Kuutazama Ulimwengu
Kuielewa Lugha ya Mbwa
Kulingana na Shirika la Habari la Japan, kampuni moja ya kutengeneza vitu vya kuchezea huko Japan imebuni kifaa ambacho inasemekana kinatafsiri mibweko ya mbwa katika lugha inayoeleweka. Kifaa hicho kina maikrofoni inayowekwa kwenye shingo ya mbwa na kifaa kingine kidogo kinanasa sauti hiyo. Kifaa hicho huchanganua mibweko hiyo ya mbwa na kuigawanya katika vikundi sita: mfadhaiko, hasira, furaha, huzuni, tamaa, na ukali. Matokeo huonyeshwa kwenye kifaa hicho kidogo, na zinatia ndani semi kama vile “Naona raha!” “Inaudhi sana!” na “Jamani, cheza nami!” Kampuni hiyo ilisema kwamba iliuza vifaa 300,000. Kila kimoja kiliuzwa kwa dola 100 za Marekani na kampuni hiyo inatarajia kuuza vingine milioni moja wakati kitakapopelekwa huko Korea Kusini na Marekani.
Watu Hawatumaini Makanisa
Gazeti Leipziger Volkszeitung linasema kwamba “Wajerumani hutumaini sana polisi na jeshi, lakini si makanisa.” Kongamano la Uchumi Ulimwenguni lilifanya “uchunguzi kuhusu kile ambacho watu hutumaini,” na likagundua kwamba kati ya mashirika 17 makubwa ya umma, makanisa hutumainiwa kidogo zaidi. Mwanasosiolojia Armin Nassehi alisema kwamba wakati huu ambapo watu wana wasiwasi mwingi, Wajerumani hutumaini mashirika ambayo “yanatofautisha kati ya wema na uovu,” kama vile polisi na jeshi. Kwa nini makanisa hayatumainiwi? Nassehi anasema: “Ingawa dini zimeongezeka, watu hawaamini kwamba makanisa yanaweza kutatua matatizo yao.” Anasema kwamba makanisa ya Ujerumani “yamebaki na desturi tu.”
Watu wa Makamo Wanatalikiana
Huko Ujerumani “wenzi wengi wa ndoa wanatengana baada ya miaka mingi ya ndoa,” lasema gazeti Berliner Morgenpost. Gina Kästele, mshauri wa ndoa huko Munich, Ujerumani, asema kwamba jambo hilo linasababishwa na wanawake wengi zaidi kujitegemea, hasa kifedha. Kästele anasema kwamba “mwanamume amepoteza daraka lake la kuruzuku familia.” Wengi wanafikiri kwamba watu wa makamo wanatalikiana kwa sababu wanaahirisha talaka mpaka watoto wanapoondoka nyumbani. Hata hivyo, Kästele anasema, mara nyingi talaka hizo husababishwa na waume wanaozini.
Faida za Kutabasamu
“Karibu asilimia 74 ya watu waliohojiwa walisema kwamba hawangependa kushughulika na watu ambao wamenuna, na asilimia 69 hawawezi kufanya urafiki nao.” Ndivyo gazeti Wprost lilivyosema kuhusu uchunguzi uliofanywa na Taasisi ya Sosiolojia katika Chuo Kikuu cha Jagiellonian huko Kraków, Poland. Sababu moja iliyotajwa ni kwamba mara nyingi inadhaniwa kwamba watu ambao wamenuna wanaficha mambo fulani. Watu, wanaofanya kazi katika umma wamejua hilo kwa muda mrefu na ndiyo sababu “wanasiasa, wafanyabiashara, wanamuziki mashuhuri, watangazaji wa televisheni, maafisa wa uhusiano, na maafisa wa mauzo hutabasamu” mara nyingi, lasema gazeti Wprost. Watafiti pia waligundua kwamba tunapotabasamu, damu nyingi zaidi hufika ubongoni na hilo hutusaidia kuchangamka. Mwanamke mmoja mfanyabiashara alisema: “Mimi hujaribu kutabasamu hata wakati sina furaha. Ninapotabasamu, hisia zangu hubadilika, nami hujihisi vizuri.”
Tahadhari Kuhusu Moto Kambini
Zaidi ya asilimia 70 ya visa vya watoto wanaoungua kambini huko Australia “husababishwa na majivu yenye moto wala si miale ya moto,” lasema jarida Medical Journal of Australia. Isitoshe, huko Australia, watu huungua kambini “asubuhi baada ya moto kudhaniwa kuwa ulizimwa.” Jinsi gani? Wachunguzi waligundua kwamba moto ulipozimwa kwa maji, joto la majivu lilipungua mpaka nyuzi 16 za Selsiasi baada ya saa nane. Lakini mioto iliyozimwa kwa kutumia mchanga ilibaki na kiwango cha juu cha joto la nyuzi 91 za Selsiasi baada ya saa nane—joto linaloweza kuunguza ngozi baada ya sekunde moja. Jarida hilo linasema, ‘kwa kuwa kuzima moto kwa kutumia mchanga hupumbaza watu kuwa moto umezimika, njia bora zaidi ya kuuzima ni kutumia maji.’
Vidonda Vyenye Kansa
Vidonda vingi vya ngozi si hatari. Hata hivyo, si vizuri kupuuza vidonda vyenye kansa. Kulingana na gazeti Milenio la Mexico City, unapaswa kutafuta ushauri wa daktari ikiwa: Upande mmoja wa kidonda hautoshani na mwingine, maumbo yake si ya kawaida, rangi na ukubwa unabadilika, kipenyo chake kinazidi sentimeta 0.6, au kinavuja damu au kuwasha. Dakt. Nancy Pulido Díaz, wa Kituo cha Kitaifa cha Tiba cha La Raza, anasema: “Vidonda vinavyopaswa kutiliwa maanani zaidi ni vile ambavyo mtu amezaliwa navyo na vile vinavyotokea kwenye kiganja cha mikono na nyayo.”
Kujifunza Lugha ya Kigeni
Je, ungependa kujifunza lugha ya kigeni? Gazeti Poradnik Domowy la Poland linatoa mashauri kadhaa. “Ni kawaida kukosea unapokuwa ukijifunza lugha. Hatua ya kwanza ya kufanikiwa ni kukubali jambo hilo.” Pia “ni muhimu kujaribu kuongea hata usipokuwa na uhakika.” Ikiwa hatujui kusema jambo fulani, “nyakati nyingine tunahitaji kusema yale tunayofikiri, au kukisia tu,” na hilo ni afadhali kuliko kunyamaza. Gazeti hilo linasema: “Mara nyingi hatutambui kwamba huenda matatizo yetu yanatokana na woga au haya. Tukifaulu kushinda udhaifu huo, bila shaka tutafanya maendeleo haraka.” Mwalimu mzuri anaweza pia kumsaidia mtu ashinde woga na kufanya maendeleo haraka.
“Watu Milioni 1.6 Walikufa Kutokana na Jeuri”
Gazeti The Wall Street Journal linasema kwamba “watu milioni 1.6 walikufa kutokana na jeuri katika mwaka wa 2000, idadi inayolingana na vifo vilivyosababishwa na kifua-kikuu na inayozidi vifo vilivyosababishwa na malaria. Hiyo ni kulingana na ripoti mpya ya Shirika la Afya Ulimwenguni, iliyojaribu kuonyesha kwa mara ya kwanza idadi ya visa vya ukatili wa aina mbalimbali.” Makadirio hayo yanategemea habari iliyokusanywa katika nchi 70 na inatia ndani vifo vilivyosababishwa na vita, mashambulizi, kujiua, na kupigwa risasi. Makala hiyo inaongeza hivi: “Watafiti waligundua kwamba vifo vinavyosababishwa na jeuri ni asilimia 3 hivi ya vifo vyote ulimwenguni. Idadi ya vifo vilivyosababishwa na jeuri dhidi ya wanawake, watoto, wazee, vijana na jamii kwa ujumla ilikuwa kubwa kuliko walivyotarajia. Kulingana na watafiti hao, hiyo ni kwa sababu mara nyingi visa hivyo haviripotiwi.” Asilimia 50 walijiua, asilimia 30 waliuawa, na asilimia 20 walikufa vitani. Visa vingi vya kujiua vilitukia Ulaya Mashariki, na nchi ya Urusi na Lithuania ndizo zilizoongoza. Visa vingi vya watu waliopigwa risasi vilitukia Albania—vifo 22 kwa kila watu 100,000. Marekani ilikuwa na vifo 11.3 kwa kila watu 100,000, Uingereza na Japan vifo 0.3 na 0.1 kwa kila watu 100,000.
Magari Yenye Muziki
Ni gari lipi linalopiga muziki kwa sauti ya juu zaidi? Jambo hilo limetokeza mashindano mapya ya kimataifa ya magari yenye mdundo wa juu zaidi, yaripoti idhaa ya National Public Radio, nchini Marekani. Kwenye mashindano hayo, vifaa huwekwa ndani ya magari ili kupima sauti za muziki katika vipimo vya desibeli. Sauti inayosikika nje ya gari haipimwi, kwa hiyo wenye magari huyatengeneza kwa njia inayozuia sauti isitoke. Mshiriki mmoja wa mashindano hayo, Wayne Harris, anasema: “Magari yaliyoundwa kwa njia nzuri zaidi, . . . yana vioo vyenye unene wa inchi tatu [au] nne (sentimeta saba au kumi) na milango yake imeimarishwa kwa saruji na vyuma.” Inaeleweka ni kwa nini washiriki wa mashindano hayo hawaketi ndani ya magari yao muziki unapokuwa ukicheza.