Kupanga Uzazi—Maoni ya Kikristo
KWENYE Mkutano wa kwanza wa Idadi ya Watu wa Ulimwengu, katika 1974, mataifa 140 yaliyokutana yaliazimia kwamba waume na wake wote “wana haki ya msingi ya kuamua kwa hiari na kwa kujali daraka idadi na kipindi cha kuachana kwa watoto wao na kupata habari, elimu, na njia za kufanya hivyo.”
Wengi huliona azimio hilo kuwa jema. Ni kweli, Mungu aliwaambia Adamu na Hawa, na baadaye familia ya Noa, ‘wazae, waongezeke, waijaze nchi,’ lakini Wakristo hawakupewa amri kama hiyo. (Mwanzo 1:28; 9:1) Maandiko hayatii moyo waume na wake Wakristo wawe na watoto wala hayawaambii wasiwe nao. Waume na wake waliofunga ndoa waweza kujiamulia wao wenyewe kama watakuwa na watoto au la na, wakipanga kuwa nao watakuwa na wangapi na watakuwa nao wakati gani.
Daraka la Kupewa na Mungu
Ingawa hivyo, je, uliona kwamba taarifa ya Mkutano wa Idadi ya Watu wa Ulimwengu ilisema kwamba waume na wake wapaswa kuamua “kwa kujali daraka idadi na kipindi cha kuachana kwa watoto wao”? Kanuni hiyo ya daraka yapatana pia na Biblia. Wazazi Wakristo hutambua kwamba ingawa watoto ni zawadi yenye thamani kutoka kwa Mungu, daraka kubwa huja pamoja nayo.
Kwanza kabisa, kuna lile daraka la kutunza watoto kimwili. Biblia husema hivi: “Lakini mtu ye yote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake hasa, ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.”—1 Timotheo 5:8.
Kuandalia familia ya mtu kunahusu mengi zaidi ya kutoa riziki na kulipa madeni, ingawa mara nyingi hiyo yenyewe ni kazi kubwa. Waume na wake Wakristo wenye kujali daraka, wanaopangia ukubwa wa washiriki wa familia yao, hufikiria masilahi ya kimwili pamoja na ya kihisiamoyo, kiakili na kiroho ya mama. Kutunza mtoto huchukua wakati mwingi, na watoto wanapofuatana mmoja baada ya mwingine, mara nyingi mama hawadhabihu tu pumziko, tafrija, usitawi wa kibinafsi, na ushiriki wao katika utendaji mbalimbali wa Kikristo bali pia afya yao ya kimwili na ya kiroho.
Wazazi Wakristo wenye kujali daraka hufikiria pia mahitaji ya watoto wao. The State of the World’s Population 1991 chasema hivi: “Watoto ambao huzaliwa kwa kufuatana karibu-karibu katika familia kubwa hulazimika kushindana na ndugu na dada zao wapate chakula, mavazi na shauku ya wazazi wao. Pia huelekea zaidi kupatwa na maambukizo. Watoto hao wakiokoka ile miaka hatari ya utoto wao, ukuzi wao utaelekea zaidi kudumaa na usitawi wao wa kiakili kupungua. Matarajio ya watoto hao katika maisha ya mtu mzima hupungua sana.” Bila shaka, haiko hivyo kwa habari ya kila familia kubwa, lakini ni jambo ambalo waume na wake Wakristo wapaswa kufikiria wanapopanga idadi ya watoto watakaokuwa nao.
Wazazi Wakristo wana wajibu wa kutunza watoto wao kiroho, kama vile Biblia huamuru: “Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana [Yehova, NW].”—Waefeso 6:4.
Emeka, Mkristo afundishaye sheria katika Naijeria, amefunga ndoa kwa mwaka mmoja naye hana haraka ya kuwa baba ya familia kubwa. “Mke wangu nami tumezungumzia idadi ya watoto tutakaokuwa nao. Tulifikiria kuwa na watano lakini tukaamua kuwa na watatu. Baadaye tulifikia mkataa kwamba wawili wangekuwa afadhali. Ni vigumu kulea watoto kulingana na kanuni za Biblia. Ni daraka kubwa.”
Waume na wake wengine Wakristo wameamua kutokuwa na watoto ili watumie wakati wao wote kutumikia Mungu. Mishonari mmoja katika Afrika aliyeafikiana na mume wake wakae bila watoto alitaarifu hivi: “Mimi sihisi kwamba nimekosa chochote kwa kutozaa watoto. Ijapokuwa mume wangu nami hatukupata shangwe ya uzazi, maisha zetu zimejaa shangwe nyinginezo. Kwa kujihusisha katika kusaidia wengine wajifunze kweli ya Biblia, sisi tuna watoto wengi wa kiroho katika sehemu nyingi za ulimwengu. Tunawapenda, nao wanatupenda. Kuna kifungo cha pekee kati yetu. Kukiwa na sababu nzuri, mtume Paulo alijifananisha na mama mlezi kwa sababu ya shauku nyororo aliyokuwa nayo kwa wale aliosaidia kiroho.”—1 Wathesalonike 2:7, 8.
Kudhibiti Uzazi
Je! Biblia hushutumu kudhibiti uzazi? La, haifanyi hivyo. Uchaguzi huachiwa mume na mke. Mume na mke waliofunga ndoa wakiamua kutumia njia za kudhibiti uzazi, chaguo la vizuia-mimba ni jambo la kibinafsi. Hata hivyo, njia ya kudhibiti uzazi ambayo mume na mke Wakristo wanachagua yapasa kuongozwa na staha yao kwa utakatifu wa uhai. Kwa kuwa Biblia huonyesha kwamba uhai wa mtu huanza wakati wa mtungo wa mimba, Wakristo wangeepuka vizuia-mimba ambavyo huharibu mimba, au kuangamiza uhai wa mtoto anayekuwa.—Zaburi 139:16; linganisha Kutoka 21:22, 23; Yeremia 1:5.
Kwa hiyo, waume na wake waweza kwa kufaa kufanya uchaguzi mbalimbali inapohusu kupanga uzazi. Huenda wengine wakataka kupunguza idadi ya watoto watakaokuwa nao. Wengine, wakitumia vizuia-mimba huenda wakaamua kutokuwa na watoto wowote kabisa. Njia nyingi za kudhibiti uzazi zinapatikana, kila moja ikiwa na faida na hasara zayo. Katika kuamua ni njia ipi inayowafaa zaidi, waume na wake wapaswa kukumbuka kwamba njia fulani uzazi ni zenye mafanikio zaidi ya nyingine. Wapaswa pia kuuliza juu ya yale yanayoweza kuwa matokeo mabaya. Madaktari na kliniki za kupanga uzazi zimetayarishwa ili kutoa shauri juu ya njia za kudhibiti uzazi na kusaidia waume na wake wachague ile inayotimiza vizuri zaidi mahitaji yao.
Uamuzi wafanyao waume na wake wa kuwa na watoto wengi, wachache, au kutokuwa nao ni wa kibinafsi. Pia ni uamuzi wa maana wenye matokeo makubwa. Waume na wake waliofunga ndoa wangekuwa na hekima wakipima jambo hilo kwa uangalifu na kwa sala.
[Sanduku katika ukurasa wa 8, 9 ]
Njia za Kawaida za Kudhibiti Uzazi
Kufunga Uwezo wa Kuzaa
Katika wanaume: Utaratibu rahisi wa upasuaji ambapo mkato kidogo hufanywa katika kifuko cha mapumbu na mirija ambayo hupeleka shahawa hukatwa.
Katika wanawake: Utaratibu wa upasuaji ambapo mirija ya Falopia hufungwa au kukatwa ili kuzuia yai lisipite kuingia ndani ya tumbo la uzazi.
Manufaa: Kati ya njia zote za kudhibiti uzazi, kufunga uwezo wa kuzaa ndiyo yenye mafanikio zaidi.
Hasara: Yaweza kuwa yenye kudumu. Katika wanaume na wanawake pia, upasuaji umerudisha uzazi, lakini jambo hilo haliwezi kuhakikishwa.a
Vibonge vya Kudhibiti Uzazi
Hizo hutia ndani kibonge kidogo chenye projestini-tu. Hufanya kazi ili kutatiza viwango vya kawaida vya homoni za mwanamke ili kuzuia yai lisikomae na kuachiliwa litoke.b
Manufaa: Ni yenye mafanikio sana katika kuzuia mimba.
Hasara: Matokeo fulani mabaya ya kimwili, ni machache kwa wanawake wenye afya ambao hawavuti tumbaku wenye umri wa chini ya miaka 40.
Kiwambo na Viua-shahawa
Kiwambo ni kikombe cha mpira chenye umbo la mviringo ambacho hutanuliwa juu ya kizingo chenye kupindika. Baada ya kupaka jeli au krimu yenye kuua-shahawa kwenye kikombe hicho, kikombe hicho hutiwa ndani ya uke ili kifunike vizuri shingo ya mji wa mimba.
Manufaa: Ni namna salama, yenye kutegemeka sana ya kudhibiti uzazi ikitumiwa ifaavyo.
Hasara: Lazima kitumiwe kila wakati mume na mke wanapofanya ngono. Ustadi hutakwa ili kukitia kidude ifaavyo, chapasa kutiwa kabla ya kufanya ngono na kuachwa ndani kwa saa sita kufika nane baada ya hapo.
Kifuniko cha Shingo ya Mji wa Mimba
Kidude cha mpira au plastiki kifananacho na kikombe na kilicho kidogo zaidi ya kiwambo. Kama kiwambo, kinatiwa juu ya shingo ya mji wa mimba lakini hicho hufunika vizuri zaidi na hakihitaji krimu au jeli nyingi ya viua-shahawa.
Manufaa: Mafanikio ya kifuniko hicho ni kama ya kiwambo, na kinaweza kubaki mahali pacho kwa saa 48. Viua-shahawa havihitaji kutumiwa wakati wa kurudia kufanya ngono.
Hasara: Ni vigumu zaidi kukitia ndani kuliko kiwambo, na lazima kuchunguza jinsi kinavyokaa juu ya shingo ya mji wa mimba kabla na baada ya kila kitendo cha ngono. Maambukizo ya shingo na mji wa mimba ni hatari ziwezekanazo kutukia. Kifuniko chapasa kutumiwa na wanawake waliofanyiwa michunguzo ya kansa kwa njia ya “Pap” peke yao.
Sifongo
Ni sifongo ya poliyurethene yenye viua-shahawa ambayo hutiwa ndani ya uke ili kufunika shingo ya mji wa mimba, hivyo ikifanyiza kizuizi halisi na cha kemikali kwa shahawa. Hutupwa baada ya kutumiwa.
Manufaa: Sifongo yaweza kuachwa mahali hapo kufikia saa 24 na huwa na mafanikio ngono ikirudiwa katika wakati huo.
Hasara: Visa fulani vya kutukia kwa mizio na vya kushikwa na mshtuko wa sumu vimeripotiwa.
Kidude Kitiwacho Ndani ya Mji wa Mimba
Huitwa pia IUD, tanzi, au pindi, kidude hiki cha chuma au plastiki hutiwa ndani ya tumbo la uzazi. Ingawa hakuna uhakika juu ya jinsi kifanyavyo kazi hasa, madaktari huamini kwamba huzuia uzazi kwa njia kadhaa. Mojapo hizo labda ni kuzuia yai lililotungika mimba lisijishikishe kwenye ukuta wa tumbo la uzazi.
Manufaa: Ni njia yenye kutegemeka ya kudhibiti uzazi.
Hasara: Nyakati nyingine hutokeza kuvuja damu au maumivu, na jinsi kitumikavyo huenda nyakati nyingine ikawa sawa na kuharibu mimba.c
Kondomu (Mipira)
Ala ifunikayo uume kuzuia shahawa zisiingie ndani ya uke.
Manufaa: Njia salama, yenye mafanikio ya kudhibiti uzazi. Hupunguza uwezekano wa kuambukizwa magonjwa yapitishwayo kingono, kutia na UKIMWI.
Hasara: Haipendwi na wengine kwa sababu kuitumia hukatiza-katiza kitendo cha ngono.
Kuondoa Uume
Kuondoa uume ndani ya uke kabla tu ya kutokwa shahawa.
Manufaa: Haina gharama, haitaki kujitayarisha, au kitu chochote cha nje.
Hasara: Hairidhishi kingono, huhitaji kujidhibiti sana, na haitegemeki kabisa.
Njia ya Mwendo
Mume na mke hujizuia kufanya ngono wakati wa siku za mzingo wa hedhi ya mwanamke ambapo kuna uwezekano mkubwa zaidi wa kupata mimba.
Manufaa: Salama, haina matokeo yenye kudhuru, haihitaji tendo lolote wakati wa kufanya ngono.
Hasara: Si njia yenye mafanikio sana ya kuzuia mimba isipokuwa mume na mke wameazimia kabisa na kushikamana sana na maagizo ya kutumia njia hiyo.
Kupachikwa Homoni
Njia mpya kabisa ya kuzuia mimba katika uwanja wa kudhibiti uzazi, mfululizo wa silinda ndogo sana za silikoni hupachikwa chini ya ngozi ya mkono wa mwanamke. Kwa muda wa kufikia miaka mitano, silinda hizo hufuliza kutoa kiasi kidogo sana cha homoni katika damu. Wakati huo analindwa asipate mimba.
Manufaa: Njia yenye mafanikio sana. Uzazi waweza kurudishwa kwa kuondoa homoni zilizopachikwa.
Hasara: Kidogo sana. Yafanana na kibonge projestini-tu (kibonge-kidogo) cha kudhibiti uzazi. Wakati mipachiko inayotumiwa ni ya projestini-tu, labda mimba huzuiwa kwa njia zenye kuharibu mimba.d
[Maelezo ya Chini]
a Mazungumzo juu ya kama matumizi ya kidude IUD yapatana na kanuni za Kikristo hupatikana katika Mnara wa Mlinzi wa Oktoba 15, 1979, kurasa 22, 23.
b Mazungumzo ya jinsi vibonge vya kudhibiti uzazi huzuia uzazi yapatikana katika Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 1989, ukurasa 29
c Mazungumzo ya jinsi vibonge vya kudhibiti uzazi huzuia uzazi yapatikana katika Mnara wa Mlinzi la Juni 15, 1989, ukurasa 29..
d Mazungumzo juu ya kama kufunga uwezo wa kuzaa kunapatana na kanuni za Kikristo yapatikana katika Mnara wa Mlinzi la Oktoba 1, 1985, ukurasa 31.