, ikiwa imeshonwa pande zote na kutokunjwa juu, na kama tokeo, ilikuwa rahisi zaidi kigharama katika utumizi wayo wa kitambaa. Mbali na kuwa cheupe chote, kitambaa hicho nyakati fulani kiliwekwa mistari myembamba mirefu yenye rangi tofauti-tofauti, au kuongezwa matamvua. Baadhi ya rangi zenye kupendwa sana zilizotumiwa zilikuwa dhahabu-nyekundu na nyekundu. Baadaye katika kipindi cha Kiyunani, uvutano wa Kiasia ulileta rangi nyangavu, kama vile nyekundu-nyeupe, samawati, rangi ya urujuani, na manjano. Vitu vingine vilivyorembeshwa kwa dhahabu au vilivyotariziwa kwa maua, viliwekwa hasa kwa ajili ya sanamu za vijimungu au waigizaji waliowaigiza.
Ni Nini Kingine Ambacho Mwanamke Mwathene Angevalia?
Hakuna mwanamke Mwathene aliyejiheshimu ambaye angetoka nyumbani kwake bila kuvalia hi·maʹti·on, au mtandio wake. Kipande hiki cha kitambaa kilicho pembe-mraba kingevaliwa kwa njia nyingi—kuwekwa mabegani kama kashida, kikivikwa juu ya bega la kushoto na chini ya bega la kulia, au kuvutwa juu kichwani kama kinga kwa jua. Mitandio ilipatikana kwa ukubwa tofauti-tofauti pia, ile mikubwa zaidi kwa ajili ya baridi ilikuwa kama joho. Mara kwa mara hi·maʹti·on ilikuwa na mipaka ya urembeshaji, na kule kukunjwa na kuning’inizwa kwayo katika njia ya kwamba mikunjo hiyo ilionekana kama mifinyo kulihitaji ustadi mkubwa.
Ky·pas·sis, aina ya koti fupi lililofungwa kwa vifungo upande wa mbele, nyakati fulani lilivaliwa badala ya hi·maʹti·on. Kofia, kama tuzijuavyo leo, hazikuvaliwa na wanawake, ingawaje katika siku yenye joto sana, ski·aʹdei·on, au mwavuli wa kukinga jua, ungeweza kubebwa. Wanawake matajiri wa Kigiriki mara kwa mara walivalia peʹplos, au shela. Maandiko ya Kigiriki pia hurejezea “vazi la kichwani” (Kigiriki, pe·ri·boʹlai·on) katika maandishi ya Paulo.—1 Wakorintho 11:15, NW.
Wakiwa ndani ya nyumba, Wagiriki wa kale kwa kawaida walikuwa hawavai viatu, na wakati mwingine hata walipokuwa nje. Kulingana na mtunga-shairi Hesiod, watu wa mashambani walivalia makubadhi yaliyotiwa kwa ndani namna ya nguo iliyofumwa kwa manyoya na kugandamizwa. Wanawake wafupi wakati fulani walivalia viatu vilivyokuwa na soli nene ya gome ili waonekane warefu.
Kuvalia Madoido ya Dhahabu
Madoido yalitengenezwa kwa mabamba ya dhahabu yaliyorembwa kwa michoro ya kimazingira, hasa ya wanyama na mimea, yalikuwa ya kawaida sana. Madoido mengine yaliyopendwa na wengi yalikuwa skarabu na skaraboidi, yaliyobandikwa katika pete yenye kuzunguka. Vikuku—vilivyoitwa wakati mwingine oʹphis (joka) au draʹkon (drakoni)—vilikuwa vipande vya johari vilivyopendwa sana.
Uchimbuzi umefukua taji, madini zilizochorwa, mikufu, jebu, pete, na madoido mengine. Vitu hivyo vya kujiremba kwa kawaida vilitengenezwa kutokana na dhahabu, chuma, na shaba na mara chache sana kutokana na fedha, hali shanga zilikuwa za kauri au mawe yaliyo nusu-johari.
Vipuli vilipendwa na wengi pia. Wakati mwingine vilikuwa alama ya nje ya heshima, alama ya uwezo, au wonyesho wenye ushaufu wa ufanisi wa kimwili. Wasichana kwa kawaida walitobolewa masikio wakiwa na umri mdogo.
Mitindo ya Kusuka Nywele
Katika Ugiriki wa kale mitindo ya nywele ilikuwa mingi na tofauti-tofauti. Mmoja wa mitindo iliyopendwa sana ulikuwa na mgawanyo wa nywele katikati zikifungwa nyuma kwa utepe wenye rangi. Wanawake wengine walikuwa na nywele zilizokusanywa kwenye kifundo juu ya kichwa. Wengine walikuwa na nywele fupi zilizofunika kipaji. Wakati mwingine tepe zilifungwa kuzunguka kipaji na kurembwa kwa kifungo kidogo cha chuma mbele. Koleo za chuma za kupinda zilitumiwa ili kutengeneza nywele zilizoviringana. Kuna uhakika kwamba katika Athene ya kale wanawake wengi walitia nywele zao rangi. Mwalimu wa kufundisha usemaji Lucian alishutumu upuzi wa wanawake waliotumia “mashine” ili kutengeneza nywele zilizoviringana na waliofuja mali za waume zao kwa ajili ya rangi za nywele za Kiarabu.
Mitindo ya nywele iliyopendwa na wengi, ambayo wanawake wa matajiri wa Kigiriki walikuwa nayo ilihusisha mambo mengi mno na ilikuwa yenye kutumia wakati mwingi sana. Mitindo hiyo ilihitaji saa nyingi za matayarisho ya warembeshaji na matumizi yenye gharama ya juu, na ilikuwa mishaufu sana, ikivuta uangalifu wa watu kwa mwenye mtindo huo.
Wanawake Wanaojiremba Wenyewe
Utumizi wa virembeshi ulikuwa zoea jingine la Mashariki lililoletwa Ugiriki na wafanya-biashara na wasafiri. Katika karne ya tano K.W.K., wanawake Waathene walitumia unga-unga wa risasi ili kufanya nyuso zao kuwa nyeupe zaidi. Midomo ilifanywa kuwa myekundu kwa kutumia unga mwekundu uliotengenezwa ama kwa mwani ama kutoka mizizi ya mimea. Nyushi ziliongezwa rangi kwa masizi, na kope zilifanywa kuwa nyeusi zaidi kwa kohli (kama vile unga-unga wa antimoni-salfidi), huku maskara ikitengenezwa kutokana na samadi ya ng’ombe au kutokana na mchanganyiko wa sehemu nyeupe ya yai na gundi.
Utafiti wa kiakiolojia katika kasri, maziara, na vijiji vidogo vya kale vya Kigiriki umefunua vitu vingi vinavyohusiana na urembeshi wa wanawake. Vifaa hivyo vya aina nyingi na vyombo vyatia ndani vioo, vichana, pini zenye umbo la ndoana, visu vidogo vyenye kupendeza, pini za nywele, nyembe, na vijichupa vya marashi, virimu, na rangi.
Urembo wa Kweli
Kwa wazi, licha ya dhihaka za washutumu wa kale wa Kigiriki, hali ya kimtindo ilikuwa sifa iliyokuwa na uvutio katika mwanamke na ambayo mwanamke wa kale Mgiriki alitolea wakati wake mwingi, bidii, utunzi, na uangalifu.
Kwa mwanamke Mkristo, hili kwa urahisi lingefunika mkazo ambao ungewekwa katika sifa za kiroho. Hiyo ndiyo sababu mtume Petro anakazia kwamba mwanamke mrembo zaidi na mavazi ya maana zaidi ambayo mwanamke aweza kuvaa ni “utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo na thamani kuu mbele za Mungu.” (1 Petro 3:3, 4) Mwanamke yeyote anayekuwa na mtindo huo wa urembo wa utu wa ndani, pamoja na mavazi safi na yenye kiasi, kila wakati atakuwa akivalia kwa uvutio, katika fashoni isiyo na waa na isiyofuata wakati fulani. Paulo alimwandikia Timotheo hivi: “Hivyohivyo natamani wanawake wajirembe wenyewe katika mavazi yenye mpangilio mzuri, pamoja na kiasi na utimamu wa akili, si kwa mitindo ya kusuka nywele na dhahabu au lulu au mavazi yaliyo ghali sana, bali katika njia ifaayo wanawake wanaodai kumstahi Mungu, yaani, kupitia matendo yaliyo mema.”—1 Timotheo 2:9, 10, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Khi·tonʹ hutajwa mara 11 katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo na hutafsiriwa kuwa “vazi la juu” na “vazi la ndani” katika New World Translation of the Christian Greek Scriptures. Ona Expository Dictionary of New Testament Words, ya W. E. Vine, Buku 1, ukurasa 198, chini ya “Clothing.”
[Sanduku katika ukurasa wa 24]
Madoido na Dini
Mara nyingi sana picha zinazopatikana kwenye madoido ya kale ya Kigiriki ni ya asili ya kidini. Nyingine zilikuwa mawe yaliyochorwa sanamu yaliyowakilisha vijimungu na vijimungu-kike kadhaa, kama vile Artemi, na nusu-miungu kama vile Hercules. Zawadi za kawaida sana zilizotolewa kwenye madhabahu kotekote katika Ugiriki zilikuwa madoido yenye mandhari za kawaida za kidini. Yakionyesha itikadi za kipagani kwamba nafsi ya kibinadamu huokoka kifo cha mwili, madoido mengi ya kurembesha yaliwekwa kaburini pamoja na mfu.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kushoto: Ile Parthenoni, hekalu lililowekwa wakfu kwa kijimungu-kike Athena
Juu: Medalioni iliyochorwa kichwa na kifua cha Artemi Kulia: Kulia: Msichana akiwa amevalia “hi·maʹti·on”
Chini kulia: Sanamu ya kijimungu
Kushoto kabisa: Kijimungu-Kike kikiwa kimevalia “khi·tonʹ” na “hi·maʹti·on”
Kushoto: Vikuku vya dhahabu vikikomea kwenye vichwa vya nyoka
[Hisani]
Juu kulia: Acropolis Museum, Greece
Picha nyingine zote: National Archaeological Museum, Athens
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]
Acropolis, Athens, Greece