1 Yohana
Ya Kwanza ya Yohana
1 Kile kilichokuwako tangu mwanzo, ambacho tumesikia, ambacho tumeona kwa macho yetu, ambacho tumetazama kwa uangalifu na mikono yetu ikagusa, kuhusu neno la uhai, 2 (ndiyo, uhai ulifanywa dhahiri, na sisi tumeona na tunatoa ushahidi na kuripoti kwenu uhai udumuo milele ambao ulikuwa pamoja na Baba na ukafanywa dhahiri kwetu,) 3 kile ambacho tumeona na kusikia tunaripoti kwenu pia, ili nyinyi pia mwe mkiwa na ushirika pamoja na sisi. Zaidi ya hilo, ushirika huu wetu ni pamoja na Baba na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo. 4 Na kwa hiyo tunaandika mambo haya ili shangwe yetu ipate kuwa katika kipimo kilichojaa.
5 Na huu ndio ujumbe ambao tumesikia kutoka kwake na tunawatangazia nyinyi, kwamba Mungu ni nuru na hakuna giza kamwe katika muungano na yeye. 6 Ikiwa twatoa taarifa: “Sisi tunakuwa na ushirika pamoja na yeye,” na bado tunaendelea kutembea katika giza, tunasema uwongo na hatuzoei kweli. 7 Hata hivyo, ikiwa tunatembea katika nuru kama yeye mwenyewe alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi, na damu ya Yesu Mwana wake hutusafisha kutoka katika dhambi yote.
8 Ikiwa twatoa taarifa: “Sisi hatuna dhambi yoyote,” tunajiongoza wenyewe vibaya na kweli haimo katika sisi. 9 Ikiwa twaungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na mwadilifu hata kutusamehe dhambi zetu na kutusafisha ukosefu wote wa uadilifu. 10 Ikiwa twatoa taarifa: “Sisi hatujafanya dhambi,” tunamfanya yeye mwongo, na neno lake halimo ndani yetu.