Majiji Makubwa Yanasongwa Pumzi Polepole
ULIMWENGUNI pote majiji makubwa, miji mikubwa sana, inakua, ikivutia mamilioni wanaotafuta kazi, makao, na starehe za maisha ya jiji. Lakini gharama ni kubwa. Hata kupumua kwenyewe katika majiji haya yanayotandawaa kunakuwa hatari zaidi kwa afya ya kibinadamu.
Ripoti moja ya hivi majuzi kutoka UNEP (Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa) na Shirika la Afya Ulimwenguni yaonyesha kwamba uchafuzi wa hewa katika 20 kati ya majiji yaliyo makubwa zaidi ulimwenguni imekuwa ikizidi kuharibika sana. “Katika visa fulani,” lasema Our Planet, gazeti lililochapishwa katika Kenya na UNEP, “uchafuzi wa hewa ni mbaya kama zile kungumoshi zilizokuwa na sifa mbaya sana London miaka 40 iliyopita.” Wakaaji wa Mexico City ndio wenye kuathiriwa zaidi, lakini makumi ya mamilioni ya watu wanaoishi katika majiji kama vile Bangkok, Beijing, Cairo, na São Paulo hawako afadhali.Hewa iliyo katika majiji hayo ni hatari kadiri gani? Kadiri kubwa za vichafuzi vikuu, kama salfa dayoksaidi, kaboni monoksaidi, na plumbi, ni hatari kwa njia kadhaa. Matokeo yazo juu ya mwili hutofautiana sana: matatizo ya kupumua na ya mishipa ya moyo, madhara ya mishipa ya fahamu, na hata uboho wa mifupa, ini, na matatizo ya figo.
Ni nini kinachosababisha uchafuzi huo? Kulingana na Our Planet, kisababishi kimoja kikubwa zaidi katika majiji haya ni magari. Kwa kuwa hesabu ya sasa ya magari ulimwenguni—milioni 630—“yatarajiwa kurudufika mnamo miaka 20-30 ijayo, sana-sana katika maeneo ya mijini,” yaonekana kwamba hali ya hewa majijini itakuwa ya kusikitisha. Isitoshe, hatua za uzuizi hazijafuatwa sana, kwa kuwa, kama vile ripoti hiyo isemavyo, katika majiji makubwa yaliyo mengi “kuna ufahamu haba juu ya uzito wa tatizo hilo.” Basi, haishangazi kwamba Our Planet lahimiza kwamba majiji hayo yatangulie kuchukua hatua zenye shabaha ya kuisafisha hewa. Hili lisipofanywa, wakati ujao una dalili mbaya. Kulingana na kadirio la jarida hilo, “majiji haya yakabili kusongwa pumzi polepole kwa kadiri hali ya hewa iendeleavyo kuwa mbaya zaidi.”