Fumbo—Ni Nani Kahaba Babuloni Mkubwa?
MWANAMKE, kahaba mwenye sifa mbaya, ambaye amekuwa na uvutano kwa maisha za mabilioni ya watu, anauawa, anafishwa. Lakini huo si ufishaji wa kawaida. Ni nini kinachoufanya uwe tofauti? Mfishaji ni mnyama, hayawani-mwitu anayemvua awe uchi, kunofua mnofu wake, halafu kuacha masalio yake yaharibiwe na moto. Ni nani mwanamke huyo mwenye uvutano mwingi? Kwa nini hayawani-mwitu anamshambulia? Amefanya nini kustahili mwisho huu wenye jeuri?a—Ufunuo 17:16, 17.
Huu ungeweza kuwa msingi wa hadithi ya kifumbo yenye kuvutia—ila tu ni kwamba utatanishi wa kisa chenyewe hauvuti fikira kwenye kitabu fulani cha hadithi. Ni uhalisi wa kihistoria unaoendelea kutimizwa. Na ni wa maana kwako kwa sababu kahaba huyu mwenye sifa mbaya huenda akawa anatolea maisha yako uvutano sasa hivi. Zaidi ya hilo, kubaki kwako pamoja naye au kuvunja uhusiano naye ndiko kutamaanisha tofauti kati ya uhai na kifo. Kwa hiyo yeye ni nani?
Wanaofanya Ununuzi kwa Mwanamke wa Fumbo
Huyu mwanamke mwenye utongozi hatari, huyu mshawishi asiye na aibu, anaelezwa na Yohana katika Ufunuo kitabu cha Biblia cha kiunabii, tunaposoma hivi: “Na [malaika] akapeleka mimi mbali kwa nguvu ya roho kuingia ndani ya nyika. Na mimi nikashika mwono wa mwanamke akiwa ameketi juu ya hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu ambaye alikuwa amejaa majina ya kufuru na ambaye alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Na huyo mwanamke alikuwa amepambwa zambarau na nyekundu-nyangavu, na alikuwa amerembwa kwa dhahabu na jiwe la thamani na lulu na katika mkono wake alikuwa na kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa vitu vya kunyarafisha na vitu visivyo safi vya uasherati wake. Na juu ya kipaji cha uso wake paliandikwa jina, fumbo: ‘Babuloni Mkubwa, mama ya makahaba na ya vitu vya kunyarafisha vya dunia.’”—Ufunuo 17:3-5, NW.
Sasa ni lazima huyu “Babuloni Mkubwa” awe ni mwanamke mwenye nguvu nyingi za kuhofisha, kwa maana usimulizi unasema katika mstari wa 1 kwamba yeye “huketi juu ya maji mengi.” Hiyo inamaanisha nini? Malaika wa Mungu alimweleza Yohana hivi: “Maji ambayo wewe uliona, ambapo kahaba anaketi, humaanisha vikundi vya watu na umati wa watu na mataifa na ndimi.” (Ufunuo 17:15, NW) Bila shaka huyu ni malaya mwenye uvutano ulimwenguni pote. Lakini si mkware wa kikawaida tu. Yeye ndiye “mama ya makahaba,” bibi mkubwa wa shughuli hiyo. Yeye ndiye hutoa maagizo ili uasherati ufanywe. Lakini ana wanunuzi maalumu pia.
Malaika anafunua ni akina nani wanunuzi hao wenye upendeleo wa kahaba mkubwa. Anawatambulishaje? Anasema kwamba Babuloni Mkubwa ndiye “wafalme iva dunia walifanya uasherati na yeye, huku wale ambao huikaa dunia walifanywa kulewa divai ya uasherati wake.” (Ufunuo 17:2, NW) Ni lazima iwe huyu ni kahaba mshawishi aliye na njia thabiti za kuweza kuvutia watawala wa kisiasa wa ulimwengu, “wafalme wa dunia” wenyewe! Basi yeye ni nani?
Malaika anasema ana jina, jina la kifumbo, “Babuloni Mkubwa.” Sasa vidokezi viwili ni hivi vya kumtambulisha—kimoja ni wanunuzi anaowapendelea na kile kingine ni jina lake, Babuloni Mkubwa. Vidokezi hivyo vinaongoza kukata shauri gani?
[Maelezo ya Chini]
a Hili ndilo la kwanza la matoleo manne ya Mnara wa Mlinzi yatakayozungumzia maswali hayo na mengine yanayohusu mwanamke Huyu wa kifumbo.