SURA YA KUMI NA SITA
Alitenda kwa Hekima, Ujasiri, na Bila Ubinafsi
1-3. (a) Esta alihisije alipokuwa akienda mbele ya mfalme? (b) Mfalme alitendaje alipomwona Esta?
ESTA alielekea polepole kwenye kiti cha mfalme, huku moyo ukimdunda. Wazia kimya kilichotanda katika jumba la mfalme wa Uajemi huko Shushani, kimya kikubwa hivi kwamba Esta angesikia nyayo za miguu yake na sauti ya mavazi yake alipokuwa akitembea. Hangeruhusu akengeushwe na ua wa jumba la mfalme, nguzo zilizopambwa, dari lenye michongo mingi lililotengenezwa kwa mierezi iliyoletwa kutoka nchi ya mbali ya Lebanoni. Alimkazia fikira mwanamume aliyeketi kwenye kiti cha mfalme, mwanamume ambaye angeamua ikiwa Esta angeendelea kuishi.
2 Mfalme alimtazama Esta kwa makini alipokaribia, kisha akamnyooshea fimbo yake ya dhahabu. Lilikuwa jambo dogo, lakini liliokoa uhai wa Esta, kwa maana kwa kufanya hivyo mfalme alimsamehe kosa alilokuwa amefanya—kwenda mbele ya mfalme bila kualikwa. Alipokaribia kiti cha mfalme, Esta alinyoosha mkono wake na kwa shukrani akagusa ncha ya ile fimbo.—Esta 5:1, 2.
3 Kila kitu kumhusu Mfalme Ahasuero kilionyesha utajiri na ukuu wa mamlaka yake. Mavazi ya wafalme wa Uajemi wa nyakati hizo yalikuwa na thamani inayolingana na mamia ya mamilioni ya dola. Ingawa hivyo, Esta aliona uchangamfu fulani katika macho ya mumewe; alipendwa na mume wake. Mfalme akasema: “Una nini, Ee Esta, malkia, na ombi lako ni nini? Hata nusu ya ufalme—na upewe wewe!”—Esta 5:3.
4. Esta alikabili hali gani ngumu?
4 Tayari Esta alikuwa ameonyesha imani na ujasiri mwingi; alikuwa ameenda mbele ya mfalme ili kuwalinda watu wake kutokana na njama ya kuwaangamiza. Kufikia sasa, alikuwa amefaulu, lakini angekabili hali ngumu zaidi. Alipaswa kumsadikisha mtawala huyo mwenye kiburi kwamba mshauri wake aliyemwamini zaidi alikuwa mtu mwovu ambaye alimdanganya aagize watu wa Esta wauawe. Angemsadikishaje, na tunajifunza nini kutokana na imani yake?
Alichagua kwa Hekima “Wakati wa Kusema”
5, 6. (a) Esta alifuataje kanuni ya Mhubiri 3:1, 7? (b) Nini kinachoonyesha kwamba Esta alizungumza na mumewe kwa hekima?
5 Je, Esta angemfunulia mfalme tatizo lake mbele ya watumishi wake? Kama angefanya hivyo angemfedhehesha mfalme na kumpa mshauri wake Hamani nafasi ya kupinga mashtaka hayo. Hivyo, Esta alifanya nini? Karne nyingi mapema, Mfalme Sulemani mwenye hekima aliongozwa na roho ya Mungu kuandika: “Kuna wakati uliowekwa wa kila kitu, . . . wakati wa kukaa kimya na wakati wa kusema.” (Mhu. 3:1, 7) Tunaweza kumwazia mwanamume mwaminifu Mordekai, baba mlezi wa Esta, akimfundisha mwanamke huyo mchanga kanuni hizo alipokuwa akikua chini ya utunzaji wake. Bila shaka, Esta alielewa umuhimu wa kuchagua kwa hekima “wakati wa kusema.”
6 Esta alisema: “Mfalme akiona vema, mfalme na aje leo pamoja na Hamani kwenye karamu ambayo nimemwandalia.” (Esta 5:4) Mfalme alikubali na akaagiza Hamani aitwe. Unaona jinsi Esta alivyozungumza kwa hekima? Hakumvunjia mumewe heshima, badala yake alitafuta wakati unaofaa zaidi wa kumfunulia mahangaiko yake.—Soma Methali 10:19.
7, 8. Karamu ya kwanza ya Esta ilikuwaje, na kwa nini alikawia kuzungumza na mfalme?
7 Bila shaka, Esta alitayarisha karamu hiyo kwa makini, akihakikisha kwamba kila kitu kingempendeza mumewe. Karamu hiyo ilitia ndani divai nzuri ili wawe wenye furaha. (Zab. 104:15) Ahasuero alifurahia karamu hiyo, na akamuuliza tena Esta aseme ombi lake. Je, alipaswa kuzungumza wakati huo?
8 Esta hakufikiri hivyo. Badala yake, alimkaribisha mfalme na Hamani kwenye karamu nyingine, siku iliyofuata. (Esta 5:7, 8) Kwa nini alikawia? Kumbuka, Wayahudi wote wangeuawa kupatana na agizo la mfalme. Kwa sababu ya hatari hiyo kubwa, Esta alipaswa kuzungumza wakati unaofaa. Hivyo basi alingoja, akaandaa nafasi nyingine ya kumwonyesha mume wake jinsi alivyomheshimu sana.
9. Kwa nini subira ni sifa muhimu, na kama Esta tunawezaje kuonyesha subira?
9 Subira ni sifa muhimu sana. Ingawa alihangaika na alitaka sana kusema yaliyokuwa moyoni, Esta alisubiri wakati unaofaa. Tunajifunza mengi kutoka kwake, kwa sababu inaelekea sote tumewahi kuona makosa yanayohitaji kurekebishwa. Ikiwa tunataka kumsadikisha mtu mwenye mamlaka ashughulikie tatizo fulani, huenda tukahitaji kumwiga Esta na kuwa na subira. Andiko la Methali 25:15 linasema: “Kwa subira kiongozi hushawishiwa, na ulimi wa upole unaweza kuvunja mfupa.” Tukisubiri wakati unaofaa, kisha tuzungumze kwa upole, kama Esta, tunaweza hata kuvunja upinzani mgumu kama mfupa. Je, Yehova, Mungu wa Esta alibariki subira na hekima yake?
Subira Yatokeza Haki
10, 11. Kwa nini hisia za Hamani zilibadilika alipoondoka kwenye karamu ya kwanza, na mkewe na rafiki zake walimwomba afanye nini?
10 Subira ya Esta iliongoza kwenye matukio makubwa yaliyofuatana. Hamani aliondoka kwenye karamu ya kwanza akiwa mchangamfu sana, “akiwa na shangwe na furaha moyoni” kwa sababu alialikwa na mfalme na malkia wake. Hata hivyo, Hamani alipokuwa akipita kwenye lango la jumba la mfalme, alimwona Mordekai, Myahudi aliyekataa kumwinamia. Kama tulivyoona katika sura iliyotangulia, Mordekai hakutaka kumvunjia heshima, badala yake, alihangaikia dhamiri yake na uhusiano wake pamoja na Yehova Mungu. Ingawa hivyo, ‘upesi Hamani alijawa na ghadhabu.’—Esta 5:9.
11 Hamani alipomwambia mkewe na rafiki zake kumhusu Mordekai, walimwambia atengeneze mti mkubwa, wenye urefu wa mita 22, kisha amwombe mfalme ruhusa ili amtundike Mordekai juu yake. Hamani alipendezwa na wazo hilo na mara moja akaanza mipango.—Esta 5:12-14.
12. Kwa nini mfalme aliomba asomewe kwa sauti rekodi rasmi za Taifa, na alikumbuka jambo gani?
12 Wakati huohuo, mfalme alishindwa kulala. Biblia inasema: “Usingizi wa mfalme ulimtoka,” na akaagiza asomewe kwa sauti rekodi rasmi za Taifa. Usomaji huo ulitia ndani ripoti kuhusu njama ya kumuua Ahasuero. Alikumbuka tukio hilo; watu waliotaka kumuua walikuwa wamekamatwa na kuuawa. Namna gani Mordekai, ambaye alifunua njama hiyo? Kwa ghafula, mfalme akauliza ikiwa Mordekai alipewa chochote. Alijibiwaje? Hakupewa chochote.—Soma Esta 6:1-3.
13, 14. (a) Mambo yalianzaje kumharibikia Hamani? (b) Mkewe Hamani na rafiki zake walimwambia nini?
13 Akiwa amekasirika, mfalme aliuliza ni maofisa gani wa jumba la mfalme waliokuwapo ili kumsaidia kurekebisha jambo hilo. Hamani ndiye aliyekuwepo, inaonekana alikuwa amefika mapema kwa sababu alitaka sana kupata kibali cha kumuua Mordekai. Lakini kabla ya kutoa ombi lake, mfalme alimuuliza Hamani njia bora zaidi ya kumheshimu mwanamume ambaye alikuwa amepata kibali cha mfalme. Hamani alifikiri mfalme alikuwa akizungumza kumhusu. Hivyo akapendekeza atuzwe kifahari: Mwanamume huyo avishwe mavazi ya kifalme, na apewe ofisa wa cheo cha juu aandamane naye kuzunguka Shushani akiwa amepanda juu ya farasi wa mfalme, akisifiwa kwa sauti ili watu wote wasikie. Wazia jinsi Hamani alivyokata tamaa alipoambiwa kwamba mtu ambaye angeonyeshwa heshima hiyo ni Mordekai! Na mfalme alimpa nani kazi ya kumsifu Mordekai kwa nyimbo? Hamani!—Esta 6:4-10.
14 Bila kutaka, Hamani alifanya kazi hiyo iliyomchukiza, kisha akakimbia kwenda nyumbani akiwa amevunjika moyo. Mkewe na rafiki zake, walimwambia hali hiyo ilionyesha kwamba angepatwa na mabaya; angeshindwa katika vita vyake dhidi ya Mordekai Myahudi.—Esta 6:12, 13.
15. (a) Subira ya Esta ilikuwa na matokeo gani mazuri? (b) Kwa nini ni jambo la hekima kwetu kuwa na ‘mtazamo wa kungoja’?
15 Kwa sababu Esta alionyesha subira, akangoja siku moja zaidi kabla ya kutoa ombi lake kwa mfalme, Hamani alijiletea aibu kubwa. Na je, inawezekana kwamba Yehova Mungu ndiye aliyefanya mfalme akose usingizi? (Met. 21:1) Haishangazi kwamba Neno la Mungu linatutia moyo tuwe na ‘mtazamo wa kungoja’! (Soma Mika 7:7.) Tunapomngojea Mungu, huenda tukatambua kwamba njia yake ya kutatua matatizo ni bora kuliko yetu.
Alisema kwa Ujasiri
16, 17. (a) ‘Wakati wa Esta kusema’ ulitokeaje? (b) Esta alitofautianaje na Vashti, mke wa kwanza wa mfalme?
16 Esta hangethubutu kumfanya mfalme aendelee kusubiri; lazima angemweleza mambo yote kwenye karamu ya pili. Angesemaje? Mfalme alimpa nafasi ya kujieleza, akamuuliza tena kuhusu ombi lake. (Esta 7:2) ‘Wakati wa Esta wa kusema’ ulikuwa umefika.
17 Tunaweza kuwazia Esta akisali kimyakimya kwa Mungu kabla ya kusema maneno haya: “Ikiwa nimepata kibali machoni pako, Ee mfalme, na mfalme akiona vema, na nipewe nafsi yangu mwenyewe kuwa ombi langu na watu wangu kuwa haja yangu.” (Esta 7:3) Ona kwamba alimhakikishia mfalme kuwa aliheshimu uamuzi wake kuhusu mambo yaliyofaa. Esta alikuwa tofauti sana na Vashti ambaye alimfedhehesha mumewe kimakusudi! (Esta 1:10-12) Isitoshe, Esta hakumkosoa mfalme kwa kumwamini Hamani. Badala yake, alimwomba mfalme amlinde kutokana na hatari iliyomkabili.
18. Esta alimfunuliaje mfalme tatizo lake?
18 Bila shaka, ombi hilo lilimshtua sana mfalme. Ni nani angethubutu kumuua malkia? Esta aliendelea kusema: “Tumeuzwa, mimi na watu wangu, tuangamizwe, tuuawe na kuharibiwa. Basi ikiwa tungaliuzwa tuwe watumwa na wajakazi, ningalinyamaza kimya. Lakini taabu hii haifai ikiwa inamletea mfalme hasara.” (Esta 7:4) Ona kwamba Esta alifunua tatizo hilo waziwazi, lakini akasema angenyamaza ikiwa hatari ilikuwa kuuzwa tu kama watumwa. Hata hivyo, hangenyamaza kwa sababu mauaji hayo yangemletea mfalme hasara kubwa.
19. Tunajifunza nini kutoka kwa Esta kuhusu kuzungumza kwa ushawishi?
19 Mfano wa Esta unatufunza mengi kuhusu kuzungumza kwa ushawishi. Ikiwa ungependa kufunua tatizo zito kwa mtu unayempenda au hata mtu mwenye mamlaka, utafaulu ikiwa utaonyesha subira, heshima, na kusema mambo waziwazi.—Met. 16:21, 23.
20, 21. (a) Esta alifunuaje njama ya Hamani, na mfalme alitendaje? (b) Hamani alitendaje alipofunuliwa kuwa mwoga mwenye hila?
20 Ahasuero aliuliza: “Ni nani huyo, na yuko wapi mtu huyo ambaye amejipatia ujasiri wa kufanya hivyo?” Wazia Esta akinyoosha kidole chake na kusema: “Mtu huyo, mpinzani na adui, ni huyu Hamani mtu mbaya.” Mambo yalikuwa yameharibika. Hamani akajawa na hofu. Wazia jinsi uso wa mfalme huyo mwenye hasira ulivyokuwa mwekundu alipotambua kwamba mshauri wake aliyemwamini alikuwa amemdanganya atie sahihi agizo ambalo lingemwangamiza mke wake mpendwa! Mfalme akatoka kwa hasira na kwenda kwenye bustani ili atulie.—Esta 7:5-7.
21 Hamani, aliyekuwa amefunuliwa kuwa mwoga mwenye hila aliinama miguuni pa malkia. Mfalme aliporudi chumbani na kumwona Hamani akimsihi Esta kitandani, kwa hasira alisema kwamba Hamani alikuwa akijaribu kumlala malkia kinguvu katika nyumba ya mfalme. Hiyo ilikuwa hukumu ya kifo kwa Hamani. Aliondolewa huku uso wake ukiwa umefunikwa. Kisha, mmoja wa maofisa wa mfalme akapaaza sauti na kumwambia mfalme kuhusu mti mkubwa ambao Hamani alikusudia kumtundika Mordekai. Mara moja, Ahasuero akaagiza Hamani atundikwe kwenye mti huo.—Esta 7:8-10.
22. Mfano wa Esta unawezaje kutusaidia tusikate tamaa, tusiwe na shaka, wala kukosa imani?
22 Katika ulimwengu wa leo usio na haki, ni rahisi kuwazia kwamba haki haitawahi kutekelezwa. Umewahi kuhisi hivyo? Esta hakukata tamaa kamwe, hakuwa na shaka, wala kukosa imani. Wakati ulipofika, alisema kwa ujasiri kuhusu mambo yaliyofaa, na aliamini kwamba Yehova angechukua hatua. Acheni tufanye hivyo pia! Yehova hajabadilika tangu siku za Esta. Bado anaweza kuwanasa waovu na wenye hila katika mitego yao wenyewe, kama alivyomnasa Hamani.—Soma Zaburi 7:11-16.
Alitenda Bila Ubinafsi kwa Ajili ya Yehova na Watu Wake
23. (a) Mordekai na Esta walithawabishwaje na mfalme? (b) Unabii ambao Yakobo alitoa alipokaribia kufa kuhusu Benyamini ulitimizwaje? (Ona sanduku “Unabii Watimizwa.”)
23 Mwishowe, mfalme alijua Mordekai alikuwa nani. Hakuwa tu mtu aliyemlinda asiuawe bali pia baba mlezi wa Esta. Ahasuero alimpa Mordekai cheo cha Hamani cha kuwa waziri mkuu. Kisha, akampa Esta nyumba ya Hamani kutia ndani utajiri wake mwingi, naye Esta akamweka Mordekai kuwa msimamizi wa nyumba hiyo.—Esta 8:1, 2.
24, 25. (a) Kwa nini Esta hangestarehe baada ya njama ya Hamani kufunuliwa? (b) Esta alihatarishaje uhai wake tena?
24 Sasa kwa kuwa Esta na Mordekai walikuwa salama, je, malkia angestarehe? Angefanya hivyo tu ikiwa angekuwa na ubinafsi. Wakati huo, agizo la Hamani la kuwaua Wayahudi wote bado lilikuwa likisambazwa kotekote katika milki hiyo. Hamani alikuwa amepiga kura, au Puri—aina ya uwasiliano roho—ili kuamua wakati uliofaa wa kutekeleza mashambulizi hayo ya kikatili. (Esta 9:24-26) Miezi kadhaa ilibaki kabla ya siku hiyo kufika, lakini muda ulikuwa unayoyoma. Je, msiba huo ungeepukwa?
25 Esta alitenda bila ubinafsi na akahatarisha uhai wake tena kwa kwenda mbele ya mfalme bila kuitwa. Wakati huu, alilia kwa ajili ya watu wake, na kumsihi mume wake afutilie mbali agizo alilokuwa ametoa. Lakini sheria zilizopitishwa katika jina la mfalme wa Uajemi hazingebadilishwa. (Dan. 6:12, 15) Hivyo, mfalme alimpa Esta na Mordekai mamlaka ya kuandika sheria mpya. Basi, tangazo la pili likatolewa, na kuwapa Wayahudi haki ya kujilinda. Wapanda-farasi wakaenda upesi kila sehemu ya milki hiyo, na kuwapelekea Wayahudi habari hizo njema. Wengi wakawa na matumaini. (Esta 8:3-16) Tunaweza kuwazia Wayahudi kotekote katika milki hiyo kubwa wakijihami kwa silaha, tayari kupigana, jambo ambalo hawangefanya ikiwa sheria hiyo mpya haingepitishwa. Lakini jambo muhimu ni, je, “Yehova wa majeshi” angekuwa pamoja na watu wake?—1 Sam. 17:45.
26, 27. (a) Ushindi ambao Yehova aliwapa watu wake dhidi ya adui zao ulikuwa mkubwa kadiri gani? (b) Ni unabii gani uliotimizwa baada ya wana wa Hamani kuangamizwa?
26 Siku iliyochaguliwa ilipofika, watu wa Mungu walikuwa tayari. Hata maofisa wengi wa Uajemi sasa waliwaunga mkono, kwa kuwa habari zilikuwa zimesambaa kumhusu waziri mkuu mpya, Mordekai yule Myahudi. Yehova akawapa watu wake ushindi mkubwa. Bila shaka, aliwalinda watu wake ili wasishambuliwe tena kwa kuhakikisha kwamba waliwashinda kabisa adui zao.a—Esta 9:1-6.
27 Zaidi ya hayo, Mordekai hangesimamia nyumba ya Hamani akiwa salama huku wana kumi wa mwanamume huyo mwovu wakiwa hai. Wao pia waliuawa. (Esta 9:7-10) Hivyo, unabii wa Biblia ukatimia, kwa sababu Mungu alikuwa ametabiri mapema kwamba Waamaleki, ambao walikuwa maadui waovu wa watu wake, wangeangamizwa kabisa. (Kum. 25:17-19) Yaelekea wana wa Hamani ndio waliokuwa watu wa mwisho kuangamizwa kutoka katika taifa hilo lililolaaniwa.
28, 29. (a) Kwa nini Yehova alitaka Esta na watu wake wapigane vita? (b) Kwa nini mfano wa Esta ni muhimu kwetu?
28 Esta alilazimika kutimiza majukumu mazito, yaliyotia ndani kutoa maagizo ya kifalme yaliyohusisha vita na mauaji. Haikuwa rahisi. Lakini mapenzi ya Yehova yalikuwa kwamba watu wake walindwe ili wasiangamizwe; taifa la Israeli lingetokeza Masihi aliyeahidiwa, ambaye angekuwa chanzo pekee cha tumaini la wanadamu wote! (Mwa. 22:18) Leo, watumishi wa Mungu wanafurahi kujua kwamba yule Masihi, Yesu, alipokuja duniani, aliwaagiza wafuasi wake kutoka wakati huo na kuendelea wasipigane vita vya kimwili.—Mt. 26:52.
29 Hata hivyo, Wakristo wanapigana vita vya kiroho; Shetani anatamani sana kuharibu imani yetu kwa Yehova Mungu. (Soma 2 Wakorintho 10:3, 4.) Ni baraka iliyoje kuwa na mfano kama wa Esta! Kama yeye, na tuonyeshe imani kwa kuwa na ujasiri, kutumia ushawishi kwa subira na hekima, na kuwa tayari kutenda bila ubinafsi katika kuwatetea watu wa Mungu.
a Mfalme aliwaruhusu Wayahudi waendelee kupigana na adui zao siku iliyofuata ili wawashinde kabisa. (Esta 9:12-14) Mpaka leo, Wayahudi husherehekea ushindi huo kila mwaka katika mwezi wa Adari, ambao unalingana na mwishoni mwa Februari na mwanzoni mwa Machi. Sherehe hiyo inaitwa Purimu, na ilipata jina kutokana na kura ambayo Hamani alipiga alipokuwa akipanga kuwaangamiza Waisraeli.