Kwa Nini Uhitaji wa Ushirika Ulitokea
VITA YA ULIMWENGU YA 1 ilikuwa teketezo kuu la miaka minne la kifo na uharibifu, kwa kiasi kisichopata kuonwa kamwe hapo mbeleni. Zikiwa zimejigawanya katika vikundi viwili vyenye kupingana, serikali kubwa zote za ulimwengu, na nyinginezo, zilienda vitani, kila upande ukiwa na uhakika wa kushinda, zikitiwa moyo na heko za idadi za watu waliodanganyika kufikiri kwamba vita ni jasirio tukufu.
Lakini katika muda wa miezi michache, ulimwengu ulijifunza kwa uchungu mno matokeo mabaya ya vita. Na ilipokwisha, machinjo, upotevu mwingi wa uhai na vifaa, uliacha ulimwengu ukiwa na deni kubwa sana la baada ya vita. Ilikuwa lazima jambo fulani lifanywe kuzuia vita nyingine kama hiyo isitokee tena. Kwa nini kusingekuwa na mpango ambao kupitia huo mataifa yangeweza kusuluhisha mabishano yao kiamani badala ya kijeshi? Wazo jipya? Sivyo hasa.
Kwa Nini Jitihada za Kwanza Zilishindwa
Kabla ya Vita ya Ulimwengu ya 1, mahakama ilikuwa imeanzishwa kujaribu kusuluhisha mabishano kiamani. Hiyo ni Mahakama ya kudumu ya Maamuzi katika Hague, Uholanzi. Katika miaka ya mapema ya 1900, watu wengi walikuwa na matumaini kwamba huenda mahali hapo pakawa kituo ambacho mapatano yangechukua mahali pa vita. Lakini ni nini kilichotendeka kwenye Mikutano ya Kuzungumzia Amani katika Hague mnamo 1899 na 1907 kikaongoza kwenye kuanzishwa kwa mahakama hii, ijulikanayo na wengi kama Mahakama ya Hague?
Katika mikutano hiyo yote miwili mataifa yaliyowakilishwa hayakukubali kufuata hukumu iliyotolewa kiamri, wala hayakukubali kuweka mipaka au mpunguzo wa mirundiko yao ya silaha. Kwa kweli, walikataa dokezo lolote la kupunguza silaha na wakazuia mpango wowote ambao ungewashurutisha kusuluhisha tofauti zao kwa mapatano.
Hivyo, Mahakama ya Hague ilipoanza kufanya kazi hatimaye, mataifa yalikuwa yamehakikisha haikuzuia uhuru wao kamili. Jinsi gani? Kwa njia rahisi: Yalifanya kuleta kesi mbele ya mahakimu kuwe kwa hiari. Na nchi ambazo zilipeleka migogoro yao mbele ya mahakama hii hazikushurutishwa kukaa kwa kufuata maamuzi yoyote yaliyotolewa nayo.
Hata hivyo, ulinzi huu wenye hadhari wa enzi ya kitaifa ulikuwa unahatarisha amani na usalama wa ulimwengu. Hivyo shindano la kuunda silaha liliendelea bila uzuizi mpaka lilipovurumisha ainabinadamu moja kwa moja ndani ya milipusho ya risasi zilizovunja kabisa amani ya ulimwengu katika kiangazi cha 1914.
Ni jambo la kutofautiana kwamba katika zile dakika za mwisho-mwisho za amani wakati ambapo Serbia, katika kujibu neno mkataa kutoka Austria, ilionyesha kuwa ilikuwa tayari “kukubali mapatano ya amani, kwa kuweka swala hilo . . . katika uamuzi wa Baraza la Hukumu la Kimataifa la Hague.” Lakini kwa kuwa utumizi wa Mahakama ya Hague ulikuwa wa hiari, Austria haikuhisi ikiwa na daraka la kukubali uwezekano huu wa kufanya “mapatano ya amani.” Hivyo vita ilitangazwa ili kudumisha amani—na malipo yakawa ni maiti za raia na wanajeshi zaidi ya milioni 20!
Makasisi Waomba Ushirika Uweko
Katika Mei 1919, askofu Mwepiskopali Chauncey M. Brewster alijulisha wazi katika mkusanyiko wa dayosisi katika United States kwamba “tumaini la ulimwengu la amani ya uadilifu na yenye kudumu linategemea kupangwa upya kwa sheria za mataifa katika mamlaka mpya. . . . Sheria ya kimataifa lazima ishirikishwe na mamlaka ambayo ni yenye kushurutisha kuliko mikataa iliyofanywa na ule Mkutano wa Hague [ulioanzisha Mahakama ya Hague]. Hivyo, ushirikiano wa mataifa lazima uwe katika ushirika fulani wa pamoja ulio kama agano au ushirika.”
Kardinali wa Katoliki ya Roma Mercier wa Ubelgiji alikuwa na maoni hayo hayo. “Mimi ninaona,” akasema katika mahoji katika Machi 1919, “kwamba jukumu kuu la Serikali mbalimbali kuelekea kizazi kinachokuja ni kufanya isiwezekane kuwe tena na vitendo vile vya uhalifu ambavyo vingali vikiuumiza ulimwengu.” Aliwaita wapatanishi wa mkataba wa amani wa Versailles “watengenezaji wa ulimwengu mpya” na akapendekeza kuundwa kwa ushirika wa mataifa ili kutimiza mradi huo. Alitumaini kwamba shirika hilo lingedumisha amani kikamilifu.
Kwenye jalada la juu la The New York Times ya Januari 2, 1919, kulikuwako kichwa kikuu hiki: “Papa Atumaini Kuanzishwa kwa Ushirika wa Mataifa.” Fungu layo la kwanza lilitangaza: “Katika ujumbe wa Mwaka Mpya kwa Amerika, . . . Papa Benedict alionyesha tumaini la kwamba Mkutano wa Kuzungumzia Amani labda ungetokeza utengemano mpya wa ulimwengu, kukiwa na Ushirika wa Mataifa.” Papa hakukitumia kifungu chenyewe hasa cha maneno “utengemano mpya wa ulimwengu” katika ujumbe wake. Hata hivyo, matumaini aliyoonyesha ya Ushirika yalikuwa na matukuzo ya kuvutia sana hivi kwamba kwa wazi Shirika la Utangazaji Habari au Habari ya Utangazaji ya Vatikani ilikifikiria kifungu hicho cha maneno kuwa chafaa.
Fikiria matumaini hayo katika muktadha wa nyakati zake. Ainabinadamu yenye kutatizwa ilikuwa inatamani kuona mwisho wa vita. Vita vingi mno katika karne nyingi mno vilikuwa vimeleta hasara kubwa sana. Na sasa iliyokuwa kubwa zaidi ya zote ilikuwa imekwisha hatimaye. Kwa ulimwengu ambao ulikuwa unatamani sana kuwa na tumaini, maneno ya papa yalivuma hivi: “Na kuanzishwe Ushirika wa Mataifa ambao, kwa kuondolea mbali kuingiza watu jeshini kwa nguvu, utapunguza silaha; ambao, kwa kuanzisha mahakama za kimataifa, utaondoa au kusuluhisha mabishano, ambao, kwa kuweka amani juu ya msingi wa mwamba imara, utahakikishia kila mtu uhuru na usawa wa haki.” Ikiwa Ushirika wa Mataifa ungeweza kutimiza yote hayo, kwa kweli ungefanyiza “utengemano mpya wa ulimwengu.”
Kwa Nini Ulishindwa
Kwenye karatasi malengo na taratibu za Ushirika huo zilisikika kuwa nzuri sana, zinazowezekana sana, na kutekelezeka. Agano la Ushirika wa Mataifa lilisema kwamba kusudi layo ni “kuendeleza ushirikiano wa kimataifa na kupata amani na usalama wa kimataifa.” Kupata amani na usalama kulitegemea ushirikiano baina ya mataifa na “ukubali wao wa wajibu wa kutogeukia vita.”
Hivyo, ikiwa kulizuka mabishano makali, mataifa walio washirika wenye kuhusika, yakiwa yamechukua daraka la kuendeleza amani, yangepaswa kuleta kesi yao “iamuliwe au ihukumiwe au ichunguzwe na Baraza” la Ushirika huo. Isitoshe, Ushirika wa Mataifa ulikuwa umehusisha Mahakama ya Kudumu ya Maamuzi, katika The Hague, ndani ya mfumo wake wa kuendeleza amani. Ilidhaniwa kwa uhakika kwamba yote hayo yangeondoa hatari ya vita nyingine kubwa. Lakini haikuondolewa.
Kulingana na wanahistoria fulani, sababu moja ya Ushirika kushindwa ukiwa mwendeleza amani ilikuwa ni kukosa kwa wengi wa “washirika wake kutambua bei ambayo ingelipwa ili kuwe na amani.” Kuweka mipaka ya silaha kulikuwa sehemu ya maana ya bei hiyo. Lakini mataifa hayangekubali kulipa bei hiyo. Hivyo historia ilijirudia yenyewe—kwa ghadhabu. Mataifa yakaanza tena shindano la kuunda silaha. Ushirika haukuweza kusadikisha mataifa yashirikiane kukomesha shindano hilo. Sihi na hoja zote hazikusikilizwa. Mataifa yakasahau somo kubwa la 1914: Mabohari makubwa ya kuwekea silaha huelekea kufanyiza hali ya kujiona bora kuliko wengine kijeshi.
Sehemu nyingine muhimu ya hasara ya kutokuwa na amani ilikuwa ni kule kulazimika kutambua ubora wa “usalama wa kijumuiya.” Ushambulizi wa taifa moja ulipasa kuonwa kuwa ushambulizi wa wote. Lakini ni nini kilichotendeka hasa wakati mmoja wao alipogeukia ugomvi badala ya mashauriano? Badala ya kutenda kwa umoja ili kukomesha hitilafiano hilo, mataifa yalijigawanya yenyewe katika vikundi vya mapatano mbalimbali, yakitafuta ulinzi wa wao kwa wao. Hayo yalikuwa madanganyo yale yale yaliyokuwa yamewaingiza katika ile vuruvuru ya tatanisho la 1914!
Ushirika huo ulidhoofishwa pia na kukataa kwa United States kujiunga nao. Wengi hufikiri kwamba hiyo tu ilikuwa “ndiyo serikali moja ya pekee iliyokuwa na uwezo wa kuufanya uwe na matokeo mazuri” na kwamba kuwamo kwa Amerika katika Ushirika huo kungaliweza kuwa kumeufanya utambuliwe ulimwenguni pote kwa kadiri iliyokuwa muhimu kuufanya ufanikiwe.
Lakini kulikuwako sababu nyingine zilizofanya Ushirika huo ushindwe. Fikiria sehemu hii hasi iliyo mwanzoni mwa Agano lao: “Mshiriki yeyote wa Ushirika aweza kujiondoa kwenye Ushirika, baada ya kutoa taarifa ya miaka miwili, kuhusu madhumuni hayo.” (Fungu la 1(3)) Uchaguzi huo, hata uwe wenye makusudio mazuri jinsi gani, ulifanya Ushirika ukose uthabiti, na hilo, nalo, likadhoofisha azimio la mataifa kushikamana na huo kwa uaminifu.
Mlango huo wazi wa kujiondoa ulitia uendelevu wa Ushirika chini ya uwezo wa washirika wake, ambao wangeweza kujiondoa wakati wowote walipopenda. Mataifa moja moja yalipata umaana mwingi zaidi ya Ushirika wenyewe. Hivyo, kufikia Mei 1941, mataifa 17 hayakuwamo tena ndani ya Ushirika. Mizinga mikubwa ya Vita ya Ulimwengu ya 2 ilikuwa inaondolea mbali tumaini la “utengemano mpya wa ulimwengu” na kusababisha anguko la Ushirika.
Ilikuwa lazima kuwe na njia bora zaidi!
[Blabu katika ukurasa wa 7]
Ushirika wa Mataifa ulishindwa kuzuia Vita ya Ulimwengu ya 2
[Picha katika ukurasa wa 7]
Cassino, Italia, ikishambuliwa kwa makombora, Machi 15, 1944
[Hisani]
U.S. Army