Maji—Uhai wa Sayari
YAKIWA hayana rangi, harufu, ladha, na kalori, maji ni muhimu kwa uhai wote ulio duniani. Hakuna mwanadamu, mnyama, au mmea uwezao kuishi bila maji. Kuanzia tembo hadi kijiumbe, maji ni ya muhimu; na hakuna kibadala cha maji. Kila mmoja kati ya zaidi ya watu bilioni tano duniani huhitaji kutumia, katika vitu vya majimaji na chakula, lita mbili na nusu hivi za maji kila siku ili kudumisha afya nzuri. Bila maji hakuna uhai.
Bila maji, haiwezekani kukuza mazao au kufuga wanyama. Bila maji, hakuna chakula—bila chakula, hakuna uhai.
Kwa uzuri, kuna maji tele. Ipigwapo picha kutoka anga za nje, sayari yetu maridadi ya buluu huonekana kana kwamba yapasa kuitwa Maji, si Dunia. Kwa hakika, ikiwa maji ya ulimwengu yangefunika kwa usawa uso wa sayari, yangefanyiza bahari-kuu ya tufeni pote yenye kina cha kilometa 2.5. Mabara yote ya dunia yangetoshea katika Bahari-Kuu ya Pasifiki, na nafasi ibaki.
Bila shaka, mengi ya maji ya dunia yako baharini, na maji ya bahari ni ya chumvi. Mtu akinywa maji ya bahari pekee, angekufa upesi kwa kiu na kwa kupoteza maji mwilini wakati mwili unapojaribu kuondosha chumvi ya ziada. Maji ya bahari si mazuri kwa kilimo au viwanda—hayo huua mimea mingi ya mazao na kutia kutu haraka mashine nyingi. Kwa hiyo, kwa sehemu kubwa, wanadamu waweza kutumia maji ya bahari wakiondoa tu chumvi, na huo ni utaratibu wenye kugharimu sana.
Ni asilimia 3 tu ya maji ya ulimwengu yaliyo matamu, yasiyo na chumvi. Karibu maji yote hayo matamu—asilimia 99 hivi—yamefungiwa katika barafuto na ncha za barafu au yamo ndani sana chini ya ardhi. Ni asilimia 1 tu ipatikanayo kwa urahisi kwa wanadamu.
Asilimia 1 yaonekana kuwa kidogo sana. Je, yaelekea tutapungukiwa na maji matamu? Labda sivyo. Gazeti People & the Planet lataarifu hivi: “Hata hii [asilimia 1], ikisambazwa kwa usawa ulimwenguni pote na kutumiwa kwa uwiano mzuri, itatosha kutegemeza mara mbili au mara tatu ya idadi ya sasa ya ulimwengu.”
Kwa msingi, kiwango cha jumla cha maji duniani hakiongezeki wala hakipungui. Gazeti Science World lataarifu: “Maji unayoyatumia leo huenda wakati mmoja yalizima kiu cha dinosau. Hiyo ni kwa sababu maji yote tuliyo nayo Duniani sasa ndiyo yote ambayo tumepata kuwa nayo—au tutakayopata kuwa nayo.”
Hii ni kwa sababu maji yaliyo ndani na yanayozunguka ulimwengu huzunguka bila kikomo—kutoka baharini hadi angahewa, hadi barani, kuingia mitoni, na kurudi baharini tena. Ni kama vile yule mwanamume mwenye hekima alivyoandika zamani za kale: “Vijito vyote huingia baharini, hata hivyo bahari haifuriki kamwe; mahali ambapo vijito vilitoka hivyo hurudi ili vitoke tena.”—Mhubiri 1:7, New English Bible.
Hata hivyo, japo wingi wa maji matamu duniani, maeneo mengi yana shida. Makala zifuatazo zachunguza matatizo na matazamio ya kuyatatua.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]
Picha ya NASA