Sura ya 35
Kufisha Babuloni Mkubwa
1. Malaika anaelezaje habari ya hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu, na ni hekima ya aina gani inayohitajiwa kuelewa mifananisho ya Ufunuo?
KATIKA kueleza zaidi habari ya hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu wa Ufunuo 17:3, malaika anamwambia Yohana: “Hapa ndipo elimu iliyo na hekima inapofaa: Vichwa saba humaanisha milima saba, ambako mwanamke huketi juu ya kilele. Na wako wafalme saba: watano wameanguka, mmoja yupo, mwingine hajawasili bado, lakini yeye awasilipo lazima yeye abaki kitambo kifupi.” (Ufunuo 17:9, 10, NW) Malaika anawasilisha hekima kutoka juu, hekima pekee inayoweza kutoa uelewevu wa mifananisho katika Ufunuo. (Yakobo 3:17) Hekima hii inaipa jamii ya Yohana na waandamani wayo nuru juu ya hatari ya nyakati tunamoishi. Inajenga katika mioyo yenye kujitoa uthamini wa hukumu za Yehova, ambazo sasa karibu kutimizwa, na inakaza kikiki hofu yenye afya kuelekea Yehova. Kama Mithali 9:10, NW inavyotaarifu: “Hofu ya Yehova ndio mwanzo wa hekima, na maarifa ya kumjua Mmoja Aliye Mtakatifu Zaidi Sana ndio uelewevu.” Hekima ya kimungu inatufunulia nini juu ya hayawani-mwitu?
2. Ni nini maana ya vichwa saba vya hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu, na inakuwaje kwamba “watano wameanguka, mmoja yupo”?
2 Vichwa saba vya hayawani-mwitu mkali sana husimamia “milima” saba, au “wafalme” saba. Semi zote mbili hutumiwa Kimaandiko kurejezea mamlaka za kiserikali. (Yeremia 51:24, 25; Danieli 2:34, 35, 44, 45) Katika Biblia, serikali za ulimwengu sita hutajwa kuwa zikiathiri mambo ya watu wa Mungu: Misri, Ashuru, Babuloni, Umedi-Uajemi, Ugiriki, na Roma. Kati ya hizi, tano zilikuwa tayari zimekuja na zikaenda kufikia wakati Yohana alipopokea Ufunuo, lakini Roma ilikuwa ingali sana serikali ya ulimwengu. Hii inalingana vizuri na maneno haya, “watano wameanguka, mmoja yupo.” Lakini namna gani juu ya “mwingine” aliyekuwa akitazamiwa kuja?
3. (a) Milki ya Roma ilikujaje kugawanywa? (b) Ni matukio gani yaliyotukia katika Magharibi? (c) Milki Takatifu ya Roma yapasa ionweje?
3 Milki ya Roma ilidumu na hata ikapanuka kwa mamia ya miaka baada ya siku ya Yohana. Katika 330 W.K. Maliki Konstantino alihamisha jiji kuu lake kutoka Roma kwenda Bizanshamu, ambalo alilipa jina Konstantinopo. Katika 395 W.K., Milki ya Roma iligawanywa ikawa sehemu za Mashariki na Magharibi. Katika 410 W.K., Roma liliangushwa na Alariki, mfalme wa Wavisigothi (kabila la Kijeremani ambalo lilikuwa limeongolewa kuwa la “Ukristo” wa aina ya Aria). Makabila ya Kijeremani (ya “Kikristo” pia) yalishinda Hispania na eneo lililo kubwa zaidi la Roma katika Afrika Kaskazini. Zilikuwako karne za misukosuko, kutotulia, na kujirekebisha upya katika Ulaya. Wamaliki wenye sifa waliinuka katika Magharibi, kama vile Charlemagne, ambaye alifanya fungamano na Papa Leo 3 katika karne ya 9, na Frederick 2, ambaye alitawala katika karne ya 13. Lakini milki yao, ingawa iliitwa Milki Takatifu ya Roma ilikuwa ndogo zaidi ya ile Milki ya Roma ya mapema zaidi, wakati wa kilele cha usitawi wayo. Ilikuwa zaidi mrudisho au mwendelezo wa hiyo serikali ya kale kuliko kuwa milki mpya.
4. Milki ya Mashariki ilikuwa na mafanikio gani, lakini kulitukia nini kwa sehemu kubwa ya lililokuwa eneo la Roma ya kale katika Afrika Kaskazini, Hispania, na Siria?
4 Milki ya Mashariki ya Roma, yenye kitovu katika Konstantinopo, iliendelea ikiwa na uhusiano wenye wasiwasi na Milki ya Magharibi. Katika karne ya sita, maliki wa Mashariki Justiniani 1 aliweza kushinda sehemu kubwa ya Afrika ya Kaskazini, na pia akaingilia Hispania na Italia. Katika karne ya saba, Justiniani 2 alikombolea Milki hiyo maeneo ya Makedonia ambayo yalikuwa yameshindwa na wanamakabila wa Kislavi. Hata hivyo, Kufikia karne ya nane eneo kubwa la zamani la Roma ya kale katika Afrika Kaskazini, Hispania, na Siria lilikuwa limekuja chini ya milki mpya ya Islamu na hivyo likapita kutoka udhibiti wa Konstantinopo na Roma pia.
5. Ingawa jiji la Roma lilianguka 410 W.K., ilikuwaje kwamba ilichukua karne nyingi zaidi kabla ya visehemu vyote vya Milki ya Roma ya kisiasa kutoweka katika mandhari ya ulimwengu?
5 Jiji la Konstanipo lenyewe lilidumu kwa muda mrefu zaidi kidogo. Liliokoka mashambulizi ya mara nyingi kutoka kwa Waajemi, Waarabu, Wabulgari, na Warusi mpaka mwishowe katika 1203 likaangushwa—si na Waislamu bali na Wakrusedi kutoka Magharibi. Ingawa hivyo, katika 1453, lilikuja chini ya mamlaka ya mtawala Mwislamu wa Ottomani Mehmedi 2 na upesi likawa jiji kuu la Milki ya Ottomani, au ya Kituruki. Hivyo, ijapokuwa jiji la Roma lilianguka katika 410 W.K., ilichukua karne nyingi zaidi kabla ya visehemu vyote vya Milki ya Roma ya kisiasa kutoweka katika mandhari ya ulimwengu. Na hata hivyo, uvutano wayo bado ulitambulikana katika milki za kidini zenye msingi wa upapa wa Roma na makanisa ya Orthodoksi ya Mashariki.
6. Ni milki zipi mpya kabisa zilizotokea, na ni ipi iliyopata kuwa yenye kufanikiwa zaidi sana?
6 Hata hivyo, kufikia karne ya 15, nchi fulani zilikuwa zikijenga milki mpya kabisa. Ingawa baadhi ya serikali hizi mpya za kibepari zilipatikana katika maeneo ambayo hapo kwanza yalikuwa makoloni ya Roma, milki zazo hazikuwa mwendelezo vivi hivi wa Milki ya Roma. Ureno, Hispania, Ufaransa, na Uholanzi zote zikawa makao ya milki zilizotapakaa sana. Lakini iliyofanikiwa zaidi sana ilikuwa Uingereza, ambayo ikaja kusimamia milki kubwa mno ambayo juu yayo ‘jua halikutua kamwe.’ Milki hii ilienea katika nyakati mbalimbali juu ya sehemu kubwa ya Amerika Kaskazini, Afrika, India, na Esia Kusini-mashariki, pamoja na maeneo ya Pasifiki Kusini.
7. Serikali ya ulimwengu ya uwili ilikujaje kuwako, na Yohana alisema ni kwa muda gani ‘kichwa’ au serikali ya ulimwengu ya saba ingeendelea?
7 Kufikia karne ya 19, baadhi ya makoloni katika Amerika Kaskazini yalikuwa yamekwisha kujitenga na Uingereza yakaunda United States ya Amerika yenye kujitawala. Kisiasa, hitilafu fulani ziliendelea kati ya taifa jipya na iliyokuwa nchi-mama yao. Hata hivyo, vita ya ulimwengu ya kwanza ilizilazimisha hizo nchi zote mbili kutambua masilahi yazo ya pamoja na zikatia nguvu uhusiano maalumu kati yazo. Hivyo, namna ya serikali ya ulimwengu ya uwili ikatokea, ikiwa inafanyizwa na United States ya Amerika, sasa ikiwa ndilo taifa la ulimwengu lenye ukwasi zaidi sana, na Uingereza, kao la milki ya ulimwengu iliyo kubwa zaidi sana. Basi, hiki, ndicho ‘kichwa’ cha saba, au serikali kubwa ya ulimwengu, ambayo inaendelea mpaka ndani ya wakati wa mwisho na katika maeneo ambamo Mashahidi wa ki-siku-hizi wa Yehova walijiimarisha kwanza. Kikilinganishwa na utawala mrefu wa kichwa cha sita, hiki cha saba ‘chabaki kitambo kifupi’ mpaka Ufalme wa Mungu uangamizapo mataifa yote.
Kwa Nini Huitwa Mfalme wa Nane?
8, 9. Malaika anamwitaje hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu na ni katika njia gani huchipuka kutoka kwa wafalme saba?
8 Malaika anamweleza Yohana zaidi hivi: “Na hayawani-mwitu ambaye alikuwako lakini hayuko, yeye pia mwenyewe ni mfalme wa nane, lakini huchipuka kutoka kwa wale saba, na yeye huenda zake ndani ya uharibifu.” (Ufunuo 17:11, NW) Hayawani-mwitu wa ufananisho rangi-nyekundu-nyangavu “huchipuka kutoka” kwa vichwa saba; yaani, yeye anazaliwa na, au yuko kwa sababu ya vichwa hivyo vya ‘hayawani-mwitu kutoka bahari,’ ambaye hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu ni mfano wake. Kwa njia gani? Basi, katika 1919 serikali ya Uingereza-Amerika ilikuwa ndiyo kichwa chenye kutawala. Vile vichwa sita vilivyotangulia vilikuwa vimeanguka, nacho cheo cha serikali kubwa ya ulimwengu yenye kutawala kilikuwa kimepitishwa kwenye kichwa hiki cha uwili na sasa kikawa katika kitovu chacho. Hiki kichwa cha saba, kikiwa ndicho mwakilishi wa sasa wa mstari wa serikali za ulimwengu, kilikuwa ndicho kani yenye kutenda katika kusimamisha Ushirika wa Mataifa na kingali ndicho mwendelezaji na mtegemezaji kifedha mkuu wa Umoja wa Mataifa. Hivyo, kwa njia ya ufananisho hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu—mfalme wa nane—“huchipuka kutoka” kwa vile vichwa saba vya kwanza. Ikionwa katika njia hii, taarifa ya kwamba yeye alichipuka kutoka kwa vichwa saba inapatana vizuri na ufunuo wa mapema zaidi kwamba hayawani-mwitu mwenye pembe mbili mithili ya mwana-kondoo (Serikali ya Ulimwengu Uingereza-Amerika, kichwa cha saba cha hayawani-mwitu wa kwanza) alihimiza kufanyizwa kwa huo mfano na akaupa uhai.—Ufunuo 13:1, 11, 14, 15.
9 Kwa kuongezea, washiriki wa kwanza kabisa wa Ushirika wa Mataifa walikuwamo, pamoja na Uingereza, serikali ambazo zilitawala katika makao ya baadhi ya vichwa vilivyotangulia, yaani, Ugiriki, Irani (Uajemi), na Italia (Roma). Hatimaye, serikali zenye kutawala maeneo yaliyodhibitiwa na serikali za ulimwengu sita zilizotangulia zikaja kuwa washiriki waungaji mkono wa mfano wa hayawani-mwitu. Katika maana hii, vilevile, ingeweza kusemwa kwamba huyu hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu alichipuka kutoka kwa serikali za ulimwengu saba.
10. (a) Inaweza kusemwaje kwamba hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu “yeye pia mwenyewe ni mfalme wa nane”? (b) Kiongozi mmoja wa nchi zilizokuwa Muungano wa Sovieti alionyeshaje uungaji-mkono wake wa Umoja wa Mataifa?
10 Angalia kwamba hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu “yeye pia mwenyewe ni mfalme wa nane.” Hivyo, Umoja wa Mataifa leo unakusudiwa uonekane kuwa serikali ya ulimwengu. Nyakati fulani hata umetenda hivyo, ukituma majeshi uwanjani kusuluhisha magomvi ya kimataifa, kama vile katika Korea, Peninsula ya Sinai, nchi fulani za Kiafrika, na Lebanoni. Lakini huo ni mfano tu wa mfalme. Kama vile mfano wa kidini, huo hauna uvutano au uwezo halisi isipokuwa ule ambao unapewa na wale ambao waliutokeza na wanaouabudu. Katika pindi fulani, hayawani-mwitu huyu wa ufananisho huonekana dhaifu; lakini hajapatwa kamwe na aina ya kuachwa kwa wingi na washiriki wenye maelekeo ya udikteta ambao walifanya Ushirika wa Mataifa utetereke na kutumbukia ndani ya abiso. (Ufunuo 17:8) Ingawa anashikilia maoni yanayotofautiana sana katika maeneo mengine, kiongozi mmoja mashuhuri wa nchi zilizokuwa Muungano wa Sovieti katika 1987 alijiunga na mapapa wa Roma katika kuonyesha uungaji-mkono wa UM. Yeye hata alitaka kuwe na “mfumo mpana wa usalama wa kimataifa” wenye kutegemea UM. Kama Yohana ajifunzavyo upesi, wakati utakuja ambapo UM utatenda kwa mamlaka kubwa. Kisha huo, katika zamu yao, “huenda zake ndani ya uharibifu.”
Wafalme Kumi kwa Saa Moja
11. Malaika wa Yehova anasema nini juu ya pembe kumi zilizo juu ya hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu wa ufananisho?
11 Katika sura ya Ufunuo iliyotangulia, malaika, wa sita na wa saba walimimina mabakuli ya kasirani ya Mungu. Hivyo sisi tuliarifiwa kwamba wafalme wa dunia wanakusanywa kwenye vita ya Mungu kwenye Har–Magedoni na kwamba ‘Babuloni Mkubwa apaswa kukumbukwa katika mwono wa Mungu.’ (Ufunuo 16:1, 14, 19, NW) Sasa tutajifunza kirefu zaidi jinsi hukumu za Mungu juu ya hawa zitatekelezwa. Sikiliza tena malaika wa Yehova anaponena kwa Yohana. “Na pembe kumi ambazo wewe uliona humaanisha wafalme kumi, ambao bado kupokea ufalme, lakini wao hupokea mamlaka wakiwa wafalme saa moja pamoja na hayawani-mwitu. Hawa wana fikira moja, na hivyo wao humpa hayawani-mwitu nguvu na mamlaka yao. Hawa watapigana na Mwana-Kondoo, lakini, kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme, Mwana-Kondoo atashinda wao. Pia, wale wenye kuitwa na wachaguliwa na waaminifu pamoja na yeye watafanya hivyo.”—Ufunuo 17:12-14, NW.
12. (a) Pembe kumi ni picha ya nini? (b) Ni jinsi gani pembe kumi za ufananisho ‘hazikuwa zimepokea ufalme’? (c) Pembe kumi za ufananisho zinakuwaje na “ufalme” sasa, na ni kwa muda gani?
12 Pembe kumi ni picha ya serikali zote za kisiasa ambazo zinatawala sasa katika mandhari ya ulimwengu na ambazo huunga mkono hayawani-mwitu. Ni nchi chache sana zilizoko sasa ambazo zilijulikana katika siku ya Yohana. Na zile zilizojulikana, kama Misri na Uajemi (Irani), leo zina muundo wa kisiasa ulio tofauti kabisa. Kwa sababu hiyo, katika karne ya kwanza, ‘pembe kumi hazikuwa zimepokea ufalme.’ Lakini sasa katika siku ya Bwana, zina “ufalme,” au mamlaka ya kisiasa. Milki kubwa-kubwa za kikoloni zilipoanguka, hasa tangu vita ya ulimwengu ya pili, mataifa mengi mapya yamezaliwa. Hizi, pamoja na serikali ambazo zimeimarika muda mrefu, lazima zitawale pamoja na hayawani-mwitu kwa kipindi kifupi—“saa moja” tu—kabla Yehova hajakomesha mamlaka zote za kisiasa za ulimwengu kwenye Har–Magedoni.
13. Ni katika njia gani pembe kumi zina “fikira moja,” na hiyo huhakikisha mwelekeo gani kwa Mwana-Kondoo?
13 Leo, utukuzo wa taifa ndio mojapo kani zenye nguvu zaidi sana zinazosukuma pembe kumi hizi. Zina “fikira moja” kwa kuwa hizo zinataka kuhifadhi enzi zao za kitaifa badala ya kukubali Ufalme wa Mungu. Hilo ndilo lilikuwa kusudi lao katika kuchangia Ushirika wa Mataifa na tengenezo la Umoja wa Mataifa katika ile mara ya kwanza—kuhifadhi amani ya ulimwengu na hivyo kulinda salama kuwako kwazo. Mwelekeo kama huo unahakikisha kwamba pembe kumi zitapinga Mwana-Kondoo, “Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme,” kwa sababu Yehova amekusudia kwamba Ufalme wake chini ya Yesu Kristo hivi karibuni utachukua mahali pa falme hizi.—Danieli 7:13, 14; Mathayo 24:30; 25:31-33, 46.
14. Inawezekanaje kwa watawala wa ulimwengu kupigana na Mwana-Kondoo, na tokeo litakuwa nini?
14 Bila shaka, watawala wa ulimwengu huu hawawezi kufanya kitu chochote dhidi ya Yesu mwenyewe. Yeye yumo mbinguni, mbali sana wasimoweza kumfikia. Lakini ndugu za Yesu, wabakio wa mbegu ya mwanamke, wangali duniani na inaonekana wazi wanaumizika. (Ufunuo 12:17) Nyingi za pembe zimekwisha onyesha uhasama mkali kuwaelekea, na katika njia hii zimepigana na Mwana-Kondoo. (Mathayo 25:40, 45) Ingawa hivyo, karibuni, wakati utakuja wa Ufalme wa Mungu ‘kuponda-ponda na kuweka mwisho kwenye falme hizi zote.’ (Danieli 2:44, NW) Ndipo, wafalme wa dunia watakuwa katika pigano hadi tamati pamoja na Mwana-Kondoo, kama tutakavyoona karibuni. (Ufunuo 19:11-21) Lakini hapa tunajifunza mambo ya kutosha kung’amua kwamba mataifa hayatafanikiwa. Ingawa hayo pamoja na hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu wa UM wana “fikira moja” yao, wao hawawezi kumshinda “Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme” aliye mkubwa, wala hawawezi kushinda “wale wenye kuitwa na wachaguliwa na waaminifu pamoja na yeye,” kutia ndani wafuasi wapakwa-mafuta wake ambao wangali duniani. Hawa pia watakuwa wamekwisha shinda kwa kushika ukamilifu katika kujibu mashtaka maovu ya Shetani.—Warumi 8:37-39; Ufunuo 12:10, 11.
Kuteketeza Kahaba
15. Malaika anasema nini juu ya kahaba na mwelekeo na tendo la pembe kumi na hayawani-mwitu kuelekea yeye?
15 Watu wa Mungu sio peke yao wanaochukiwa na pembe kumi. Malaika sasa anavuta uangalifu wa Yohana kwenye kahaba: “Na yeye anasema kwangu mimi: ‘Maji ambayo wewe uliona, ambapo kahaba anaketi, humaanisha vikundi vya watu na umati wa watu na mataifa na ndimi. Na pembe kumi ambazo wewe uliona, na hayawani-mwitu, hizi zitachukia kahaba na zitafanya yeye kuwa mwenye kuteketezwa na mwenye uchi, na zitakula kabisa sehemu zake zenye mnofu na zitachoma yeye kabisa kabisa kwa moto.’”—Ufunuo 17:15, 16, NW.
16. Ni kwa nini Babuloni Mkubwa hataweza kutegemea maji yake yamuunge mkono wa himaya wakati serikali za kisiasa zinapomgeukia?
16 Kama vile Babuloni wa kale alivyotegemea ulinzi wa maji yake, Babuloni Mkubwa leo anategemea washiriki wake wengi mno “vikundi vya watu na umati wa watu na mataifa na ndimi.” Kwa kufaa malaika huelekeza uangalifu wetu kwenye hao kabla ya kusimulia tukio lenye kugutusha: Serikali za kisiasa za dunia hii zitamgeukia kijeuri Babuloni Mkubwa. “Vikundi vya watu na umati wa watu na mataifa na ndimi” wote hao watafanya nini wakati huo? Tayari watu wa Mungu wanaonya Babuloni Mkubwa kwamba maji ya mto Eufrati yatakauka. (Ufunuo 16:12) Mwishowe maji hayo yatakauka kabisa. Hayo hayataweza kumpa kahaba kizee mwenye kunyarafisha tegemezo lolote lenye kufaa katika saa yake ya uhitaji ulio mkubwa zaidi sana.—Isaya 44:27; Yeremia 50:38; 51:36, 37.
17. (a) Ni kwa sababu gani ukwasi wa Babuloni Mkubwa hautamwokoa? (b) Mwisho wa Babuloni Mkubwa utakuwaje wenye aibu kabisa? (c) Mbali na pembe kumi, au mataifa moja moja, ni nini kingine kinachojiunga katika jeuri dhidi ya Babuloni Mkubwa?
17 Kwa hakika, ukwasi mkubwa mno wa vitu vya kimwili hautaweza kumwokoa Babuloni Mkubwa. Huenda hata ukaharakisha kuharibiwa kwake, kwa kuwa njozi huonyesha kwamba wakati hayawani-mwitu na pembe kumi wanapomwonyesha chuki yao watamvua majoho yake ya kifalme na vito vyake vyote vya thamani. Wao watapora ukwasi wake. ‘Wanamfanya kuwa uchi,’ wakifichua kiaibu tabia yake halisi. Mteketezo wee! Pia mwisho wake ni wenye aibu kabisa. Wanamharibu, na ‘kula sehemu zake zenye mnofu,’ wakimwacha mifupa mitupu isiyo na uhai. Mwishowe, wao ‘humchoma kabisa kabisa kwa moto.’ Yeye huchomwa kabisa kama mwenye ugonjwa wa tauni, bila hata maziko ya heshima! Si mataifa yale tu, kama yanavyowakilishwa na pembe kumi, yanayomharibu kahaba mkubwa, bali pia “hayawani-mwitu,” kumaanisha UM wenyewe, hujiunga nayo katika kuonyesha jeuri hii. Utatoa idhini yao ili dini bandia iharibiwe. Yaliyo mengi ya yale mataifa 190 na zaidi yaliyo ndani ya UM yameonyesha tayari, kwa kiolezo chayo cha kupiga kura, uhasama wayo kuelekea dini, hasa ile ya Jumuiya ya Wakristo.
18. (a) Ni uwezekano gani wa mataifa kugeukia dini za Kibabuloni ambao tayari umeonekana? (b) Ni nini itakayokuwa sababu ya msingi ya shambulio la ujumla juu ya kahaba mkubwa?
18 Ni kwa nini hayo yangemtenda kijeuri hivyo hawara wao wa zamani? Sisi tumeona katika historia ya hivi majuzi uwezekano kama huo wa kugeukia dini ya Kibabuloni. Upinzani rasmi wa kiserikali umepunguza sana uvutano wa dini katika nchi kama vile China na nchi zilizokuwa Muungano wa Sovieti. Katika maeneo ya Kiprotestanti ya Ulaya, ubaridi wenye kuenea pote na mashaka vimeyaacha makanisa yakiwa tupu, hivi kwamba karibu dini imekufa. Milki kubwa mno ya Kikatoliki imegawanywa na uasi na kutoafikiana ambavyo viongozi wake wameshindwa kutuliza. Ingawa hivyo, haitupasi kupoteza mwono wa uhakika wa kwamba hili shambulio la mwisho kabisa, la ujumla juu ya Babuloni Mkubwa linakuja likiwa wonyesho wa hukumu ya Mungu isiyobadilika juu ya kahaba mkubwa.
Kufikiliza Fikira ya Mungu
19. (a) Utekelezo wa hukumu ya Yehova dhidi ya kahaba mkubwa unaweza kutolewaje kielezi na hukumu yake dhidi ya Yerusalemu asi-imani katika 607 K.W.K.? (b) Hali ya ukiwa, ya kutokaliwa ya Yerusalemu baada ya 607 K.W.K. ilitangulia kutoa tamathali ya nini kwa siku yetu?
19 Yehova anatekelezaje hukumu hii? Hii inaweza kutolewa kielezi na tendo la Yehova dhidi ya watu wake waasi-imani katika nyakati za kale, ambao kuwahusu yeye alisema: “Katika manabii wa Yerusalemu mimi nimeona vitu vibaya sana, kufanya uzinzi na kutembea katika ubandia; na wao wameimarisha mikono ya watenda maovu ili kwamba isiwapase kurudi, kila mmoja kutoka ubaya wake mwenyewe. Kwangu mimi wao wote wamekuwa kama Sodoma, na wakaaji wake ni kama Gomora.” (Yeremia 23:14, NW) Katika 607 K.W.K., Yehova alitumia Nebukadneza ‘avue mavazi, atwae vitu vizuri, na aache uchi na bila nguo’ jiji hilo lenye uzinzi wa kiroho. (Ezekieli 23:4, 26, 29, NW) Yerusalemu la wakati huo lilikuwa kigezo cha Jumuiya ya Wakristo ya leo, na kama alivyoona Yohana katika njozi ya mapema zaidi, Yehova ataipa Jumuiya ya Wakristo na dini nyingine yote bandia adhabu inayofanana na hiyo. Ukiwa, hali ya kutokaliwa ya Yerusalemu baada ya 607 K.W.K. huonyesha vile Jumuiya ya Wakristo ya kidini itakavyoonekana baada ya kuvuliwa ukwasi wayo na kufichuliwa kiaibu. Na sehemu inayobaki ya Babuloni Mkubwa haitakuwa afadhali.
20. (a) Yohana anaonyeshaje kwamba kwa mara nyingine tena Yehova atatumia watawala wa kibinadamu kutekeleza hukumu? (b) “Fikira” ya Mungu ni nini? (c) Ni katika njia gani mataifa yatafikiliza “fikira moja,” yayo lakini kwa kweli ni fikira ya nani itatimizwa?
20 Kwa mara nyingine tena Yehova anatumia watawala wa kibinadamu kutekeleza hukumu. “Kwa maana Mungu alitia hilo ndani ya mioyo yao kufikiliza fikira yake, hata kufikiliza fikira yao moja kwa kumpa ufalme wao hayawani-mwitu, mpaka hapo maneno ya Mungu yatakuwa yametimilizwa.” (Ufunuo 17:17, NW) “Fikira” ya Mungu ni nini? Kupangia wafishaji wa Babuloni Mkubwa waungane pamoja, ili kumharibu kabisa. Bila shaka, matilaba ya watawala katika kumshambulia yatakuwa kufikiliza “fikira moja” yao wenyewe. Wao watahisi kwamba ni kwa masilahi yao ya utukuzaji wa taifa kumgeukia huyo kahaba mkubwa. Huenda wakaja kuona kule kuendelea kwa dini iliyopangwa kitengenezo ndani ya mipaka yao kuwa tisho kwa enzi zao. Lakini Yehova atakuwa kwa kweli akiongoza mambo kwa werevu; wao watafikiliza fikira yake kwa kuharibu kwa dharuba moja adui yake mzinzi wa muda mrefu!—Linga Yeremia 7:8-11, 34.
21. Kwa kuwa hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu atatumiwa katika kuharibu Babuloni Mkubwa, kwa wazi mataifa yatafanya nini kwa habari ya Umoja wa Mataifa?
21 Ndiyo, mataifa yatatumia hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu, Umoja wa Mataifa, katika kuharibu Babuloni Mkubwa. Wao hawatendi kwa utangulizi wao wenyewe, kwa maana Yehova hutia ndani ya mioyo yao “hata kufikiliza fikira moja yao kwa kumpa ufalme wao hayawani-mwitu.” Wakati ujapo, kwa wazi mataifa yataona uhitaji wa kuimarisha Umoja wa Mataifa. Itakuwa kana kwamba, wanaupa meno, wakiupa mamlaka yoyote na nguvu waliyo nayo ili kwamba uweze kugeukia dini bandia na kupiga vita kwa kufaulu dhidi yayo “mpaka hapo maneno ya Mungu yatakuwa yametimilizwa.” Hivyo, kahaba wa kale atakuja kwenye mwisho wake kabisa. Na apotelee mbali!
22. (a) Kwenye Ufunuo 17:18, ni nini kinachoashiriwa kwa njia ambayo malaika humalizia ushahidi wake? (b) Mashahidi wa Yehova wanaitikiaje kufumbuliwa kwa fumbo hilo?
22 Kana kwamba anakazia uhakika wa kutekelezwa kwa hukumu ya Yehova juu ya milki ya ulimwengu ya dini bandia, malaika anamalizia ushahidi wake kwa kusema: “Na mwanamke ambaye wewe uliona anamaanisha jiji kubwa ambalo lina ufalme juu ya wafalme wa dunia.” (Ufunuo 17:18, NW) Kama Babuloni wa wakati wa Belshaza, Babuloni Mkubwa “amepimwa uzani katika mizani na akapatikana anapungukiwa.” (Danieli 5:27, The New English Bible) Kufishwa kwake kutakuwa kwepesi na kwa kukata maneno. Nao Mashahidi wa Yehova wanaitikiaje kufumbuliwa kwa fumbo la kahaba mkubwa na la hayawani-mwitu rangi-nyekundu-nyangavu? Wao huonyesha bidii katika kupiga mbiu ya siku ya hukumu ya Yehova, huku wakijibu “kwa upendezi” watafutaji wa ukweli wenye mioyo myeupe. (Wakolosai 4:5, 6; Ufunuo 17:3, 7, NW) Kama vile sura yetu ifuatayo itakavyoonyesha, wote wenye kutamania kuokoka wakati kahaba mkubwa anapofishwa lazima watende, na kutenda chakachaka!
[Picha katika ukurasa wa 252]
Mfuatano wa Serikali Saba za Ulimwengu
MISRI
ASHURU
BABULONI
UMEDI-UAJEMI
UGIRIKI
ROMA
UINGEREZA-AMERIKA
[Picha katika ukurasa wa 254]
“Yeye pia mwenyewe ni mfalme wa nane”
[Picha katika ukurasa wa 255]
Wakimgeuzia Mwana-Kondoo visogo vyao, “wao humpa hayawani-mwitu nguvu na mamlaka yao”
[Picha katika ukurasa wa 257]
Jumuiya ya Wakristo ikiwa ndiyo sehemu kuu ya Babuloni Mkubwa itashabihi Yerusalemu la kale kuwa gofu kabisa