Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g91 8/8 kur. 26-28
  • Uchunguzi Mnyofu wa Mitindo ya Viatu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Uchunguzi Mnyofu wa Mitindo ya Viatu
  • Amkeni!—1991
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tofauti Katika Namna za Msingi
  • Kujua Aina za Msingi
  • Jinsi Mitindo ya Viatu Ilivyoanza
  • Je, Viatu Vyako Vinakutoshea Vizuri?
    Amkeni!—2003
  • Msaada kwa Nyayo Zinazouma
    Amkeni!—1997
  • Kutoka kwa Wasomaji Wetu
    Amkeni!—2003
  • Yaliyomo
    Amkeni!—2003
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1991
g91 8/8 kur. 26-28

Uchunguzi Mnyofu wa Mitindo ya Viatu

HIVI karibuni umetazama ndani ya dirisha la wonyesho wa duka la viatu? Hata kama unapenda au hupendi yale unayoona, kitu kimoja ni wazi: Mitindo mbalimbali ya viatu, hasa ya wanawake, yaonekana haina mwisho.

Katika United States peke yake miundo mipya kama 200,000 hubuniwa kila mwaka, na wabuni katika Ulaya hutokeza kiasi icho hicho ikiwa si zaidi. Lakini hata kabla viatu hivi havijafika sokoni, karibu nusu yavyo hukataliwa, na kati ya nusu inayobaki ni kama 25,000 tu ambavyo huleta faida. Hata hivyo, kiasi hiki ni kikubwa na cha kushangaza. Haishangazi kwamba kununua viatu ni onyo lenye kusisimua kwa wengine lakini ni la kuchokesha kwa wengine.

Tofauti Katika Namna za Msingi

Maoni yako yawe ni gani juu ya hii mitindo inayotofautiana, je! utasadiki ya kwamba yale maelfu ya mitindo ya viatu kwa kweli ni namna-namna tu za miundo michache ya msingi ya viatu?

Vielezi vinavyoandama vitakupa wazo zuri juu ya zile namna saba za msingi za viatu: oksfodi, buti, pampu, klogi, myuli, kubazi na mokasia. Ingawa tunavamiwa na maelfu ya miundo mipya kila mwaka—na wale wenye bidii ya kufuata mitindo wanajivunia kufuatia ya kisasa—ukweli ni kwamba kwa miaka 350 tangu muundo wa oksfodi ubuniwe na kutolewa, hakuna muundo wowote mpya uliopata kutolewa. Miundo ya zamani ya msingi, kama kubazi na mokasia, ni ya maelfu ya miaka iliyopita.

Hivi leo, viatu vya wanawake ni vingi kupita vile vya wanaume kwa namna na wingi. Hata hivyo, miundo saba ya msingi ilibuniwa na wanaume, tena kwa ajili yao. Yote ilitarajiwa iwe ya wanaume. Ndiyo, sura, ufundi, na vifaa vilivyotumiwa vimebadilika sana katika miaka ya karibuni lakini ni kutokana na miundo michache hii kwamba maelfu ya namna mbalimbali katika viini vya mitindo yamesitawi kutosheleza mahitaji mbalimbali. Lakini miundo hii saba ya msingi imetokea jinsi gani?

Kujua Aina za Msingi

Oksfodi ndio muundo wa karibuni zaidi kati ya ile miundo saba. Kwa kufaa, jina hilo lilitoka Oxford, Uingereza. Hapo ndipo mara ya kwanza kiatu hiki chenye kufungwa kwa kanda kiliwapendeza sana wanafunzi wa chuo kikuu katika miaka ya 1600. Kiatu cha buti, ambacho kilitokea kabla ya oksfodi kilianza kikiwa kiatu cha sehemu mbili, kiatu kikiwa chini na ngozi ile yenye kufunika mguu ikiwa juu. Nadharia moja ilikuwa kwamba kwa kuwa kilionekana kama ndoo, Wafaransa walikiita butt, ikimaanisha “ndoo ya maji.” Hatua kwa hatua neno hilo likawa boute, na Waingereza walipoiga muundo huo kutoka kwa Wanomani katika karne ya 11, walikiita “boot” (buti).

Leo pampu ni kiatu cha kimtindo, kinachofunika vidole tu, kikiwa na wayo mwembamba na kisigino kifupi. Kilitumika kwa mara ya kwanza nyakati za Malkia Elizabeth. Baadhi ya watu wanadokeza kwamba muundo wa pampu ulitumiwa kwanza na waendeshaji gari-farasi kwa miguu ambao walilazimika kukanyaga vikanyago vya kisafirio hicho kwa nyayo zao. Hatua kwa hatua kiatu cha wanawake kikawa mtindo wenye kupendwa sana, kilichovaliwa nyakati rasmi za kisherehe na za kujipamba kikamili. Kwa sababu hiyo, wenye mamlaka fulani huamini kwamba jina hilo lilitokana na neno la Kifaransa pompe, linalomaanisha fahari, sherehe, hadhi yenye uzito, utukufu, kujionyesha.

Aina nyingine ya zamani ni klogi (kiatu cha magongo) ambacho chapata jina lacho kutokana na neno la Kiingereza la zamani linalomaanisha “pande la mti.” Hii ni kwa sababu viatu vya kwanza vya aina hii vilitengenezwa kutokana na miti. Vilivaliwa na wakulima na wafanya kazi kwa sababu ya urahisi wa kuvitengeneza. Leo, watu wengi huonea shangwe klogi ambavyo vina ngozi upande wa juu iliyoshikanishwa na mbao ya chini au na vitu vingine. Aina ya myuli haina sehemu ya nyuma kama klogi lakini aina hii imefanyiwa maendeleo zaidi na kwa kawaida huvaliwa ndani ya nyumba. Muundo wake umetokana na mulu ya Wasumeria, ambacho kilikuwa aina fulani ya sapatu yenye ngozi ya wayo laini. Muundo wa siku hizi una visigino na umekuwa mtindo mpya wa viatu.

Za zamani sana kati ya aina hizi saba, ni kubazi na mokasia. Kati ya aina hizi mbili, kubazi ilitumika zaidi na ndio uliokuwa mtindo wa kawaida nyakati za Biblia. Kilikuwa kipande cha mti tu au ngozi iliyofungwa miguuni kwa kanda. Mokasia nazo zilijulikana sana kwa sababu ya Wahindi wa Amerika ya Kaskazini waliovipa jina hilo, ambalo humaanisha tu “kifuniko cha mguu.”

Utakapoona jozi ya viatu mara nyingine, je, unaweza kutambulisha ni muundo gani kati ya aina hizo saba? Kwa kutupa macho tu haionekani kuwa rahisi sana. Hiyo ni kwa sababu aina za msingi zimebadilishwa mara nyingi miaka iliyopita ili kutosheleza mabadiliko ya ladha na mitindo. Lakini uchunguzi wa ukaribu zaidi utakuwezesha kuitambua vizuri. Kwa mfano, viatu vya kukimbilia huenda visifanane na yoyote ya namna hizi saba, lakini ukweli ni kwamba viatu hivyo ni aina za oksfodi zilizotengenezwa kwa vifaa tofauti. Kiatu cha mwanamke kilicho wazi nyuma kwa kweli ni myuli tu iliyoongezewa kanda, na Loafer kwa msingi ni mokasia ambacho kina ngozi ya wayo iliyo ngumu zaidi.

Jinsi Mitindo ya Viatu Ilivyoanza

Kwa mamia ya miaka, mitindo ya viatu ilikuwa ya matajiri na watawala peke yao. Kwa watu wa kawaida, viatu vilikuwa viatu tu—kitu cha kufunika na kulinda miguu—na jambo la maana hasa lilikuwa kwamba vifanye kazi viliyokusudiwa: sura yavyo haikufikiriwa sana. Mawazo ya mtindo ya viatu na biashara yavyo tuionayo sasa yameanza juzijuzi tu.

Jambo moja ambalo lilizuia biashara ya viatu isisitawi lilikuwa kwamba kwa karne nyingi viatu viliundwa kwa mikono. Ilichukua muda kuvitengeneza, na vilikuwa vya bei ghali. Watu walio wengi hawakuweza kununua viatu vipya wakati wowote walipotaka. Hali hiyo ilibadilika katika miaka ya kati ya 1800 mashine za kutengeneza viatu zilipoanza kutumiwa huko United States. Upesi ufundi wa mikono ukawa shughuli ya viwandani. Hata hivyo, ilichukua matukio mengine mawili kuanzisha mfululizo wa viatu: kupitishwa kwa Kifungu cha Sheria ya Volstead ya 1919 (kinachojulikana pia kuwa Katazo) na idhini katika 1920 ya badiliko la Katiba ikithibitisha haki ya wanawake kupiga kura.

Haya matukio yalileta upesi mabadiliko makubwa katika jamii ya watu wa Amerika. Amri ya marufuku ilileta namna mpya za tafrija, dansi, na muziki. Wanawake, na uhuru wao mpya, walijifurahisha kwa ule ulioitwa eti utendaji wenye kujipatia uhuru na wakafuatia kila kitu kilichokuwa kipya na tofauti. Pamoja na vitu vya kujipaka, marinda mafupi zaidi na aina za mitindo ya nywele, ukaja msisimuo wa mitindo ya viatu. “Kizazi cha Watapatapaji” wakaidi kilipata jina lacho kutokana na wanawake vijana walioacha viatu vyao bila kufunga kwa bizimu, kimakusudi. Walipotembea viatu vyao vilikuwa ‘vikitapatapa’ kwa sauti kubwa, kwa njia hiyo vikivuta fikira kwa wanawake hao na kusudio lao.

Lote hili lilitokeza kutakiwa sana kwa viatu vya madaha na vyenye kununulika. Jambo hili, pamoja na mbinu mpya na vifaa vipya vilivyotumiwa kutengenezea viatu, lilikuza mitindo ya viatu ikawa ilivyo leo. Sasa, kwa mara ya kwanza katika historia, viatu vya kimtindo si haki ya matajiri na wenye mamlaka, bali vinapatikana na karibu kila mtu.

Ajabu ni kwamba ijapokuwa kulikuwa na kelele nyingi kuhusu mitindo na miundo ya viatu katika karne zilizopita, zile aina saba za msingi hazijabadilika sana. Hata hivyo, namna nyingi sana na maelfu ya miundo na sura za viatu vinavyopatikana leo zinathibitisha ustadi wa wale walio katika biashara hiyo. Aina hizi mbalimbali zinaonyesha pia kwamba ladha na mitindo ni vitu vinavyobadilika haraka sana hivi kwamba mtu aweza kudanganywa na nia na misisimuko ya muda, ya wale wenye kuanzisha mambo hayo.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

Hadithi za Zamani Juu ya Viatu

◻ Ili kutuliza maumivu ya kichwa, Wamisri wa kale walikuwa wakichoma kubazi na kunusa moshi wake.

◻ Ili kutuliza maumivu ya tumbo, wahamiaji wa Kiamerika walikuwa wakilala chini na kuweka jozi ya buti nzito juu ya tumbo.

◻ Wakati fulani, mwanamume Mwarabu angeweza kumpa mke wake talaka kwa kutupa viatu vyake nje kupitia mlangoni, kama vile tu angetupa jozi ya kubazi zilizochakaa.

◻ Hadithi ijulikanayo sana juu ya viatu bila shaka ni lile simulizi juu ya Cinderella. Hadithi hii imesimuliwa na jamii za watu katika mamia ya njia tofauti-tofauti kuzunguka ulimwengu, ya zamani kuliko zote kuchapishwa ikiwa ni ya Wachina. Ilirekodiwa katika karne ya 19, miaka 800 kabla ya ile namna maarufu ya nchi za Magharibi.

[Picha katika ukurasa wa 27]

Kubazi

Pampu

Buti

Klogi

Oksfodi

Myuli

Mokasia

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki