Sura ya 28
Kupambana na Hayawani Wawili Wakali Sana
Njozi ya 8—Ufunuo 13:1-18
Habari: Hayawani-mwitu mwenye vichwa saba, hayawani-mwitu mwenye vichwa viwili, na mfano wa hayawani-mwitu
Wakati wa utimizo: Kutoka siku ya Nimrodi hadi dhiki kubwa
1, 2. (a) Yohana anasema nini juu ya drakoni? (b) Yohana kwa lugha ya ufananisho, huelezaje habari ya tengenezo lionekanalo linalotumiwa na drakoni?
YULE drakoni mkubwa ametupwa chini kwenye dunia! Funzo letu juu ya Ufunuo limedhihirisha kwamba Nyoka au wafuasi wake roho waovu hawataruhusiwa tena kamwe warudi ndani ya mbingu. Lakini hatujamaliza habari ya “mmoja ambaye huitwa Ibilisi na Shetani, ambaye anaongoza vibaya dunia nzima yote inayokaliwa.” Simulizi linafuata kutambulisha kirefu njia anayotumia Shetani kupiga vita dhidi ya ‘mwanamke na mbegu yake.’ (Ufunuo 12:9, 17, NW) Yohana anasema hivi juu ya drakoni huyo wa kinyoka: “Na huyo akasimama tuli juu ya mchanga wa bahari.” (Ufunuo 13:1a, NW) Kwa hiyo acheni sisi tutue na kuchunguza njia ya utendaji ya huyo drakoni.
2 Mbingu takatifu hazisumbuliwi tena na kuwapo kwa Shetani na roho waovu wake. Hao roho waovu wamekwisha fukuzwa nje ya mbingu na kufungiwa kwenye ujirani wa dunia. Hapana shaka hii ndiyo sababu ya ukuzi mkubwa mno wa mazoea ya uwasiliano na roho nyakati hizi. Nyoka mwenye hila angali anadumisha tengenezo la roho lenye ufisadi. Lakini je! yeye pia anatumia tengenezo linaloonekana ili kuongoza vibaya aina ya binadamu? Yohana hutuambia hivi: “Na mimi nikaona hayawani-mwitu akipanda kutoka bahari, mwenye pembe kumi na vichwa saba, na juu ya pembe zake mataji kumi, lakini juu ya vichwa vyake majina yenye kufuru. Sasa hayawani-mwitu ambaye mimi niliona alikuwa kama chui, lakini nyayo zake zilikuwa kama zile za dubu, na kinywa chake kilikuwa kama kinywa cha simba. Na drakoni akampa hayawani nguvu zake na kiti cha ufalme chake na mamlaka kubwa.”—Ufunuo 13:1b, 2, NW.
3. (a) Ni hayawani gani wakali sana alioona nabii Danieli katika njozi? (b) Hayawani wakubwa mno wa Danieli 7 waliwakilisha nini?
3 Huyu hayawani wa kiajabu ni nini? Biblia yenyewe hutoa jibu. Kabla ya anguko la Babuloni katika 539 K.W.K., Danieli nabii Myahudi aliona njozi zilizohusu hayawani wakali sana. Kwenye Danieli 7:2-8, NW yeye anaeleza habari za hayawani wanne wakitoka baharini, wa kwanza akishabihi simba, wa pili dubu, wa tatu chui, na “ona kule! hayawani wa nne, mwenye kuhofisha na mwenye kutisha na mwenye nguvu isivyo kawaida . . . na alikuwa na pembe kumi.” Huyu ni sawa kabisa na hayawani aliyeonwa na Yohana wapata mwaka 96 W.K. Pia hayawani huyo ana hulka za simba, dubu, na chui, na ana pembe kumi. Ni nini ulio utambulisho wa wale hayawani wakubwa mno walioonwa na Danieli? Yeye anatuarifu: “Hayawani hawa wakubwa mno . . . ni wafalme wanne ambao watasimama katika dunia.” (Danieli 7:17, NW) Ndiyo, hayawani hao wanawakilisha “wafalme,” au serikali kubwa za kisiasa za dunia.
4. (a) Katika Danieli 8, kondoo-dume na mbuzi-dume ni taswira ya nini? (b) Ni nini kilichoonyeshwa wakati upembe mkubwa wa mbuzi-dume ulipovunjwa na nyingine nne zikachukua mahali pao?
4 Katika njozi nyingine, Danieli anaona kondoo-dume mwenye pembe mbili ambaye anapigwa mpaka chini na mbuzi mwenye upembe mkubwa. Malaika Gabrieli anamweleza maana yayo: “Kondoo-dume . . . husimama kwa ajili ya wafalme wa Umedi na Uajemi. Na mbuzi-dume mwenye manyoya anasimama kwa ajili ya mfalme wa Ugiriki.” Gabrieli anaendelea kutoa unabii kwamba upembe mkubwa wa mbuzi-dume ungevunjwa na kufuatwa na pembe nne. Kwa kweli hilo lilitukia miaka zaidi ya 200 baadaye Aleksanda Mkuu alipokufa na ufalme wake ukagawanywa kuwa falme nne zilizotawalwa na wanne wa majenerali wake.—Danieli 8:3-8, 20-25, NW.a
5. (a) Neno la Kigiriki kwa hayawani linawasilisha maana gani? (b) Hayawani-mwitu wa Ufunuo 13:1, 2, pamoja na vichwa vyake saba anasimamia nini?
5 Kwa hiyo, ni wazi kwamba Mtungaji Biblia iliyovuviwa huziona serikali za kisiasa za dunia kuwa hayawani. Ni hayawani wa aina gani? Mfasili mmoja anaita hayawani-mwitu wa Ufunuo 13:1, 2 “mshenzi,” na kuongeza: “Sisi tunakubali maana zote ambazo θηρίον [the·riʹon, neno la Kigiriki kwa “hayawani”] huwasilisha, kama dubwana mkatili, mharibifu, mwenye kutia kikuli, mlafuaji, n.k.”b Lo! jinsi hiyo inavyoeleza vizuri mfumo wa kisiasa wenye madoa ya damu ambao kwa huo Shetani ametawala aina ya binadamu! Vichwa saba vya huyu hayawani-mwitu husimama kwa ajili ya serikali sita kubwa za ulimwengu ambazo zimeelezwa katika historia ya Biblia kufikia siku ya Yohana—Misri, Ashuru, Babuloni, Umedi-Uajemi, Ugiriki, na Roma—na serikali kubwa ya ulimwengu ya saba iliyotolewa unabii kutokea baadaye.—Linga Ufunuo 17:9, 10.
6. (a) Vichwa saba vya hayawani-mwitu vilichukua uongozi katika nini? (b) Roma ilitumiwaje na Yehova katika kufikiliza hukumu zake mwenyewe juu ya mfumo wa mambo wa Kiyahudi, na Wakristo katika Yerusalemu walikuwa katika hali gani?
6 Ni kweli, kumekuwako serikali nyinginezo kubwa za ulimwengu katika historia mbali na zile saba—kama vile hayawani-mwitu ambaye Yohana aliona alivyokuwa na mwili pamoja na vichwa saba na pembe kumi. Lakini vichwa saba huwakilisha zile serikali kubwa ambazo, kila mojapo katika zamu yayo, imechukua uongozi katika kuonea watu wa Mungu. Katika 33 W.K., wakati Roma ilipokuwa mamlaka kuu yenye kutawala, Shetani alitumia hicho kichwa cha hayawani-mwitu kuua Mwana wa Mungu. Wakati huo, Mungu aliuacha mfumo wa mambo wa Kiyahudi usioaminika na baadaye, katika 70 W.K., akaruhusu Roma itekeleze hukumu yake juu ya taifa hilo. Kwa furaha, Israeli wa kweli wa Mungu, kundi lililopakwa mafuta la Wakristo, alikuwa ameonywa kimbele, na wale ambao walikuwa katika Yerusalemu na Yudea walikuwa wamekimbilia usalama ng’ambo ya Mto Yordani.—Wagalatia 6:16; Mathayo 24:15, 16.
7. (a) Kungetukia nini wakati umalizio wa mfumo wa mambo ungewasili na siku ya Bwana kuanza? (b) Ni nini kilichothibitika kuwa ndicho kichwa cha saba cha hayawani-mwitu wa Ufunuo 13:1, 2?
7 Hata hivyo, kufikia mwisho wa karne ya kwanza W.K., wengi katika hili kundi la mapema walikuwa wameanguka kutoka ukweli, na ngano ya kweli ya Kikristo, “wale wana wa ufalme,” ilikuwa imesongwa sana na magugu, “wale wana wa yule mwovu.” Lakini wakati umalizio wa mfumo wa mambo ulipowasili, Wakristo wapakwa-mafuta walitokea tena wakiwa kikundi kilichopangwa kitengenezo. Wakati wa siku ya Bwana, ulikuwa umefika wakati wa waadilifu ‘waangaze kwa uangavu kama jua.’ Kwa sababu hiyo, kundi la Kikristo lilipangwa kitengenezo kwa ajili ya kazi. (Mathayo 13:24-30, 36-43, NW) Kufikia wakati huo, Milki ya Roma haikuwapo tena. Milki kubwa ya Uingereza, pamoja na United States ya Amerika yenye nguvu nyingi, zilishikilia kitovu cha jukwaa la ulimwengu. Hii serikali ya ulimwengu ya uwili ilithibitika kuwa ndiyo kichwa cha saba cha hayawani-mwitu.
8. Ni kwa nini haipasi kushtusha kwa vile Uingereza-Amerika serikali kubwa ya uwili, inafananishwa na hayawani?
8 Lakini je! haishtushi kutambulisha serikali za kisiasa na hayawani-mwitu? Ndivyo baadhi ya wapinzani walivyodai wakati wa Vita ya Ulimwengu 2, hadhi ya Mashahidi wa Yehova, wakiwa tengenezo na wakiwa watu mmoja mmoja, ilipokuwa ikitiliwa shaka katika mahakama za sheria kotekote duniani. Lakini tua ufikirie! Je! mataifa yenyewe hayatumii hayawani au viumbe-mwitu kuwa ishara za kitaifa zao? Mathalani, kuna simba wa Uingereza, tai wa Amerika, na drakoni wa Uchina. Basi sababu gani yeyote apinge ikiwa Mtungaji wa kimungu wa Biblia Takatifu anatumia pia hayawani kufananisha serikali za ulimwengu?
9. (a) Ni kwa nini mmoja hapaswi kupinga Biblia inaposema kwamba Shetani humpa hayawani-mwitu mamlaka yake kubwa? (b) Shetani anaelezwaje katika Biblia, naye anatumiaje uvutano juu ya serikali?
9 Zaidi ya hilo, sababu gani yeyote apinge Biblia inaposema kwamba Shetani ndiye anayewapa hawa hayawani-mwitu mamlaka yao kubwa? Mungu ndiye Chimbuko la taarifa hiyo, na mbele zake ‘mataifa ni kama tone kutoka ndoo na kama filamu tu ya vumbi.’ Mataifa hayo yangefanya vizuri kutafuta kibali cha Mungu kuliko kuudhikia njia ambayo Neno lake hueleza habari zayo. (Isaya 40:15, 17; Zaburi 2:10-12, NW) Shetani si mtu wa hadithi ya uwongo mwenye mgawo wa kuzitesa nafsi zilizoondoka katika moto. Hakuna mahali kama hapo. Badala ya hivyo, Shetani anaelezwa habari zake katika Maandiko kuwa “malaika wa nuru”—stadi wa udanganyi anayetumia uvutano wenye nguvu katika mambo ya kisiasa kwa ujumla.—2 Wakorintho 11:3, 14, 15; Waefeso 6:11-18.
10. (a) Ni nini inayoonyeshwa na uhakika wa kwamba juu ya kila mojapo pembe kumi palikuwa na taji? (b) Pembe kumi na mataji kumi huwakilisha nini?
10 Hayawani-mwitu ana pembe kumi juu ya vichwa vyake saba. Labda kila kimoja cha vichwa vinne kilikuwa na upembe mmoja na kila kimoja cha vichwa vitatu kilikuwa na pembe mbili. Zaidi ya hilo, alikuwa na mataji kumi juu ya pembe zake. Katika kitabu cha Danieli, hayawani wenye kuhofisha wanaelezwa, na hesabu ya pembe yapasa ifasiriwe kihalisi. Mathalani, pembe mbili za kondoo-dume huwakilisha milki ya ulimwengu yenye washirika wawili, Umedi na Uajemi, hali pembe nne zilizo juu ya mbuzi huwakilisha milki nne zilizokuwako wakati ule ule ambazo zilikua kutokana na milki ya Ugiriki ya Aleksanda Mkuu. (Danieli 8:3, 8, 20-22) Hata hivyo, juu ya hayawani ambaye Yohana aliona hesabu ya pembe kumi yaonekana kuwa ya ufananisho. (Linga Danieli 7:24; Ufunuo 17:12.) Zinawakilisha ukamili wa serikali zenye enzi ambazo hujumlika kuwa tengenezo la kisiasa la Shetani. Pembe hizi zote ni zenye jeuri na zenye kutaka vita, lakini kama inavyoonyeshwa na vichwa saba, ukichwa hukaa katika serikali kubwa moja ya ulimwengu, wakati mmoja. Hali kadhalika, yale mataji kumi huonyesha kwamba serikali zote zenye enzi zingetumia mamlaka yenye kutawala wakati ule ule mmoja na dola kuu au serikali kubwa ya ulimwengu, ya wakati huo.
11. Ni nini kinachoonyeshwa na uhakika wa kwamba hayawani-mwitu ana “juu ya vichwa vyake majina ya kufuru”?
11 Huyo hayawani-mwitu ana “juu ya vichwa vyake majina yenye kufuru,” akijifanyia madai yanayoonyesha utovu mkubwa wa kustahi Yehova Mungu na Kristo Yesu. Ametumia majina ya Mungu na Kristo kuwa kisingizio cha kutimizia makusudi yake ya kisiasa; naye amecheza pamoja na dini bandia, hata kukubali viongozi wa kidini washiriki sehemu katika mambo ya siasa. Mathalani, Nyumba ya Mabwana ya Uingereza hutia ndani maaskofu. Makardinali wa Kikatoliki wamekuwa na vyeo vya umashuhuri katika Ufaransa na Italia, na hivi majuzi mapadri wametwaa vyeo vya kisiasa katika Amerika ya Kilatini. Serikali huchapa shime za kidini, kama “IN GOD WE TRUST” (Sisi Twaitibari Mungu), kwenye noti zao za benki, na juu ya sarafu zao zinadai kwamba watawala wazo wana kibali cha kimungu, wakitaarifu, mathalani, kwamba hao wanawekwa rasmi “kwa neema ya Mungu.” Kwa kweli yote haya ni makufuru, kwa kuwa hujaribu kumhusisha Mungu katika uwanja wa kisiasa wa kitaifa wenye kutiwa uchafu.
12. (a) Ni nini kinachoashiriwa na kutoka kwa hayawani-mwitu katika “bahari,” naye alianza kutokea wakati gani? (b) Ni nini kinachoonyeshwa na uhakika wa kwamba drakoni anampa hayawani wa ufananisho mamlaka yake kubwa?
12 Hayawani-mwitu hutoka katika “bahari,” ambayo ni ufananisho wenye kufaa wa yale matungamo yenye msukosuko ambayo kwayo serikali za kibinadamu huchipuka. (Isaya 17:12, 13) Hayawani-mwitu huyu alianza kuibuka katika bahari yenye msukosuko huko nyuma katika siku za Nimrodi (yapata karne ya 21 K.W.K.), wakati mfumo wa mambo wa baada ya Furiko, wenye kupinga Yehova, ulipojidhihirisha kwa mara ya kwanza. (Mwanzo 10:8-12; 11:1-9) Lakini ni katika pindi ya ile siku ya Bwana tu ndipo kichwa chake cha saba kimejidhihirisha kabisa. Vilevile angalia, drakoni ndiye “akampa hayawani nguvu zake na kiti cha ufalme chake na mamlaka kubwa.” (Linga Luka 4:6.) Hayawani huyo ni ubuni wa Shetani miongoni mwa matungamo ya aina ya binadamu. Kwa kweli Shetani ndiye “mtawala wa ulimwengu huu.”—Yohana 12:31, NW.
Dharuba ya Kifo
13. (a) Ni baa gani linalompata hayawani-mwitu mapema katika siku ya Bwana? (b) Ni jinsi gani hayawani-mwitu mzima wote aliumia wakati kichwa kimoja kilipopokea dharuba-kifo?
13 Mapema katika siku ya Bwana, baa linampiga hayawani-mwitu. Yohana huripoti: “Na mimi nikaona kimoja cha vichwa vyake kana kwamba kimechinjwa hadi kifo, lakini dharuba-kifo yake ikaponeshwa, na dunia nzima yote ikafuata hayawani-mwitu kwa kusifu mno.” (Ufunuo 13:3, NW) Mstari huu husema kwamba kichwa kimoja cha huyu hayawani-mwitu kilipokea dharuba ya kifo, lakini mstari wa 12 husema kana kwamba hayawani mzima wote aliumia. Ni kwa nini hivyo? Basi, si vichwa vyote vya huyo hayawani vinavyodhibiti pamoja mamlaka kuu. Kila kimoja katika zamu yacho kimepiga ubwana juu ya aina ya binadamu, hasa juu ya watu wa Mungu. (Ufunuo 17:10) Hivyo, siku ya Bwana inapoanza, kuna kichwa kimoja tu, kile cha saba, kikitenda kuwa ndicho serikali kubwa ya ulimwengu yenye kutawala. Dharuba ya kifo kwenye kichwa hicho humletea hayawani-mwitu mzima wote taabu kubwa.
14. Ni lini dharuba-kifo ilipopigwa, na ofisa mmoja wa kijeshi alielezaje tokeo layo juu ya hayawani-mwitu wa Shetani?
14 Ni nini iliyokuwa dharuba-kifo? Baadaye, huitwa dharuba-upanga, na upanga ni ufananisho wa vita. Dharuba-kifo hii, iliyopigwa mapema katika siku ya Bwana, lazima ihusiane na vita ya ulimwengu ya kwanza, iliyokumba na ikamkausha hayawani-mwitu wa kisiasa wa Shetani. (Ufunuo 6:4, 8;13:14) Mtunga vitabu Maurice Genevoix, aliyekuwa ofisa wa kijeshi katika vita hiyo, alisema kuihusu hivi: “Kila mmoja anakubali katika kutambua kwamba katika historia ya aina ya binadamu kwa ujumla, tarehe chache zimekuwa na umaana wa Agosti 2, 1914. Kwanza Ulaya na upesi baadaye karibu binadamu wote walijikuta wametumbukia ndani ya tukio lenye kuhofisha. Kawaida, miafaka, sheria za kiadili, misingi yote ilitikisika; kutoka siku moja hadi inayofuata, kila kitu kilitiliwa shaka. Tukio hilo lilipasa kuzidi mabashiri ya kisilika na mataraja ya kiasi pia. Likiwa kubwa mno, lenye machafuko, lenye kutia hofu, lingali laburuta sisi katika njia yalo.”—Maurice Genevoix, mshiriki wa Acadeʹmie Française, aliyenukuliwa katika kitabu Promise of Greatness (1968).
15. Ni jinsi gani kichwa cha saba cha hayawani mwitu kilipokea dharuba-kifo?
15 Vita hiyo ilikuwa msiba mkubwa wa kichwa kikuu cha saba cha hayawani-mwitu. Pamoja na mataifa mengine ya Ulaya, Uingereza ilipoteza vijana wayo kwa hesabu yenye kuumiza sana. Katika pigano moja pekee, lile Pigano la Mto Somme katika 1916, kulikuwa na askari-jeshi 420,000 wa Uingereza waliokufa au kupotea vitani, pamoja na 194,000 wa Ufaransa na 440,000 wa Ujeremani—jumla ya watu zaidi ya 1,000,000 waliokufa au kupotea vitani! Kiuchumi, vilevile, Uingereza—pamoja na sehemu nyingine ya Ulaya—ilivunjwavunjwa. Milki kubwa mno ya Uingereza ilitetereka chini ya hilo pigo na haikupona kikamili kamwe. Kweli kweli, vita hiyo, ikiwa na mataifa mashuhuri 28 ilifanya ulimwengu mzima wote uyumbeyumbe kana kwamba kwa pigo la kifo. Katika Agosti 4, 1979, miaka 65 tu baada ya kufyatuka Vita ya Ulimwengu 1, The Economist, la London, Uingereza lilieleza: “Katika 1914 ulimwengu ulipoteza ushikamano ambao haujaweza kuupata tena tangu hapo.”
16. Wakati wa vita ya ulimwengu ya kwanza, United States ilionyeshaje kwamba ilikuwa sehemu ya serikali kubwa ya ulimwengu ya uwili?
16 Wakati ule ule, ile Vita Kubwa, kama ilivyoitwa wakati huo, ilifungulia njia United States kuibuka waziwazi ikiwa sehemu ya Serikali Kubwa ya Ulimwengu ya Uingereza-Amerika. Katika miaka ya kwanza ya vita hiyo, maoni ya umma yaliondoa United States katika pambano hilo. Lakini kama alivyoandika mwanahistoria Esmé Wingfield-Stratford, hayo “yote yalikuwa swali la kama, katika saa hii ya hatari kubwa mno, Uingereza na United States zingezamisha tofauti zao katika kupata umoja [wao] wenye ushindi na udhamini wa pamoja.” Kama vile matukio yalivyopata kuwa, zilifanya hivyo. Katika 1917 United States ilichanga rasilimali na askari-jeshi ili kusaidia jitihada za Mataifa-Mafungamani yaliyokuwa yakiyumbayumba. Hivyo, kichwa cha saba, kikiunganisha Uingereza na United States, kikatokea kikiwa upande wenye kushinda.
17. Kukawa nini kwa mfumo wa kidunia wa Shetani baada ya vita?
17 Ulimwengu baada ya vita hiyo ulikuwa tofauti sana. Mfumo wa kidunia wa Shetani, ujapokuwa ulikumbwa na pigo la kifo, ulipona na ukawa wenye nguvu zaidi kuliko wakati wowote na hivyo ukasifiwa sana na wanadamu kwa sababu ya nguvu zao za kupona.
18. Inaweza kusemwaje kwamba aina ya binadamu kwa ujumla ‘imefuata hayawani-mwitu kwa kusifu mno’?
18 Mwanahistoria Charles L. Mee, Jr., anaandika: “Anguko la utaratibu wa kale [lililosababishwa na vita ya ulimwengu ya kwanza] lilikuwa utangulizi uliohitajiwa kabisa kwa mtandazo wa kujitawala, ule ukombozi wa mataifa mapya na matabaka, kuachiliwa kwa uhuru na kujitegemea kupya.” Chenye kuongoza katika mwendeleo wa kipindi hiki cha baada ya vita kilikuwa kichwa cha saba cha hayawani-mwitu, kikiwa sasa kimepona, na United States ya Amerika ikichukua daraka kuu. Hiyo serikali kubwa ya ulimwengu ya uwili ilichukua uongozi katika kutetea Ushirika wa Mataifa na Umoja wa Mataifa. Kufikia mwaka wa 2005, nguvu za kisiasa za U.S. zilikuwa zimeongoza mataifa yenye mapendeleo zaidi katika kubuni kiwango cha juu zaidi cha maisha, katika kupigana na magonjwa, na katika kuendeleza tekinolojia. Hata ilikuwa imepeleka watu 12 kwenye mwezi. Basi, si ajabu, kwamba aina ya binadamu kwa ujumla ‘imefuata hayawani-mwitu kwa kusifu mno.’
19. (a) Ni jinsi gani aina ya binadamu imepita kiasi katika kusifu mno hayawani-mwitu? (b) Ni nani aliye na mamlaka isiyopingwa juu ya falme zote za dunia, na sisi tunajuaje? (c) Shetani huwakilishaje mamlaka hiyo kwa hayawani-mwitu, na kukiwa na tokeo gani juu ya halaiki ya watu?
19 Aina ya binadamu imepita kiasi cha kusifu mno huyo hayawani-mwitu, kama Yohana anavyofuata kutaarifu: “Na wao wakaabudu drakoni kwa sababu alimpa mamlaka hayawani-mwitu, na wao wakaabudu hayawani-mwitu kwa maneno haya: ‘Ni nani aliye kama hayawani-mwitu, na ni nani anayeweza kufanya pigano na yeye?’” (Ufunuo 13:4, NW) Yesu alipokuwa hapa duniani, Shetani alidai kuwa na mamlaka juu ya falme zote za dunia. Yesu hakupinga hilo; kwa kweli, yeye alirejeza kwa Shetani kuwa mtawala wa ulimwengu na akakataa kushiriki katika siasa za siku hiyo. Baadaye Yohana aliandikia Wakristo wa kweli hivi: “Sisi twajua kwamba sisi tunatokana na Mungu, lakini ulimwengu kwa ujumla unalala katika nguvu za mwovu.” (1 Yohana 5:19; Luka 4:5-8; Yohana 6:15; 14:30, NW) Shetani huwakilisha mamlaka kwa hayawani-mwitu, naye hufanya hivyo kwa msingi wa utukuzo wa taifa. Hivyo, badala ya kuunganishwa na vifungo vya upendo wa kimungu, aina ya binadamu imegawanywa na kiburi cha kabila, jamii, na taifa. Halaiki kubwa ya watu, kwa kweli, huabudu sehemu ya hayawani-mwitu iliyo na mamlaka katika bara wanamojikuta wakiishi. Hivyo hayawani kwa ujumla hupata kusifiwa na kuabudiwa mno.
20. (a) Ni katika maana gani watu huabudu hayawani-mwitu? (b) Ni kwa nini Wakristo ambao huabudu Yehova Mungu hawashiriki ibada hiyo ya hayawani-mwitu, nao wanafuata kielelezo cha nani?
20 Ibada katika maana gani? Katika maana ya kuweka upendo wa nchi mbele ya upendo wa Mungu. Watu walio wengi wanapenda bara la uzawa wao. Wakiwa wananchi wema, Wakristo wa kweli wanaheshimu pia watawala na mifano ya nchi ambako wao wanakaa, wanatii sheria, na kuchangia kihakika masilahi ya jumuiya yao na majirani wao. (Warumi 13:1-7; 1 Petro 2:13-17) Hata hivyo, wao hawawezi kujitoa kipumbavu kwa ajili ya nchi moja dhidi ya zile nyingine zote. “Nchi yetu, ikosee isikosee” si fundisho la Kikristo. Kwa hiyo Wakristo wanaomwabudu Yehova Mungu hawawezi kushiriki kutoa ibada ya kizalendo yenye kiburi kwa sehemu yoyote ya hayawani-mwitu, kwa kuwa hiyo ingekuwa ni kuabudu drakoni—chimbuko la mamlaka ya huyo hayawani. Wao hawawezi kuuliza kwa kusifu mno: “Ni nani aliye kama hayawani-mwitu?” Badala ya hivyo, wao wanafuata kielelezo cha Mikaeli—jina lake likimaanisha “Ni Nani Aliye Kama Mungu?”—wanapotegemeza enzi kuu ya ulimwengu wote mzima ya Yehova. Kwenye wakati wa Mungu uliowekwa, huyu Mikaeli, Kristo Yesu, atapigana na hayawani-mwitu na kumshinda, hata kama alivyopata ushindi wenye shangwe katika kumfukuza Shetani kutoka mbinguni.—Ufunuo 12:7-9; 19:11, 19-21.
Kupiga Vita Dhidi ya Watakatifu
21. Yohana anaelezaje jinsi Shetani anavyotumia kwa hila huyo hayawani-mwitu?
21 Shetani mjanja alikuwa na mipango ya kutumia hayawani-mwitu kwa makusudi yake mwenyewe. Yohana anaeleza hilo: “Na kinywa kinachosema mambo makubwa na makufuru akapewa [huyo hayawani mwenye vichwa saba], na mamlaka ya kutenda kwa miezi arobaini na miwili akapewa. Na yeye akafungua kinywa chake katika makufuru dhidi ya Mungu, kukufuru jina lake na kao lake, hata wale wanaokaa katika mbingu. Na yeye akapewa ruhusa kupiga vita na wale watakatifu na kuwashinda, na mamlaka akapewa juu ya kila kabila na kikundi cha watu na ulimi na taifa. Na wale wote wanaokaa juu ya dunia wataabudu yeye; hakuna jina la hata mmoja wao limesimama likiwa limeandikwa katika hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo ambaye alichinjwa, kutoka kuasisiwa kwa ulimwengu.”—Ufunuo 13:5-8, NW.
22. (a) Ile miezi 42 inarejezea kipindi gani cha wakati? (b) Wakati wa miezi 42, Wakristo wapakwa-mafuta ‘walishindwaje’?
22 Miezi 42 inayotajwa hapa inaonekana kuwa kipindi kile kile cha miaka mitatu na nusu ambacho katika hicho wale watakatifu wanasumbuliwa na ule upembe uliozuka katika mmoja wa wale hayawani katika unabii wa Danieli. (Danieli 7:23-25; ona pia Ufunuo 11:1-4.) Hivyo, kufikia mwishoni mwa 1914 kuendelea mpaka ndani ya 1918, wakati mataifa yenye kupigana yalipokuwa yakiraruana kihalisi kama hayawani-mwitu, wananchi wa mataifa hayo walibanwa wamwabudu hayawani-mwitu, washiriki dini ya utukuzo wa taifa, hata kuwa tayari kufia nchi yao. Mbano kama huo uliongoza kwenye mateso makali upande wa wengi wa wapakwa-mafuta ambao walihisi kwamba utii wao wa juu zaidi ulikuwa wa Yehova Mungu na Mwana wake, Kristo Yesu. (Matendo 5:29) Majaribu yao yalifikia upeo katika Juni 1918, wakati wao ‘waliposhindwa.’ Katika United States, maofisa mashuhuri na wawakilishi wa Sosaiti ya Mnara wa Mlinzi walitiwa gerezani kimakosa, na kazi ya kuhubiri iliyopangwa kitengenezo ya ndugu zao Wakristo ilizuiwa sana. Akiwa na mamlaka “juu ya kila kabila na kikundi cha watu na ulimi na taifa,” hayawani-mwitu alizuia sana kazi ya Mungu ulimwenguni pote.
23. (a) Ni nini iliyo “hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo”? (b) Ni kwa nini ushindi wowote kwa ajili ya tengenezo lionekanalo la Shetani juu ya “watakatifu” ulikuwa wa bure tu?
23 Huu ulionekana kuwa ushindi kwa Shetani na tengenezo lake. Lakini haungeweza kuwaletea manufaa za muda mrefu, kwa kuwa hakuna mmoja aliye katika tengenezo lionekanalo la Shetani aliyekuwa ameandikisha jina lake katika “hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo.” Kitamathali, hati-kunjo hii ina majina ya wale ambao watatawala na Yesu katika Ufalme wake wa kimbingu. Majina ya kwanza yaliandikwa ndani yayo kwenye Pentekoste 33 W.K. Na katika miaka iliyofuata tangu hapo, majina zaidi na zaidi yameongezwa. Tangu 1918, kutiwa muhuri kwa wabakio wa warithi wa Ufalme 144,000 kumekuwa kukiendelea hadi utimilifu. Karibuni, majina yao wote yataandikwa bila kufutika katika hati-kunjo ya uhai ya Mwana-Kondoo. Kwa habari ya wapinzani ambao huabudu hayawani-mwitu, hakuna mmoja wa hao atakayekuwa na jina lake likiwa limeandikwa katika hati-kunjo hiyo. Kwa hiyo wowote unaoonekana kuwa kama ushindi ambao huenda hawa wakawa nao juu ya “watakatifu” ni wa bure, wa kitambo tu.
24. Yohana anawaomba wale walio na ufahamu wasikie nini, nayo maneno yanayosikiwa humaanisha nini kwa watu wa Mungu?
24 Sasa Yohana anawaomba wale walio na ufahamu wasikilize kwa makini sana: “Ikiwa yeyote ana sikio, acha yeye asikie.” Kisha anazidi kusema: “Ikiwa yeyote akusudiwa utekwa, yeye aenda zake ndani ya utekwa. Ikiwa yeyote ataua kwa upanga, ni lazima yeye auawe kwa upanga. Hapa ndipo humaanisha uvumilivu na imani ya watakatifu.” (Ufunuo 13:9, 10, NW) Yeremia aliandika maneno yanayofanana sana na hayo katika miaka iliyotangulia 607 K.W.K., kuonyesha kwamba hakukuwa na kubadilika kwa hukumu za Yehova kwa jiji lisilo na uaminifu la Yerusalemu. (Yeremia 15:2; ona pia Yeremia 43:11; Zekaria 11:9.) Katika wakati wake wa jaribu kubwa, Yesu alifanya iwe wazi kwamba lazima wafuasi wake wasiache msimamo wao wakati aliposema: “Wote wale ambao huchukua upanga watapotelea mbali kwa upanga.” (Mathayo 26:52, NW) Hali kadhalika, sasa katika siku ya Bwana watu wa Mungu lazima washikilie sana kanuni za Biblia. Hakutakuwa na kuponyoka kwa mwisho kwa wale wasiotubu ambao huabudu hayawani-mwitu. Sisi sote tutahitaji uvumilivu, pamoja na imani isiyotikisika, ili tuokoke minyanyaso na majaribu yaliyoko mbele.—Waebrania 10:37-39; 11:6.
Hayawani-Mwitu Mwenye Pembe Mbili
25. (a) Yohana anaelezaje habari za hayawani-mwitu mwingine ambaye yuaja juu kwenye mandhari ya ulimwengu? (b) Ni nini kinachoonyeshwa na pembe mbili za hayawani-mwitu mpya na kutokea kwake katika dunia?
25 Lakini sasa hayawani-mwitu mwingine yuaja juu kwenye mandhari ya ulimwengu. Yohana aripoti: “Na mimi nikaona hayawani-mwitu mwingine akipanda kutoka katika dunia, na alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akaanza kusema kama drakoni. Na anatumia mamlaka yote ya hayawani-mwitu wa kwanza katika mwono wake. Na hufanya dunia na wale wanaokaa ndani yayo waabudu hayawani-mwitu wa kwanza, ambaye dharuba-kifo yake iliponeshwa. Na yeye hufanya ishara kubwa, hivi kwamba amepaswa hata kufanya moto uje chini duniani kutoka katika mbingu katika mwono wa aina ya binadamu.” (Ufunuo 13:11-13, NW) Hayawani-mwitu huyu ana pembe mbili, kuonyesha ushirika wa serikali mbili za kisiasa. Na anaelezwa kuwa anatoka katika dunia, si kutoka katika bahari. Hivyo, anakuja kutoka mfumo wa mambo wa kidunia wa Shetani ambao tayari umeimarishwa. Ni lazima awe serikali ya ulimwengu, ambayo tayari ipo, inayochukua daraka la maana wakati wa siku ya Bwana.
26. (a) Hayawani-mwitu mwenye pembe mbili ni nini, naye anahusianaje na yule hayawani-mwitu wa awali kabisa? (b) Ni katika maana gani pembe za hayawani-mwitu mwenye pembe mbili ni kama za Mwana-kondoo naye yukoje “kama drakoni” anaposema? (c) Watukuzaji wa taifa wanaabudu nini kikweli, nao utukuzaji wa taifa umefananishwa na nini? (Ona kielezi cha chini.)
26 Anaweza kuwa nini? Ni Serikali ya Uliwengu, Uingereza-Amerika—kile kile kichwa cha saba cha hayawani-mwitu wa kwanza lakini katika daraka la pekee! Kumtenga katika njozi hiyo kuwa hayawani-mwitu tofauti hutusaidia sisi kuona kwa wazi zaidi jinsi anavyotenda kwa kujitegemea juu ya jukwaa la ulimwengu. Huyu hayawani-mwitu wa kitamathali mwenye pembe mbili ni mfanyizo wa serikali mbili za kisiasa zilizoko wakati ule ule mmoja ambazo zinajitegemea, lakini zinashirikiana pamoja. Pembe zake mbili “kama mwana-kondoo” hudokeza kwamba hujifanya kuwa mpole na asiyechokoza, akiwa na namna ya serikali iliyotiwa nuru ambayo ulimwengu wote wapaswa kuiendea. Lakini anasema “kama drakoni” kwa kuwa anatumia mbano na vitisho na jeuri ya moja kwa moja wakati wowote namna yake ya utawala isipokubaliwa. Hakutia moyo watu wanyenyekee Ufalme wa Mungu chini ya utawala wa Mwana-Kondoo wa Mungu bali, badala ya hivyo, ni kwa mapendezi ya Shetani, yule drakoni mkubwa. Ametetea migawanyiko ya utukuzaji wa taifa na chuki ambazo hujumlika kuwa ibada kwa hayawani-mwitu wa kwanza.c
27. (a) Ni mwelekeo gani wa hayawani-mwitu mwenye pembe mbili unaoonyeshwa na uhakika wa kwamba yeye anafanya moto ushuke chini kutoka mbinguni? (b) Watu wengi wanaonaje kifani cha ki-siku-hizi cha huyo hayawani-mwitu mwenye pembe mbili?
27 Huyu hayawani-mwitu mwenye pembe mbili hufanya ishara kubwa, hata kufanya moto ushuke kutoka katika mbingu. (Linga Mathayo 7:21-23.) Hii ishara ya pili hukumbusha sisi juu ya Eliya, nabii wa Mungu wa kale ambaye alijitia katika ushindani na manabii wa Baali. Yeye alipoitisha moto ushuke kutoka katika mbingu kwa kufaulu katika jina la Yehova, ulithibitisha kupita shaka lolote kwamba yeye alikuwa nabii wa kweli na kwamba wale manabii wa Baali walikuwa bandia. (1 Wafalme 18:21-40) Kama hao manabii wa Baali, huyo hayawani-mwitu mwenye pembe mbili huhisi kwamba yeye ana vitambulisho vya kuwa nabii. (Ufunuo 13:14, 15; 19:20) Kwani, yeye hudai kwamba amezima kani za uovu katika vita viwili vya ulimwengu, na alishinda ule unaoitwa eti ukomunisti unaokana kuwako kwa mungu! Kweli kweli, wengi, hukiona kifani cha ki-siku-hizi cha hayawani-mwitu mwenye pembe mbili kuwa mlinda uhuru na kibubujiko cha vitu vizuri vya kimwili.
Mfano wa Hayawani-Mwitu
28. Yohana anaonyeshaje kwamba hayawani-mwitu mwenye pembe mbili si asiye na hatia kama vile pembe zake kama za mwana-kondoo zingeonyesha?
28 Je! huyu hayawani-mwitu mwenye pembe mbili ni asiye na hatia kama vile pembe zake kama za mwana-kondoo zingeonyesha? Yohana huzidi kusema: “Na yeye huongoza vibaya wale ambao hukaa juu ya dunia, kwa sababu ya ishara ambazo yeye alipewa ruhusa kufanya katika mwono wa hayawani-mwitu, huku akiambia wale ambao hukaa juu ya dunia wafanye mfano kwa hayawani-mwitu ambaye alikuwa na dharuba-upanga na hata hivyo akahuika. Na yeye alipewa ruhusa kuupa pumzi huo mfano wa hayawani-mwitu, ili kwamba mfano wa hayawani-mwitu upaswe kunena na kusababisha pia kuuawa kwa wale wote ambao kwa njia yoyote hawangeabudu mfano wa hayawani-mwitu.”—Ufunuo 13:14, 15, NW.
29. (a) Ni nini kusudi la mfano wa hayawani-mwitu, na mfano huo uliundwa lini? (b) Ni kwa nini mfano wa hayawani-mwitu si sanamu tu isiyo na uhai?
29 Huu “mfano wa hayawani-mwitu” ni nini, na kusudi lao ni nini? Kusudi lao ni kuendeleza ibada ya hayawani-mwitu mwenye vichwa saba ambaye huo ni mfano wake na hivyo, kwa kweli, kudumisha kuwako kwa hayawani-mwitu. Huu mfano unaundwa baada ya hayawani-mwitu mwenye vichwa saba kupona dharuba yake ya upanga, yaani, baada ya vita ya ulimwengu ya kwanza. Si sanamu isiyo na uhai, kama ile aliyosimamisha Nebukadreza kwenye nyanda za Dura. (Danieli 3:1) Hayawani-mwitu huvuvia uhai ndani ya mfano huu hivi kwamba mfano unaweza kuishi na kutimiza daraka katika historia ya ulimwengu.
30, 31. (a) Mambo ya hakika ya historia ya ulimwengu yanautambulisha mfano huu kuwa nini? (b) Je! wowote wameuawa kwa kukataa kuabudu mfano huu? Fafanua.
30 Kutimia kwa historia hutambulisha mfano huu kuwa tengenezo lililopendekezwa, lililoendelezwa, na kutegemezwa na Uingereza na United States na hapo kwanza likijulikana kuwa Ushirika wa Mataifa. Baadaye, katika Ufunuo sura ya 17, utatokea chini ya umbo tofauti, lile la hayawani-mwitu anayeishi, anayepumua mwenye rangi-nyekundu-nyangavu mwenye kuwako kwa kujitegemea. Hili baraza la kimataifa ‘hunena,’ katika maana ya kwamba hufanya madai ya kujisifu kuwa ndilo pekee linaloweza kuleta amani na usalama kwa aina ya binadamu. Lakini kwa uhakika kwa mataifa washiriki limekuwa baraza la kubadilishana mashutumu na matukano ya mdomo. Limetoa tisho la kutengwa mbali, au la kifo hai, kwa taifa lolote au kikundi cha watu kisichoinamia mamlaka yalo. Ushirika wa Mataifa ulifukuza mataifa ambayo yalishindwa kufuata mawazo yalo. Kwenye mwanzo wa ile dhiki kubwa, “pembe” za kivita za huu mfano wa hayawani-mwitu zitatimiza daraka lenye kukumba sana.—Ufunuo 7:14; 17:8, 16.
31 Tangu Vita ya Ulimwengu 2, mfano wa hayawani-mwitu—sasa ukidhihirishwa kuwa tengenezo la Umoja wa Mataifa—umekwisha ua kwa njia halisi. Mathalani, katika 1950, jeshi la UM liliingia uwanjani katika vita kati ya Korea Kaskazini na Korea Kusini. Jeshi la UM, pamoja na lile la Korea Kusini, yaliua Wakorea wa Kaskazini na Wachina waliokadiriwa kuwa 1,420,000. Hali kadhalika, kutoka 1960 kufika 1964, majeshi ya Umoja wa Mataifa yalikuwa yakitenda katika Kongo (Kinshasa). Zaidi ya hilo, viongozi wa ulimwengu, kutia na mapapa Paul wa Sita na John Paul wa Pili, wameendelea kuthibitisha kwamba mfano huu ndio tumaini la mwisho na lililo bora kwa ajili ya amani. Aina ya binadamu ikishindwa kuutumikia, wao wanasisitiza, jamii ya kibinadamu itajiangamiza yenyewe. Hivyo kitamathali wao husababisha wauawe wanadamu wote ambao hukataa kufuatana na mfano na kuuabudu.—Kumbukumbu 5:8, 9.
Alama ya Hayawani-Mwitu
32. Yohana anaelezaje jinsi Shetani anavyotumia kwa werevu tengenezo lake lionekanalo ili kusababisha mateso kwa wabakio wa mbegu ya mwanamke wa Mungu?
32 Sasa Yohana anaona jinsi Shetani huongoza kwa werevu sehemu za tengenezo lake lionekanalo ili kusababisha mateso makubwa sana kwa wabakio wa mbegu ya mwanamke wa Mungu. (Mwanzo 3:15) Yeye anarudi kueleza habari za “hayawani-mwitu” mwenyewe: “Na yeye huweka chini ya mshurutisho watu wote, wadogo na wakubwa, na matajiri na maskini, na walio huru na watumwa, kwamba imewapasa wao kuwapa hawa alama katika mkono wao wa kulia au juu ya kipaji cha uso wao, na kwamba yeyote asipate kuweza kununua au kuuza isipokuwa mtu aliye na alama, jina la hayawani-mwitu au nambari ya jina lake. Hapa ndipo hekima inatakwa: Acheni mmoja aliye na elimu akokotoe nambari ya hayawani-mwitu, kwa maana hiyo ni nambari ya binadamu; na nambari yake ni mia sita sitini na sita.”—Ufunuo 13:16-18, NW.
33. (a) Ni nini jina la hayawani-mwitu? (b) Nambari sita inashirikishwa na nini? Fafanua.
33 Huyo hayawani-mwitu ana jina, na jina hilo ni nambari: 666. Sita, ikiwa nambari, inashirikishwa na maadui wa Yehova. Mwanamume Mfilisti Mrefaimu alikuwa wa “kimo kisicho cha kawaida,” na “vidole vyake vya mikono na vidole vya miguu vilikuwa sita-sita.” (1 Nyakati 20:6, NW) Mfalme Nebukadreza aliinua mfano wa dhahabu kyubiti 6 upana na kyubiti 60 urefu wa kwenda juu, ili kuunganisha maofisa wake wa kisiasa katika ibada moja. Wakati watumishi wa Mungu walipokataa kuabudu mfano huo wa dhahabu, mfalme akaamuru watupwe ndani ya tanuri ya moto. (Danieli 3:1-23) Nambari sita inapungukia saba, ambayo inasimamia ukamilifu katika maoni ya Mungu. Kwa hiyo, sita mara tatu huwakilisha utokamilifu mkubwa sana.
34. (a) Ni nini kinachoonyeshwa na uhakika wa kwamba nambari ya hayawani-mwitu “ni nambari ya binadamu”? (b) Ni kwa nini nambari 666 ni jina lenye kufaa mfumo wa kisiasa wa ulimwengu wa Shetani?
34 Jina hutambulisha mtu. Hivyo nambari hii hutambulishaje hayawani huyo? Yohana anasema kwamba ni “nambari ya mwanadamu,” si ya mtu wa roho, hivyo jina hilo husaidia kuthibitisha kwamba huyo hayawani-mwitu ni wa kidunia, kufananisha serikali ya kibinadamu. Kama vile sita hushindwa kufikia saba, ndivyo 666—sita katika kipeo cha tatu—ni jina linalofaa mfumo wa ulimwengu wa kisiasa mkubwa mno ambao hushindwa kwa njia yenye kusikitisha kufikia kiwango cha Mungu cha ukamilifu. Hayawani-mwitu wa kisiasa wa ulimwengu hutawala akiwa na cheo kikuu kwa jina-nambari 666, huku siasa kubwa-kubwa, dini kubwa-kubwa, na biashara kubwa-kubwa zikiendeleza huyo hayawani-mwitu kutenda akiwa mwonezi wa aina ya binadamu na mnyanyasi wa watu wa Mungu.
35. Inamaanisha nini kutiwa alama ya jina la hayawani-mwitu juu ya kipaji cha uso au katika mkono wa kulia?
35 Humaanisha nini kutiwa alama ya jina la hayawani-mwitu juu ya kipaji cha uso au katika mkono wa kulia? Wakati Yehova alipowapa Israeli Sheria, yeye aliwaambia: “Ni lazima nyinyi mtumie maneno yangu haya kwenye moyo wenu na nafsi zenu na kuyafunga hayo kama ishara juu ya mikono yenu, na hayo lazima yatumike kuwa ukanda wa pajini kati ya macho yenu.” (Kumbukumbu 11:18, NW) Hiyo ilimaanisha kwamba ilikuwa sharti Waisraeli waweke daima Sheria hiyo mbele yao, hivi kwamba ikavuta matendo na mawazo yao yote. Wapakwa-mafuta 144,000 wasemwa kuwa wana jina la Baba na la Yesu limeandikwa juu ya vipaji vya nyuso zao. Hilo huwatambulisha kuwa ni wa Yehova Mungu na Yesu Kristo. (Ufunuo 14:1) Katika kuiga, Shetani anatumia alama ya roho waovu ya hayawani-mwitu. Mtu yeyote anayeshughulika na utendaji wa kila siku kama vile kununua na kuuza hubanwa afanye kwa njia ambayo hayawani-mwitu hufanya, kama, mathalani, katika kusherehekea sikukuu. Wao wanatarajiwa kuabudu hayawani-mwitu, wakimruhusu atawale maisha zao, ili kupokea alama yake.
36. Wale wanaokataa kukubali alama ya hayawani-mwitu wamekuwa na matatizo gani?
36 Wale wanaokataa kukubali alama ya hayawani-mwitu wamekuwa na matatizo daima. Mathalani, kuanzia miaka ya 1930, wao walilazimika kupiga mapigano mengi ya mahakamani na kuvumilia kufanyiwa ghasia nyingi za kijeuri na minyanyaso mingine. Katika nchi za watawala wenye kudai utii wote, walitupwa ndani ya kambi za mateso, ambamo wengi walikufa. Tangu vita ya ulimwengu ya pili, vijana wasiohesabika wametaabishwa na vifungo virefu, baadhi yao hata wakateswa na kuuawa, kwa sababu ya kukataa kuacha msimamo wao wa kutokuwamo kwa Kikristo. Katika mabara mengine Wakristo hawawezi kununua au kuuza kihalisi; wengine hawawezi kumiliki mali; wengine wanalalwa kinguvu, wanauawa kimakusudi, au wanafukuzwa kutoka bara la uzawa wao. Kwa sababu gani? Kwa sababu katika dhamiri njema wao wanakataa kununua kadi ya chama cha kisiasa.d—Yohana 17:16.
37, 38. (a) Ni kwa nini ulimwengu ni mahali penye magumu kwa wale wanaokataa kuwa na alama ya hayawani-mwitu? (b) Ni nani wanaoshika ukamilifu, nao wameazimia kufanya nini?
37 Katika maeneo fulani ya dunia, dini imeimarika sana katika maisha ya watu wa jumuiya hivi kwamba yeyote anayechukua msimamo kwa ajili ya ukweli wa Biblia anatengwa mbali na jamaa na marafiki wa zamani. Inataka imani kubwa kuvumilia. (Mathayo 10:36-38; 17:22) Katika ulimwengu ambamo wengi huabudu ukwasi wa kimwili na ambao utovu wa haki unaenea pote, mara nyingi Mkristo wa kweli sharti aitibari Yehova kabisa kabisa kwamba Yeye atamtegemeza katika kufuatia mwendo wa unyofu. (Zaburi 11:7; Waebrania 13:18) Katika ulimwengu wenye kufurika ukosefu wa adili, inataka azimio kubwa ili kubaki safi na mwenye kutakata. Wakristo wanaokuwa wagonjwa mara nyingi hubanwa na madaktari na waaguzi wavunje sheria ya Mungu juu ya utakato wa damu; hata inakuwa lazima wakinze maagizo ya mahakama ambayo hupingana na imani yao. (Matendo 15:28, 29; 1 Petro 4:3, 4) Na katika siku hizi za kupanda kwa ukosefu wa kazi, inazidi kuwa vigumu kwa Mkristo wa kweli kuepuka kazi ambayo ingemaanisha kuvunja ukamilifu wake mbele za Mungu.—Mika 4:3, 5.
38 Ndiyo, ulimwengu ni mahali penye magumu kwa wale ambao hawana alama ya hayawani-mwitu. Ni wonyesho wenye kutokeza wa nguvu za Yehova na baraka kwamba wabakio wa mbegu ya mwanamke, pamoja na zaidi ya milioni sita za umati mkubwa, wanashika ukamilifu ijapokuwa mibano yote ya kuvunja sheria za Mungu. (Ufunuo 7:9) Kwa umoja, kotekote duniani, sisi sote na tuendelee kumtukuza Yehova na njia zake za uadilifu, tukataapo kupokea ile alama ya hayawani-mwitu.—Zaburi 34:1-3.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa habari zaidi, tafadhali ona kurasa 165-179 za kitabu “Sikiliza Unabii wa Danieli!” kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova
b The Interpretation of St. John’s Revelation, cha R. C. H. Lenski, kurasa 390-1.
c Waelezaji wameona kwamba utukuzo wa taifa, kwa kweli, ni dini. Kwa sababu hiyo, watu ambao ni watukuzaji wa taifa kwa kweli wao wanaabudu sehemu ya hayawani-mwitu inayowakilishwa na nchi ambayo katika hiyo wanaishi. Kwa habari ya utukuzaji wa taifa katika United States, sisi tunasoma hivi: “Utukuzaji wa taifa, ukionwa kuwa dini, una mengi yanayohusiana na mifumo mikubwa ya dini za wakati uliopita . . . Mtetea taifa wa kidini wa ki-siku-hizi anaona utegemeo wake ni mungu wake mwenyewe wa kitaifa. Yeye anahisi yuahitaji msaada Wake wenye nguvu. Katika Yeye hutambua mna chimbuko lake mwenyewe la ukamilifu na furaha. Yeye anajitiisha kwake Huyo, kwa maana halisi ya kidini. . . . Taifa linaonwa kuwa la milele, na kifo cha wana walo washikamanifu huongeza tu sifa na utukufu walo usiokufa.”—Carlton J. F. Hayes, kama alivyonukuliwa katika ukurasa 359 wa kitabu What Americans Believe and How They Worship, cha J. Paul Williams.
d Mathalani, ona Watchtower matoleo ya Septemba 1, 1971, ukurasa 520; (Kiswahili) Desemba 15, 1974, kurasa 558, 559; Desemba 1, 1975, kurasa 544, 545; (Kiingereza) Februari 1, 1979, ukurasa 23; Juni 1, 1979, ukurasa 20; Mei 15, 1980, ukurasa 10.
[Picha katika ukurasa wa 195]
Alipewa ruhusa kuupa pumzi mfano wa hayawani-mwitu