HADITHI YA 58
Daudi Na Goliathi
TENA Wafilisti wanakuja kupigana na Israeli. Wakati huu ndugu zake Daudi wakubwa watatu wamo katika jeshi la Sauli. Basi siku moja Yese amwambia Daudi hivi: ‘Wapelekee ndugu zako nafaka na mikate. Kaone kama ni wazima.’
Daudi anapofika kwenye kambi ya jeshi, anapiga mbio kwenda kwenye mapigano akawatafute ndugu zake. Goliathi (Goliata), jitu la Wafilisti anajitokeza ili awacheke Waisraeli. Kwa muda wa siku 40 amekuwa akifanya hivyo asubuhi na jioni. Anapaza sauti: ‘Haya, chagueni mmoja apigane nami.’
Daudi anauliza askari fulani hivi: ‘Atapata nini mtu anayemwua Mfilisti huyu na kuwaondolea Waisraeli aibu hii?’
‘Sauli atampa mtu huyo mali nyingi,’ askari anasema. ‘Naye atampa binti yake awe mke wake.’
Lakini Waisraeli wote wanamwogopa Goliathi kwa sababu ni mkubwa mno. Urefu wake ni zaidi ya mita tatu, na ana askari mwingine wa kumchukulia ngao.
Askari fulani wanakwenda kumwambia Mfalme Sauli kwamba Daudi anataka kupigana na Goliathi. Lakini Sauli anamwambia Daudi hivi: ‘Wewe huwezi kupigana na Mfilisti huyu. Wewe ni mtoto tu, yeye amekuwa askari maisha yake yote.’ Daudi anajibu hivi: ‘Mimi niliua dubu na simba aliyechukua kondoo wa baba. Na Mfilisti huyu atakuwa kama huyo. Yehova atanisaidia.’ Basi Sauli anasema: ‘Nenda, Yehova awe nawe.’
Daudi anatelemkia njia ya kijito na kuchagua mawe matano laini, na kuyaweka mfukoni mwake. Kisha anachukua kombeo lake na kwenda kukutana na jitu lile. Goliathi anapomwona anamdharau. Anadhani itakuwa rahisi sana kumwua Daudi.
‘Wewe njoo tu kwangu,’ Goliathi asema, ‘nami nitawapa ndege na wanyama wapate kula mwili wako.’ Lakini Daudi anasema: ‘Wewe unakuja kwangu kwa upanga na mkuki, lakini mimi ninakuja kwako kwa jina la Yehova. Leo hii Yehova atakutia wewe mikononi mwangu nami nitakuangusha chini.’
Papo hapo Daudi anamkimbilia Goliathi. Anachukua jiwe katika mfuko wake, analiweka katika kombeo lake, na kulitupa kwa nguvu zake zote. Jiwe hilo linaingia moja kwa moja kichwani mwa Goliathi, anaanguka na kufa! Wafilisti wanapoona bingwa wao ameanguka, wote wanageuka na kukimbia. Waisraeli wanawafuatia mbio na kushinda vita.