Waamuzi
4 Baada ya Ehudi kufa, Waisraeli wakaanza tena kutenda maovu machoni pa Yehova.+ 2 Kwa hiyo Yehova akawatia mikononi mwa* Yabini mfalme wa Kanaani,+ aliyetawala Hasori. Mkuu wa jeshi lake aliitwa Sisera, naye aliishi Haroshethi+ ya mataifa.* 3 Waisraeli wakamlilia Yehova+ kwa sababu Yabini alikuwa na magari 900 ya vita yenye miundu ya chuma,*+ na kwa miaka 20 aliwakandamiza sana Waisraeli.+
4 Basi Debora, nabii wa kike,+ mke wa Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati huo. 5 Naye alizoea kuketi chini ya mtende wa Debora uliokuwa kati ya Rama+ na Betheli+ katika eneo lenye milima la Efraimu; Waisraeli walikuwa wakienda kwake ili kupata maamuzi. 6 Akatuma mjumbe amwite Baraka+ mwana wa Abinoamu kutoka Kedesh-naftali,+ akamwambia, “Yehova Mungu wa Israeli anakuamuru hivi: ‘Nenda* katika Mlima Tabori ukiwa na wanaume 10,000 kutoka kabila la Naftali na la Zabuloni. 7 Nitakuletea Sisera, mkuu wa jeshi la Yabini na magari yake ya vita na majeshi yake kwenye kijito cha* Kishoni,+ nami nitamtia mikononi mwako.’”+
8 Ndipo Baraka akamwambia, “Ukienda pamoja nami, nitaenda, lakini usipoenda pamoja nami, sitaenda.” 9 Basi Debora akamwambia, “Hakika nitaenda pamoja nawe. Hata hivyo, hutapata sifa katika vita hivyo, kwa kuwa Yehova atamtia Sisera mikononi mwa mwanamke.”+ Ndipo Debora akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi.+ 10 Baraka akawaita watu wa kabila la Zabuloni na Naftali+ waje Kedeshi, na wanaume 10,000 wakamfuata. Debora pia akamfuata.
11 Lakini Heberi Mkeni alikuwa amejitenga na Wakeni,+ waliokuwa wazao wa Hobabu, baba mkwe wa Musa,+ naye alipiga hema lake karibu na mti mkubwa uliokuwa Saananimu, kule Kedeshi.
12 Wakamwambia Sisera kwamba Baraka mwana wa Abinoamu amepanda kwenda kwenye Mlima Tabori.+ 13 Mara moja Sisera akakusanya magari yake yote ya vita—magari 900 yenye miundu ya chuma*—na wanajeshi wote walioandamana naye kutoka Haroshethi ya mataifa na kwenda kwenye kijito cha* Kishoni.+ 14 Ndipo Debora akamwambia Baraka: “Inuka! Kwa maana hii ndiyo siku ambayo Yehova atamtia Sisera mikononi mwako. Yehova anakutangulia.” Na Baraka akashuka Mlima Tabori akifuatwa na wanaume 10,000. 15 Kisha Yehova akamvuruga+ Sisera na magari yake yote ya vita na jeshi lake lote na kuwaangamiza kwa upanga wa Baraka. Ndipo Sisera akatoka katika gari lake na kukimbia kwa miguu. 16 Baraka akayafuatia yale magari ya vita na lile jeshi mpaka Haroshethi ya mataifa. Jeshi lote la Sisera likaangamizwa kwa upanga; hakubaki hata mtu mmoja.+
17 Lakini Sisera akakimbia kwa miguu mpaka kwenye hema la Yaeli+ mke wa Heberi Mkeni,+ kwa maana kulikuwa na amani kati ya Yabini+ mfalme wa Hasori na nyumba ya Heberi Mkeni. 18 Kisha Yaeli akatoka nje kumpokea Sisera, akamwambia, “Karibu bwana wangu, karibu ndani. Usiogope.” Basi akaingia ndani ya hema lake, naye Yaeli akamfunika kwa blanketi. 19 Sisera akamwambia, “Tafadhali, nipe maji kidogo ya kunywa, kwa maana nina kiu.” Basi Yaeli akafungua kiriba cha ngozi chenye maziwa na kumpa anywe,+ kisha akamfunika tena. 20 Sisera akamwambia, “Simama kwenye mlango wa hema, na mtu yeyote akija kukuuliza kama kuna yeyote hemani, mwambie, ‘Hakuna!’”
21 Lakini Yaeli mke wa Heberi akachukua kigingi cha hema na nyundo. Kisha Sisera alipokuwa amelala usingizi mzito kwa sababu ya uchovu, Yaeli akaenda kimyakimya na kukipigilia kile kigingi kichwani mwake,* nacho kikapenya mpaka udongoni, akafa.+
22 Baraka alipokuwa anamtafuta Sisera, Yaeli akatoka nje kumpokea, akamwambia, “Njoo nikuonyeshe mtu unayemtafuta.” Baraka akamfuata hemani, akamwona Sisera akiwa amekufa, kigingi kikiwa kichwani mwake.
23 Basi siku hiyo, Mungu akamshinda Yabini mfalme wa Kanaani mbele ya Waisraeli.+ 24 Na Waisraeli wakaendelea kuwa na nguvu* na kumshinda Yabini mfalme wa Kanaani,+ mpaka walipomwangamiza Yabini mfalme wa Kanaani.+