Kuutazama Ulimwengu
Maradhi Yenye Kufisha Katika Australia
“Idadi ya Waaustralia wanaokufa kutokana na magonjwa yanayohusiana na UKIMWI imeshuka sana kwa mara ya kwanza tangu kuwekwa kwa rekodi kuhusu athari ya kirusi hicho,” laripoti gazeti Herald Sun la Melbourne. Yakitegemea habari ya hivi majuzi iliyotolewa katika Australian Bureau of Statistics, matokeo hayo yaonyesha kwamba watu 666 walikufa katika 1995 kutokana na UKIMWI—upungufu wa asilimia 13. Kiwango cha jumla cha kitaifa cha kifo kilipungua kwa asilimia 4, kansa na maradhi ya moyo bado yakiongoza kuwa visababishi vikuu vya vifo. Hata hivyo, idadi yenye kuongezeka ya Waaustralia wanakufa kutokana na maradhi ya Alzheimer na maradhi mengineyo yanayohusiana na kuzorota kwa uwezo wa akili. Kulingana na katibu wa kitaifa wa Alzheimer’s Association Australia, “ongezeko la haraka lililotabiriwa katika idadi ya wanaougua kuzorota kwa uwezo wa akili litaweka mkazo mkubwa sana kwenye vifaa vilivyopo vya kusaidia watu wenye maradhi hayo na kwa wale wanaowatunza.”
Maoni Kuhusu Wakati Ujao
Karne ya 21 ikiwa inakaribia, kuna maoni mengi sana kuhusu wakati ujao. Katika uchunguzi uliofanywa na gazeti Newsweek Marekani, watu waliulizwa kuhusu mataraja yao kwa karne ijayo. Asilimia 64 hivi ya wale waliohojiwa wanatabiri kwamba wataalamu wa kusafiri anga za nje watatembea kwenye sayari Mihiri. Asilimia 55 hivi wanatarajia wanadamu hatimaye wakae mahali pengine kwenye ulimwengu wote mzima. Asilimia 70 wanafikiri kwamba wanasayansi watapata tiba ya UKIMWI, na asilimia 72 wanatabiri kwamba tiba ya kansa itafanyizwa. Kwa maoni ya kutotazamia mazuri, asilimia 73 ya waliohojiwa wanaona kimbele pengo kubwa zaidi kati ya matajiri na maskini, na asilimia 48 wanatazamia vita vingi zaidi kuliko miaka 100 iliyopita. Asilimia 70 hivi wanafikiri kwamba mwanadamu hataweza kumaliza njaa ya ulimwenguni pote.
Kiwewe Chenye Kuogofya
Kulingana na FDA Consumer, matukio na ubaya wa majeraha ya kuungua katika Marekani yamepungua kwa kiasi kikubwa katika miaka 20 ambayo imepita. Kiwango cha kusalimika cha wahasiriwa wa kuungua kimeboreka pia. Ofisa wa Food and Drug Administration, Charles Durfor, alitaja kwamba “miaka 30 hadi 40 iliyopita, wagonjwa wengi wa kuungua hawakusalimika. Maendeleo katika tiba yamefanyiza idadi mpya kabisa ya wagonjwa ambao hawasalimiki tu, bali pia hupata hali ya maisha inayozidi kuwa bora.” Kila mwaka, zaidi ya Wamarekani 50,000 huungua kiasi cha kuhitaji kulazwa hospitali. Kulingana na American Burn Association, wahasiriwa 5,500 hivi hufa. “Kuungua vibaya ni moja ya viwewe vyenye kuogofya zaidi ambavyo mwili waweza kupata,” lasema FDA Consumer.
Ulaghai “wa Kufuatia Haki”
Makampuni ya bima katika Argentina yanapoteza dola milioni 200 hivi kila mwaka kwa sababu ya mazoea ya ulaghai ya wateja wake. Tokeo ni kwamba bima ya magari inagharimu hadi asilimia 30 zaidi kuliko nchi nyinginezo nyingi. Kulingana na gazeti la habari Ambito Financiero, “karibu nusu ya ulaghai ulitendwa na wale wawezao kuitwa eti ‘raia wenye kufuatia haki.’” Yasemekana kwamba asilimia 40 hivi ya wenye kumiliki hati za bima wametumia vibaya kampuni yao ya bima kwa njia fulani. Gazeti hilo la habari lamalizia kwamba utendaji huo wa ulaghai huonyesha namna fulani ya kisasi kinacholipwa na wateja wasiotosheka ambao wanahisi kwamba wamefanyiwa ulaghai na makampuni yao ya bima.
Bahari Inayokufa
Bahari Iliyokufa inanywea. “Ikiwa tayari mahali penye maji palipo chini kuliko pote Duniani (meta 410 chini ya kiwango wastani cha bahari kuu za ulimwenguni), Bahari Iliyokufa inaendelea kupungua,” lasema gazeti U.S.News & World Report. Kwa nini? Mbali na athari za uvukizaji, mifumo kadhaa ya umwagiliaji wa maji na mabwawa hugeuza maji kutoka Mto Yordani, chanzo kikuu cha maji ya Bahari Iliyokufa. Pia, “viwanda vya kemikali ambavyo hupiga pampu maji ya Bahari Iliyokufa hadi kwenye vidimbwi vya uvukizaji ili kuondoa madini vimechochea kunywea huko.” Tangu katikati ya miaka ya 1950, Bahari Iliyokufa imeshuka kwa meta 20 hivi. Hatua moja ya kurekebisha ambayo kwa sasa inajadiliwa ni kujengwa kwa mfereji wa maji wenye urefu wa kilometa 190 ambao utaleta maji kutoka kwenye Bahari Nyekundu. Italazimu maji hayo yapigwe pampu kupanda juu kwa meta 120 halafu kuteremka chini meta 530 kuingia katika Bahari Iliyokufa.
Nadhiri Zilizovunjwa
Katika Ujerumani ni wenzi wa ndoa wachache zaidi wanaotimiza nadhiri zao za ndoa. Tokeo, laripoti gazeti Nassauische Neue Presse, ni kuongezeka kwa kiwango cha talaka na idadi yenye kuongezeka ya watoto wanaoteseka. Katika 1995 ndoa zikaribiazo 170,000 zilivunjika, zikiathiri watoto wapatao 142,300. Hiyo yawakilisha ongezeko la asilimia 5 katika watoto walioathiriwa kupita mwaka uliotangulia. Gazeti hilo la habari lilitaja kwamba kati ya ndoa zilizofungwa kwa kawaida ya kidini katika 1950, ni 1 katika 10 iliyoshindwa kufaulu katika kipindi cha miaka 25. Kati ya wenzi waliofunga ndoa katika 1957, ni 1 hivi katika 8 waliotengana katika kipindi cha miaka 25. Kiwango cha ndoa zilizovunjika katika kipindi cha miaka 25 katika 1965 ni 1 kati ya 5. Kati ya wale waliooana tangu 1970, 1 kati ya kila wenzi 3 waliishia katika talaka.
Tiba ya Kila Kitu Imepatikana?
Kulingana na uchunguzi mmoja, “ulaji maalumu usio na mafuta mengi na uliojaa matunda na mboga umepatikana kwa mara ya kwanza kuwa wenye kupunguza msongo wa damu haraka na kwa matokeo kama vile dawa,” laripoti gazeti The New York Times. Dakt. Denise Simon-Morton, kiongozi wa Prevention Scientific Research Group kwenye National Heart, Lung and Blood Institute, asema kwamba uchunguzi huo wadokeza kwamba “ulaji mmoja tu waweza kuzuia matatizo mengi ya afya”—usaidie kuzuia maradhi ya moyo, msongo wa juu wa damu, na aina nyingi za kansa. Uchunguzi huo ulijaribu athari za mabadiliko ya ulaji katika mamia ya watu wazima kwenye vitovu sita vya kitiba nchini kote. Washiriki walitenganishwa katika vikundi vitatu. Kikundi kimoja kilipewa ulaji ulio sawa na ulaji wa “wastani” wa Wamarekani. Cha pili kilipewa ulaji wenye matunda mengi na mboga, vitu vingine vyote vikibaki vilevile. Cha tatu kilipewa ulaji uliojaa matunda, mboga, na bidhaa za maziwa zisizo na mafuta mengi ambazo pia hazikuwa na mafuta kamili mengi, wala kolesteroli nyingi, wala mafuta kifu mengi. Kikundi cha pili na cha tatu vilikuwa na upungufu wa msongo wa damu uliokuwa wa maana kitiba, lakini ulaji wa kikundi cha tatu ulionyesha matokeo mazuri zaidi. Kwa washiriki wenye msongo wa juu wa damu, matokeo yalikuwa mazuri kama au bora zaidi kuliko yale yaliyopatikana kwa kutumia dawa. Aina hizo mbili za ulaji zilitia ndani viasi 9 hadi 10 vya wastani vya matunda na mboga kila siku.
Wanadamu Wanatumiwa Kazini Tena Katika Japani
“Badiliko kubwa liko karibu kutokea katika viwanda vya Japani,” lataja gazeti la habari Far Eastern Economic Review. “Kwa miongo miwili, viwanda vya Japani vimekuwa vikitafuta ubora wa matokeo kwa kutumia mashine badala ya binadamu. Sasa mwanadamu anatumiwa tena. Viwanda vikuu vichache sasa vinaondoa roboti hasa kutoka mahali pa utengenezaji na kuweka wanadamu mahali pake.” Kwa nini? Kwa sababu wanadamu wana jambo ambalo roboti hazina—uwezo wa kubadilikana. Unapokuja wakati wa kutengeneza aina tofauti ya bidhaa, wanadamu wanabadilikana haraka, ilhali yaweza kuchukua miezi ili kuratibu roboti. “Hapo awali, tulikuwa tukiwatumia watu kana kwamba walikuwa roboti,” asema Tomiaki Mizukami, msimamizi wa kiwanda wa NEC. “Lakini sasa ni lazima tutumie akili zao. Lilikuwa jambo zuri kutumia roboti, lakini sasa twatambua kwamba kutumia watu kwa hakika kunafanya mambo yaende haraka.” Kwa kielelezo, ilipatikana kwamba wafanyakazi kwenye NEC waweza kuunganisha pamoja sehemu za simu kwa matokeo zaidi kwa asilimia 45 kuliko ziwezavyo roboti. Watu pia huchukua nafasi chache zaidi kuliko mashine, na mashine sahili hutokeza urekebishaji mchache zaidi na gharama za chini zaidi za udumishaji. “Baada ya miaka miwili au mitatu ya kujaribia kukiwa na mashine chache, viwanda vinasisitiza kwa dhati kwamba vimeokoa gharama nyingi sana na kiwango cha utokezaji kimeongezeka,” lasema gazeti hilo.
Piramidi “Mpya” za Kuonwa
Kwa miaka mingi watalii wengi sana wamekuwa wakimiminika kuona Piramidi Kuu huko Giza, iliyojengwa na Mfalme Khufu—aitwaye pia Cheops. Lakini ni wachache wameona majengo ya kumbukumbu yaliyoachwa na baba yake, Snefru. Hiyo ni kwa sababu watu walizuiwa kuyaona, yakiwa yamefichwa kwenye kituo cha kijeshi katika Dahshûr. Lakini hilo limebadilika. Baraza kuu la Vitu vya Kale la Misri sasa limefungua eneo hilo kwa umma. Kati ya piramidi 11 zilizopo hapo, 3 zilijengwa na Snefru—alijenga tano kwa jumla—nazo hutia ndani Piramidi Nyekundu, ya kwanza kujengwa ikiwa na sehemu za kando zilizo laini. Piramidi zilizokuwa zimejengwa hapo awali zilikuwa na sehemu za kando zilizo na ngazi. Labda yenye kupendeza sana ni Piramidi Iliyopindwa, ikiitwa hivyo kwa sababu mwinamo wake katika sehemu ya chini hubadilika ghafula kwenye nusu ya juu. Mwinamo wake kwa wazi umewakatisha tumaini wezi wa mawe, sababu ambayo huenda ndiyo imefanya piramidi hii iwe na kizingio cha nje kilichohifadhiwa vyema zaidi kuliko piramidi zote za Misri. Ingawa wafalme wa hapo awali walifanywa kuwa miungu kikamili wakati wa kifo tu, Snefru “alijitangaza kuwa mungu-jua Re anayeishi,” lataja gazeti Time. “Snefru alizikwa katika Piramidi Nyekundu, katika kaburi la kifahari lenye vyumba vitatu lionwalo kuwa bora zaidi kuliko yote katika kipindi cha Ufalme wa Kale.”