Kahaba Mwenye Sifa Mbaya Sana Uharibifu Wake
“Sifuni Yah, enyi watu! Wokovu na utukufu na nguvu ni za Mungu wetu, kwa sababu hukumu zake ni za kweli na za uadilifu. Kwa maana yeye ametekeleza hukumu juu ya kahaba mkubwa ambaye alifisidi dunia kwa uasherati wake, na yeye amelipiza kisasi cha damu ya watumwa wake katika mkono wake.”—UFUNUO 19:l, 2, NW.
1. Kahaba mkubwa amefanyaje uasherati pamoja na “wafalme wa dunia,” na hiyo imetokeza nini?
YOTE ambayo tumekuwa tukizungumzia ni mazito vya kutosha. Hata hivyo, inatupasa tuangalie kwamba Ufunuo 17:2, NW, unanena juu ya uasherati wa kahaba mkubwa pamoja na “wafalme wa dunia.” Ingawa yeye amepata anguko, angali sana rafiki ya ulimwengu, naye hujaribu kutumia werevu kuwaelekeza watawala walimwengu kama atakavyo ili apate makusudio yake. (Yakobo 4:4) Ukahaba huu wa kiroho, ulio na ngono haramu kati ya Babuloni Mkubwa na watawala wa kisiasa, umetokeza kifo cha mapema cha makumi ya mamilioni ya watu wasio na hatia! Ulikuwa ubaya wa kutosha kwamba kahaba mkubwa alihusika katika pande zote mbili za kupigana katika Vita ya Ulimwengu 1. Lakini kwa uhakika madhambi yake kuhusiana na Vita ya Ulimwengu 2 “yametungamana pamoja moja kwa moja hadi kwenye mbingu”! (Ufunuo 18:5, NW) Kwa nini tunasema hivyo?
2. (a) Franz von Papen alimsaidiaje Adolf Hitler kuwa mtawala wa Ujeremani, na chansela Mjeremani aliyetangulia alielezaje juu ya mheshimiwa huyo wa kipapa? (b) Katika Mapatano kati ya Serikali ya Nazi na Vatikani, ni vifungu gani viwili vya maneno vilivyowekwa kuwa siri? (Ona maelezo ya chini.)
2 Basi, kwa kuchukua kielelezo kimoja, mtawala mkatili Adolf Hitler alikuwaje chansela—na mtawala mtumia mabavu—wa Ujeremani? Ilikuwa ni kupitia mbinu-siasa ya kisiri-siri ya mheshimiwa mmoja wa kipapa ambaye chansela mtangulizi wa Ujeremani, Kurt von Schleicher, alimsimulia kuwa “aina ya haini ambaye Yuda Iskariote akiwa kando yake ni mtakatifu.” Huyu alikuwa Franz von Papen, aliyeiongoza kwa bidii Aksio ya Kikatoliki na viongozi wapinge ukomunisti na kuunganisha Ujeremani chini ya Hitler. Ikiwa ni sehemu ya mapatano ya usaliti, von Papen alifanywa chansela-mdogo. Hitler alipeleka Roma wajumbe wenye kuongozwa na von Papen wakafanye mapatano kati ya Serikali ya Nazi na Vatikani. Papa Pius 11 alieleza wajumbe hao Wajeremani kwamba alifurahishwa sana na jambo la kwamba “sasa Serikali ya Ujeremani ilikuwa na kichwa ambaye ni mwanamume asiyekubali kuuacha msimamo wa kupinga Ukomunisti,” na siku ya Julai 20, 1933, kwenye sherehe yenye madoido mengi katika Vatikani, Kardinali Pacelli (ambaye baada ya muda mfupi angekuwa ndiye Papa Pius wa 12) alitia sahihi mapatano hayo.a
3. (a) Mwanahistoria fulani aliandika nini juu ya Mapatano kati ya Serikali ya Nazi na Vatikani? (b) Wakati wa miadhimisho kule Vatikani, ni heshima gani iliyowekwa juu ya Franz von Papen? (c) Ni fungu gani ambalo Franz von Papen alitimiza katika mpokonyo wa Nazi wa mamlaka ya Austria?
3 Mwanahistoria mmoja anaandika hivi: “Mapatano hayo [pamoja na Vatikani] yalikuwa ushindi mkubwa kwa Hitler. Ulikuwa ndio utegemezo wa kwanza wa kiadili aliokuwa amepokea kutoka ulimwengu wa nje, na isitoshe, kuupata kutokana na chanzo kilichokwezeka zaidi ya vyote.” Wakati wa miadhimisho kule Vatikani, Pacelli alimpa von Papen medali yenye heshima ya juu ya kipapa ya Msalaba Mtukufu wa Daraja la Pius.b Winston Churchill, katika kitabu chake The Gathering Storm, kilichotangazwa kwa chapa katika 1948, anaeleza jinsi von Papen alivyozidi kutumia “sifa yake akiwa Mkatoliki mwema” ili kanisa limuunge mkono kufanya Nazi ipokonye mamlaka ya Austria. Katika 1938, kwa kuheshimu siku ya kuzaliwa kwa Hitler, Kardinali Innitzer aliagiza kwamba makanisa yote ya Kiaustria yapeperushe ile bendera-swastika, yapige kengele zao, na kusali kwa ajili ya mtawala huyo mtumia mabavu wa Kinazi.
4, 5. (a) Kwa nini hatia mbaya sana ya damu inakalia Vatikani? (b) Maaskofu Wakatoliki wa Ujeremani walimuungaje Hitler mkono waziwazi?
4 Kwa hiyo hatia mbaya sana ya damu inakalia Vatikani! Ikiwa sehemu yenye kuongoza ya Babuloni Mkubwa, hiyo ilisaidia sana kumtia Hitler katika mamlaka na kumpa utegemezo “wa kiadili.” Vatikani ilisonga hatua moja zaidi kwa kukubaliana na matendo yake ya unyama kwa unyamavu Wakati wa ule mwongo mrefu wa miaka ya maogofyo ya Kinazi, papa wa Kiroma aliendelea kunyamaza huku mamia ya maelfu ya askari Wakatoliki wakipigana na kufia utukufu wa utawala wa Nazi na huku mamilioni ya maskini wasiojiweza wakimalizwa katika vyumba vyenye gesi vya Hitler.
5 Maaskofu Wakatoliki wa Ujeremani hata walimuunga mkono Hitler waziwazi. Siku ile ile ambapo Japani, mwenzi wa Ujeremani wa wakati wa vita, iliponyemelea na kushambulia Pearl Harbor, The New York Times ilikuwa na ripoti hii: “Mkutano wa Maaskofu Wakatoliki wa Ujeremani waliokusanyika katika Fulda umependekeza ianzishwe ‘sala ya vita’ iliyo maalumu, itakayosomwa mwanzoni na mwishoni mwa ibada zote. Sala hiyo husihi Mungu abariki silaha za Ujeremani kwa ushindi na kutoa himaya kwa maisha na afya ya askari-jeshi wote. Zaidi ya hilo maaskofu hao waliwaagiza makasisi Wakatoliki wawaweke na kuwakumbuka askari-jeshi Wajeremani ‘wa barani, baharini na hewani angalau mara moja kwa mwezi katika mahubiri maalumu ya Jumapili.’”
6. Ulimwengu ungaliweza kuepushwa na maumivu gani yaliyo makali sana na matendo ya unyama kama kusingalikuwa na uasherati wa kiroho kati ya Vatikani na Wanazi?
6 Kama kusingalikuwa na uhusiano wa kimapenzi kati ya Vatikani na Wanazi, huenda ikawa ulimwengu usingalipata yale maumivu makali sana ya kuuawa na vita kwa mamilioni ya askari na raia, kuuawa kwa Wayahudi milioni sita kwa sababu hawakuwa wa asili ya Kiarya, na—jambo lililo la thamani zaidi machoni pa Yehova—kuuawa kwa maelfu ya Mashahidi wake, wapakwa-mafuta na “kondoo wengine” pia, ambao walitendwa matendo ya unyama mkubwa, huku Mashahidi wengi wakifa katika kambi za mateso za Nazi.—Yohana 10:10, 16.
Kumwona Kahaba kwa Ukaribu
7. Mtume Yohana anaelezaje juu ya alivyomwona kahaba mkubwa kwa ukaribu?
7 Inafaa kama nini njozi ile inayofunuka katika Ufunuo baada ya hapo! Tukifungua Ufu sura ya 17, mistari 3 hadi 5, NW, tunapata Yohana akisema hivi juu ya yule malaika: “Na yeye akapeleka mimi mbali kwa nguvu ya roho kuingia jangwani. Na mimi nikaona mwanamke akiwa ameketi juu ya hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu ambaye alikuwa amejaa majina ya kufuru na ambaye alikuwa na vichwa saba na pembe kumi. Na huyo mwanamke alikuwa amepambwa zambarau na nyekundu-nyangavu, na alikuwa amerembwa kwa dhahabu na jiwe la thamani na lulu na katika mkono wake alikuwa na kikombe cha dhahabu ambacho kilikuwa kimejaa vitu vya kunyarafisha na vitu visivyo safi vya uasherati wake. Na juu ya kipaji cha uso wake paliandikwa jina, fumbo: ‘Babuloni Mkubwa, mama ya makahaba na ya vitu vya kunyarafisha vya dunia.’”
8. (a) Kahaba mkubwa anachukua nini katika kikombe chake cha dhahabu, hivyo akijitambulisha yeye mwenyewe? (b) Ni kwa njia gani ya kitamathali Babuloni Mkubwa ‘amepambwa zambarau na nyekundu-nyangavu’ na kurembwa “dhahabu na jiwe la thamani na lulu”?
8 Hapa Yohana anamwona Babuloni Mkubwa kwa ukaribu. Kwa kweli mwanamke huyo anafaa sana kuwa katika jangwa hilo, miongoni mwa hayawani-mwitu wanaokaa humo. Huyu kahaba mkubwa anatambulishwa wazi na kitu kile anachochukua kikiwa kikombeni mwake, ingawa kikombe chenyewe kinadanganya macho kuwa cha thamani kubwa kinapotazamwa njenje. Kwa maoni ya Mungu yeye anakunywa mkorogo ulio wa kunyarafisha. Urafiki wake pamoja na ulimwengu, mafundisho yake bandia, uendekevu wake kuhusu maadili, kufanya-fanya mapenzi ya kiutani pamoja na serikali za kisiasa—hakuna lolote la mambo haya linalovumiliwa na Yehova, “Hakimu wa dunia yote.” (Mwanzo 18:22-26; Ufunuo 18:21, 24, NW) We, yeye ajivika kwa uzuri ulioje! Yeye ana sifa ya kuwa na makanisa makubwa-makubwa ya kuvutia yenye madirisha yaliyoundwa kistadi yakiwa na vioo vilivyotiwa madoa-doa ya kuvutia sana, mapagoda na mahekalu yake ya Kibuddha yaliyopambwa majohari, mahekalu na maabadi yake yenye kuheshimiwa kwa muda mrefu. Kwa kulingana na mitindo ya mavazi ya kistaili ambayo imewekwa na huyo kahaba mkubwa, makuhani na watawa wake wa kiume wamevalia kanzu za bei sana zilizo nyekundu-nyangavu, za kizambarau, na zafarani.—Ufunuo 17:1.
9. Babuloni Mkubwa ana historia gani ndefu ya hatia ya damu, na kwa kufaa Yohana anamaliziaje uelezaji wake kumhusu?
9 Ingawa hivyo, jambo la kulaumika zaidi ni kiu yake ya damu. Kwa sababu hiyo Yehova atafanya naye mhesabiano wa tangu zamani! Yeye amewadhamini watawala watumia-mabavu wenye kiu ya damu nyakati za ki-siku-hizi, na historia yake ya unyarafu wa kutiririsha damu inatandaa kurudi nyuma muda wote wa karne zilizopita, muda wa vile vita vya kidini, yale Mabaraza ya Kuhukumu Wazushi wa Kidini, zile Krusedi, ndiyo, kurudi nyuma kwenye kuuliwa imani kwa baadhi ya mitume na kuchinjwa kwa Mwana wa Mungu mwenyewe, Bwana Yesu Kristo, na mbele zaidi. (Matendo 3:15; Waebrania 11:36, 37) Kwenye hayo yote ongezea yale mauaji ya Mashahidi wa Yehova katika miaka ya majuzi zaidi kwa kikosi cha kupiga bunduki, kunyongwa, kukatwa shoka, kukatwa kichwa kwa mashine ya kukatia vichwa, upanga, na kutendwa unyama katika magereza na kambi za mateso. Si ajabu kwamba Yohana anamalizia uelezaji wake kwa kusema: “Na mimi nikaona kwamba mwanamke alikuwa amelewa damu ya watakatifu na damu ya mashahidi wa Yesu”!—Ufunuo 17:6, NW.
‘FUMBO LA MWANAMKE NA HAYAWANI’
10. (a) Kahaba mkubwa amenyanyasaje Mashahidi wa Yehova mpaka leo hii? (b) Makasisi wa Babuloni Mkubwa ni viongozi wa aina gani?
10 Yohana ‘alistaajabu kwa staajabu kubwa’ kwa kuona alichoona. Leo, sisi pia tunastaajabu! Katika miaka ya 1930 na 1940, yule kahaba mkubwa alitumia Aksio ya Kikatoliki na njama ya kisiasa ili kuwanyanyasa na kuwapiga marufuku mashahidi waaminifu wa Yehova. Mpaka leo hii, mahali ambapo Babuloni Mkubwa anaweza kujizoeza uvutano wa kutosha, yeye anaendelea kuiwekea migogoro, kuiwekea vizuizi, na kuisingizia kazi ya Mashahidi wa Yehova, ambao wanapiga mbiu ya tumaini tukufu la Ufalme wa Mungu. Kwa kuendeleza mamia ya mamilioni wakiwa watekwa katika matengenezo ya kidini ya kahaba mkubwa, makasisi wake wanatumikia wakiwa ‘viongozi vipofu wa vipofu,’ wakiongoza watu hawa kuelekea shimo la uharibifu. Huyu kahaba mwenye sifa mbaya sana hawezi kamwe kamwe kusema hivi pamoja na mtume Paulo: “Mimi nawaita nyinyi mshuhudie . . . kwamba mimi niko safi kutokana na damu ya wanadamu wote.”—Mathayo 15:7-9, 14; 23:13; Matendo 20:26, NW.
11, 12. Ni nini fumbo la “hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu” ambaye anabeba kahaba mwenye sifa mbaya sana, na Mashahidi wa Yehova walipokea nuru gani ya kielimu juu ya fumbo hili katika 1942?
11 Kwa kuona staajabu ya Yohana, malaika alisema kwake hivi: “Kwa nini wewe ulistaajabu? Mimi nitakuambia fumbo la mwanamke na la hayawani-mwitu ambaye anabeba yeye na ambaye ana vichwa saba na pembe kumi.” (Ufunuo 17:7, NW) “Hayawani” huyu ni nini? Zaidi ya miaka 600 mapema zaidi, mnabii Danieli alikuwa ameona hayawani wa kinjozi, na alikuwa ameelezwa kwamba waliwakilisha “wafalme,” au tawala za kisiasa hapa duniani. (Danieli 7:2-8, 17; 8:2-8, 19-22) Hapa Yohana anaona katika njozi muungano wa tawala hizo—“hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu.” Huyu ndiye ule Ushirika wa Mataifa wenye kufanyizwa na wanadamu uliotokea katika mandhari ya ulimwengu katika 1920 lakini ukatumbukizwa ndani ya abiso ya kutotenda wakati Vita ya Ulimwengu 2 ilipofika katika 1939. Ingawa hivyo, ni nini lile “fumbo la mwanamke na la hayawani-mwitu”?
12 Kwa maongozi ya kimungu, Mashahidi wa Yehova walipokea nuru ya kielimu juu ya fumbo hilo katika 1942. Wakati huo Vita ya Ulimwengu 2 ilikuwa ikiwaka moto kufikia upeo, na wengi walifikiri ingeongezeka mpaka iwe Har–Magedoni. Lakini Yehova alikuwa na fikira tofauti! Kulikuwa kungali na kazi nyingi ya kufanywa na Mashahidi wake! Kwenye Ulimwengu Mpya Kusanyiko la Kitheokrasi ambalo walifanya Septemba 18-20, 1942, huku jiji kuu la kusanyiko, Cleveland, Ohio, likiwa limeunganishwa kwa kamba za simu pamoja na sehemu nyingine 51 katika United States, msimamizi wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi, Nathan H. Knorr, aliitoa hotuba ya watu wote, “Amani—Je! Inaweza Kudumu?” Humo yeye aliupitia Ufunuo 17:8, 2VW, unaosema juu ya yule “hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu” kwamba “alikuwako, lakini hayuko, na bado yu karibu kupanda atoke ndani ya abiso, na yeye apaswa kwenda zake ndani ya uharibifu.” Alionyesha jinsi Ushirika wa Mataifa ‘ulivyokuwako’ kuanzia 1920 mpaka 1939. Halafu ile hatua ya “hayuko” ikafikiwa kwa sababu ya kufa kwa Ushirika. Lakini baada ya Vita ya Ulimwengu 2, muungano huu wa mataifa ungepanda utoke ndani ya abiso. Je! utabiri huo wenye msingi wa Biblia ulitimizwa? Kwa kweli ulitimizwa! Katika 1945 “hayawani-mwitu” wa kimataifa aliibuka kutoka kwenye abiso ya kutotenda akiwa Umoja wa Mataifa.
13. Babuloni Mkubwa ameendeleaje kufuatia njia zake za kikahaba pamoja na “hayawani” wa UM?
13 Ingawa alitiwa unyonge na anguko lake, Babuloni Mkubwa ameendelea kufuatia njia zake za kikahaba pamoja na “hayawani” wa UM. Kwa kielelezo, katika Juni 1965, waheshimiwa wa kutoka yale matawi saba makubwa zaidi ya dini ya ulimwengu, yanayoitwa eti ya Kikristo na yasiyo ya Kikristo, yanayosemwa kuwa yanawakilisha nusu moja ya idadi ya watu wa ulimwengu, walikusanyika katika San Francisco kuadhimisha mwaka wa 20 wa siku ya kuzaliwa kwa UM.c Mwaka uo huo, Papa Paul wa 6 aliusimulia UM kuwa ndilo “tumaini la mwisho kwa mapatano na amani,” na baadaye Papa John Paul wa 2 akaeleza tumaini lake kwamba “Umoja wa Mataifa utabaki daima ukiwa ndilo baraza kubwa zaidi la amani na haki.” Katika 1986 milki ya ulimwengu ya dini bandia ilichukua uongozi katika kuudhamini Mwaka wa Amani ya Kimataifa wa UM. Lakini je! amani na usalama wa kweli vilikuja kwa kuitikia sala zao za kidini? Wapi! Mataifa yaliyo washiriki wa UM yanazidi kuonyesha kwamba hayana upendo halisi kwa kahaba mkubwa.
Kumwondolea Mbali Kahaba
14. “Hayawani” wa UM ana utumishi gani maalumu wa kufanya, nao unaelezwaje na malaika wa Mungu?
14 Muda si muda. ni lazima yule “hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu” mwenyewe aende zake ndani ya uharibifu. Lakini kabla haijawa hivyo, na hata kabla ya shambulio lake la kihayawani juu ya watu wa Mungu, hayawani huyo aliye UM ana utumishi maalumu wa kufanya. Yehova anatia ‘fikira yake ndani ya mioyo ya huyo hayawani-mwitu na pembe zake za kijeshi.’ Tokeo likiwa nini? Malaika wa Mungu anajibu: “Na pembe kumi ambazo wewe uliona, na hayawani-mwitu, hizi zitachukia kahaba na zitafanya yeye kuwa mwenye kuteketezwa na mwenye uchi, na zitakula kabisa sehemu zake zenye mnofu na zitachoma yeye kabisa kabisa kwa moto.” “Yeye alijitukuza mwenyewe na akaishi katika anasa ya kutoona aibu,” lakini sasa yote haya yamekuwa kinyume. Majengo yake yenye uvutio wa kujionyesha na mali zake nyingi za mashamba makubwa sana hayatamwokoa. Kama vile malaika anavyojulisha wazi: “Hiyo ndiyo sababu katika siku moja tauni zake zitakuja, kifo na ombolezo na njaa kuu, na yeye atachomwa kabisa kwa moto, kwa sababu Yehova Mungu, ambaye alihukumu yeye, ni imara sana.” —Ufunuo 17:16, 17; 18:7, 8.
15. Hawara za kisiasa za kahaba, pamoja na wakwasi wa biashara kubwa-kubwa, watatendaje kuhusu kifo chake?
15 Hawara zake za kisiasa wataomboleza kifo chake, wakijulisha wazi hivi: “Ni vibaya mno, ni vibaya mno, wewe jiji kubwa, Babuloni wewe jiji imara, kwa sababu katika saa moja hukumu yako imewasili!” Vilevile, wakwasi wa biashara kubwa-kubwa, waliopata faida pamoja naye kwa kutofuata haki, “watatoa machozi na kuomboleza, kusema, ‘Ni vibaya mno, ni vibaya mno . . . kwa sababu katika saa moja utajiri mwingi hivyo umeteketezwa!’ “—Ufunuo 18:9-17, NW.
16. Ni itikio gani ambalo watu wa Mungu watafanya kuhusu uharibifu wa kahaba mkubwa, na Ufunuo unahakikishaje hilo?
16 Hata hivyo, ni itikio gani ambalo watu wa Mungu mwenyewe watatoa? Wote hawa wanahusishwa ndani ya yale maneno ya malaika: “Uwe na nderemo juu yake, 0 mbingu, pia nyinyi watakatifu na nyinyi mitume na nyinyi wanabii, kwa sababu kwa kuhukumu Mungu ametoza adhabu kutoka kwake yeye kwa ajili yenu nyinyi!” Babuloni Mkubwa atakuwa amevurumishwa chini kwa mrusho wa kasi, asipate tena kusuta jina takatifu la Yehova. Uharibifu wa kahaba mkubwa utahitaji kuwe na mwadhimisho na nyimbo za ushindi kwa kumsifu Yehova. Kikiwa ndicho cha kwanza cha ule mfululizo wa korasi za haleluyah, kile kibwagizo chenye shangwe kitatokezwa kwa mvumo: “Sifuni Yah, nyinyi watu! Wokovu na utukufu na nguvu ni za Mungu wetu, kwa sababu hukumu zake ni za kweli na za uadilifu. Kwa maana yeye ametekeleza hukumu juu ya kahaba mkubwa ambaye alifisidi dunia kwa uasherati wake, na yeye amelipiza kisasi cha damu ya watumwa wake katika mkono wake.” —Ufunuo 18:20–19:3, NW.
17. Baada ya kuondolewa mbali kwa kahaba mkubwa, vitendo vya hukumu ya Mungu vitaendeleaje mpaka vikakamilike?
17 Vitendo vya hukumu ya Mungu vitapita kasi vikamalizike huku “Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana” akivyoga-vyoga “shinikizo la divai ya kasirani ya hasira-kisasi ya Mungu Mweza Yote” kwenye Har–Magedoni. Kule yeye atawaondolea mbali watawala waovu na wabakiaji wengine wote wa tengenezo la Shetani duniani. Ndege wala nyamafu watanyafua mizoga yao. (Ufunuo 16:14, 16; 19:11-21) Inatupasa kuwa wenye furaha kama nini kwamba wakati wa Mungu uliowekwa u karibu wa kukiondoa katika dunia yetu nzuri kila kitu kisicho na utakatifu, chenye kinyaa, na chenye kufisidi!
18. Ni nini upeo mtukufu wa kitabu cha Ufunuo?
18 Je! huo ndio upeo wa kitabu cha Ufunuo? Sivyo, mambo bado! Kwa maana ukiisha kukamilishwa ufufuo wa kuwapeleka mbinguni wale 144,000, ndoa ya Mwana-Kondoo inatukia. “Bibi-arusi” wake, aliyepambwa kwa ajili ya mumeye, anatawazwa katika “mbingu mpya,” na kwa usemi wa kitamathali yeye anashuka kutoka huko, akiwa mwenzi-msaidizi wa Bwana-arusi katika kutekeleza kusudi la Yehova ‘kufanya vitu vyote kuwa vipya.’ Uzuri ya kiroho wa bibi-arusi ni ule wa jiji takatifu, Yerusalemu Jipya, ambalo Yehova Mungu Mweza Yote ananurisha kwa utukufu wake, na Mwana-Kondoo ndiye taa yalo. (Ufunuo 21:1-5, 9-11, 23) Kwa hiyo hapa Ufunuo unafikia upeo wao mtukufu huku jina la Yehova likitakaswa, na Mwana-Kondoo, Yesu Kristo, pamoja na bibi-arusi wake, Yerusalemu Jipya, akianza kubariki aina ya binadamu watiifu kwa uhai wa milele katika Paradiso ya kidunia.
19. Zaidi ya kutoka ndani ya Babuloni Mkubwa, ni nini kingine kinachohitajiwa sana kwa wokovu? (b) Ni mwaliko gani wa haraka ambao ungali wazi, na itikio letu linapasa kuwa nini?
19 Je! Wewe umeamka ukauona udanganyifu wa dini bandia na ukatoka ndani ya Babuloni Mkubwa? Na je! Wewe umechukua ile hatua zaidi ya kuja kwa Yehova Mungu, kupitia Kristo Yesu, katika wakfu wa moyo mzima unaoongoza kwenye ubatizo? Hilo linahitajiwa sana pia ili kupata wokovu! Kwa kadiri ambavyo wakati uliowekwa ili Yehova afikilize hukumu ya mwisho unakaribia, mwaliko huu unavumisha mwangwi kwa uharaka wenye kusukuma: “Roho na bibi-arusi hufuliza kusema: ‘Njoo!’” Wote wale wanaotii wito huo na waweke maisha zao wakfu kwa Yehova na wawe wenye bidii katika kusema “Njoo!” kwa wengine bado. Ndiyo, “acheni mmoja yeyote anayeona kiu aje; acheni mmoja yeyote ambaye anataka atwae maji ya uhai bure.” (Ufunuo 22:17, NW) Mwaliko ungali wazi. Wewe utafurahi kweli kweli ukichukua msimamo wako na kudumisha msimamo huo mbele ya kiti cha ufalme cha Mungu na Mwana-Kondoo ukiwa mmoja wa watu wa Yehova waliojiweka wakfu na kubatizwa. Wakati uliowekwa u karibu kuliko vile huenda ukafikiri! Ndiyo, upeo mtukufu wa Ufunuo u karibu!. Kama umalizio wa Funzo la Mnara wa Mlinzi la juma hili, kiongozi anapaswa kuomba Azimio linalofuata lisomwe na kupitiwa kwa msaada wa maswali yaliyoandaliwa. Hili ndilo Azimio lililotokezwa ulimwenguni pote kwenye “Haki ya Kimungu” Mkusanyiko wa Wilaya wa Mashahidi wa Yehova katika 1988 wakati wa kumalizika kwa hotuba “‘Kahaba’ Mwenye Sifa Mbaya Sana—Anguko na Uharibifu Wake.”
[Maelezo ya Chini]
a Kwa sababu zilizo wazi, vifungu viwili vya Mapatano hayo viliwekwa vikiwa siri wakati huo, vikihusu lengo moja la ujumla dhidi ya Urusi na kuhusu kazi za mapadri Wakatoliki waliolazimishwa kuingia katika jeshi la Hitler. Lazimisho hilo lilivunja masharti ya Mkataba wa Versailles (1919) ambao Ujeremani ilikuwa ingali na wajibu wa kuufuata; kama halaiki ya watu ingalijua mambo ya kifungu hiki, hiyo ingaliudhi pande zile nyingine zilizohusika katika kuutia sahihi mkataba huo wa Versailles.
b Franz von Papen alikuwa miongoni mwa Wanazi waliojaribiwa kama wahalifu wa vita kule Nuremberg, Ujeremani, katika miaka ya mwishoni mwa 1940. Yeye aliwekwa huru na hatia lakini baadaye akapata hukumu kali kutoka mahakama moja ya Ujeremani yenye kushughulikia mabaya yaliyotendwa na chama cha Nazi. Na bado baadaye, katika 1959, alifanywa Chambaleni wa Baraza la Faragha la Papa.
c Akitoa maelezo juu ya kusanyiko hili, Papa Paul wa 6 alisema: “Ni sawasawa na inafaa kweli kweli kwamba kusanyiko la kidini kwa ajili ya amani limetiwa miongoni mwa sherehe za kukumbuka kutiwa sahihi kwa Mkataba wa Umoja wa Mataifa miaka ishirini iliyopita.”
[Sanduku katika ukurasa wa 11]
KIMYA CHA PAPA
Katika kitabu chake Franz von Papen—His Life and Times, kilichotangazwa kwa chapa katika 1939, H. W. Blood-Ryan anaeleza kirefu mbinu za hila alizotumia mheshimiwa huyo wa kipapa ili kumleta Hitler mamlakani na kufanya ushauriano juu ya mapatano ya Vatikani pamoja na Wanazi. Kuhusu mauaji mabaya sana yaliyopangwa kimakusudi, yaliyohusisha ndani Wayahudi, Mashahidi wa Yehova, na wengine, mtungaji anataarifu hivi: “Mbona Pacelli [Papa Pius wa 12] alikaa kimya? Ni kwa sababu yeye aliona kwamba mpango wa von Papen wa kuwako kwa Milki Takatifu ya Kiroma ya Wajeremani wa Magharibi kungefanya Kanisa Katoliki liwe imara zaidi, huku Vatikani ikiwa imerudia kukalia kiti cha mamlaka ya kidunia . . . Pacelli uyo huyo sasa anatumia mamlaka ya kiroho ya kutawala kimabavu juu ya mamilioni ya nafsi, na bado hata mnong’ono mdogo haukutokezwa kupinga uchokozi na unyanyasi wa Hitler. . . . Ninapoandika mistari hii, siku tatu za machinjo zimepita na hakuna hata sala moja imetoka Vatikani kuombea nafsi za washindani hao, nusu yao hasa wakiwa ni Wakatoliki. Wanaume hawa watatozwa hesabu mbaya sana wakati watakaposimama mbele ya Mungu wao wakiwa wamevuliwa vyeo vyao vyote vya umashuhuri wa kidunia, Naye atawaomba watoe hesabu. Udhuru wao unaweza kuwa nini? Hakuna!”
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
MHUSIKO WA VATIKANI
The New York Times ya Machi 6, 1988, iliripoti kwamba Vatikani ilitarajia upungufu usiopata kuwako tena katika mipango ya matumizi, wa dola milioni 61.8 kwa 1988. Nyusipepa hiyo ilitaarifu hivi: “Gharama moja kubwa inadhaniwa kuwa inahusisha ndani ahadi iliyofanywa katika 1984 kuwalipa dola karibu milioni 250 wakopeshaji wa Banco Ambrosiano. Vatikani ilihusika kwa kina kirefu na benki ya Milani kabla ya anguko layo katika 1982.” Ilihusika kwa kina kirefu kweli kweli katika kashifa hiyo hivi kwamba Vatikani imekataa kabisa kuwatoa maofisa watatu wa cheo cha juu katika Vatikani, kutia na askofu mkuu Mwamerika, wawe mikononi mwa wenye mamlaka ili kujaribiwa katika mahakama za Kiitalia!
[Picha katika ukurasa wa 12]
Vatikani inashiriki hatia mbaya sana ya damu pamoja na von Papen na Hitler
[Hisani]
UPI/Bettmann Newsphotos
UPI/Bettmann Newsphotos
[Picha katika ukurasa wa 15]
Badala ya kutetea Ufalme wa Mungu, mapapa wamepiga mbiu kwamba UM ndilo ‘tumaini la mwisho la amani’
[Hisani]
Insets: UN photos