Sherehe ya Sapporo ya Theluji na Barafu
Na mleta habari za Amkeni! katika Japani
WAKATI wa miezi mirefu ya kipupwe, Sapporo, jiji la kaskazini la Japani, huwa limefunikwa kwa theluji. Kwa miezi mitano hadi sita mwakani, wakazi walo hawakuwa na mengi ya kufanya kwa habari ya tafrija hadi wasimamizi wa jiji walipozungumza pamoja na kupata wazo zuri: sherehe ya theluji yenye sanamu kubwa za theluji.
Katika 1950, wanafunzi wa shule ya upili walisaidiwa kujenga sanamu sita, zenye ukubwa wa kuanzia meta 3 hadi 4 kwa urefu. Watu karibu 50,000 walikuja kuona “Venus de Milo” ya theluji na sanamu nyinginezo. Yuki Matsuri, au Sherehe ya Theluji, ilikuwa na mwanzo mzuri.
Kwa muda wa miaka, sherehe hiyo imekua kwa ukubwa na umashuhuri. Kila mwaka sasa, watalii wapatao milioni mbili, kutia na wengi kutoka nchi za kigeni, huja kutazama kwa mshangao mamia ya michongo ya barafu na theluji. Tukio hilo lisilo la kidini la kutazamisha la siku saba limekuja kuwa kubwa zaidi la aina yalo katika Japani nzima.
Matembezi Wakati wa Sherehe Hiyo
Kati ya mahali patatu pa sherehe, Uwanja wa Ōdori ndio mkuu. Mahali hapo ambapo mwanzoni palikuwa mahali pa kutupa theluji paenea eneo la wanja 11 za jiji katikati mwa Sapporo. Hapa na kwenye jiji la Makomanai, lililo umbali mdogo, mtu aweza kuona michongo mikubwa yenye kutazamisha. Watoto huvutiwa na sanamu zenye ukubwa usio wa kawaida za watu wawapendao sana katika maonyesho ya televisheni na vitabu vya vichekesho. Kuna yule mtu wa angani asiye wa kawaida aitwaye Ultraman ambaye wavulana wadogo hupenda kumwiga. Na karibu na hapo kuna watoto ambao huonyeshwa katika kipindi cha televisheni cha katuni kinachopendwa cha Chibi Maruko-chan pamoja na rafiki zake.
Watu wazima pia wastaajabishwa. Jumba la Michezo la Paris lililofanyizwa vizuri ajabu, lenye kuta zilizochongwa kwa umaridadi na hata sanamu za wanamuziki zikiwa paani, huvuta uangalifu. Kuna Jumba la Baraza la Ujerumani la kale, ambalo ni jengo la theluji la mtindo wa kale wa madoido mengi. Ngome ya Uarabuni iliyo kubwa ikionyesha Aladdin na ‘taa yake ya mizungu’ ni rahisi kutambua.
Michongo iliyo katika Uwanja wa Raia ambayo mingi yayo huwa na ujumbe wa kipekee, hufanywa ionekane kuwa midogo kwa kulinganisha na ile michongo mingine mikubwa zaidi. Mchongo wa Lango la Brandenburg ni ukumbusho wa muungano wa Ujerumani wa hivi karibuni. Baadhi ya michongo yaonyesha hangaiko kwa ajili ya dunia, mazingira yayo, na wanyama.
Mwishoni mwa Uwanja wa Ōdori twapata Uwanja wa Kimataifa ambapo timu kutoka nchi nyingi hushindana. Baadhi ya wachongaji ni wastadi ambao kwa kawaida hufanya kazi na marmar, mawe, na vitu vinginevyo. Kila mmoja wao alipewa kyubu ya meta tatu za theluji iliyotangulia kugandishwa na kupewa siku tatu kukamilisha michongo yao.
Lakini michongo hiyo mikubwa hufanyizwaje, nao wachongaji huzifanyizaje kwa usahihi mambo madogo-madogo kwa njia ya kustaajabisha?
Jinsi Michongo ya Theluji Ifanyizwavyo
Kuchonga mchongo mkubwa hivyo si kazi rahisi. Katika mradi mmoja, ujenzi wenyewe waweza kuchukua karibu mwezi mmoja, ukitumia zaidi ya siku 1,500 za kazi ya mtu.[5] Mchongo mmoja mkubwa ulikuwa mfano wa kituo cha garimoshi cha Flinders Street Station, Melbourne, Australia. Ulikuwa meta 35 kwa urefu na meta 35 kwa upana na meta 15 kwa kimo. Ilichukua safari 1,400 za malori yenye kubeba uzito wa tani tano kupeleka tani 7,000 za theluji zilizotumiwa kuujenga.[6] Si ajabu kwamba tangu 1955 sehemu kubwa ya kazi ya kuchonga michongo mikubwa imefanywa na majeshi ya ulinzi, walioungwa mkono baadaye na wenye kuzoezwa katika idara ya moto. Acheni tuone jinsi wanavyojenga sanaa hiyo ya theluji yenye kustaajabisha.
Kwanza, ni lazima kitu chenyewe kichaguliwe. Habari na picha hukusanywa. Kwa kutegemea hizo, violezo hufanyizwa kwa udongo, karatasi ya kufinyangia, au vitu vinginevyo. Halafu, mwezi mmoja hivi kabla ya sherehe, theluji safi hukusanywa na kusafirishwa hadi kwenye mahali pa ujenzi. Huko, hiyo hupakuliwa, hushindiliwa katika fremu kubwa za mbao na kugandizwa kwa maji. Halafu fremu hiyo huondolewa, ngazi za kukanyagia husimamishwa, na kazi ya kuchonga inaanza kwa bidii.[7]
Mara nyingi wakifanya kazi usiku wote wakati ambapo hali-joto ziko chini ya sufuri, mafundi hutumia mashoka na koleo kwa kazi ya mwanzoni na vyombo vidogo zaidi vya kuchongea kwa ajili ya mambo madogo-madogo.
Watu mmoja-mmoja na vikundi vidogo waweza pia kushiriki furaha hiyo. Karibu theluthi moja ya mamia ya wenye kushindana kutoka nchini kote wanaochaguliwa kwa droo hupewa miongozo kutoka kwa timu ya kipekee ya wastadi. Kila mshindani hupewa kyubu ya meta mbili ya theluji iliyogandishwa na siku tano ili akamilishe ubuni wake.[8]
Uvutio Wenye Kustaajabisha
Michongo ya barafu pekee huongeza uzuri mwingine zaidi kwenye sherehe hiyo. Hiyo hufanywa hasa na washiriki wa Shirika la Wachongaji-Barafu.[9] Wengi wao ni wapishi katika hoteli maarufu ambao kwa kawaida huonyesha ustadi wao katika vyumba vya mlo. Wao huwa na hamu ya kuja Sapporo, na matokeo huwa ya kufurahisha.
Maonyesho na michezo ya muziki huongezea ile hali ya sherehe. Kunakuwa na mashindano, bendi zenye kutembea kwa miguu, dansi, kuruka hewani baada ya kuteleza kwenye theluji na mengine mengi. Watoto pia hufurahishwa na vitelezi vingi vya barafu vinavyojengwa ndani ya michongo hiyo, vinavyoandaliwa ili wavifurahie.
Wakati wa usiku ni wakati mzuri hasa wa kutazama sherehe hiyo. Maelfu ya taa ndogo nyeupe zilizoning’inizwa kutoka matawi matupu ya miti katika uwanja huo, pamoja na taa nyingi zenye rangi-rangi zinazomulika michongo hiyo yenye kung’aa, hufanyiza mmeremeto wenye kuvutia wa nuru na rangi katika nchi hiyo ya ajabu ya kipupwe. Baada ya kuona sherehe hiyo, ungeweza kuvutiwa na yale ambayo ubuni na mikono yenye ustadi ya mwanadamu ya kupewa na Mungu yaweza kutimiza.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Michongo mikubwa ya barafu kama hii iliyo chini yaweza kuwa na upana wa meta 35 na meta 15 kwa kimo, ikihitaji karibu tani 7,000 za theluji ili kuijenga