Thamani Ya “Chombo Dhaifu Zaidi”
‘ENYI waume, endeleeni kukaa na [wake zenu] kulingana na ujuzi,’ akaandika mtume Petro, “mkiwapa heshima kama chombo dhaifu zaidi, yaani, mwanamke.” (1 Petro 3:7) Je, Andiko hili linalomtaja mwanamke kuwa “chombo dhaifu zaidi” linawadharau wanawake kwa njia yoyote ile? Hebu tuone mwandishi huyo aliyeongozwa kwa roho ya Mungu alimaanisha nini.
Neno la Kigiriki linalotafsiriwa “heshima” humaanisha “bei, thamani, . . . staha.” Kwa hiyo, mume Mkristo anapaswa kumtendea mke wake kwa wororo, na kumjali sana kama chombo dhaifu chenye thamani. Kwa hiyo, wanawake hawadharauliwi kwa njia yoyote. Kwa mfano, fikiria taa yenye umbo la yungiyungi iliyotengenezwa na msanii aitwaye Tiffany. Taa hiyo maridadi sana inaweza kuonwa kuwa chombo dhaifu. Je, thamani ya taa hiyo inapungua kwa sababu ya hali yake? Sivyo hata kidogo! Mnamo mwaka wa 1997, taa ya kale zaidi ya Tiffany ilipigwa bei mnadani kwa dola milioni 2.8 za Marekani! Umbo lake tata halikupunguza thamani yake, badala yake liliongeza thamani yake.
Vivyo hivyo, kumpa mwanamke heshima kama chombo dhaifu zaidi hakupunguzi thamani yake wala kumdharau. Mume anayeishi na mke wake “kulingana na ujuzi” anazingatia uwezo wake na udhaifu wake, mambo anayopenda na yale asiyopenda, maoni na hisia zake. Mume mwenye kujali hutambua na kuheshimu tofauti za utu kati yake na mke wake. Humjali mke wake ‘kusudi sala zake zisizuiwe.’ (1 Petro 3:7) Mume anayeshindwa kuheshimu sifa nzuri za kike za mke wake anahatarisha uhusiano wake na Mungu. Ni wazi kwamba Neno la Mungu haliwadharau wanawake. Badala yake, linawastahi na kuwaheshimu.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 32]
© Christie’s Images Limited 1997