Matendo Mabaya Mno ya Ukatili Juu ya Wakristo Malawi
UKATILI mwingine wa kuhuzunisha unatendwa kwa wachache wasio na ulinzi katika nchi ya Afrika Mashariki ya Malawi. Ni jambo la kinyama, la kutokuwa na kanuni zo zote za adabu na za huruma ya kibinadamu. Linaonyesha jinsi wanadamu wanavyoweza kutendea wenzao kwa njia yenye kuhuzunisha—watu wa kabila na taifa lao wenyewe. Ni jambo ambalo limepaswa kuvuta fikira za watu wote wanaopenda haki, naam, wanaopenda wote wawe na uhuru bila kujali kabila, rangi wala dini.
Siku hizi, mtu mmoja tu anapotekwa na maharamia, jambo hilo hutangazwa sana. Watu hupenda sana kuona jitihada zikifanywa za kumfungua aliyeshikwa. Lakini katika Malawi tangu Septemba wa 1975, makumi ya maelfu ya mashahidi wa Yehova, wenyeji wa Malawi, wamekuwa wakiogofishwa. Miaka mitatu iliyopita walikimbilia Msumbiji na Zambia kuepuka utawala wa Malawi wa kutumia maogofyo. Sasa wamelazimishwa kurudi. Wametukanwa katika nchi yao wenyewe, wamefanyiwa jeuri katika miili yao na kutendwa namna zote za mambo ya kuwavunjia heshima. Wamenyang’anywa mali zao chache wakaachwa bila njia za kujipatia riziki wao wenyewe na watoto wao.
Katika mambo hayo yote hawapati msaada kwa wenye kufikiliza sheria. Hakuna hata mmoja kati ya wakuu wote wa Malawi wanayeweza kumwendea akawalinde na washambuliaji wanaowapiga, kuwanyang’anya na kuwanajisi wapendavyo. Wao ni mateka katika nchi yao wenyewe, nchi ambamo walizaliwa na kulelewa. Mipaka ya nchi hiyo imekuwa kwao kama kuta za gereza kubwa. Hali hizo zafanana na zilizokuwako katika Ujeremani ya Nazi, ambako maelfu ya mashahidi wa Yehova walifungwa na kuuawa. Nazo hali hizo zinazidi kufanana sasa, kwa maana Malawi imeanzisha kambi zake yenyewe za mateso za kuwekea mashahidi wa Yehova. Hata imefikia hatua ya kupita kiasi ya kutengamsha baba na mama za Kikristo na watoto wao, hata vikiwa ni vitoto vichanga tu.
Na sababu gani haya yote yanafanywa? Je! watu hawa ni hatari kwa nchi—ni wenye kutaka mapinduzi, wenye hila? Sivyo walivyo kabisa. Bila shaka wao wamo miongoni mwa raia wenye kutaka zaidi amani, wenye bidii zaidi na wenye kutii sheria zaidi katika nchi yote. Ukatili na matendo ya kuwavunjia heshima yanafanywa kwa sababu moja, tena sababu moja tu. Hiyo ni kwa sababu wao hawahusiki na siasa. Hawajiungi nazo kwa sababu ya imani zao katika Biblia na mafundisho ya Kristo Yesu, aliyesema kwamba wafuasi wake “si wa ulimwengu.” (Yohana 15:17-19) Kwa hiyo, dhamiri yao haiwaruhusu kununua kadi yenye kuwatangaza kuwa wanachama wa chama cha kisiasa chenye kutawala cha Malawi—Malawi Congress Party. Kwa sababu hiyo, wanatendwa kama wenye kustahili kutendwa vile ambavyo kwa kawaida wanadamu hutenda wanyama.
Huenda wengine wakaelekea kusema, ‘Hicho ni kitu kidogo. Sababu gani wasinunue kadi hiyo wasipatwe na matata?’ Bila shaka hilo ndilo lingekuwa jambo jepesi zaidi kufanya. Kama ingalikuwa ni kulipa kodi au kulipia hati fulani ya kujitambulisha au cedula (ambayo mashahidi wa Yehova katika nchi nyingi hulipa na kuchukua kwa kutii sheria za nchi zao mbalimbali), wao wangalilipa. Lakini hapa suala linahusu shina lenyewe hasa la imani yao na msimamo wao wa Kikristo. Kristo Yesu alimwambia gavana wa Kirumi Pontio Pilato hivi: “Ufalme wangu sio wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu, watumishi wangu wangenipigania.” (Yohana 18:36) Kama mashahidi wa Yehova wangeanza kujiunga na vyama vya kisiasa vya ulimwengu huu wangekuwa wakikana waziwazi kile wanachodai kuamini na kutetea. Ingawa wao hawatamani kuteswa, watakubali kufanyiwa hivyo hata kufa badala ya kuwa wasioaminika kwa Mungu na Mwanawe.
Ndivyo walivyoona Wakristo katika karne za kwanza. Unaweza kusoma vitabu vya historia juu ya jitihada zilizofanywa na wakuu wa Kirumi kufanya Wakristo wa kwanza watoe dhabihu kwa “akili nyingi” za mfalme, hata kwa kitendo kidogo cha kuweka ubani kidogo tu juu ya madhabahu kama dhabihu. Historia moja yasema hivi juu ya Wakristo walioingizwa katika arena (wanja kubwa za michezo kama ya kupambana na wanyama n. k.) za Kirumi wakafe: “Ni Wakristo wachache sana walioacha imani zao, ingawa katika uwanja wa michezo kulikuwa na moto uliokuwa ukiwaka juu ya madhabahu kwa kawaida waweze kuutumia. Jambo moja tu alilopaswa kufanya mfungwa ni kufukiza ubani kidogo sana katika mwali wa moto naye alipewa Hati ya Kutoa Dhabihu na kuachiliwa. . . . Hata hivyo, karibu Wakristo wote walikosa kujipatia nafasi ya kufanya hivyo ndiyo waokoke.”—Those About to Die, Daniel P. Mannix, kur. 135, 137.
Jiulize hivi, Ni jambo jipi linaloonyesha vizuri zaidi kwamba mtu ni raia mwema, kununua kadi ya chama cha kisiasa na kuichukua unapotembea—jambo ambalo linaweza kufanywa na mhalifu ye yote au hata msaliti—au kuishi kwa kutii sheria za nchi na kujihakikisha kuwa mwenye bidii, mwenye adabu, mwaminifu na mwenye kuheshimu watu, kupenda jirani kama ujipendavyo? Hata wakuu wa Malawi wanajua jinsi ulivyo upuzi kuona uchukuaji wa kadi ya kisiasa kama ndiyo njia bora ya kujaribia raia wema. Kama wasingalijua hivyo wasingalikana mara kwa mara kwamba hiyo siyo sababu ya mambo hayo kutendeka, wala wasingalikana kwamba hakuna mtu anayejaribu kulazimisha watu wanunue kadi hizo.
Lakini mambo ya hakika yako wazi kabisa, nayo yaonyesha matendo ya ukatili, ya kuogofya, ya kuhuzunisha sana. Sasa angalia kwa ufupi mambo ambayo mashahidi wa Yehova wamelazimika kuvumilia Malawi miaka kumi iliyopita hata leo hii.
[Picha katika ukurasa wa 220]
1975
KWACHA!
DR. H. KAMUZU BANDA
(KHADI LA UMEMBALA).
MALAWI CONGRESS PARTY.
Chopereka 22t.
KADI YA UANACHAMA
Kwacha! = Kumepambauka, yaani, Uhuru umepatikana.
Khadi la Umembala = Kadi ya Uanachama.
Chopereka 22t = Mchango tambala 22 [karibu shilingi 2 au 14Kb].