Soma Upanue Mipaka ya Maarifa Yako
JE! UMEPATA kutamani kutembelea sehemu za mbali; kukutana na watu wa tamaduni mbalimbali; kuona na kutembelea maajabu ya asili kama vile maporomoko ya maji yenye kutazamisha, milima yenye fahari, na misitu isiyoelezeka na watu bado; na kujifunza juu ya ndege, wanyama, na mimea migeni? Au je! ungependa kujitoma chini kabisa ndani ya maji mpaka kwenye sakafu ya bahari; kupanda kwenda kwenye anga ya nje; kuchungulia kwenye ulimwengu wa vitu vidogo mno; kuchunguza maajabu ya ubongo, jicho, na moyo; au kushuhudia muujiza wa kuzaa? Labda hata kujikumbusha ya wakati uliopita kwa kufuatilia historia au akiolojia?
Misisimuo yote hiyo iko wazi kwako kupitia kurasa zilizochapwa. Bila ya wewe kuondoka nyumbani mwako, waweza kuona mambo hayo yote kwa kusoma vitabu na vichapo vingine ambavyo ni bohari la maarifa ya kila upande wa maisha. Kama vile Biblia isemavyo: “Hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi.” (Mhubiri 12:12) Usomaji mzuri utakuwezesha kuchota habari kutoka bohari hili wakati wowote upendapo.
Kikwazo Kinachostahili Kushindwa
Kwa kuhuzunisha, watu zaidi ya milioni 800 ulimwenguni pote wenye umri zaidi ya miaka 15 hawawezi kusoma na kuandika. Jambo hilo hupunguza sana uwezo wao wa kujifunza na kuwasiliana. Hukandamiza uwezo wao wa kufikiri na kuwafanya wategemee wale wawezao kusoma, hivyo wakiwa katika hatari ya kuelekezwa vibaya au kutumiwa kwa faida ya wengine.
Hata mambo ya msingi ya kila siku yaweza kuwa tatizo kwa wale wasiojua kusoma. Kwa mfano, kusafiri, kwa vyovyote vile, kwaweza kuvuruga ikiwa mtu hawezi kusoma ishara za barabara na maelekezo katika vituo vya basi, stesheni za magari-moshi, na nyanja za ndege. Pia kuna kutatizika na kuona haya kwa sababu ya mtu kuomba mwingine amsomee au amwandikie barua na hati za kibinafsi au hata kujaza fomu sahili. Akina mama wasioweza kusoma maagizo kuhusu chakula au dawa huwa katika hatari ya kuwapa watoto wao vitu vinavyoweza kuwadhuru.
Kwa wazi, kutojua kusoma na kuandika ni kikwazo kikubwa sana. Na bado, kwa msaada kidogo, chaweza kushindwa. Hali hiyo iko kama ile ya Marthe. Akiwa na umri wa miaka 70 alikuwa amekuwa kipofu kwa miaka zaidi ya 20 na alikuwa tu na kumbukumbu la jinsi ulimwengu wa mwangaza na rangi ulivyoonekana. Ndipo mpasuaji alipompasua. Jambo hilo likamwezesha kuwa tena katika ulimwengu mzuri ajabu wa kuona—na raha za kusoma. Halafu kuna Kalu, ambaye sasa ana miaka 70. Akiwa mwanamume mchanga, alikuwa “kipofu” wa ukurasa uliochapwa—hangeweza kusoma. Lakini alijiandikisha katika darasa la kujifunza kusoma na kuandika. Sasa yeye husoma na kuandika katika lugha tatu.
Labda kuna watu wachache walio kama Marthe, lakini kuna maelfu walio kama Kalu ambao wameshinda kikwazo chao kwa kujifunza kusoma. Bila shaka, huwa si jambo linalotimizwa mara moja. Huchukua wakati na jitihada na, zaidi ya yote, kitia moyo na msaada mkubwa. Je! wewe waweza kusaidia mtu yeyote? Mashahidi wa Yehova katika nchi nyingi huongoza masomo ya kujifunza kusoma na kuandika kama yale yaliyosaidia Kalu, na hilo limechangia kile kiasi cha juu cha kujua kusoma na kuandika miongoni mwa Mashahidi. Kwa mfano, katika Nigeria, kiasi cha kujua kusoma na kuandika miongoni mwa Mashahidi wa Yehova ni mara mbili zaidi ya idadi ya watu wote kwa ujumla.
Uwe Msomaji Bora Zaidi
Labda wewe huna tatizo la kujua kusoma na kuandika. Lakini wewe ni msomaji mzuri kadiri gani? Labda wewe husoma kwa kutumia jitihada nyingi na kurudia-rudia, yaani, inakuwa tabia yako kusoma kufikia nusu ya mstari au sentensi halafu unarudi nyuma tena kuurudia. Au labda unatamka maneno vibaya au una tatizo la kufahamu maana ya maneno. Je! matatizo hayo yaweza kushindwa?
Beatrice mwenye umri wa miaka kumi-na-mitatu angeweza kuhusianisha maneno na mawazo lakini alikuwa na tatizo la kuyatamka. Yeye angesoma “mtu” kuwa “fulani” au “jengo” kuwa “nyumba.” Mtu fulani alimfunza jinsi ya kutamka sauti za maneno—jinsi sauti za vokali na konsonanti zinavyounganika kufanyiza sauti nyingine—na jinsi ya kutamka maneno kwa silabi. Pia alimtia moyo kusoma Kitabu Changu cha Hadithi za Biblia huku akisikiliza mrekodio wake.a Uelewevu wake wa maneno na jinsi yanavyotamkwa ulizidi kukua, na sasa yeye hupata furaha nyingi katika kusoma.
Labda wewe pia unahitaji kusitawisha uwezo wako wa kutamka sauti za maneno. Kwa sababu unasoma makala hii, tayari unajua silabi ni nini. Fanyiza kazi maarifa hayo katika mazoezi ya kutamka maneno. Chukua neno moja, ligawanye katika silabi, na kutamka kila silabi. (Kwa mfano: ku-ta-m-ka) Halafu unganisha neno hilo tena na kulitamka likiwa zima. Jizoeze kufanya hivyo na maneno mengine, halafu jaribu kuyasoma bila kutenganisha kila silabi. Jifunze kutambua maneno mazima bila kuyatamka kihalisi.
Wasomaji wazuri hawasomi neno kwa neno. Wao huona vifungu vizima vya maneno na kuelewa maneno yakiwa katika vikundi vya wazo au mawazo kamili. Hivyo badala ya kusimamisha macho na kutazama kila neno, jaribu kuona maneno kadhaa katika kila mtazamo wa jicho, na kila mtazamo wapasa uwe kutua kwa jicho lako bila ya wewe kufahamu, mtazamo mfupi. Kwa kujizoeza utaweza kufanya hilo. Lakini uwe macho kwa mwelekeo wowote wa kurudia ile hali ya kwanza. Kurudia ili kusoma tena sehemu za sentensi kutakatiza mtiririko wako wa mawazo na kukuzuie ufahamu. Hivyo jizoeze kusoma moja kwa moja bila kurudia.
Hata unapoweza kusoma kwa ufasaha, kuna mambo mengine yanayohusika katika kuwa msomaji mzuri. Ufahamu, uwezo wa kukumbuka, na msamiati mwingi—yote hiyo ni miradi inayostahili kufuatwa. Visanduku vinavyoandama vinatoa madokezo fulani juu ya jinsi ya kutimiza miradi hiyo. Kwa nini usijichunguze kwa kuangalia madokezo hayo?
Chagua Mambo ya Kusomwa Yanayofaa
Ukiwa na uwezo wa kusoma uliokuzwa, maarifa mengi—hazina kubwa ya habari kwenye kurasa zilizochapwa—inapatikana kwako. Bila shaka, unaweza kujifunza mengi ya mambo hayo kupitia televisheni na tepe za video, lakini kusoma huchochea na kusitawisha mwendo wako wa kufikiri, mawazo yako, na uwezo wako wa kujieleza mwenyewe. Hukupa maneno pamoja na picha za akilini zinazokusaidia kukumbuka, kuzungumzia, na kuandika kwa uelewevu juu ya habari nyingi, hilo likifanya uwe mtu wa kupendeza zaidi wa kushirikiana naye.
Hata hivyo, kwa kuwa kuna aina nyingi za habari za kusoma, utaanzia wapi? Mstari wa Biblia unaosema, “Hakuna mwisho wo wote wa kutunga vitabu vingi,” pia husema, “Kusoma sana huuchosha mwili.” (Mhubiri 12:12) Huwezi kusoma kila kitu—na si kila kitu kinafaa na cha kweli. Kwa hiyo uwe mchaguzi. Kwa vyovyote soma habari zitakazounda utu wako uwe bora zaidi na zitakazokusaidia katika kazi yako, shuleni, au katika kushughulikia madaraka yako ya familia. Unaweza kupanua sana mipaka ya maarifa yako kwa kusoma vichapo vya kimataifa kama Amkeni! Katika kurasa chache tu, waweza kufurahia habari zilizokusanywa kutoka sehemu nyingi kuzunguka ulimwengu.
Uchaguzi utafanya usomaji wako uwe wenye kusudi na ukuletee faida zenye mafaa, za uelewevu, na za kiroho. Hivyo chagua vizuri, na ununue wakati kusomea nyumbani, katika vipindi vya mapumziko kazini, unapongoja, unaposafiri, na katika nyakati nyinginezo. Soma—kufanya hivyo kutapanua mipaka ya maarifa yako.
[Maelezo ya Chini]
a Kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New ● York, Inc.
[Sanduku katika ukurasa wa 26]
Jinsi ya Kufanya Maendeleo ya Ufahamu
● Fikiri kwa bidii unaposoma, ukiuliza maswali na kukata maneno.
● Weka akilini kichwa cha makala na vichwa vyovyote vidogo.
● Jaribu kuona jinsi kila fungu linavyofungamana na kichwa kikuu.
● Husianisha habari hiyo na kile unachojua tayari.
● Tumia habari hiyo maishani mwako na katika mambo uliyoona.
Kuza Msamiati Zaidi
● Tia alama maneno usiyoyafahamu unaposoma.
● Angalia jinsi maneno kama hayo yanavyotumiwa katika muktadha (habari zinazozunguka).
● Chunguza kamusi kwa maana za maneno unaposoma.
● Jifunze kutamka maneno kwa usahihi.
Jizoeze kutumia maneno mapya katika mazungumzo na wengine.