Uhuru wa Dini Waungwa Mkono Japani
KWA miaka mingi katika Japani, wanafunzi vijana walio Mashahidi wa Yehova wamekabili tatizo hili: Je, wafuate dhamiri yao iliyozoezwa na Biblia, au wafuate utaratibu wa masomo ya shule unaopinga dhamiri yao. Kwa nini kuna tatizo hilo? Kwa sababu mazoezi ya kupigana ni sehemu ya mtaala wa elimu ya mazoezi ya mwili katika shule zao. Mashahidi vijana walihisi kwamba mazoezi hayo hayakupatana na kanuni za Biblia, kama ile inayopatikana kwenye Isaya sura ya 2, mstari wa 4. Hiyo husomeka hivi: “Nao watafua panga zao ziwe majembe, na mikuki yao iwe miundu; taifa halitainua upanga juu ya taifa lingine, wala hawatajifunza vita tena kamwe.”
Kwa sababu ya kutotaka kujifunza stadi za kupigana, zinazohusisha kumdhuru mtu mwingine, Mashahidi Wakristo vijana waliwaeleza walimu wao kwamba wasingeweza kwa dhamiri safi kushiriki katika hayo mazoezi ya kupigana. Baada ya kujaribu kuwashawishi wanafunzi hao ili wakubali utaratibu wa masomo ya shule, walimu wengi wenye uelewevu walikubali hatimaye kustahi dhamiri za wanafunzi hao na kuandaa utendaji mbalimbali wa badala.
Hata hivyo, walimu fulani wakawa wenye kuathiriwa kihisia-moyo, na shule fulani zikakataa kuwapa Mashahidi vijana vyeti vya kuhitimu vya elimu ya mazoezi ya mwili. Katika 1993, Mashahidi angalau tisa hawakuruhusiwa kuendelea hadi kidato kifuatacho nao wakalazimika ama kukomesha masomo ya shuleni ama kufukuzwa shuleni kwa sababu ya kutokushiriki katika mazoezi ya kupigana.
Kwa wazi, wakati ulikuwa umefika wa kutetea haki ya Wakristo vijana ya kupokea elimu bila kulazimika kupinga dhamiri yao. Wanafunzi watano waliokatazwa kuendelea hadi kidato cha pili kwenye chuo kiitwacho Kobe Municipal Industrial Technical College (kwa ufupi Kobe Tech) waliamua kuchukua hatua ya kisheria.
Ni Jambo Gani Lililohusika?
Katika masika ya 1990 wale wanafunzi watano walipoingia Kobe Tech, waliwaeleza walimu kwamba wasingeweza kushiriki katika mazoezi ya kendo (ustadi wa kutumia upanga wa Kijapani) kwa sababu ya maoni yao yenye kutegemea Biblia. Kitivo cha mazoezi ya mwili kilipinga kwa uthabiti na kikawanyima njia nyingineyo ya badala ya kupata cheti cha kuhitimu cha elimu ya mazoezi ya mwili. Hatimaye, hao wanafunzi walianguka mtihani wa somo la elimu ya mazoezi ya mwili na tokeo likawa kwamba walilazimika kurudia kidato cha kwanza (mwaka wa kwanza wa mtaala wa chuo). Katika Aprili 1991 walitoa shtaka kwenye Mahakama ya Wilaya ya Kobe, wakidai kwamba hatua iliyochukuliwa na hiyo shule ilipinga uhakikishio wa kikatiba wa uhuru wa dini.a
Hiyo shule ilidai kwamba kuandaa utendaji mbalimbali wa badala kungekuwa sawa na kuonyesha upendeleo kwa dini hususa na hivyo kungekuwa ni kuonyesha ubaguzi shuleni. Isitoshe, ilidai kwamba haikuwa na vifaa wala walimu wa kuandaa programu ya badala ya elimu ya mazoezi ya mwili.
Uamuzi wa Mahakama ya Wilaya Wachochea Wale Wenye Kujua juu Yao
Kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea, wawili miongoni mwa wale wanafunzi watano walianguka tena maksi za kupita za elimu ya mazoezi ya mwili, huku watatu wengineo walipita maksi hizi kidogo tu wakaweza kuendelea hadi kidato kifuatacho. Kanuni za shule zilitaarifu kwamba wanafunzi ambao maksi zao shuleni zilikuwa mbaya na waliorudia kidato kilekile kwa miaka yoyote miwili yenye kufuatana wangeweza kufukuzwa shuleni. Kwa sababu hiyo, mmoja wa wale wanafunzi wawili akaamua kukomesha masomo ya shuleni kabla ya kufukuzwa shuleni, lakini yule mwingine, Kunihito Kobayashi, alikataa kukomesha masomo. Kwa hiyo alifukuzwa shuleni. Kwa kupendeza, wastani wa Kunihito wa masomo yote kutia ndani elimu ya mazoezi ya mwili, aliyoanguka akiwa na maksi 48, ulikuwa maksi 90.2 kati ya 100. Alikuwa wa kwanza katika darasa lake lenye wanafunzi 42.
Katika Februari 22, 1993, Mahakama ya Wilaya ya Kobe ilitoa hukumu kwa kuunga mkono Kobe Tech ikasema hivi: “Hatua zilizochukuliwa na shule hazikuipinga katiba,” ingawa ilikiri kwamba “haiwezi kukanushwa kwamba uhuru wa ibada wa washtaki ulikuwa umezuiwa kwa njia fulani na takwa la shule la kushiriki katika mazoezi ya kendo.”
Sawa na mtume Paulo katika karne ya kwanza, washtaki waliamua kukata rufani kwa mamlaka za kisheria za juu zaidi. (Matendo 25:11, 12) Hiyo kesi ikaenda hadi Mahakama ya Juu ya Osaka.
Mtazamo Usio na Ubinafsi wa Washtaki
Msomi maarufu, Profesa Tetsuo Shimomura wa Chuo Kikuu cha Tsukuba, alikubali kutoa ushuhuda akiwa shahidi mstadi katika Mahakama ya Juu ya Osaka. Akiwa mwenye ustadi katika elimu na sheria, alikazia jinsi hatua za shule zilivyokosa ufikirio katika kushughulikia hao wanafunzi. Kunihito Kobayashi aliieleza mahakama hisia zake, na mtazamo wake wenye moyo mweupe ulisukuma mioyo ya wale waliokuwamo mahakamani. Zaidi ya hayo, katika Februari 22, 1994, shirika liitwalo Kobe Bar Association, likitangaza kwamba hatua za hiyo shule ziliingilia uhuru wa ibada wa Kunihito na haki yake ya kupokea elimu, lilipendekeza kwamba shule imrudishe masomoni.
Wakati ulipokuwa ukikaribia wa kutolewa kwa uamuzi kwenye Mahakama ya Juu ya Osaka, Wakristo wote vijana waliohusika walikuwa na hamu ya kushiriki katika mng’ang’ano huo mpaka mwisho wao. Walihisi kwamba walikuwa wakipigana vita ya kisheria kwa niaba ya maelfu ya Mashahidi vijana ambao hukabili suala lilo hilo katika shule kotekote Japani. Lakini kwa kuwa hawakufukuzwa kutoka hiyo shule, iliwezekana sana kwamba mahakama isingesikiza kesi yao. Nao waliweza kuona kwamba ikiwa wangetangua majiteteo yao, hali ya kutokubali sababu ya hiyo shule katika kumfukuza Kunihito ingekaziwa. Hivyo, wanafunzi wote wakaamua kukomesha kesi hiyo isipokuwa Kunihito.
Katika Desemba 22, 1994, Hakimu Mkuu Reisuke Shimada wa Mahakama ya Juu ya Osaka alitoa uamuzi uliotangua hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Kobe. Mahakama ilipata kwamba sababu iliyomfanya Kunihito akatae mazoezi ya kendo ilikuwa ya moyo mweupe na kwamba hasara aliyopata kwa sababu ya hatua yake iliyotegemea itikadi yake ya kidini ilikuwa kubwa mno. Hiyo shule, akasema Hakimu Mkuu Shimada, ingalipaswa kuandaa utendaji mbalimbali wa badala. Uamuzi huo mzuri ulipokewa vizuri na wale waliohangaikia haki za kibinadamu. Hata hivyo, hiyo shule, ilikata rufani kwa Mahakama ya Juu Zaidi ya Japani, ikimnyima Kunihito elimu kwa zaidi ya mwaka mwingine mmoja.
Hadi Mahakama ya Juu Zaidi
Safu ya mhariri katika gazeti la habari la Kobe Shimbun ilitaarifu hivi baadaye: “Baraza la Shule la Jiji la Kobe na hiyo shule ingalipaswa kukubali kumrudisha Bw. Kobayashi shuleni wakati huo [baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Osaka]. . . . Mtazamo wao wa kutaka makabiliano isivyo lazima umemnyima mtu kipindi cha maana cha ujana wake.” Hata hivyo, Kobe Tech ilichukua msimamo thabiti katika kesi hiyo. Likiwa tokeo, habari hiyo ikawa jambo la kuzungumziwa katika ripoti za habari za taifa lote. Walimu na wenye mamlaka wa shule kotekote nchini walikazia habari hiyo uangalifu wao, na uamuzi kutoka katika mahakama ya juu zaidi katika hiyo nchi ungekuwa mfano wenye nguvu zaidi wa kufuatwa katika kesi kama hizo wakati ujao.
Katika Januari 17, 1995, karibu juma moja baada ya shule kukata rufani kwa Mahakama ya Juu Zaidi, tetemeko la dunia la Kobe lilipiga Jiji la Ashiya alikoishi Kunihito na familia yake. Karibu saa kumi na moja u nusu alfajiri hiyo, dakika chache kabla ya tetemeko kupiga hilo eneo, Kunihito aliondoka nyumbani mwake kwenda kwenye kazi yake isiyo ya wakati wote. Alikuwa akiendesha baiskeli kwenye barabara iliyo chini ya Barabara Kuu ya Hanshin ipitayo juu, na tetemeko lilipopiga, alikuwa akikaribia tu ile sehemu iliyoporomoka. Mara hiyo hiyo alirudi nyumbani akapata orofa ya kwanza ya nyumba yake ikiwa imeporomoka kabisa. Kunihito akaona kwamba angalipoteza uhai wake kwa urahisi katika hilo tetemeko naye akamshukuru Yehova kwa kumruhusu asalimike. Ikiwa angalikufa, yamkini kwamba ile kesi ya kendo ingaliisha bila uamuzi wa Mahakama ya Juu Zaidi.
Kwa kawaida Mahakama ya Juu Zaidi katika Japani huchunguza rufani zilizoandikwa tu na huamua kama maamuzi ya mahakama za chini yalikuwa sahihi au la. Isipokuwa kama kuna sababu nzito ya kutangua uamuzi wa mahakama ya chini, kesi huwa haisikilizwi. Hiyo mahakama haijulishi washtaki wala washtakiwa ni lini uamuzi utakapotolewa. Kwa hiyo Kunihito alishangaa asubuhi ya Machi 8, 1996, alipoambiwa kwamba uamuzi utatolewa asubuhi hiyo. Kwa shangwe na furaha yake, alipata kujua kwamba Mahakama ya Juu Zaidi ilikuwa imeunga mkono uamuzi wa Mahakama ya Juu ya Osaka.
Mahakimu wanne, pamoja na Hakimu Shinichi Kawai akisimamia, walitoa hukumu kwa umoja kwamba “matendo yaliyohusika yalipasa kuonwa kuwa yasiyofaa kabisa kulingana na desturi za kijamii zinazokubalika, yenye kupita mipaka ya haki, na kwa hiyo kutokuwa halali.” Mahakama ilitambua weupe wa moyo wa kukataa kwa Kunihito kufanya mazoezi ya kendo ikasema hivi: “Sababu iliyomfanya mtu huyo ambaye dhidi yake rufani ilikatwa akatae kushiriki katika mazoezi ya kendo ilikuwa yenye bidii na ilihusiana kwa ukaribu na msingi hasa wa imani yake.” Mahakama ya Juu Zaidi ilitoa hukumu kwamba shule ingaliweza na ingalipaswa kuandaa njia ya badala ili itikadi ya kidini ya mtu huyo ambaye dhidi yake rufani ilikatwa iweze kustahiwa.
Tokeo Lenye Kuhusisha Mengi
Bila shaka uamuzi huo utaweka mfano mzuri wenye kuunga mkono uhuru wa ibada katika shule. Gazeti The Japan Times lilisema hivi: “Hiyo hukumu ni ya kwanza ya Mahakama ya Juu Zaidi juu ya suala la elimu na uhuru wa dini.” Hata hivyo, huo uamuzi hauondoi daraka la kila mwanafunzi kijana la kuchukua msimamo wake mwenyewe wa kufuata dhamiri anapokabili majaribu ya imani.
Profesa Masayuki Uchino wa Chuo Kikuu cha Tsukuba alieleza kwamba mojawapo mambo yaliyowasukuma mahakimu wampe Kunihito ushindi ni kwamba “alikuwa mwanafunzi mwenye moyo mweupe ambaye maksi zake za kielimu zilikuwa zenye kutokeza.” Biblia hutoa shauri hili kwa Wakristo wakabilio majaribu ya imani yao: “Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.” (1 Petro 2:12) Wakristo vijana waaminifu waweza kuonyesha kwamba msimamo wao wa Kibiblia unastahili kustahiwa na watu kwa kuishi maisha yao yote kulingana na viwango vya Biblia.
Baada ya uamuzi wa Mahakama ya Juu Zaidi, Kunihito Kobayashi alirudishwa tena kwenye Kobe Tech. Walio wengi wa wanafunzi walioingia shule hiyo pamoja na Kunihito walikuwa wamehitimu tayari. Sasa Kunihito anajifunza na wanafunzi walio wadogo wake kwa miaka mitano. Machoni pa watu wengi wa ulimwengu, yaonekana kama miaka mitano yenye thamani ya ujana wake imepotezwa. Hata hivyo, uaminifu-maadili wa Kunihito ni wenye thamani machoni pa Yehova Mungu, na kwa hakika dhabihu aliyotoa si ya bure.
[Maelezo ya Chini]
a Ili kupata habari zaidi, tafadhali ona ukurasa wa 10 hadi 14 wa toleo la Amkeni! la Oktoba 8, 1995, lililochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 20]
Kushoto: Nyumba ya Kunihito baada ya tetemeko la dunia
Chini: Kunihito leo