Swali la 4
Je, Uhai Wote Umetokana na Chanzo Kimoja?
Darwin alifikiri kwamba huenda uhai wote ulitokana na chanzo kimoja. Aliwazia kwamba historia ya uhai duniani inafanana na mti mkubwa. Baadaye, watu fulani waliamini kwamba huo “mti wa uhai” ulianza ukiwa shina moja lenye chembe sahili za kwanza. Spishi mpya zikachipuka kutoka katika shina na kuendelea kujigawanya kuwa viungo, au jamii za mimea na wanyama, na kisha machipukizi, yaani, spishi zote zilizopo leo katika jamii za mimea na wanyama. Kweli hivyo ndivyo ilivyokuwa?
Wanasayansi wengi husema nini? Wengi huhisi kwamba rekodi ya visukuku huunga mkono nadharia ya kuwapo kwa chanzo kimoja cha uhai. Pia, wanadai kwamba kwa kuwa vitu vyote vilivyo hai vinatumia “lugha ileile ya kompyuta,” au DNA, basi lazima uhai ulitokana na chanzo kimoja.
Biblia inasema nini? Masimulizi ya kitabu cha Mwanzo yanasema kwamba mimea, viumbe vya baharini, wanyama wa nchi kavu, na ndege viliumbwa “kulingana na aina yake.” (Mwanzo 1:12, 20-25) Masimulizi hayo yanaonyesha kwamba kuna unamna-namna katika “aina,” hata hivyo, yanamaanisha kwamba aina hizo mbalimbali zinatofautiana kabisa. Pia, masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji hutufanya tutazamie kwamba aina mpya za viumbe zingetokea ghafula katika rekodi ya visukuku zikiwa kamili.
Uthibitisho unafunua nini? Je, uthibitisho huo unaunga mkono masimulizi ya Biblia au Darwin alikuwa sahihi? Mavumbuzi ya miaka zaidi ya 150 iliyopita yamefunua nini?
MTI WA DARWIN WAKATWA
Katika miaka ya karibuni, wanasayansi wamefaulu kulinganisha chembe za urithi za viumbe mbalimbali wenye chembe moja na vilevile za mimea na wanyama. Waliamini kwamba kwa kufanya hivyo wanaweza kuthibitisha ule “mti wa uhai” wenye kutoa matawi uliopendekezwa na Darwin. Lakini, haijawa hivyo.
Utafiti umefunua nini? Mnamo 1999 mwanabiolojia Malcolm S. Gordon aliandika: “Inaonekana uhai ulikuwa na vyanzo vingi. Inaonekana chini ya ule mti wa uhai kulikuwa na mizizi mingi.” Kuna uthibitisho wowote kwamba yale matawi makuu ya uhai yanatoka katika shina moja, kama Darwin alivyoamini? Gordon aendelea: “Yaelekea ufafanuzi wa awali wa nadharia ya chanzo kimoja cha uhai haihusu himaya kama zinavyotambuliwa leo. Huenda nadharia hiyo haihusu faila zote, na huenda pia haihusu matabaka ndani ya faila.”29a
Utafiti wa karibuni unaendelea kupinga nadharia ya Darwin ya kuwapo kwa chanzo kimoja cha uhai. Kwa mfano, mwaka wa 2009, makala katika gazeti New Scientist ilimnukuu mwanasayansi wa mageuzi Eric Bapteste akisema: “Hatuna uthibitisho wowote kuonyesha kwamba mti wa uhai ni hakika.”30 Makala hiyohiyo inamnukuu mwanabiolojia wa mageuzi Michael Rose akisema: “Mti wa uhai unaendelea kuzikwa taratibu, sote twajua hilo. Kile tusichokubali hasa ni wazo la kwamba tunahitaji kubadili maoni yetu yote kuhusu biolojia.”31b
NAMNA GANI REKODI YA VISUKUKU?
Wanasayansi wengi huona rekodi ya visukuku kuwa inaunga mkono dhana ya kwamba uhai ulitokana na chanzo kimoja. Kwa mfano, wao hudai kwamba rekodi ya visukuku huonyesha kwamba samaki waligeuka na kuwa amfibia na reptilia wakawa mamalia. Hata hivyo, visukuku huthibitisha nini hasa?
Mwanamageuzi ambaye pia ni mtaalamu wa visukuku, David M. Raup anasema: “Badala ya kuchunguza jinsi uhai ulivyotokea hatua kwa hatua, kile ambacho wanajiolojia wa siku za Darwin na wa leo wanapata ni rekodi isiyolingana au isiyo na mpangilio; kwamba spishi zinaonekana ghafula kwa mfuatano, zinakuwa na mabadiliko madogo au hata bila mabadiliko yoyote, kisha zinatoweka ghafula kutoka katika rekodi.”32
Kusema kweli, visukuku vingi huonyesha kwamba aina tofauti-tofauti za viumbe hazijabadilika hata baada ya muda mrefu sana. Uthibitisho hauonyeshi vikigeuka kutoka kwa aina moja hadi nyingine. Maumbo ya kipekee hutokea ghafula. Sehemu mpya hutokea ghafula. Kwa mfano, popo wenye mfumo wa sona ambao wana uwezo wa kugundua mahali kitu fulani kinapatikana kwa kutumia mawimbi ya sauti, hawana uhusiano ulio wazi na popo wa kale.
Inaonekana zaidi ya nusu ya vikundi vyote vikuu vya wanyama vilitokea kwa muda mfupi wa wakati. Kwa kuwa aina nyingi mpya za uhai zinazotofautiana sana zinatokea ghafula kwenye rekodi ya visukuku, wataalamu wa visukuku hukiita kipindi hicho “mlipuko wa Cambria.” Huo ulikuwa wakati gani?
Tuchukulie kwamba makadirio ya watafiti ni sahihi. Hivyo basi, historia ya dunia inaweza kuwakilishwa na matukio yaliyotokea kwa kipindi cha wakati kinachoweza kunyooshwa na kutoshana na uwanja wa mpira wa kandanda (1). Kwa kipimo hicho, utahitaji kutembea asilimia 88 ya uwanja huo kabla ya kufikia kile ambacho wataalamu wa visukuku wanakiita kipindi cha Cambria (2). Katika muda mfupi wa kipindi hicho, vikundi vikubwa vya wanyama vinaonekana katika rekodi ya visukuku. Vinatokea ghafula kadiri gani? Unapoendelea kutembea kwenye uwanja huo, viumbe vyote hivyo tofauti-tofauti vinatokea upesi kwa muda unaopungua hatua moja!
Kutokea ghafula kwa aina hizo tofauti-tofauti za uhai kumefanya watafiti fulani wa nadharia ya mageuzi kutilia shaka masimulizi ya jadi ya nadharia ya Darwin. Kwa mfano, kwenye mahojiano ya mwaka 2008, mwanamageuzi, Stuart Newman, alizungumzia uhitaji wa kuwa na nadharia nyingine ya mageuzi inayoweza kufafanua kutokea ghafula kwa aina mpya mbalimbali za uhai. Alisema: “Nadharia ya Darwin iliyokuwa ikifafanua mabadiliko yote ya mageuzi itashushwa, iwe tu kama mojawapo ya nadharia nyingi—huenda hata isiyo muhimu sana inapohusu kuelewa mageuzi makubwa, mageuzi ya mabadiliko makubwa katika maumbo ya mwili.”33
MATATIZO YA “UTHIBITISHO”
Hata hivyo, namna gani visukuku vinavyotumiwa kuonyesha samaki wakibadilika kuwa amfibia, na reptilia kuwa mamalia? Je, vinaandaa uthibitisho thabiti kuhusu hatua za mageuzi? Rekodi ya visukuku inapochunguzwa kwa makini, matatizo mengi huwa wazi.
Kwanza, nyakati nyingine ukubwa wa viumbe katika mfuatano wa mabadiliko kutoka reptilia-hadi-mamalia hupotoshwa katika vitabu. Badala ya kuwa sawa kwa ukubwa, viumbe fulani katika mfuatano huwa vikubwa, huku vingine vikiwa vidogo.
Pili, tatizo kubwa hata zaidi ni ukosefu wa uthibitisho unaoonyesha kwamba viumbe hao wanahusiana kwa njia fulani. Kulingana na makadirio ya watafiti, mara nyingi wanyama walio kwenye mfuatano hutenganishwa na mamilioni ya miaka. Kuhusiana na wakati unaotenganisha visukuku hivyo, mwanazuolojia Henry Gee anasema: “Muda unaotenganisha visukuku ni mrefu sana hivi kwamba hatuwezi kusema kwa uhakika ikiwa vinahusiana kupitia nasaba na ukoo.”34c
Akizungumzia visukuku vya samaki na amfibia, mwanabiolojia Malcolm S. Gordon, anasema kwamba visukuku vilivyopatikana vinawakilisha sehemu ndogo tu “huenda isiyowakilisha kabisa aina mbalimbali ya mimea na wanyama waliokuwako katika vikundi hivyo wakati huo.” Anaendelea kusema: “Hatuwezi kujua ni kwa kiasi gani viumbe hao walihusika katika ukuzi wa baadaye, au jinsi walivyohusiana.”35d
“FILAMU” INAONYESHA NINI HASA?
Makala iliyochapishwa mwaka wa 2004 katika jarida la National Geographic lilifananisha rekodi ya visukuku na “filamu ya mageuzi ambayo kati ya kila picha 1,000, imepoteza picha 999 katika chumba cha kuhariri.”36 Fikiria matokeo ya mfano huo.
Wazia umepata picha 100 ya filamu ambayo mwanzoni ilikuwa na picha 100,000. Utajuaje mfuatano wa matukio katika filamu hiyo? Huenda ukawa na maoni fulani, lakini namna gani ikiwa ni 5 tu kati ya zile picha 100 ulizopata zinazoweza kupangwa ili kuunga mkono hadithi unayopendelea, huku zile nyingine 95 zikiwa na hadithi tofauti? Lingekuwa jambo la hekima kudai kwamba maoni yako kuhusu filamu hiyo ni sahihi kwa sababu tu ya hizo picha tano? Inawezekana kwamba uliweka picha hizo tano kwa mpangilio ambao unapatana na maoni yako? Je, halingekuwa jambo la busara kuacha zile picha nyingine 95 zikusaidie kuwa na maoni yanayofaa?
Ni kwa njia gani mfano huo unatusaidia kuelewa jinsi wanamageuzi wanavyoiona rekodi ya visukuku? Kwa miaka mingi, watafiti hawakukubali kwamba visukuku vingi—zile picha 95 za filamu—vilionyesha kwamba spishi hubadilika kidogo sana baada ya muda. Kwa nini hawasemi lolote kuhusu uthibitisho huo muhimu? Mwandikaji Richard Morris anasema: “Yaelekea wataalamu wa visukuku walianza kushikilia maoni yaliyokubaliwa na wengi kwamba kulikuwa na mabadiliko ya hatua kwa hatua katika mageuzi, hata baada ya kupata uthibitisho unaokanusha jambo hilo. Wamekuwa wakijaribu kufafanua uthibitisho wa visukuku kulingana na maoni yanayokubaliwa kuhusu mageuzi.”37
Namna gani wanamageuzi leo? Inawezekana kwamba wanapanga visukuku katika mpangilio fulani, si kwa sababu mfuatano huo unaungwa mkono na visukuku vingi na uthibitisho wa kinasaba, bali kwa sababu kufanya hivyo kunapatana na maoni yanayokubaliwa leo kuhusu mageuzi?e
Una maoni gani? Ni kauli gani inayopatana kabisa na uthibitisho? Fikiria ukweli wa mambo ambao tumezungumzia kufikia sasa.
◼ Uhai wa kwanza duniani haukuwa “duni.”
◼ Uwezekano wa hata visehemu vya chembe kujitokeza vyenyewe ni mdogo sana.
◼ DNA, “programu ya kompyuta,” au mfumo, huendesha chembe, nayo ni tata sana na ina uwezo wa hali ya juu sana kupita programu au mfumo wowote wa kuhifadhi habari ambao umewahi kutengenezwa na mwanadamu.
◼ Utafiti wa kinasaba umeonyesha kwamba uhai haukutokana na chanzo kimoja. Isitoshe, vikundi vikubwa vya wanyama huonekana ghafula katika rekodi ya visukuku.
Baada ya kuchunguza ukweli huo, je, unafikiri inafaa kukata kauli kwamba uthibitisho huo unapatana na masimulizi ya Biblia kuhusu chanzo cha uhai? Hata hivyo, watu wengi hudai kwamba sayansi hupinga mambo mengi ambayo Biblia husema kuhusu uumbaji. Je, ni kweli? Biblia husema nini hasa?
[Maelezo ya Chini]
a Neno la kibiolojia faila linarejelea kikundi kikubwa cha wanyama wenye sifa zinazofanana. Njia moja ambayo wanasayansi huainisha vitu vyote vilivyo hai ni kwa kutumia mfumo wa hatua saba, ambapo kila hatua iko wazi zaidi kuliko ile inayoitangulia. Hatua ya kwanza ni himaya, ambayo ndiyo kikundi kikubwa zaidi. Kisha faila, tabaka, oda, jamii, jenasi, na spishi. Kwa mfano, farasi ameainishwa kwa njia ifuatayo: himaya, Animalia; faila, Kodata; tabaka, Mamalia; oda, Perissodactyla; jamii, Equidae; jenasi, Equus; spishi, Caballus.
b Kumbuka kwamba wala makala ya gazeti la New Scientist, wala maoni ya Bapteste, wala ya Rose, hayadokezi kwamba nadharia ya mageuzi si ya kweli. Badala yake, wanachosema ni kwamba ule mti wa uhai wa Darwin ambao ndiyo msingi wa nadharia yake, haungwi mkono na uthibitisho. Wanasayansi kama hao bado wanatafuta njia nyingine ya kufafanua nadharia ya mageuzi.
c Henry Gee hadokezi kwamba nadharia ya mageuzi si ya kweli. Maelezo yake yamekusudiwa kuonyesha kwamba watu hawawezi kujifunza mengi kutokana na visukuku.
d Malcom S. Gordon anaunga mkono fundisho la mageuzi.
e Kwa mfano, ona sanduku “Namna Gani Mageuzi ya Mwanadamu?”
[Blabu katika ukurasa wa 25]
“Kuchukua visukuku kadhaa na kudai kwamba vinawakilisha nasaba fulani si maoni ya sayansi yanayoweza kuthibitishwa, balini dai linaloweza kulinganishwa na hadithi zinazosimuliwa kabla ya kulala—zinazosisimua, huenda hata zenye mafunzo, lakini zisizo za kisayansi.”—In Search of Deep Time—Beyond the Fossil Record to a New History of Life, cha Henry Gee, uku. 116-117
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
UKWELI WA MAMBO NA MASWALI
◼ Ukweli wa mambo: Dhana mbili za msingi za fundisho la mageuzi—kwamba uhai unatokana na chanzo kimoja na kwamba maumbo mapya kabisa yanatokana na mrundamano wa mabadiliko madogo—zimekuwa zikipingwa na watafiti ambao hawaungi mkono masimulizi ya Biblia kuhusu uumbaji.
Swali: Kwa kuwa kuna ubishi juu ya dhana hizo za Darwin, je, kweli ufafanuzi wake kuhusu mageuzi unaweza kuthibitishwa kuwa sahihi kisayansi?
◼ Ukweli wa mambo: Viumbe vyote vilivyo hai vina DNA zinazofanana, ile “lugha ya kompyuta” au mfumo unaoongoza umbo na utendaji wa chembe.
Swali: Je, kufanana huko hakuwezi kuwa si kwa sababu vinatokana na mzazi mmoja, bali kwa sababu vina Mbuni mmoja?
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 27-29]
Namna Gani Mageuzi ya Mwanadamu?
Angalia mada za mageuzi ya mwanadamu kwenye vitabu vingi na ensaiklopedia, utaona mfuatano wa picha— upande mmoja utaona kiumbe aliyeinama anayefanana na sokwe akifuatwa na viumbe wanaoanza kuwa wima hatua kwa hatua na walio na vichwa vikubwa. Mwishoni kabisa utamwona mwanadamu jinsi alivyo leo. Taswira hizo pamoja na ripoti motomoto za ugunduzi wa vile vinavyoitwa eti visukuku vilivyokuwa vikikosekana, hufanya ionekane kana kwamba kuna uthibitisho wa kutosha kwamba mwanadamu alitokana na sokwe. Je, madai hayo yanategemea uthibitisho thabiti? Fikiria mambo ambayo watafiti wa mageuzi husema kuhusu habari zifuatazo.f
KILE KINACHOTHIBITISHWA HASA NA VISUKUKU
◼ Ukweli wa mambo: Mwanzoni mwa karne ya 20, visukuku vyote vilivyotumiwa kuunga mkono nadharia ya kwamba mwanadamu na sokwe waligeuka kutoka kwa mzazi mmoja vingeweza kutoshea kwenye meza ya biliadi. Tangu wakati huo, idadi ya visukuku vinavyotumiwa kuunga mkono nadharia hiyo imeongezeka. Inadaiwa kwamba sasa visukuku hivyo vinaweza kujaza behewa la gari-moshi.38 Hata hivyo, idadi kubwa ya visukuku hivyo ni mfupa mmojammoja na meno hapa na pale. Ni vigumu sana kupata mafuvu kamili au viunzi kamili vya mifupa.39
Swali: Je, kupatikana kwa idadi kubwa ya visukuku vinavyodaiwa ni vya “ukoo” wa mwanadamu kumejibu swali ambalo baadhi ya wataalamu wa mageuzi wameuliza kuhusu wakati na jinsi ambavyo wanadamu waligeuka kutokana na sokwe?
Jibu: Hapana. Kuhusiana na jinsi visukuku hivyo vinapaswa kuainishwa, Robin Derricourt wa Chuo Kikuu cha New South Wales, nchini Australia, aliandika hivi mnamo 2009: “Huenda makubaliano pekee ambayo yamefikiwa sasa ni kwamba, hakuna makubaliano.”40 Mwaka 2007 jarida la sayansi, Nature, lilichapisha makala ya wagunduzi wa vile vinavyodaiwa kuwa visukuku vilivyokuwa vikikosekana katika ule mti wa mageuzi. Jarida hilo lilisema kwamba hakuna chochote kinachojulikana kuhusu wakati au jinsi jamii ya mwanadamu ilivyotokea kutokana na sokwe.41 Gyula Gyenis, mtafiti katika Idara ya Biolojia ya Anthropolojia, ya Chuo Kikuu cha Eötvös Loránd, nchini Hungaria, aliandika hivi mwaka wa 2002: “Kufahamu uainishaji wa visukuku vya hominidi na kuelewa mahali ambapo mageuzi ya hominidi yalitokea, ni jambo linaloendelea kubishaniwa.”g Mwandikaji huyo anasema pia kwamba visukuku ambavyo vimekusanywa kufikia sasa havitusaidii kujua kwa hakika wakati, mahali, au jinsi ambavyo mwanadamu aligeuka kutokana na viumbe vinavyofanana na sokwe.42
MATANGAZO YA KUPATIKANA KWA “VISUKUKU VILIVYOKUWA VIKIKOSEKANA”
◼ Ukweli wa mambo: Vyombo vya habari hutangaza mara nyingi kugunduliwa kwa vile vinavyoitwa “visukuku vilivyokuwa vikikosekana.” Kwa mfano, mwaka wa 2009 kisukuku kilichopewa jina la utani Ida kiligunduliwa. Kulingana na jarida moja kisukuku hicho kilitangazwa kwa msisimko mkubwa.43 Matangazo hayo yalitia ndani kichwa hiki cha habari katika gazeti la The Guardian la Uingereza: “Kisukuku Ida: Uvumbuzi wa Pekee wa ‘Kisukuku Kilichokuwa Kikikosekana’ katika Mageuzi ya Mwanadamu.”44 Hata hivyo, siku kadhaa baadaye, gazeti la mambo ya kisayansi la Uingereza, New Scientist, lilisema: “Ida si ‘kisukuku kilichokuwa kikikosekana’ katika mageuzi ya mwanadamu.”45
Swali: Kwa nini kugunduliwa kwa kile kinachoitwa eti “kisukuku kilichokuwa kikikosekana” hutangazwa sana, ilhali kinapoondolewa katika ule “mti wa ukoo” hakuna lolote linalosemwa?
Jibu: Kuhusu wale wanaofanya magunduzi hayo, Robin Derricourt, aliyenukuliwa mapema, anasema: “Kiongozi wa timu ya uchunguzi huenda akahitaji kukazia jambo la pekee na lenye kusisimua la ‘ugunduzi’ fulani ili aweze kupata pesa zaidi za kudhamini mradi huo kutoka katika taasisi nyingine mbali na zile za kawaida za kielimu. Bila shaka, taasisi hizo huchochewa na habari zenye kusisimua za vyombo vya habari, iwe ni habari zilizochapishwa au za elektroni.”46
MICHORO YA VITABU NA SANAMU ZA SOKWE
◼ Ukweli wa mambo: Michoro katika vitabu na majumba ya makumbusho ya wale wanaoitwa eti wazazi wa kale wa mwanadamu mara nyingi huonyeshwa ikiwa na umbo la uso, rangi ya ngozi, na kiasi fulani cha nywele. Kwa kawaida michoro hiyo huonyesha “wazazi” wa zamani sana wakiwa na sura kama za nyani, na wanaodhaniwa kuwa wanakaribiana zaidi na wanadamu huonyeshwa wakiwa na umbo la uso, rangi ya ngozi, na nywele kama za mwanadamu.
Swali: Je, wanasayansi wanaweza kutengeneza upya maumbo hayo kwa kutegemea mabaki ya visukuku wanavyopata?
Jibu: Hapana. Mwaka 2003, mwanasayansi Carl N. Stephan, anayefanya kazi katika Idara ya Sayansi ya Anatomia ya Chuo Kikuu cha Adelaide, nchini Australia, aliandika hivi: “Nyuso za wazazi wa kale haziwezi kuundwa kwa usahihi au kufanyiwa majaribio.” Anasema kwamba majaribio ya aina hiyo yanayotegemea sokwe wa kisasa “yatakuwa yenye kupendelea upande mmoja, yasiyo sahihi hata kidogo, na ya ubatili.” Alikata maneno jinsi gani? “Yaelekea maumbo yoyote ya nyuso za hominidi wa kale ‘yaliyoundwa upya,’ yatakuwa yenye kupotosha.”47
KUAMUA UWEZO WA AKILI KWA KUANGALIA UKUBWA WA UBONGO
◼ Ukweli wa mambo: Mojawapo ya njia ambazo wanamageuzi wanatumia kuamua ikiwa kiumbe kina uhusiano wa karibu au wa mbali na mwanadamu ni kwa kuchunguza ukubwa wa ubongo wa kiumbe hicho.
Swali: Je, ukubwa wa ubongo ni kipimo sahihi cha kuamua uwezo wa akili?
Jibu: Hapana. Kikundi kimoja cha watafiti waliochunguza ukubwa wa ubongo ili kukisia ni kipi kati ya viumbe vilivyotoweka kilichokaribiana sana na mwanadamu, walikiri kwamba kwa kufanya hivyo ‘mara nyingi wameambulia patupu.’48 Kwa nini? Fikiria taarifa hii ya mwaka wa 2008 katika Scientific American Mind: “Wanasayansi wameshindwa kutambua uhusiano uliopo baina ya ukubwa kamili au wa kadiri wa ubongo na upevu wa akili kati ya mwanadamu na spishi nyingine za wanyama. Wala hawajaweza kutambua ulinganifu uliopo kati ya upevu wa akili na ukubwa au kuwepo kwa sehemu hususa za ubongo, isipokuwa eneo linaloitwa Broca, ambalo hudhibiti uwezo wa kusema.”49
Una maoni gani? Kwa nini wanasayansi hupanga visukuku vilivyotumiwa kuunganisha mageuzi kutoka “sokwe-mpaka-mwanadamu” kulingana na ukubwa wa ubongo ilhali ni wazi kwamba ukubwa wa ubongo si njia inayotegemeka ya kupima akili? Je, wanajaribu kulazimisha uthibitisho uunge mkono nadharia yao? Na kwa nini watafiti hubishana kila mara kutaka kujua visukuku vinavyopaswa kuhusianishwa na ule “mti wa ukoo” wa mwanadamu? Inawezekana kwamba visukuku wanavyochunguza ni vya aina fulani ya sokwe waliotoweka?
Hata hivyo, namna gani vile visukuku vinavyofanana na mwanadamu vinavyoitwa Neanderthal, ambavyo mara nyingi hutumiwa kama uthibitisho wa kuwapo kwa watu wa jamii ya sokwe? Watafiti wameanza kubadili maoni yao kuhusu kile hasa kinachowakilishwa na visukuku hivyo. Katika mwaka wa 2009, Milford H. Wolpoff, aliandika katika jarida la American Journal of Physical Anthropology kwamba “huenda Neandertal walikuwa jamii halisi ya wanadamu.”50
Watu wanyoofu hutambua kwamba kiburi, pesa, na tamaa ya kutaka kutangazwa huchochea jinsi “uthibitisho” wa mageuzi ya mwanadamu unavyotolewa. Je, uko tayari kuamini uthibitisho wa aina hiyo?
PICHA HII INA KASORO GANI?
◼ Picha za aina hii hutegemea makisio na maoni yenye kupendelea upande mmoja ya watafiti na wachoraji wala si ukweli wa mambo.51
◼ Mingi ya michoro hiyo hutegemea mafuvu nusu-nusu na meno ya hapa na pale. Si rahisi kupata mafuvu kamili wala viunzi kamili vya mifupa.
◼ Watafiti hawapatani kuhusu jinsi visukuku vya viumbe mbalimbali vinavyopaswa kuainishwa.
◼ Wachoraji hawawezi kuunda upya maumbo ya uso, rangi ya ngozi, na nywele za viumbe hao waliotoweka.
◼ Kila kiumbe kimewekwa mahali hususa katika mpangilio wa mageuzi mpaka kufikia kwa mwanadamu kwa kutegemea ukubwa wa fuvu la ubongo wake. Hilo linafanywa licha ya uthibitisho wa kwamba ukubwa wa ubongo si njia inayotegemeka ya kuamua uwezo wa akili.
[Maelezo ya Chini]
f Kumbuka: Hakuna yeyote kati ya watafiti wanaonukuliwa katika sanduku hili anayeamini mafundisho ya Biblia kuhusu uumbaji. Wote wanaunga mkono mageuzi.
g Neno “hominidi” linatumiwa kufafanua kile ambacho watafiti wa mageuzi huona kuwa kinafanyiza jamii ya mwanadamu na spishi za viumbe wengine wa kale wanaofanana na mwanadamu.
[Mchoro katika ukurasa wa 22, 23]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MWANZO WA WAKATI →→→→ “MLIPUKO LEO
HISTORIA YA DUNIA WA CAMBRIA”
1 2
[Mchoro katika ukurasa wa 24]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Kwa nini vitabu fulani hubadili kipimo cha visukuku kinachoonyeshwa katika mfuatano fulani uliopendekezwa?
KAMA INAVYOONYESHWA KATIKA VITABU FULANI
KADIRIO LA UKUBWA HALISI
[Mchoro katika ukurasa wa 25]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Mistari yenye nukta inaonyesha uhusiano unaodhaniwa
Samaki asiye na taya
Samaki aliyetoweka mwenye magamba na taya
Samaki mwenye gegedu
Samaki mwenye mifupa
Amfibia
Reptilia
Ndege
Mamalia
VIPINDI VYA WAKATI VYA KIJIOLOJIA →→→→
Uthibitisho wa visukuku halisi hauonyeshi uhusiano wowote
Samaki asiye na taya
Samaki aliyetoweka mwenye magamba na taya
Samaki mwenye gegedu
Samaki mwenye mifupa
Amfibia
Reptilia
Ndege
Mamalia
[Picha katika ukurasa wa 26]
Ikiwa “picha 95” za rekodi ya visukuku zinaonyesha kwamba wanyama hawageuki kutoka kwa aina moja hadi nyingine, kwa nini wataalamu wa visukuku wanapanga zile “picha 5” zinazobaki kuonyesha kwamba wanyama hao walitokana na mageuzi?