Watu Wakaidi Wapuza Katiba ya Malawi
KATIBA ya Jamhuri ya Malawi, iliyochaguliwa mwaka 1966, ina mpango huu katika sura yake ya kwanza:
“(iii) Serikali na watu wa Malawi wataendelea kutambua utakatifu wa uhuru wa kipekee uliowekwa katika United Nations Universal Declaration of Human Rights, na wa kushikamana na Sheria ya Mataifa.”
Ni baadhi ya mambo gani yaliyo kati ya uhuru huo wa kipekee, ambao utakatifu wayo ungetambuliwa? Makala zifuatazo zinasema hivi:
“(iv) Hakuna mtu atakayenyang’anywa mali yake bila ya kulipwa malipo anayostahili, hata ikiwa jambo hilo linatakiwa kufanywa kwa faida ya raia.
“(v) Watu wote wamepaswa kuwa na usawa wa haki na uhuru bila kujali rangi, taifa wala imani.”
Lakini muda mfupi tangu kuchaguliwa kwa katiba hiyo, watu wakaidi nchini wameyapuza maneno hayo.
Hata kabla ya kuandikwa katiba hii ya karibuni zaidi, mashahidi wa Yehova katika Malawi walifanyiwa mashambulio makali sana mwaka wa 1964. Jumla ya nyumba zao 1,081 na zaidi ya mahali 100 pa mikutano yao, panapoitwa Majumba ya Ufalme, paliteketezwa kwa moto au pakaharibiwa kwa njia nyingine. Mamia ya mashamba yao yaliharibiwa, ili kuwakosesha chakula wanachohitaji. Lakini mwaka wa 1964 msaada kidogo wa sheria ulipatikana.
Mfano wenye kuonyesha kwamba haki ilitumiwa bado ni kwamba watu wanane walioshiriki kumwua Shahidi Mmalawi aliyeitwa Elton Mwachande walifanyiwa kesi wakapasishwa adhabu. Akikataa shtaka la kwamba Shahidi huyo alikuwa ‘amechokoza’ wapinzani wake, au kwamba mashahidi wa Yehova Malawi ni waasi katika kazi zao za kiserikali, hakimu mwenye kutenda Bw. L. M. E. Emejulu alisema hivi wakati huo:
“Mimi sioni ushuhuda wo wote wa uchokozi. Ni kweli kwamba mashahidi wa Yehova walieneza imani yao kwa bidii nyingi na kujaribu kupata waongofu, lakini wao wanafanya kazi zao za kiserikali na walifanya yote waliyoagizwa, kutia na kuendeleza mitaa. Walikataa kujiunga tu na chama cho chote cha kisiasa. . . . Hakuna ushuhuda wo wote kuonyesha kwamba walilazimisha au walijaribu kulazimisha mtu ye yote akubali dini yao. Ushuhuda waonyesha vingine. Katiba yawahakikishia kabisa kupata haki ya kuwa au kutokuwa wa chama cho chote cha kisiasa. Mimi sioni ushuhuda wo wote wa uchokozi.”
HAKI YATOWEKA
Hilo lilitukia mwaka wa 1964. Walakini, tangu mwaka wa 1967 kumekuwa hakuna kitu kama haki juu ya wachache wasio na ulinzi.
Ijapokuwa iko mipango ya usawa wa haki na uhuru kwa watu wote uliohakikishwa kabisa na katiba, kama ilivyotangazwa katika The Times la Malawi, Oktoba 23, 1967 serikali ilipiga marufuku rasmi mashahidi wa Yehova kama “jamii ya watu isiyo halali.” Hiyo ilikuwa ishara ya kushambuliwa kwa mashahidi wa Yehova nchini mwote, nao wakati huo walikuwa karibu 18,000. Kwa mara nyingine nyumba zao za hali ya chini zilinyang’anywa na kuteketezwa kwa moto. Katika mji mmoja wa Lilongwe katika Malawi ya Kati, nyumba 170 ziliteketezwa kwa moto kwa siku (nyakati za usiku) tatu tu. Jumla ikawa 1,095, Majumba ya Ufalme 115 yakiwa yameharibiwa. Maelfu ya mashahidi wa Yehova walipigwa na kutiwa gerezani. Maelfu mengine walitafuta kimbilio la muda kwa kuvuka mipaka wakaingia katika nchi za ujirani za Zambia na Msumbiji.
Nayo serikali ilifanya nini, ambayo ndiyo chanzo cha ‘sheria na utengemano,’ ‘mlinzi rasmi’ wa haki za watu wote wa Malawi? Haikulaumu hata kidogo utendaji wote huo wa kuvunja sheria! Hata hivyo, serikali iliagiza wanachama wake wa kisiasa waache mateso yao makali, ilipoona jinsi jeuri hiyo ilivyokuwa ikiongezeka. Baada ya hapo, kukawa na amani na utulivu wa kadiri kwa muda fulani kisha Mashahidi waliokuwa wamekimbilia nje wakarudi nchini. Kazi yao ya kuzihubiri habari njema za ufalme wa Mungu kwa Wamalawi wenzao ikaendelea na kusitawi, ingawa haikuweza kufanywa waziwazi kwa sababu ya marufuku.
Karibu miaka miwili baadaye, Oktoba 6, 1969, rais wa Malawi, Dkt. H. Kamuzu Banda, alisema hadharani kwamba mtu ye yote nchini asilazimishwe kununua kadi ya kisiasa. Je! wakati ujao maneno hayo yangekuwa na maana na nguvu na je! yangeheshimiwa? Au matukio ya baadaye yangepuza pia maneno hayo?
JEURI YA TATU YACHOCHEWA
Mwaka wa 1972 jibu lilipatikana. Katika kusanyiko la kila mwaka la Malawi Congress Party azimio lilipitishwa. Lilisema kwa uongo kwamba mashahidi wa Yehova ‘walizuia maendeleo ya kisiasa na ya kiuchumi ya Malawi’ kisha likataja maneno haya yanayoelekea kutoaminika:
“(b) Imeazimiwa kwamba washiriki wote wa madhehebu hizi zenye ushupavu za kidini walioajiriwa biasharani na viwandani wafukuzwe, na kwamba shirika lo lote la kibiashara au kiwanda cho chote ambacho hakitafuata azimio hili kitafutiwa leseni yake.
“(c) Imeazimiwa kwamba washiriki wote wa madhehebu hizi zenye ushupavu za kidini walioajiriwa na Serikali wafukuzwe na kwamba mshiriki ye yote wa madhehebu hizi mwenye kazi yake mwenyewe, ya biashara au ya ukulima, ashauriwe aache kazi zake za kibiashara au za ukulima.
“(d) Imeazimiwa kwamba washiriki wote wa madhehebu hizi wanaoishi vijijini wafukuzwe huko, nayo Serikali imeombwa ilinde sana iwezekanavyo wanachama wanaoshughulika na wafuasi wa madhehebu hizi.”
Matokeo ya maazimio hayo ya ukatili na chuki ambayo kwa maneno mengi yalitaka mashahidi wa Yehova watupwe nje ya jamii ya kibinadamu yalikuwa nini? Muda mfupi tu baada ya hapo roho ya kufanya jeuri ilichochewa kati ya watu katika nchi yote. Kuanzia na Julai wa mwaka huo (1972), washiriki wa vita wa Ushirika wa Vijana pamoja na chama chao cha Mapainia Vijana waliongoza kushambulia mashahidi wa Yehova kweli kweli.
Katika mashambulio yao ya ukatili wanachama hawakuachilia ye yote, hata wazee wala wanawake wenye mimba. Visichana vilinajisiwa-najisiwa; wanaume walipigwa mpaka kuzimia. Namna za mateso ambayo yangeweza kuletwa na watu wenye kichaa tu, kama vile kupigilia misumari ya inchi sita katika miguu ya wanaume na kuwalazimisha kutembea, zilitumiwa kujaribu kulazimisha watu hao waache imani zao za kidini na dhamiri yao ndio wanunue kadi ya uanachama. Wakati huo ni maelfu ya nyumba zilizoharibiwa. Kupatana na azimio la Malawi Congress Party, Mashahidi walilazimishwa kutoka vijijini na mashambani mwao waingie porini na vichakani. Mifugo yao iliibwa na kuuawa.a
Katika hayo yote, hakuna hata mmoja wa wenye kufanya mashambulio hayo ya uvunjaji wa sheria aliyekamatwa au kupelekwa mahakmani! Lo! hayo yote yalifanya mipango ya katiba ionekane ya upuzi kama nini! Ahadi ya rais ya kwamba watu wasingelazimishwa kununua kadi za chama ikawa upuzi tu, maneno matupu yasiyo na nguvu hata yapaswe kuheshimiwa au kutiiwa. Mara nyingi washiriki wa Ushirika wa Vijana walijisifusifu wakisema, “Sisi ndio polisi.” Kwa matendo yao washiriki hao wa Ushirika wa Vijana walikuwa kama wanatemea mate katiba ya taifa na mipango yake ya uhuru kwa ‘watu wote bila kujali rangi, taifa wala imani.’
Kwa sababu hiyo mashahidi wa Yehova walitoka Malawi kwa wingi sana. Baadaye karibu watu elfu 36 (kutia na watoto) wakaja kuishi katika kambi kumi mbalimbali za utoro katika nchi ya ujirani ya Msumbiji. Huko wakapewa ardhi kiasi fulani walime na hivyo wakasaidiwa kuendelea kuwa hai. Wakajenga ndani ya kambi hizo Majumba ya Ufalme mengi ya kuendelezea kujifunza kwao Neno la Mungu. Walikuwa wamepata hasara ya karibu mali zao zote za kimwili lakini hawakuwa wamepata hasara ya imani yao.
WALAZIMISHWA KURUDI MIKONONI MWA WATESI
Walakini, mwaka wa 1975 nchi ya Msumbiji ilianza kuwa na badiliko ikaacha kuwa koloni la Wareno kuwa taifa lenye kujitegemea, kwa sababu ya kufaulu katika maasi yao juu ya Ureno. Wanasiasa fulani wenye kutaka mapinduzi walitumia nafasi hiyo kuchochea fitina juu ya Mashahidi Wamalawi waliokuwa katika kambi za utoro wakasisitiza kwamba wajiunge kupaza sauti wakisema misemo ya kisiasa, kama vile “Viva Frelimo [maana yake Frelimo na Kidumu. Frelimo ndilo jina la chama kikuu cha kisiasa katika Msumbiji].” Mashahidi walipokataa kuhusika katika siasa waliondolewa katika kambi za utoro za Msumbiji. Walilazimishwa kuvuka mpaka waingie tena Malawi.
Katika mpaka wa Malawi, watoro wenye kurudi wakalakiwa na Waziri wa Jimbo la Kati la Malawi, Bw. Kumbweza Banda. Akawaambia: “Mliondoka Malawi kwa kupenda kwenu wenyewe na sasa mmerudi kwa kupenda kwenu wenyewe. Rudini vijijini kwenu mkafanye kazi kwa kushirikiana na mwenyekiti wa chama na wakuu wengine wa kwenu wa chama.” Akiwataja washiriki wa Ushirika wa Vijana wa Malawi, akaendelea kusema: “Vijana wangu watahakikisha kwamba mnafanya kazi kwa kushirikiana na Chama.”
Hiyo ilionyesha watoro hao walikuwa na tumaini dogo la kuona hali nafuu, na wengi wao walikuwa wakirudi hata bila pesa za kusafiria kwa bas kwenye vijiji vyao. Hesabu kubwa kati yao walitembea kwa miguu zaidi ya maili mia moja, pamoja na vitoto vyao. Kikundi kimoja kilitembea zaidi ya maili mia tatu, wanawake wakafika miguu na nyayo zikiwa zimevimba. Wangepatwa na mambo gani?
Agosti 27, 1975, muda mfupi baada ya kuanza kurudi, Katibu wa Wilaya wa makao makuu ya Malawi Congress Party ya Nkhotakota alipeleka barua kila mahali akitaja maneno yafuatayo (yaliyotafsiriwa kutoka Cinyanja), nayo maneno ya kwanza yanapinga kabisa dai la Bw. Kumbweza Banda kwamba mashahidi wa Yehova walikuwa wakirudi Malawi kwa kupenda kwao wenyewe:
“Nawajulisheni kwamba tumepokea ujumbe kutoka afisi ya chama katika hili Jimbo la Kati katika Lilongwe. Ujumbe wasema kwamba watu wale wa kanisa lile lililopigwa marufuku la ‘Mashahidi wa Yehova’ wamefukuzwa mahali walikokimbilia katika Msumbiji. Watu hao sasa wanarudi makwao.
“Tunataka kutaja waziwazi kwamba watu hao wakifika nyumbani kwao ninyi viongozi wa Eneo na Tawi mtahakikisha, pamoja na maheadmen wenu vijijini, kwamba kila mmoja wao ananunua KADI YA CHAMA. Kama mjuavyo, ni kazi ya maana sana kila mtu katika vijiji vyenu anunue kadi ya Malawi Congress Party. Hiyo ni njia moja ya watu wa nchi hii kuonyesha wanamthamini Kiongozi wetu wa Maisha, yule Ngwazi (Dkt. Banda) kwa sababu ya kuiendeleza nchi hii ya Malawi.
“Mimi wenu katika kazi ya chama,
“[Katiwa sahihi] P. Kamsuli Chirwa
Katibu wa Wilaya”
Sasa mashambulio makali yalianza tena yakachacha sana hata zaidi ya watoro 4,000 waliorudi wakavuka tena mpaka wa Malawi, wakati huu wakaenda Sinda Misale katika Zambia, wakitumainia kupata kimbilio huko. Lakini kufikia Oktoba serikali ya Zambia ilikuwa imewalazimisha kuondoka, ikawarudisha Malawi, ambako maelfu ya Mashahidi walipatwa na mateso.
Ni mambo gani hasa ambayo mashahidi wa Yehova wanavumilia Malawi? Je! kweli mambo ni yenye kuhuzunisha sana kama yanavyoonyeshwa? Sasa soma masimulizi yanayotoka katika Malawi yenyewe.
[Maelezo ya Chini]
a Ili upate ushuhuda ulioandikwa wenye kutoa majina na mahali palipotendewa matendo hayo, tazama Awake! la Desemba 8, 1972, kurasa 9-28.