1 Wakorintho
4 Acheni mtu atukadirie sisi hivyo kama walio chini ya Kristo na wasimamizi-nyumba wa siri takatifu za Mungu. 2 mbali na hilo, katika kisa hiki, kitafutwacho katika wasimamizi-nyumba ni mtu kupatwa akiwa mwaminifu. 3 Sasa kwangu ni jambo lisilo la maana sana kwamba nichunguzwe nanyi au na baraza la kibinadamu. Hata mimi sijichunguzi mwenyewe. 4 Kwa maana sifahamu kitu chochote dhidi yangu mwenyewe. Lakini sithibitishwi kuwa mwadilifu na hilo, bali yeye anichunguzaye ni Yehova. 5 Kwa sababu hiyo msihukumu kitu chochote kabla ya wakati upasao, mpaka Bwana aje, atakayeyaleta mambo ya siri yaliyo ya giza kwenye nuru na pia kufanya mashauri ya mioyo kuwa dhahiri, na ndipo kila mmoja atakapopata sifa yake ikimjia kutoka kwa Mungu.
6 Basi, akina ndugu, mambo haya nimeyahamisha ili kuyatumia juu yangu mwenyewe na Apolo kwa faida yenu, ili katika kisa chetu mpate kujifunza kanuni: “Msiyapite mambo ambayo yameandikwa,” ili msipate kujitutumua mkiwa mtu mmoja-mmoja kwa kupendelea mmoja dhidi ya mwingine. 7 Kwa maana ni nani akufanyaye utofautiane na mwingine? Kwa kweli, ni nini ulicho nacho ambacho hukupokea? Basi, ikiwa kwa kweli ulikipokea, kwa nini wajisifu kama kwamba hukukipokea?
8 Nyinyi watu tayari mmepata shibe yenu, sivyo? Nyinyi tayari ni matajiri, sivyo? Nyinyi mmeanza kutawala mkiwa wafalme bila sisi, sivyo? Nami nataka kwa kweli kwamba mngalikuwa mmeanza kutawala mkiwa wafalme, ili sisi pia tupate kutawala pamoja nanyi tukiwa wafalme. 9 Kwa maana yaonekana kwangu kwamba Mungu ametuweka sisi mitume mwisho katika wonyesho wa hadharani kama watu waliowekewa kifo, kwa sababu tumekuwa kitu cha kutazamwa mahali pa michezo kwa ulimwengu, na kwa malaika, na kwa wanadamu. 10 Sisi ni wapumbavu kwa sababu ya Kristo, lakini nyinyi ni wenye busara katika Kristo; sisi ni dhaifu, lakini nyinyi ni wenye nguvu; nyinyi mna sifa njema, lakini sisi tumo katika kufedheheshwa. 11 Hadi kwenye saa hiihii twaendelea kuwa na njaa na pia kuwa na kiu na kuvikwa mavazi kwa uhaba na kupigwa huku na huku na kuwa bila makao 12 na kumenyeka, tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tunapotukanwa, twabariki; tunaponyanyaswa, twahimili; 13 tunapoharibiwa sifa, twasihi sana; tumekuwa kama takataka ya ulimwengu, makorokoro ya vitu vyote, hadi sasa.
14 Ninaandika mambo haya, si kuwaaibisha nyinyi, bali kuwaonya kwa upole kama watoto wangu wapendwa. 15 Kwa maana ingawa huenda mkawa mna wafunzi elfu kumi katika Kristo, hakika si baba wengi mlio nao; kwa maana katika Kristo Yesu mimi nimekuwa baba yenu kupitia habari njema. 16 Kwa hiyo, nawasihi sana nyinyi, iweni waigaji wangu. 17 Hiyo ndiyo sababu ninatuma Timotheo kwenu, kwa kuwa yeye ni mtoto wangu mpendwa na mwaminifu katika Bwana; naye atawakumbusha nyinyi njia zangu kuhusiana na Kristo Yesu, kama vile ninavyofundisha kila mahali katika kila kutaniko.
18 Wengine wamejitutumua kama kwamba sikuwa ninakuja kwenu nyinyi. 19 Lakini hakika nitakuja kwenu upesi, Yehova akipenda, nami nitapata kujua, si usemi wa wale ambao wamejitutumua, bali nguvu yao. 20 Kwa maana ufalme wa Mungu hauwi katika usemi, bali katika nguvu. 21 Mwataka nini? Je, niwajie nyinyi kwa fimbo, au kwa upendo na upole wa roho?