Matendo
6 Sasa siku hizi, wanafunzi walipokuwa wakiongezeka, mnung’uniko ulitokea kwa upande wa Wayahudi wenye kusema Kigiriki dhidi ya Wayahudi wenye kusema Kiebrania, kwa sababu wajane wao walikuwa hawaangaliwi katika ugawanyaji wa kila siku. 2 Kwa hiyo wale kumi na wawili wakauita umati wa wanafunzi kwao na kusema: “Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu ili kugawa chakula kwenye meza. 3 Kwa hiyo, akina ndugu, jitafutieni nyinyi wenyewe wanaume saba wenye kuthibitishwa kutoka miongoni mwenu, wenye kujaa roho na hekima, ili tupate kuwaweka rasmi juu ya shughuli hii ya lazima; 4 lakini sisi tutajitoa wenyewe kwa sala na kwa huduma ya neno.” 5 Na hilo jambo lililosemwa likawa lenye kuupendeza umati wote, nao wakateua Stefano, mwanamume mwenye kujaa imani na roho takatifu, na Filipo na Prokoro na Nikanori na Timoni na Parmenasi na Nikolausi, mgeuzwa-imani wa Antiokia; 6 nao wakawaweka mbele ya mitume, na, wakiisha kusali, hawa wakaweka mikono yao juu yao.
7 Kwa sababu hiyo neno la Mungu likaendelea kukua, na idadi ya wanafunzi ikafuliza kuzidi sana katika Yerusalemu; na umati mkubwa wa makuhani ukaanza kuwa mtiifu kwa imani.
8 Sasa Stefano, akiwa mwenye kujaa wema na nguvu, alikuwa akifanya mambo makubwa ya ajabu na ishara miongoni mwa watu. 9 Lakini watu fulani wakainuka kati ya wale wa kutoka liitwalo kwa kawaida Sinagogi la Watu Waliowekwa Huru, na kati ya Wakirene na Waaleksandria na kati ya wale wa kutoka Kilikia na Asia, ili kubishana na Stefano; 10 na bado hawakuweza kufaulu katika pambano dhidi ya hekima na roho aliyokuwa akisema kwayo. 11 Ndipo kwa siri wakashawishi wanaume kusema: “Tumemsikia akisema semi zenye kufuru dhidi ya Musa na Mungu.” 12 Nao wakawachochea watu na wanaume wazee na waandishi, na, wakimjia yeye kwa ghafula, wakamchukua kwa nguvu na kumwongoza hadi kwenye Sanhedrini. 13 Nao wakatokeza mbele mashahidi wasio wa kweli, waliosema: “Mtu huyu hakomi kusema mambo dhidi ya mahali patakatifu hapa na dhidi ya Sheria. 14 Kwa mfano, tumemsikia akisema kwamba Yesu huyu Mnazareti atapaangusha chini mahali hapa na kuzibadili desturi ambazo Musa alitukabidhi.”
15 Na wote wale wenye kuketi katika Sanhedrini walipokuwa wakimkodolea macho, wakaona kwamba uso wake ulikuwa kama uso wa malaika.