JE, DUNIA YETU ITAOKOKA?
HEWA
TUNAHITAJI hewa si kwa ajili ya kupumua tu. Hewa huilinda pia sayari yetu dhidi ya miale hatari ya jua. Bila hewa, kiwango cha joto duniani kingepungua na kungekuwa na baridi kali sana.
Kwa Nini Tunahitaji Kulinda Hewa Yetu
Uchafuzi wa hewa unaweza kusababisha vifo kwa viumbe duniani. Ni asilimia moja tu ya watu ulimwenguni wanaopumua hewa safi yenye kiwango cha usalama kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni.
Uchafuzi wa hewa umehusianishwa na matatizo ya upumuaji, kansa ya mapafu, na ugonjwa wa moyo. Kila mwaka, watu 7,000,000 hufa mapema kwa sababu ya uchafuzi wa hewa.
Dunia Yetu Imeumbwa Ikiwa na Uwezo wa Kuokoka
Dunia yetu ina uwezo wa kiasili wa kudumisha kiwango kinachofaa cha hewa safi kwa ajili ya viumbe hai walio duniani. Mifumo hiyo ya asili ya kutokeza hewa safi inafanya kazi vizuri wanadamu wanapotunza mazingira. Fikiria mifano michache.
Misitu inajulikana kwa uwezo wake wa asili wa kufyonza hewa ya kaboni dioksidi. Lakini jambo lisilojulikana sana ni kwamba, maeneo ya pwani yana mikoko yenye uwezo wa kupunguza kiwango cha kaboni mara tano zaidi ya uwezo wa misitu.
Utafiti uliofanywa hivi karibuni unaonyesha kwamba miani mikubwa kama vile magugu maji, hukusanya kaboni dioksidi na kuiondoa kabisa kutoka katika angahewa. Magugu hayo yana vifuko vinavyoyaruhusu kuelea juu ya maji kufikia sehemu za mbali kutoka katika maeneo ya pwani. Vikiwa huko, hupasuka na kukusanya hewa ya kaboni na kisha huzama baharini na kubaki huko kwa karne nyingi.
Uwezo wa angahewa wa kupunguza kiwango cha hewa chafu ulionekana wakati wa janga la COVID-19 amri ya kutotoka nje ilipotolewa. Mwaka wa 2020, viwanda vingi duniani vilipofungwa na vyombo vya usafiri kusitisha safari zake, ubora wa hewa uliimarika duniani pote. Kulingana na “Ripoti ya Ubora wa Hali ya Hewa Ulimwenguni ya mwaka wa 2020,” zaidi ya asilimia 80 ya mataifa yaliyoshiriki katika utafiti huo yaliripoti kwamba muda mfupi baada ya amri ya kutotoka nje kutolewa, kiwango cha hewa safi katika nchi hizo kiliongezeka.
Hatua Zinazochukuliwa Sasa
Serikali zinaendelea kuwahimiza wenye viwanda wapunguze viwango vya hewa chafu wanazozalisha. Pia, wanasayansi wanaendelea kugundua njia mpya za kupunguza uchafuzi wa hewa. Kwa mfano, njia moja ni kwa kutumia vimelea ili kuondoa sumu kutoka kwenye takataka na kuzifanya ziwe salama kwa ajili ya matumizi. Pia, wataalamu wanawashauri watu watembee kwa miguu au watumie baiskeli badala ya magari na wapunguze matumizi ya nishati katika nyumba zao.
Lakini mengi zaidi yanahitajika, kama inavyotajwa na ripoti ya mwaka wa 2020 iliyotayarishwa na Shirika la Afya Ulimwenguni na Benki ya Dunia.
Ripoti hiyo ilisema kwamba katika mwaka wa 2020, karibu theluthi ya watu ulimwenguni walitegemea nishati au mafuta yanayochafua hewa ili kupika. Katika maeneo mengi ni watu wachache tu wanaoweza kununua majiko ya kisasa au kutumia nishati mbadala isiyochafua hewa.
Sababu za Kuwa na Tumaini—Biblia Inasema Nini
“Hivi ndivyo anavyosema Mungu wa kweli, Yehova, Muumba wa mbingu na . . . Yule aliyeitandaza dunia na mazao yake, Yule anayewapa pumzi watu waliomo.”—Isaya 42:5.
Mungu ameumba hewa tunayopumua na mifumo ya asili inayosafisha hewa, na ana nguvu nyingi na upendo kuelekea wanadamu. Hivyo, haipatani na akili kuamini kwamba hatafanya jambo lolote ili kusafisha hewa. Soma makala yenye kichwa, “Mungu Anaahidi Kwamba Sayari Yetu Itaokoka” katika ukurasa wa 15.”