Mafunzo Juu ya Maandiko Yenye Pumzi ya Mungu na Habari ya Msingi Yayo
Funzo Namba 9—Akiolojia na Maandishi Yenye Pumzi ya Mungu
Funzo la magunduzi ya kiakiolojia na la maandishi ya kale ya historia ya kilimwengu yanayothibitisha maandishi ya Biblia.
1. Ni nini kinachomaanishwa na (a) akiolojia ya Biblia? (b) aathari?
AKIOLOJIA ya Biblia ni funzo la jamii za watu na matukio ya nyakati za Biblia kupitia maandishi, vyombo, majengo, na mabaki mengine yanayopatikana duniani. Utafutaji wa masalio ya kale, au aathari, katika vituo vya kale vya Biblia umetia ndani upekuzi mwingi na kuondolewa kwa mamilioni ya tani za udongo. Aathari ni kitu chochote kinachoonyesha usanii wa kibinadamu na kutoa uthibitisho wa utendaji na uhai wa binadamu. Aathari huenda ikatia ndani vitu kama vile vigae, mabomoko ya majengo, mabamba ya udongo, maandishi yaliyochongwa, hati, makaburi, na maandishi ya matukio yaliyoandikwa kwenye jiwe.
2. Akiolojia ya Biblia ni yenye thamani gani?
2 Kufikia mapema karne ya 20, akiolojia ilikuwa imekwisha sitawishwa ikawa funzo la uangalifu, kukiwa safari za kwenda kwenye mabara ya Biblia zilizodhaminiwa na vyuo vikuu vikubwa na majumba ya ukumbusho katika Ulaya na Amerika. Kama tokeo, waakiolojia wamefukua habari tele inayoelimisha juu ya jinsi mambo yalivyokuwa katika nyakati za Biblia. Nyakati nyingine magunduzi ya kiakiolojia yamedhihirisha uasilia wa Biblia, yakionyesha usahihi wayo mpaka kwenye habari iliyo ndogo zaidi.
AKIOLOJIA NA MAANDIKO YA KIEBRANIA
3. Ni mabomoko na maandishi yapi ya kale huthibitisha kuwapo kwa zigurati katika Babuloni ya kale?
3 Mnara wa Babeli. Kulingana na Biblia, Mnara wa Babeli ulikuwa kazi kubwa ya ujenzi. (Mwa. 11:1-9) La kupendeza ni kwamba waakiolojia wamefukua katika na kuzunguka mabomoko ya Babuloni ya kale vituo vya zigurati kadhaa, au minara ya hekalu yenye vigorofa iliyo kama piramidi, kutia ndani hekalu lililobomoka la Etemenanki, ambalo lilikuwa ndani ya kuta za Babuloni. Mara nyingi, maandishi ya kale kuhusu mahekalu hayo huwa na maneno haya, “Ncha yalo itafikia mbingu.” Mfalme Nebukadreza yaripotiwa alisema, “Mimi nilinyanyua kilele cha Mnara wa vigorofa kule Etemenanki hivi kwamba ncha yao ikafikia mbingu.” Kipande kimoja chasimulia anguko la zigurati kama hiyo kwa maneno haya: “Ujenzi wa hekalu hili uliudhi miungu. Katika usiku mmoja walivurumisha chini kilichokuwa kimejengwa. Wakawatawanya ng’ambo, na kufanya uneni wao kuwa wa ajabu-ajabu. Wakazuia maendeleo hayo.”a
4. Ni magunduzi gani ya kiakiolojia yaliyofanywa kule Gihoni, nayo yaweza kuwa na uhusiano gani na maandishi ya Biblia?
4 Mitaro ya Chini ya Ardhi ya Maji Penye Chemchemi ya Gihoni. Katika 1867 katika eneo la Yerusalemu, Charles Warren aligundua mtaro wa chini ya ardhi wa maji wenye kutoka Chemchemi ya Gihoni kurudi kwenye kilima, ukiwa na mtaimbo wenye kwenda juu kuelekea Jiji la Daudi. Kwa wazi, hiyo ndiyo iliyokuwa njia ambayo wanaume wa Daudi hapo kwanza walipenya ndani ya jiji hilo. (2 Sam. 5:6-10) Ilikuwa katika 1909-11 kwamba mfumo wote wa mitaro hiyo ya chini ya ardhi kutoka chemchemi ya Gihoni ilifichuliwa. Mtaro mmoja mkubwa wa chini ya ardhi, wenye wastani wa urefu wa meta 1.8 kwenda juu, ulichongowa kwa meta 533 za mwamba imara. Ulianzia Gihoni mpaka kwenye Kiziwa cha Siloamu katika Bonde la Tiropoeni (ndani ya jiji) na yaelekea ndio ule aliojenga Hezekia. Maandishi yaliyochongwa katika mwandiko wa mapema wa Kiebrania yalipatikana kwenye ukuta wa mtaro huo mwembamba wa chini ya ardhi. Yasema hivi, kwa sehemu: “Na hivi ndivyo ulivyotobolewa:—wakati [ . . . ] (kulikuwa) kungali [ . . . ] shoka (mashoka), kila mtu kuelekea mwenzake, na wakati kulikuwa kungali dhiraa tatu za kutobolewa, [kulisikiwa] sauti ya mtu akimwita mwenzake, kwa maana kulikuwako na mpishano wa mwamba upande wa kulia [na upande wa kushoto]. Na mtaro huo wa chini ya ardhi ulipotoboka, wachonga mwamba walichonga (mwamba huo), kila mtu kuelekea mwenzake, shoka juu ya shoka; na maji yakatiririka kutoka kwenye chemchemi kuelekea kiziwa kwa dhiraa 1,200, na urefu wa mwamba juu ya kichwa (vichwa) vya wachonga mwamba ulikuwa dhiraa 100.” Jinsi hicho kilivyokuwa kitendo cha kutokeza sana cha uhandisi kwa nyakati hizo!b—2 Fal. 20:20; 2 Nya. 32:30.
5. Kuna uthibitisho gani wa kiakiolojia unaopatikana kule Karnaki wa uvamizi wa Shishaki na majina ya mahali-mahali pa Biblia?
5 Maandishi Yaliyochongwa ya Ushindi wa Shishaki. Shishaki, mfalme wa Misri, ametajwa mara saba katika Biblia. Kwa sababu Mfalme Rehoboamu aliiacha sheria ya Yehova, Yehova aliruhusu Shishaki avamie Yuda, katika 993 K.W.K., lakini asiifanye ukiwa kabisa. (1 Fal. 14:25-28; 2 Nya. 12:1-12) Mpaka kufikia miaka ya karibuni, ilionekana ni maandishi ya Biblia pekee yaliyokuwako kuhusiana na uvamizi huo. Kisha ikapatikana hati kubwa ya Farao ambaye Biblia humwita Shishaki (Sheshonk I). Hiyo ilikuwa kwa namna ya maandishi ya kutokeza yaliyochongwa kwa kutumia herufi-michoro na picha kwenye ukuta wa kusini wa hekalu kubwa mno la Kimisri kule Karnaki (Thebesi ya kale). Katika mchongo huo mkubwa mno, kuna mchoro wa mungu Amoni wa Kimisri, ambaye katika mkono wake wa kulia ameshika upanga wenye umbo la mundu. Anamletea Farao Shishaki wafungwa Wapalestina 156 waliofungwa pingu mikononi, wakiwa wameshikanishwa kwa kamba katika mkono wake wa kushoto. Kila mfungwa anawakilisha jiji au kijiji, ambalo jina lalo limeonyeshwa kwa herufi-michoro. Kati ya yale ambayo yangali yaweza kutambulishwa ni Rabithu (Yos. 19:20); Taanaki, Beth-sheani, na Megido (Yos. 17:11); Shunemu (Yos. 19:18); Rehobu (Yos. 19:28); Hafaraimu (Yos. 19:19); Gibeoni (Yos. 18:25); Beth-horoni (Yos. 21:22); Aiyaloni (Yos. 21:24); Soko (Yos. 15:35); na Aradi (Yos. 12:14). Pia hati hiyo yarejezea “Shamba la Abramu,” huo ukiwa ndio mtajo wa mapema zaidi wa Abrahamu katika maandishi ya Kimisri.c
6, 7. Ni nini historia ya Jiwe la Moabu, nalo hutoa habari gani kuhusu vita kati ya Israeli na Moabu?
6 Jiwe la Moabu. Katika 1868 misionari Mjerumani F. A. Klein alifanya ugunduzi wenye kutokeza wa nakshi ya kale kule Dhibani (Diboni). Huo umekuja kujulikana kuwa Jiwe la Moabu. Maandishi yalo yalikalibiwa, lakini jiwe lenyewe lilivunjwa na Wabedouini kabla halijaweza kuondolewa. Hata hivyo, vingi vya vipande vilipatikana, na jiwe hilo sasa limehifadhiwa katika Louvre, Paris, kukiwa na nakala katika British Museum, London. Hapo awali lilikuwa limesimamishwa kule Diboni, katika Moabu, na hueleza maoni ya Mfalme Mesha juu ya kuasi kwake Israeli. (2 Fal. 1:1; 3:4, 5) Husomeka hivi, kwa sehemu: “Mimi (ni) Mesha, mwana wa Kemoshi-[ . . . ], mfalme wa Moabu, Mdiboni . . . Kwa habari ya Omri, mfalme wa Israeli, aliyenyenyekeza Moabu kwa miaka mingi (kwa halisi, siku), kwa maana Kemoshi [mungu wa Moabu] alikuwa amekasirikia bara lake. Na mwanae alimfuata na yeye pia akasema, ‘Mimi nitanyenyekeza Moabu.’ Kanena (hivyo) wakati wangu, lakini mimi nilimshinda na nyumba yake, huku Israeli imeangamia milele! . . . Na Kemoshi akaniambia, ‘Nenda, twaa Nebo kutoka Israeli!’ Kwa hiyo mimi nikaenda wakati wa usiku na kupigana juu yayo tangu alfajiri mpaka adhuhuri, nikaitwaa na kuchinja wote . . . Na mimi nikatwaa kutoka huko [vyombo] vya Yahweh, nikaviburuta mpaka mbele ya Kemoshi.”d Angalia mtajo wa jina la kimungu katika sentensi ya mwisho. Hilo laweza kuonwa katika picha iliyofuatana na Jiwe la Moabu. Liko kwenye umbo la Tetragrammatoni, upande wa kulia wa hati hiyo, katika mstari wa 18.
7 Jiwe la Moabu pia hutaja sehemu za Biblia zifuatazo: Atarothi na Nebo (Hes. 32:34, 38); Arnoni, Aroeri, Medeba, na Diboni (Yos. 13:9); Bamoth-baali, Beth-baal-meoni, Yahasa, na Kiriathaimu (Yos. 13:17-19); Bezeri (Yos. 20:8), Horonaimu (Isa. 15:5); na Beth-diblathaimu na Keriothi (Yer. 48:22, 24). Hivyo launga mkono uhistoria wa sehemu hizo.
8. Biblia huandika nini kuhusu Senakeribu, na machimbuzi ya ikulu yake yamefunua nini?
8 Mche wa Mfalme Senakeribu. Biblia huandika kirefu sana juu ya uvamizi wa Waashuri chini ya Mfalme Senakeribu katika mwaka 732 K.W.K. (2 Fal. 18:13–19:37; 2 Nya. 32:1-22; Isa. 35:1–37:38) Ilikuwa katika 1847-51 kwamba mwakiolojia Mwingereza A. H. Layard alichimbua mabomoko ya ikulu kubwa ya Senakeribu kule Ninawi katika eneo la Ashuru ya kale. Ikulu hiyo ilipatikana kuwa yenye vyumba karibu 70, kukiwa karibu meta 3,000 za kiambaza kilichotandazwa kwa mawe tambarare yaliyochongwa. Ripoti za matukio ya kila mwaka za Senakeribu ziliandikwa kwenye silinda za udongo, au miche. Chapa za mwisho-mwisho za habari hizo za matukio ya kila mwaka, ambazo yaelekea zilifanywa muda mfupi kabla ya kifo chake, huonekana kwenye kile kinachojulikana kuwa Mche wa Taylor, kilichohifadhiwa katika British Museum, lakini Taasisi ya Nchi za Mashariki ya Chuo Kikuu cha Chicago ina nakala bora hata zaidi iliyo kwenye mche uliogunduliwa karibu na kituo cha Ninawi ya kale, jiji kuu la Milki ya Kiashuri.
9. Senakeribu aandika nini, kwa kupatana na simulizi la Biblia, lakini yeye akosa kutaja nini, na kwa nini?
9 Katika ripoti hizo za mwisho-mwisho za matukio ya kila mwaka, Senakeribu anatoa fasiri yake mwenyewe ya majivuno juu ya uvamizi wake wa Yuda: “Kwa habari ya Hezekia, aliye Myahudi, yeye hakujitiisha kwa nira yangu, mimi nilizingira 46 ya majiji yake yenye nguvu, ngome zilizozungushwa kuta na vijiji visivyohesabika katika ujirani wayo, nikishinda (hayo) kupitia jukwaa (za mchanga) zilizoimarishwa kwa magogo, na magogo ya kubomolea maboma yaliyoletwa (kwa njia hiyo) karibu (na kuta hizo) (pamoja na) shambulizi kwa askari watumia miguu, (wakitumia) mabomu ya kuchimbiwa ardhini, krini na pia wahandisi wa kuchimba mahandaki. Nilifukuza (kutoka hayo) watu 200,150, vijana kwa wazee, wa kiume kwa wa kike, farasi, nyumbu, punda, ngamia, ng’ombe wakubwa kwa wadogo wasiohesabika, na kuchukua (hivyo) kuwa nyara. Hezekia [mwenyewe] nilimfanya mfungwa katika Yerusalemu, makao yake ya kifalme, kama vile nyuni ndani ya kizimba. . . . Miji yake ambayo nilikuwa nimepora, niliiondoa kwa nchi yake na kuipokeza kwa Mitinti, mfalme wa Ashdodi, Padi, mfalme wa Ekroni, na Silibeli, mfalme wa Gaza. . . . Hezekia mwenyewe . . . alinipa mimi, baadaye, nikarudi Ninawi, jiji langu la kiubwana, nikiwa na talanta 30 za dhahabu, talanta 800 za fedha, mawe yenye thamani, madini ya kutilia matiko, vipande vikubwa vya jiwe jekundu, makochi (yaliyochovywa) pembe za ndovu, viti vya nimedu (vilivyochovywa) pembe za ndovu, ngozi za ndovu, mbao za mpingo, mbao za mkunguni (na) hazina zenye thamani za aina zote, mabinti wake (mwenyewe), masuria, wanamuziki wa kiume na kike. Ili kutoa ushuru na heshima nyingi akiwa mtumwa alituma tarishi wake wa (kibinafsi).”e Kwa habari ya ushuru huo uliotozwa Hezekia na Senakeribu, Biblia huthibitisha hizo talanta 30 za dhahabu lakini hutaja talanta 300 za fedha tu. Zaidi ya hayo, hiyo huonyesha kwamba hiyo ilikuwa kabla ya Senakeribu kutishia Yerusalemu na mazingiwa. Katika ripoti ya Senakeribu yenye upendeleo kwa kusudi la historia ya Kiashuri, yeye akosa kutaja kimakusudi kushindwa kwake kabisa katika Yuda, wakati ambapo kwa usiku mmoja malaika wa Yehova aliharibu 185,000 kati ya askari wake, hivyo akalazimishwa kutoroka arudi Ninawi kama mbwa aliyetandikwa. Hata hivyo, maandishi hayo yaliyoandikwa ya majivuno kwenye mche wa Senakeribu huonyesha uvamizi mkubwa wa Yuda kabla ya Yehova kuwafukuza Waashuri baada ya wao kulitisha Yerusalemu.—2 Fal. 18:14; 19:35, 36.
10, 11. (a) Barua za Lakishi ni nini, nazo zaonyesha nini? (b) Zinaungaje mkono maandishi ya Yeremia?
10 Barua za Lakishi. Jiji lijulikanalo sana la Lakishi limetajwa zaidi ya mara 20 katika Biblia. Lilikuwa kilometa 43 magharibi ya kusini-mashariki mwa Yerusalemu. Mabomoko hayo yamechimbuliwa sana. Katika 1935, kwenye chumba kimoja cha walinzi cha nyumba ambayo pia ilitumika kuwa lango, kulipatikana vigae 18, vilivyoandikwa (3 zaidi vilipatikana katika 1938). Kumbe vilikuwa ni barua kadhaa zilizoandikwa katika herufi za Kiebrania cha kale. Mkusanyo huo wa 21 sasa wajulikana kuwa Barua za Lakishi. Lakishi ilikuwa mojawapo ngome za mwisho za Yuda kusimama kupinga Nebukadreza, ikaja kufanywa kuwa rundo la mabomoko yaliyoungua wakati wa 609-607 K.W.K. Barua hizo zaonyesha uharaka wa nyakati hizo. Zaelekea kuwa ni barua zilizoandikwa kutoka vituo vilivyosalia vya vikosi vya Kiyudea kutoka kwa Yaoshi, jemadari mmoja wa kijeshi kule Lakishi. Mojawapo hizo (namba 4) husomeka hivi kwa sehemu: “YHWH [Tetragrammatoni, “Yehova”] na aruhusu bwanangu asikie hata sasa habari za mema. . . . tunakesha kuona ishara za moto za Lakishi, kulingana na ishara zote ambazo bwanangu hutoa, kwa sababu hatulioni Azeka.” Huo ni uthibitisho wenye kutazamisha wa Yeremia 34:7, ambapo hutaja Lakishi na Azeka kuwa majiji mawili ya mwisho yenye ngome yaliyosalia. Yaelekea barua hiyo yaonyesha kwamba sasa Azeka lilikuwa limeanguka. Jina la kimungu, kwa umbo la Tetragrammatoni, huonekana mara nyingi katika barua hizo, hilo likionyesha kwamba jina Yehova lilitumiwa kila siku miongoni mwa Wayahudi wakati huo.
11 Barua nyingine (namba 3) yaanza kama ifuatavyo: “YHWH [yaani, Yehova] na asababishe bwana wangu asikie habari za amani! . . . Na imeripotiwa kwa mtumishi wako kuwa, ‘Jemadari wa jeshi, Konia mwana wa Elnathani, ameshuka ili aende kuingia Misri na kwa Hodavia mwana wa Ahiya na wanaume wake ametumana apate [ugavi] kutoka kwake.’” Barua hiyo yaelekea kuthibitisha kwamba Yuda walishuka Misri wakapate msaada, kwa kuvunja amri ya Yehova na ikawa ni kwa uharibifu wao wenyewe. (Isa. 31:1; Yer. 46:25, 26) Majina Elnathani na Hoshaya, yanayoonekana katika mwandiko kamili wa barua hiyo, yanapatikana pia kwenye Yeremia 36:12 na Yeremia 42:1. Majina mengine matatu yaliyotajwa katika barua hizo yanapatikana pia katika kitabu cha Biblia cha Yeremia. Hayo ni Gemaria, Neria, na Yaazania.—Yer. 32:12; 35:3; 36:10.f
12, 13. Maandishi ya Tarehe za Matukio ya Nabonido hueleza nini, na kwa nini ni yenye thamani maalumu?
12 Maandishi ya Tarehe za Matukio ya Nabonido. Katika nusu ya baadaye ya karne ya 19, machimbuzi karibu na Baghdad yalitokeza magunduzi mengi ya mabamba na silinda za udongo zilizoelimisha sana katika historia ya Babuloni wa kale. Mojawapo hizo ilikuwa ile hati inayojulikana kuwa Maandishi ya Tarehe za Matukio ya Nabonido, ambayo sasa iko katika British Museum. Mfalme Nabonido wa Babuloni alikuwa ndiye baba wa mtawala-mwenzi, Belshaza. Yeye aliishi zaidi ya mwanae, ambaye aliuawa usiku ule ambao vikosi vya Koreshi Mwajemi vilitwaa Babuloni, Oktoba 5, 539 K.W.K. (Dan. 5:30, 31) Maandishi ya Tarehe za Matukio ya Nabonido, ambayo ni maandishi yenye kutokeza ya tarehe ziliozotunzwa vizuri za anguko la Babuloni, husaidia kuthibitisha ni siku gani tukio hilo lilitokea. Ifuatayo ni tafsiri ya kisehemu kidogo cha Maandishi ya Tarehe za Matukio ya Nabonido: “Katika mwezi wa Tashritu [Tishri (Septemba-Oktoba)], wakati Koreshi aliposhambulia jeshi la Akadi katika Opisi kwenye Tigri . . . siku ya 14, Sipari lilitekwa bila ya pigano. Nabonido alitoroka. Siku ya 16 [Oktoba 11, 539 K.W.K., ya Julius, au Oktoba 5, ya Gregory] Gobryas (Ugbaru), liwali wa Gutiumu na jeshi la Koreshi waliingia Babuloni bila ya pigano. Baadaye Nabonido alikamatiwa Babuloni aliporejea (huko). . . . Katika mwezi wa Arahshamnu [ya Marchesva (Oktoba-Novemba)], siku ya tatu [Oktoba 28, ya Julius], Koreshi aliingia Babuloni, vitawi vya kijani-kibichi vilitandazwa mbele yake—hali ya ‘Amani’ (sulmu) iliamrishwa juu ya jiji hilo. Koreshi alipelekea Wababuloni wote salamu. Gobryas, liwali wake, aliweka maliwali (wadogo) katika Babuloni.”g
13 Yaweza kuangaliwa kwamba Dario Mmedi hatajwi katika maandishi hayo ya tarehe za matukio, na kufikia sasa, hakuna mtajo uliopatikana wa Dario huyo katika maandishi yoyote yasiyo ya Kibiblia, wala hatajwi katika hati yoyote ya kilimwengu ya kihistoria kabla ya wakati wa Yosefo (Mwanahistoria wa Kiyahudi wa karne ya kwanza W.K.). Kwa hiyo wengine wamedokeza kwamba aweza kuwa ndiye Gobryas anayetajwa katika simulizi lililo juu. Ingawa habari iliyopo kuhusu Gobryas yaelekea kulingana na ile inayohusu Dario, kitambulisho hicho hakiwezi kuonwa kuwa cha kukata maneno.h Kwa vyovyote vile, historia ya kilimwengu huthibitisha kwa uhakika kwamba Koreshi alitimiza fungu kubwa katika kushinda Babuloni na kwamba baada ya hapo alitawala huko akiwa mfalme.
14. Kumeandikwa nini kwenye Silinda ya Koreshi?
14 Silinda ya Koreshi. Wakati fulani baada ya yeye kuanza kutawala akiwa mfalme wa Mamlaka ya Ulimwengu ya Uajemi, ushindi wa Koreshi juu ya Babuloni katika 539 K.W.K. uliandikwa kwenye silinda ya udongo. Hati hiyo yenye kutokeza imehifadhiwa pia katika British Museum. Sehemu moja ya mwandiko uliotafsiriwa yafuata: “Mimi ni Koreshi, mfalme wa Ulimwengu, mfalme mkuu, mfalme halali, mfalme wa Babuloni, mfalme wa Sumeri na Akadi, mfalme wa mizingo (minne ya dunia), . . . mimi nilirejea kwenye majiji [fulani yaliyokuwa yametangulia kutajwa] matakatifu ng’ambo ile nyingine ya Tigri, mahekalu yayo ambayo yamekuwa mabomoko kwa muda mrefu, mifano ambayo (wakati mmoja ilikuwa) ikiishi humo na nikasimamisha kwa ajili yayo mahekalu ya kudumu. Mimi (pia) nilikusanya wakaaji wayo (wa hapo kwanza) na kuwarejeshea (wao) makao yao.”i
15. Silinda ya Koreshi hufunua nini juu ya Koreshi, na hilo lapatanaje na Biblia?
15 Kwa hiyo Silinda ya Koreshi hujulisha sera ya mfalme huyo ya kurejesha kwenye sehemu zao za awali vikundi vya watu vilivyotekwa. Kwa kupatana na hilo, Koreshi alitoa amri kwa Wayahudi warejee Yerusalemu na kujenga upya nyumba ya Yehova huko. Kwa kupendeza, miaka 200 hapo awali, Yehova alikuwa amemtaja kiunabii Koreshi kuwa ndiye angetwaa Babuloni na kutokeza mrejesho wa watu wa Yehova.—Isa. 44:28; 45:1; 2 Nya. 36:23.
AKIOLOJIA NA MAANDIKO YA KIGIRIKI YA KIKRISTO
16. Akiolojia imeelimisha nini kuhusiana na Maandiko ya Kigiriki?
16 Kama ilivyofanya kwa Maandiko ya Kiebrania, akiolojia imeelimisha juu ya aathari nyingi zenye kupendeza katika kuunga mkono maandishi yaliyopuliziwa na Mungu yaliyomo katika Maandiko ya Kigiriki ya Kikristo.
17. Akiolojia yaungaje mkono mazungumzo ya Yesu ya suala la kodi?
17 Sarafu ya Dinari Yenye Maandishi ya Tiberia. Biblia huonyesha waziwazi kwamba huduma ya Yesu ilitukia wakati wa utawala wa Kaisari Tiberia. Baadhi ya wapinzani wa Yesu walijaribu kumtega kwa kuuliza juu ya habari ya kulipa kodi ya kichwa kwa Kaisari. Maandishi yasomeka hivi: “Akijua unafiki wao, akawaambia, Mbona mmenijaribu? Nileteeni dinari niione. Wakaileta. Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii na anwani hii? Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Yesu akajibu, akawaambia, Mpeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na yaliyo ya Mungu mpeni Mungu. Wakamstaajabia sana.” (Mk. 12:15-17) Waakiolojia wamepata sarafu ya fedha ya dinari yenye kichwa cha Kaisari Tiberia! Ilitolewa itumike karibu 15 W.K. Hilo lapatana na kipindi cha utawala wa Tiberia akiwa maliki, kilichoanza katika 14 W.K., na launga mkono zaidi maandishi yanayoeleza kwamba huduma ya Yohana Mbatizaji ilianza katika mwaka wa 15 wa Tiberia, au masika ya 29 W.K.—Luka 3:1, 2.
18. Ni ugunduzi gani umefanywa kwa kurejezea Pontio Pilato?
18 Maandishi ya Pontio Pilato. Ilikuwa katika 1961 kwamba ugunduzi wa kwanza wa kiakiolojia ulifanywa ukirejezea Pontio Pilato. Hilo lilikuwa bamba la jiwe kule Kaisaria, lililokuwa na jina la Pontio Pilato katika Kilatini.
19. Ni nini ambacho bado kimesalia katika Athene, kuthibitisha kikao cha Matendo 17:16-34?
19 Areopago. Paulo alitoa mojawapo ya hotuba zake zenye kujulikana sana zilizoandikwa katika Athene, Ugiriki, katika 50 W.K. (Mdo. 17:16-34) Hiyo ilikuwa wakati ambapo Waathene fulani walimkamata Paulo na kumpeleka kwenye Areopago. Areopago, au Kilima cha Aresi (Kilima cha Marsi), ndilo jina la kilima chenye mwamba mtupu, kilichoinuka karibu meta 113, kaskazini-magharibi tu mwa Akropoli ya Athene. Ngazi zilizokatwa kwenye mwamba zaongoza kwenye kilele, ambako mabenchi yasiyolainika, yaliyochongwa mwambani, yakifanyiza pande tatu za mraba, yangali yaweza kuonekana. Areopago ingalipo, ikithibitisha kikao cha Biblia kilichoandikwa cha hotuba ya kihistoria ya Paulo.
20. Tao la Tito laendelea kushuhudia nini, na jinsi gani?
20 Tao la Tito. Yerusalemu na hekalu lalo liliharibiwa na Warumi chini ya Tito, katika 70 W.K. Mwaka uliofuata, katika Rumi, Tito alisherehekea ushindi wake, pamoja na babae, Maliki Vespasiani. Wafungwa mia saba wa Kiyahudi waliochaguliwa waliamrishwa kutembea katika mwandamano wenye shangwe ya ushindi. Mizigo ya nyara za vita ilionyeshwa pia, kutia ndani hazina za hekalu. Tito mwenyewe akawa maliki, akitumikia hivyo tangu 79 mpaka 81 W.K., na baada ya kifo chake kikumbusho kikubwa, Tao la Tito, kilikamilishwa na kuwekewa divo Tito (kwa Tito aliyechukuliwa kuwa mungu). Andamano lake la shangwe ya ushindi huwakilishwa kwa mchongo, uliochongwa kwenye kila upande wa kijia kinachopita kwenye tao hilo. Ng’ambo ile nyingine, kumeonyeshwa askari Warumi, walioshika mikuki isiyo na vichwa na wamevishwa taji la makoja, wamebeba fanicha (vyombo) takatifu kutoka hekalu la Yerusalemu. Hiyo ni kutia na kinara cha taa chenye matawi saba na meza ya mkate wa wonyesho, ambayo juu yayo zile tarumbeta takatifu huonekana. Mchongo ulio ng’ambo ile nyingine ya kijia huonyesha Tito mshindi amesimama katika gari la vita lenye kukokotwa na farasi wanne na kuongozwa na mwanamke anayewakilisha jiji la Rumi.j Kila mwaka maelfu ya watazama mandhari huangalia hilo Tao la Tito la shangwe ya ushindi, ambalo lingali lasimama katika Rumi likiwa ushuhuda ulio kimya wa utimizo wa unabii wa Yesu na utekelezaji wa kutisha wa hukumu ya Yehova juu ya Yerusalemu lenye kuasi.—Mt. 23:37–24:2; Luka 19:43, 44; 21:20-24.
21. (a) Ni kwa njia gani akiolojia imefanya kazi kwa umoja na ugunduzi wa hati? (b) Ni nini unaofaa kuwa mtazamo kuhusu akiolojia?
21 Kwa njia ile ile ambayo ugunduzi wa hati za kale umesaidia kurudisha maandishi-awali ya Biblia yaliyo safi ya awali, ndivyo ugunduzi wa aathari nyingi umeonyesha mara nyingi kwamba mambo yanayotajwa katika maandishi-awali ya Biblia ni yenye kutegemeka mpaka kwenye nukta ndogo zaidi ya historia, kronolojia na jiografia. Hata hivyo, lingekuwa kosa kukata shauri kwamba akiolojia hukubaliana na Biblia katika kila kisa. Lazima ikumbukwe kwamba akiolojia si uchunguzi usiokosea. Magunduzi ya kiakiolojia hutegemea mafasiri ya kibinadamu, na baadhi ya mafasiri hayo yamebadilika-badilika pindi kwa pindi. Nyakati nyingine akiolojia imeandaa tegemezo lisilo la lazima kwa ukweli wa Neno la Mungu. Na zaidi, kama ilivyoelezwa na hayati Sir Frederic Kenyon, mkurugenzi na mtunza-maktaba mkuu wa British Museum kwa miaka mingi, akiolojia imefanya Biblia kuwa yenye “kueleweka zaidi kupitia maarifa kamili zaidi ya chanzo na kikao chayo.”k Lakini lazima imani itegemee Biblia, si akiolojia.—Rum. 10:9; Ebr. 11:6.
22. Ni uthibitisho gani utakaofikiriwa katika funzo linalofuata?
22 Ndani yayo yenyewe Biblia ina uthibitisho usiobishika kwamba kwa kweli hiyo ni neno asilia “la Mungu aishiye na adumuye,” kama tutakavyoona katika funzo lifuatalo.—1 Pet. 1:23, NW.
[Maelezo ya Chini]
a Bible and Spade, 1938, S. L. Caiger, ukurasa 29.
b Ancient Near Eastern Texts, 1974, J. B. Pritchard, ukurasa 321; Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 941-2, 1104.
c Light From the Ancient Past, 1959, J. Finegan, kurasa 91, 126.
d Ancient Near Eastern Texts, ukurasa 320.
e Ancient Near Eastern Texts, ukurasa 288.
f Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 151-2; Light From the Ancient Past, kurasa 192-5.
g Ancient Near Eastern Texts, ukurasa 306.
h Insight on the Scriptures, Buku 1, kurasa 581-3.
i Ancient Near Eastern Texts, ukurasa 316.
j Light From the Ancient Past, ukurasa 329.
k The Bible and Archaeology, 1940, ukurasa 279.
[Picha katika ukurasa wa 333]
Jiwe la Moabu
Upanuzi wa Tetragrammatoni, ambao huonekana katika maandishi ya kale, katika mstari wa 18, upande wa kulia
[Picha katika ukurasa wa 334]
Mche wa Mfalme Senakeribu
[Picha katika ukurasa wa 335]
Maandishi ya Tarehe za Matukio ya Nabonido
[Picha katika ukurasa wa 336]
Sarafu ya Dinari yenye maandishi ya Tiberia
[Picha katika ukurasa wa 337]
Tao la Tito
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 337]
Sifa za Picha za Funzo 9 zimeorodheshwa kufuatana na kurasa zazo:
ukurasa 333, Musée du Louvre, Paris;
ukurasa 334, Hisani ya Taasisi ya Nchi za Mashariki, Chuo Kikuu cha Chicago;
ukurasa 335, Hisani ya Wadhamini wa British Museum;
ukurasa 336, Hisani ya Wadhamini wa British Museum.