“Katika Msafara wa Ushindi”
MSAFARA wa ushindi ulikuwa mwadhimisho wa kutazamisha wa ushindi juu ya adui. Moja ya heshima za juu zaidi ambazo Baraza Kuu la Serikali ya Kiroma liliweka juu ya jemadari mshindi ilikuwa kumruhusu aadhimishe ushindi wake kwa msafara huo rasmi, wenye gharama kubwa. Mtume Paulo alitaja msafara huo wa ushindi mara mbili katika miandiko yake. Hata hivyo, kabla hatujafikiria maneno yake jaribu kuwaza kuwa wauona msafara huo. Wazia umati wa watu wakijipanga kwenye barabara mbalimbali wakati usongapo polepole kuifuata Via Triumphalis na kuinuka juu kwenye ule mpando wenye kupindapinda hadi kwenye hekalu la Jupiter juu ya Kilima Capitoline cha Roma.
“Harufu zenye manukato kutokana na kuchoma vikolezo zilitawanywa sana katika mahekalu na kandokando za barabara, zikijaza hewa manukato yazo,” akaandika mwanachuo James M. Freeman. “Katika msafara huo lilikuwamo baraza kuu na raia wakuu wa serikali, ambao kwa kuwapo kwao hivyo waliheshimu mshindi huyo. Nyara za vita zilizo bora zaidi, kama vile dhahabu, fedha, silaha za kila namna, beramu, kazi za sanaa zilizo shida kupatikana na ghali, na kila kitu kilichoonwa kuwa chenye kuthaminika sana na mshindi ama washindwa, zilibebwa kwa kuonekana peupe na jiji lenye kusongamana watu. Wafungwa wa vita walishurutishwa pia kupiga miguu katika msafara huo. Yule jemadari, ambaye katika heshima yake ushindi uliadhimishwa, aliendeshwa katika gari-vita lenye umbo la kipekee na kuvutwa na farasi wanne. Joho lake lilirembwa kwa dhahabu, na koti lake kwa maua. Katika mkono wake wa kulia mlikuwa na tawi la loreli (majani yenye ubichi), na katika mkono wake wa kushoto fimbo ya kifalme; hali katika kipaji chake cha uso kulikuwa na shada ya loreli ya Delfiki. Kati ya kelele za askari na makofi ya halaiki, mshindi huyo alibebwa kwa kupitishwa katika barabara za hekalu la Jupiter ambako dhabihu zilitolewa, na baada ya hayo kukawa na karamu ya watu wote katika hekalu.”
Paulo alitumia huo msafara wa ushindi kwa njia ya kielezi alipoandika barua yake ya pili kwa Wakristo katika Korintho katika mwaka 55 wa Wakati wa Kawaida wetu. Alisema hivi: “Shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo [kwa kuandamana pamoja na Kristo, NW]. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali. Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea. Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo [harufu inayotoka kwenye kifo hadi kwenye kifo, NW]; lakini kwa wale wanaookolewa harufu hiyo ni uhai [harufu inayotoka kwenye uhai hadi kwenye uhai, NW].”—2 Wakorintho 2:14-16, HNWW.
Hapa Paulo na Wakristo wengine wapakwa-mafuta wawakilishwa kuwa raia za Mungu wenye kujitoa, “kwa kuandamana pamoja na Kristo.” Wao waonyeshwa kuwa wana, maofisa, na askari wenye kufuata katika mlolongo wa Yehova na kuongozwa naye katika msafara wa ushindi kwa kufuata njia iliyotiliwa manukato. (Ona Mnara wa Mlinzi, Julai 15, 1990, kurasa 10-15.) Utumizi huu wenye kielezi cha msafara wa jinsi hiyo waonyesha pia kwamba wale ambao wazikataa habari njema za Ufalme wa Mungu wana tazamio la kifo tu. Lakini jinsi ilivyo tofauti kwa wafuasi wapakwa-mafuta wa Yesu! Wao wana tumaini la kupata wokovu kwenye uhai wa kimbingu pamoja na Kristo. Namna gani waandamani wao wenye uaminifu-mshikamanifu, ambao pia wamejiweka wakfu kwa Mungu? Wao wana lile tumaini lenye shangwe la kupata uhai katika paradiso ya kidunia, ambamo Mungu “atafuta kila chozi katika macho yao, wala mauti haitakuwapo tena; wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu hayatakuwapo tena.” (Ufunuo 21:1-4, UV; Luka 23:43, ZSB) Je! wewe ni sehemu ya songamano hilo lenye furaha?
Picha tofauti yatokezwa kwenye Wakolosai 2:15, NW, ambapo Paulo aliandika hivi: “Akivua serikali na mamlaka ziwe uchi, [Mungu] alizionyesha wazi kwa watu wote kuwa zimeshindwa, akiziongoza katika msafara wenye shangwe ya ushindi kwa njia ya huo.” Hapa serikali na mamlaka adui zilizo chini ya Shetani Ibilisi zaonyeshwa kuwa ni mateka na wafungwa-gereza walio katika msafara wenye shangwe ya ushindi. Yehova Mshindi azivua ziwe uchi na huzionyesha kwa wazi kwamba zimeshindwa. Hizo zashindwa “kwa njia ya huo,” yaani, “mti wa mateso” wa Yesu. Kifo chake juu ya mti kiliandaa msingi wa kuondoa ile “hati iliyoandikwa kwa mkono” (agano la Sheria) na kufanya iwezekane Wakristo kuwekwa huru na utumwa kwa mamlaka za kishetani zenye giza. (Wakolosai 2:13, 14) Jinsi twapaswa kuthamini uhuru huo wa Kikristo!