Sura 4
“Babeli” Usio na Usalama Wahukumiwa Kuangamizwa
1. (a) Neno “Babeli” lina maana gani, na ni nani aliyeanzisha mji wenye jina hilo? (b) Ni mpango gani wa ujenzi ambao Nimrodi mwenye kujitakia makuu alianzisha, na kukawa na matokeo gani?
ULIMWENGU leo una alama ya mchafuko—kisiasa, kijamii, na kidini. Tafsiri ya Kiswahili ya neno la Biblia la Kiebrania kwa mchafuko ni “Babeli.” Katika Mwanzo, Babeli unatajwa, jina linalomaanisha “mchafuko.” Mji wenye jina hilo ulianzishwa na Nimrodi, mwasi dhidi ya Yehova. (Mwanzo 10:8-10) Huko, wanadamu wakiwa chini ya uongozi wa Nimrodi mwenye kujitakia makuu walianza kujenga mnara ambao ungepanda kuelekea mbinguni katika kumpinga Yehova. Yehova aliushinda mpango huo wenye kuvunjia Mungu heshima kwa kuchafua lugha yenye umoja ya wajenzi hao, hivi kwamba hawakuweza kufahamiana walipojaribu kufanya kazi yao pamoja.—Mwanzo 11:1-9.
2. (a) Mamlaka ya ulimwengu ya Babeli ilipatwa na nini mwaka wa 539 K.W.K., na je! huo ulionyesha mwisho wa mji huo ulioitwa kwa jina hilo? (b) Mji wa kale wa Babeli haukuthibitika kuwa nini?
2 Muda mrefu baadaye, iliandikwa kwamba mji mpya wenye jina Babeli ulikuwa huko kwenye Mto Frati. (2 Wafalme 17:24; 1 Mambo ya Nyakati 9:1) Katika mwaka 539 K.W.K. ile Mamlaka ya Ulimwengu ya kibabeli iliangushwa na Koreshi Mkuu, mfalme wa Waamedi na Waajemi, katika utimizo wa unabii wa Yehova kwenye Isaya 45:1-6. Ijapokuwa Babeli ulikuwa umepata anguko kubwa, uliruhusiwa uendelee kuwako ukiwa mji. Uliripotiwa kuwa ukiendelea kuwako hata katika nusu ya pili ya karne ya kwanza ya Wakati wa Kawaida wetu. (1 Petro 5:13) Hata hivyo, mji huo wa kale, haukuwa ndio ‘Babeli Mkuu,’ ambao mtume Yohana aliandika juu yao katika kitabu cha Ufunuo sura ya 17.
3. Ni utambulishi gani ulio wa kweli wa Babeli Mkuu?
3 ‘Babeli Mkuu,’ wa ufunuo, anayeonyeshwa kuwa mwanamke mwasherati anayempanda “mnyama mwekundu sana,” anafananisha ile milki ya ulimwengu ya dini ya uwongo, kutia dini zote zinazoitwa Jumuiya ya Wakristo.a (Ufunuo 17:3-5) Kulingana na yale mtume Yohana aliona juu yake, tengenezo hili la mfano limefanya uasherati wa kiroho na watawala wote wa kisiasa wa dunia. Milki hiyo ya kilimwengu ya dini ya uwongo, Babeli Mkuu, ingali inatumia uvutano mkubwa.
“Rafiki wa Ulimwengu”—Si wa Mungu
4. Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, Babeli Mkuu aliongezaje uhalifu aliotenda jamii ya kibinadamu?
4 Hata hivyo, Babeli Mkuu yuko katika hali isiyo na usalama hata kidogo, na sana sana imekuwa hivyo tangu mwisho wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza. Wakati wa pigano hilo, yeye alizidisha uhalifu wake dhidi ya jamii ya kibinadamu. Wale viongozi wa Jumuiya ya Wakristo, ambao hudai kuwa wafuasi wa Yesu Kristo, waliwachochea vijana kwa mahubiri yao waende kwenye uwanja wa vita. Harry Emerson Fosdick, kasisi Mprotestanti aliyekufa, mwenye kujulikana sana, aliunga mkono jitihada za vita lakini baadaye alikubali hivi: “Hata ndani ya makanisa yetu tumeziweka bendera za vita . . . Kwa pembe moja ya mdomo wetu tumemsifu Mwana-Mfalme wa Amani na kwa pembe ile nyingine tumetukuza vita.” Makasisi na viongozi wengine wa dini za Jumuiya ya Wakristo walitoa sala kwa ajili ya majeshi yenye kupigana katika mikutano ya kidini, na walitumikia wakiwa makasisi kwa ajili ya jeshi la nchi kavu, jeshi la majini, na jeshi la angani.b
5. (a) Ni maneno gani ya Yakobo 4:4 ambayo Jumuiya ya Wakristo haikuyazingatia? (b) Ni lazima hukumu ya kimungu juu yake iwe nini?
5 Jumuiya ya Wakristo, chini ya uongozi wa viongozi hao wa kidini, haijazingatia maneno haya ya Yakobo 4:4, HNWW: “Ninyi ni watu msio na uaminifu kama wazinzi. Je, hamjui kwamba kuwa rafiki wa ulimwengu ni kuwa adui wa Mungu? Ye yote anayetaka kuwa rafiki wa ulimwengu anajifanya adui wa Mungu.” Hivyo Jumuiya ya Wakristo inaendelea kuwa adui wa Mungu Aliye Juu Zaidi mpaka wakati uu huu. Bila shaka yeye hana ulinzi wa kimungu, na kwa sababu hii yenye maana kuwako kwake kunaendelea kuwa katika hali isiyo na usalama. Rafiki zake za kisiasa si wa kutumainiwa, na mwendo wa kuelekea kwenye kupinga dini unaendelea kupata nguvu. Si kwa ajili yake kwamba Mungu asema: “Enyi watu msiwaguse wapakwa mafuta wangu.”—1 Mambo ya Nyakati 16:22, NW.
“Tokeni Kwake, Enyi Watu Wangu”
6, 7. (a) Ni mwito gani wa haraka unaotolewa kwenye Ufunuo 18:4, na unaelekezwa kwa nani? (b) Ni wakati gani mwito wa mapema kama huo ulipoanza kutumika kwa Wayahudi waliokuwa wakinyong’onyea katika Babeli wa kale?
6 Kwa hao wapakwa mafuta na washiriki wao katika huu umalizio wa mfumo wa mambo, mwito wa kimungu unatolewa kwao kwa haraka: “Tokeni kwake, enyi watu wangu, msishiriki dhambi zake.” (Ufunuo 18:4) Ndiyo, tokeni kwa Babeli Mkuu, ile milki ya ulimwengu ya dini ya uwongo.
7 Mwito huo unarudia maneno ya Yeremia 50:8 na 51:6, 45, ambayo yalielekezwa kwa mabaki ya Wayahudi ambao Yehova alihukumia kutumia miaka 70 ya utekwa na uhamisho katika nchi ya Babulonia. Maneno hayo yalianza kutumika kwa Wayahudi waliokuwa wakinyong’onyea katika Babulonia mwaka wa 537 K.W.K., baada ya Koreshi Mkuu aliyetabiriwa kuongoza vikosi vyake vya Waamedi na Waajemi kupitia Mto Frati uliokuwa karibu umekauka maji kuingia katika mji wa Babeli.
8. (a) Koreshi Mkuu alitimizaje Isaya 45:1-6? (b) Kwa sababu gani yule aliyefananishwa na Koreshi Mkuu alihitaji kutenda kulingana na kiolezo hicho cha kiunabii cha mambo?
8 Katika mwaka wa kwanza wa utawala wake, Koreshi Mkuu alitenda katika kutimiza unabii wa Isaya 45:1-6. Vivyo hivyo, yule aliyefananishwa na Mfalme Koreshi, lakini ambaye ni mwenye nguvu zaidi, Yesu Kristo, alitenda kulingana na kiolezo hicho cha mambo ya kiunabii. Hiyo ilikuwa wakati ule uliowekwa baada ya kuingia kwenye utawala wake wa kifalme katika mbingu kwenye mkono wa kuume wa Yehova Mungu wakati zile “nyakati zilizowekwa za mataifa” zilipokwisha katika Oktoba 1914. (Luka 21:24, NW) Wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza ya 1914-18, mabaki ya Waisraeli wa kiroho walipatwa na utekwa mikononi mwa Babeli Mkuu na hawara zake wa kisiasa.
9, 10. (a) Ni tendo gani lililochukuliwa dhidi ya washiriki wanane wa wafanya kazi wa makao makuu ya Sosaiti? (b) Kuna ushuhuda gani kwamba Babeli Mkuu ndiye aliyeanzisha mwendo wa kukomesha kazi ya watu wa Yehova?
9 Kwa mfano, katika United States kile kitabu cha mwisho kutangazwa na Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi wakati huo, The Finished Mystery, kilipigwa marufuku kuwa kinapinga serikali. Wale watungaji wawili wa kitabu hicho waliletwa kwenye mahakama ya kitaifa katika Brooklyn, New York, na wakahukumiwa isivyo haki miaka 20 ya kizuizi katika gereza la kitaifa huko Atlanta, Georgia. Ndivyo walivyofanyiwa msimamizi wa Sosaiti hiyo yenye kutangaza, katibu-mweka hazina, pamoja na wafanya kazi wengine watatu wa makao makuu. Mtafsiri-mshirika alihukumiwa nusu ya kifungo hicho katika gereza la kitaifa.
10 Na hivyo Julai 4, 1918, Wakristo hao wanane waliojiweka wakfu waliwekwa kwenye gari-moshi kuelekea Atlanta, Georgia, wakanyang’anywe uhuru wao huko. Washiriki wa makao makuu ya Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi huko Brooklyn wakati huo walilazimika kuangalia mambo kadiri wawezavyo. Ni nani aliyekuwa wa kulaumiwa kwa sababu ya hali hiyo? Kitabu Preachers Present Arms kinajibu: “Uchanganuzi wa kesi yote hiyo unaongoza kwenye kukata maneno kwamba makanisa na viongozi wa kidini mwanzoni ndio walioanza mwendo wa kuwafutilia mbali Warusselli [Mashahidi]. . . . Wakati habari za hukumu ya vifungo hivyo vya miaka ishirini zilipowafikia wahariri wa magazeti ya kidini, karibu kila kimoja cha vichapo hivyo, kikubwa na kidogo, kilishangilia tukio hilo. Mimi nimeshindwa kuona maneno yo yote ya kusikitikia katika lo lote la majarida hayo ya dini zilizoimarishwa.”—Ray H. Abrams, kurasa 183, 184.
Anguko—Lakini Si Katika Uharibifu
11, 12. (a) Babeli Mkuu alikusudia kufanya nini? (b) Alipatwaje na anguko kuu, ijapokuwa si katika uharibifu? (c) Matokeo yalikuwa nini juu ya watu wa Yehova waliokombolewa?
11 Lakini shangwe hiyo ya Babeli Mkuu ilikuwa ya muda mfupi tu. Katika masika ya 1919, Babeli Mkuu alipatwa na anguko kuu, ambalo lazima lifuatwe na matukio fulani ya kidini kabla hajaharibiwa kabisa. Babeli Mkuu alifikiria kuwaweka watu wa Yehova wakiwa wamezuiwa na kutekwa milele. Lakini katika Machi wa 1919, milango ya gereza ililazimika kufunguliwa kwa wale wawakilishi wanane wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi nao wakatoka nje kwa dhamana. Baadaye, waliondolewa mashtaka yote kabisa kabisa.
12 Sasa shangwe ya Babeli Mkuu ikamalizika fyu! Kile Kitabu Preachers Present Arms kinasema hivi kwa habari ya uamuzi wa mahakama wa kuwaachilia huru Mashahidi: “Uamuzi huo ulipokelewa kwa ukimya na makanisa.” Lakini furaha ya watu wa Yehova ilikuwa kuu. Tengenezo lao la ulimwenguni pote lilifanyiwa marekebisho. Kwenye mkusanyiko wao mwaka wa 1919 huko Seda Pointi Ohaiyo, kwa kutumia hotuba yake yenye kichwa “Kuutangaza Ufalme,” msimamizi wa Sosaiti alichochea maelfu waliohudhuria watende. Mashahidi wa Yehova walikuwa huru tena, wakiutangaza kishujaa Ufalme wa Mungu peupe! Babeli Mkuu alikuwa amepatwa na anguko, ijapokuwa si katika uharibifu. Yule Koreshi Mkubwa Zaidi, Yesu Kristo, alikuwa amemshinda na kuweka huru wafuasi wake waaminifu.
13. Wakati Ushirika wa Mataifa ulipotokea, Babeli Mkuu alifanya nini?
13 Hivyo Babeli Mkuu alikuwa ameruhusiwa aendelee kuwapo na kuingia kwenye wakati wa baada ya vita. Wakati Ushirika wa Mataifa ulipopendekezwa uwe baraza la ulimwengu la kuhifadhi amani, Baraza la Muungano wa Makanisa ya Kristo Katika Amerika lilijitokeza likauunga mkono, likitangaza peupe kwamba huo Ushirika wa Mataifa ulikuwa “wonyesho wa kisiasa wa Ufalme wa Mungu duniani.” Wakati Ushirika huo uliopendekezwa ulipoanzishwa mwishowe, Babeli Mkuu alipanda kwenye mgongo wao na kwa njia hiyo akaanza kumpanda huyo “mnyama mwekundu sana” wa mfano.—Ufunuo 17:3.
14. (a) Wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili, ni mwendo gani uliochukuliwa na Babeli Mkuu? (b) Wakati chombo hicho kilichofanywa na wanadamu cha kuhifadhi amani kilipopanda kutoka shimo refu baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, Babeli Mkuu alifanya nini?
14 Wakati chombo hicho kisicho na uwezo cha kuhifadhi amani kilipoingia kwenye shimo refu la kutotenda ilipotokea Vita ya Ulimwengu ya Pili, Babeli Mkuu aliachwa bila mnyama wa kupanda. (Ufunuo 17:8) Walakini yeye alikuwapo papo hapo pamoja na yale mataifa 57 yaliyojiingiza katika Vita ya Ulimwengu ya Pili. Yeye hakusumbuliwa na uhakika wa kwamba alilazimika kugawanya ushikamanifu wake kati ya vikundi hivyo vyenye kupigana, kama vile asivyosumbuliwa kamwe na uhakika wa kwamba yeye amegawanyika akawa mamia mengi ya madhehebu na vikundi vya kidini vyenye mchafuko. Wakati chombo hicho cha kuhifadhi amani kilichofanyizwa na mwanadamu, kwa umbo la Umoja wa Mataifa, kilipopanda kutoka shimo refu la kutotenda mwishoni mwa Vita ya Ulimwengu ya Pili, mara moja Babeli Mkuu alipanda kwenye mgongo wacho na kuanza kutumia uvutano wake juu yacho.
Mamlaka za Kisiasa Kumgeukia Babeli
15, 16. (a) Sasa wanadamu wanakabili tamasha gani yenye kutia woga? (b) Mungu Mwenye Nguvu Zote ameazimia kufanya nini, kulingana na Ufunuo 17:15-18?
15 Ulimwengu mzima wa wanadamu sasa unakaribia kukabili tamasha yenye kutia woga. Huko kutakuwa ni kule kugeukiwa kwa Babeli Mkuu na mamlaka za kisiasa, zikiwa na lengo la kumfutilia mbali asiwepo kabisa. Hilo linaweza kusikika kama jambo la kufisha moyo kwa wale wanaoamini kwa moyo mweupe kwamba dini zote ni nzuri. Lakini, Yehova Mungu, Mwenye Enzi Kuu, ameazimia kwamba Babeli Mkuu hana mahali katika ulimwengu wote na kwamba yeye ameuchafua uumbaji kwa muda wa kutosha. Ni lazima yeye aangushwe kwa ujeuri na kuharibiwa kabisa.
16 Tayari kuna vyombo vyenye nguvu ambavyo Mungu anaweza kuruhusu vimwangamize, yaani, zile sehemu za kisiasa za ulimwengu. Kile kitabu kilichoongozwa na Mungu cha Ufunuo kinatabiri kwamba Yehova atawageuza wapenzi wake juu yake, nao watamvua mavazi yake na kumwacha uchi, wakimfunua namna alivyo kweli kweli—mlaghai aliyepagawa na mashetani! Ndipo, kwa njia ya mfano, watakapomteketeza kwa moto na kumfanya kuwa rundo la majivu. Watamtenda kama vile alivyowatenda waabudu wa Mungu wa kweli wasiobadili msimamo wao.—Ufunuo 17:15-18; 18:24.
17. Je! matendo yenye uhodari ya mamlaka za kisiasa, ya kupinga Babeli, yatazigeuza zimwabudu Yehova Mungu, na twajuaje?
17 Tendo hilo la jeuri la mamlaka za kisiasa la kupinga dini halimaanishi kwamba baada ya hapo zitageuka zimwabudu Yehova Mungu. Tendo hilo kali la kupinga Babeli halimaanishi kwamba zenyewe sasa zitakuwa rafiki za Mungu. Kama sivyo hazingechukua lile tendo la baadaye ambalo kitabu cha Ufunuo kinaonyesha zitachukua. (Ufunuo 17:12-14) Huenda zikashangilia sana kwa sababu ya matendo ya uhodari ya kupinga dini ambayo Yehova Mungu ameziruhusu kutimiza, lakini bado zitaendelea kupotezwa na “mungu wa huu mfumo wa mambo” Shetani Ibilisi, yule mpinzani wa kupindukia, asiyechoka wa Yehova Mungu.—2 Wakorintho 4:4, NW.
18, 19. (a) Ni nani ambaye hataokoka aje kuona kuondolewa malawama ya enzi kuu ya ulimwengu wote ya Yehova kupitia “Mwana-Mfalme wa Amani”? (b) Lakini ni nani watakaokuwa mashahidi wenye kuendelea kuishi wajionee kuondolewa malawama ya Yehova yaliyoletwa na Babeli Mkuu?
18 Babeli Mkuu hataokoka auone upeo mkuu, kule kuondolewa malawama ya enzi kuu ya ulimwengu wote ya Yehova kupitia “Mwana-Mfalme wa Amani,” ambaye sasa ndiye “Mungu Mwenye Nguvu” aliye kwenye mkono wa kuume wa Yule Mungu Mkuu Mwenye Nguvu Zote, Yehova.—Isaya 9:6, NW.
19 Upande ule mwingine, chini ya ulinzi usiopenyeka wa kimungu, watakuwapo Mashahidi wa Yehova. (Isaya 43:10, 12) Chini ya amri kutoka mbingu zenye uadilifu, kwa utii wao watakuwa wamekwisha toka kwa Babeli Mkuu. (Ufunuo 18:4) Furaha yao yenye uadilifu itakuwa haina mipaka kwa yale watakayoshuhudia. Baada ya hapo watakuwa Mashahidi wa Yehova na waweze kushuhudia namna alivyojiondolea milele malawama yaliyoletwa na Babeli Mkuu.—Ufunuo 19:1-3.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa utambulisho wenye maelezo zaidi, ona kitabu “Babylon The Great Has Fallen!” God’s Kingdom Rules!, kurasa 468-500, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
b Mazungumzo yenye habari nyingi juu ya namna viongozi wa kidini walivyounga mkono Vita ya Ulimwengu ya Kwanza yanatolewa katika kitabu Preachers Present Arms, cha Ray H. Abrams (New York, 1933). Kitabu hicho kinasema hivi: “Viongozi wa kidini walivipa vita umaana wa juhudi yao ya kiroho na msukumo. . . . Vita yenyewe ilikuwa ni vita takatifu ya kuendeleza Ufalme wa Mungu duniani. Mtu kutoa uhai wake kwa ajili ya nchi yake kulikuwa ni kuutoa kwa ajili ya Mungu na Ufalme Wake. Mungu na nchi yakaja kuwa maneno yenye maana moja. . . . Wajeremani na Marafiki walikuwa sawa katika jambo hilo. Kila upande uliamini kwamba Mungu alikuwa upande wao . . . Wengi wa walimu wa kidini hawakuona ugumu wo wote katika kumweka Yesu katika mstari wa mbele kabisa panapopiganiwa vita vikali akiongoza vikosi vyao kwenye ushindi. . . . Kwa njia hiyo kanisa likaja kuwa sehemu ya mfumo wa vita. . . . Viongozi [wa makanisa] hawakupoteza wakati wo wote wakijitayarisha wakati wa vita. Kwa muda wa saa ishirini na nne tu baada ya kutangazwa vita, Baraza la Muungano wa Makanisa ya Kristo Katika Amerika lilifanya mpango wa kutoa ushirikiano kamili. . . . Makanisa mengi yalifanya mengi zaidi ya yale yaliyoombwa yafanye. Yakawa vituo vya kuandikisha askari wapya kwa ajili ya vikosi.”—Kurasa 53, 57, 59, 63, 74, 80, 82.