Matendo
3 Basi Petro na Yohana walikuwa wakipanda kwenda kuingia katika hekalu kwa ajili ya saa ya sala, saa ya tisa, 2 na mwanamume fulani aliyekuwa kilema kutoka katika tumbo la uzazi la mama yake alikuwa akibebwa, nao walikuwa wakimweka kila siku karibu na mlango wa hekalu ulioitwa Mzuri, ili kuomba zawadi za rehema kutoka kwa wale wenye kuingia katika hekalu. 3 Alipoona mara hiyo Petro na Yohana wakiwa karibu kuingia ndani ya hekalu alianza kuomba apate zawadi za rehema. 4 Lakini Petro, pamoja na Yohana, wakamkodolea macho na kusema: “Tutazame.” 5 Kwa hiyo akawakazia uangalifu wake, akitarajia kupata kitu fulani kutoka kwao. 6 Hata hivyo, Petro akasema: “Fedha na dhahabu sina, lakini kile nilicho nacho ndicho nikupacho: Katika jina la Yesu Kristo Mnazareti, tembea!” 7 Ndipo akamshika mkono wa kuume na kumwinua. Hapohapo nyayo za miguu yake na vifundo vya miguu yake vikafanywa imara; 8 na, akiruka juu, akasimama na kuanza kutembea, naye akaingia pamoja nao katika hekalu, akitembea na kuruka-ruka na kumsifu Mungu. 9 Na watu wote wakapata kumwona akitembea na kumsifu Mungu. 10 Zaidi ya hayo, wakaanza kumtambua, kwamba huyu ndiye mtu aliyekuwa na kawaida ya kuketi kwa ajili ya zawadi za rehema penye Lango Zuri la hekalu, nao wakajawa na mshangao na upeo wa shangwe kwa lililokuwa limetukia kwake.
11 Basi, kwa kuwa huyo mtu alikuwa akishikilia Petro na Yohana, watu wote waliwakimbilia pamoja kwenye ile iliyoitwa safu ya nguzo ya Solomoni, wakiwa wamepotewa na akili kwa mshangao. 12 Petro alipoona hili, akawaambia hao watu: “Wanaume wa Israeli, kwa nini mnastaajabu juu ya hili, au kwa nini mnatukodolea macho kama kwamba kwa nguvu ya binafsi au ujitoaji-kimungu tumemfanya atembee? 13 Mungu wa Abrahamu na wa Isaka na wa Yakobo, Mungu wa baba zetu wa zamani, amemtukuza Mtumishi wake, Yesu, ambaye nyinyi, kwa upande wenu, mlimkabidhi na kumkana mbele ya uso wa Pilato, alipokuwa ameamua kumfungua. 14 Ndiyo, nyinyi mlimkana huyo aliye mtakatifu na mwadilifu, nanyi mkaomba mpewe kwa hiari mwanamume, muuaji-kimakusudi, 15 lakini mlimuua Wakili Mkuu wa uhai. Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, uhakika ambao sisi ni mashahidi wao. 16 Kwa sababu hiyo, kwa imani yetu katika jina lake, jina lake limemfanya awe mwenye nguvu mtu huyu ambaye mwamwona na kumjua, na imani iliyo kupitia yeye imempa mtu huyu utimamu kamili huu mbele ya macho yenu nyote. 17 Na sasa, akina ndugu, najua kwamba mlitenda kwa kutokuwa na ujuzi, kama vile watawala wenu pia walivyofanya. 18 Lakini katika njia hiyo Mungu ametimiza mambo aliyotangaza kimbele kupitia kinywa cha manabii wote, kwamba Kristo wake angeteseka.
19 “Kwa hiyo, tubuni na mgeuke kabisa ili mpate kufutiwa dhambi zenu, ili majira ya kuburudisha yapate kuja kutoka kwa utu wa Yehova 20 na kwamba apate kumtuma Kristo aliyewekwa rasmi kwa ajili yenu, Yesu, 21 ambaye mbingu, kwa kweli, lazima imweke ndani yayo yenyewe hadi nyakati za kurudishwa kwa mambo yote ambayo Mungu alisema kupitia kinywa cha manabii wake watakatifu wa wakati wa kale. 22 Kwa kweli, Musa alisema, ‘Yehova Mungu atawainulia kutoka miongoni mwa ndugu zenu nabii kama mimi. Lazima mmsikilize yeye kulingana na mambo yote awaambiayo nyinyi. 23 Kwa kweli, nafsi yoyote isiyomsikiliza Nabii huyo itaangamizwa kabisa kutoka miongoni mwa watu.’ 24 Na kwa kweli, manabii wote tangu Samweli na kuendelea na wale wenye kufuata, wengi kadiri ambayo wamesema, wamezitangaza waziwazi pia siku hizi. 25 Nyinyi ndio wana wa manabii na wa agano ambalo Mungu aliagana pamoja na baba zenu wa zamani, akimwambia Abrahamu, ‘Na katika mbegu yako familia zote za dunia zitabarikiwa.’ 26 Baada ya kumwinua Mtumishi wake, Mungu alimtuma kwenu kwanza ili kuwabariki nyinyi kwa kugeuzia mbali kila mmoja kutoka kwenye vitendo vyenu viovu.”