Sehemu Zenye Shida Zaidi
MARY, aishiye Marekani, huanza siku yake kwa kuoga katika bafu ya manyunyu, kupiga meno yake mswaki kwa maji ya mfereji yanayotiririka, kuvuta maji ya choo, halafu yeye hunawa mikono. Hata kabla ya kuketi ili apate kiamsha-kinywa, yeye aweza kutumia maji ya kuweza kujaza hodhi ya wastani. Kufikia mwisho wa siku, Mary, kama ilivyo na watu wengineo wengi waishio Marekani, huwa ametumia zaidi ya lita 350 za maji, za kutosha kujaza hodhi mara mbili na nusu. Kwake, maji safi na yaliyo mengi yako karibu sana kwenye mfereji tu. Hayo yanapatikana sikuzote; naye huyaona kuwa kitu cha kawaida tu.
Kwa Dede, aishiye Afrika Magharibi, hali ni tofauti. Yeye huamka kabla ya mapambazuko, huvaa, hubeba beseni kubwa kichwani bila kuishika, na kutembea kilometa nane hadi kwenye mto ulio karibu zaidi. Huko yeye huoga, hujaza beseni maji, kisha hurudi nyumbani. Kawaida hii ya kila siku huchukua muda wa saa nne hivi. Kwa saa nyingine ifuatayo, yeye huyachuja maji hayo ili kuondoa vimelea na kuyatenganisha katika viwekeo vitatu—kimoja cha kunywa, kimoja cha matumizi ya nyumbani, na kingine cha kuogea jioni. Nguo zozote ni lazima zifuliwe mtoni.
“Njaa ya maji inatuua hapa,” Dede asema. “Baada ya kutumia karibu nusu ya asubuhi kuchota maji, ni muda gani wa siku ubakio wa kulima na wa utendaji mwingine mbalimbali?”
Hali ya Dede si ya kipekee hata kidogo. Kulingana na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), jumla ya wakati unaotumiwa kila mwaka na wanawake wengi na watoto wengi waendao kuchota na kubeba maji kutoka mbali, ambayo mara nyingi yamechafuliwa, hufikia miaka milioni kumi!
Wengine Wanayo, Wengine Hawana
Kwa hiyo ingawa kuna maji matamu tele ulimwenguni pote, hayapo kila mahali kwa kiwango kilekile. Hilo ndilo tatizo kuu la kwanza. Kwa mfano, wanasayansi wanakadiria kwamba ingawa Asia ina asilimia 36 ya maji yanayojaza maziwa na mito ya ulimwengu, kontinenti hiyo ni makao ya asilimia 60 ya watu ulimwenguni. Tofauti na hiyo, Mto Amazon una asilimia 15 ya maji ya mito ya ulimwengu, lakini ni asilimia 0.4 tu ya watu wa ulimwenguni waishio karibu sana kuweza kuutumia. Usambazaji usio sawa pia unahusu mvua. Maeneo fulani ya dunia ni karibu makame daima; mengine, ingawa si makame sikuzote, mara kwa mara hupatwa na vipindi vya ukame.
Wataalamu kadhaa waamini kwamba huenda wanadamu wamesababisha mabadiliko fulani katika tabia ya nchi inayohusiana na mvua. Ukataji wa miti, kulima eneo fulani kupita kiasi, kulisha mifugo eneo fulani kupita kiasi vyote hufanya bara libaki bila mimea. Watu wengine wasababu kwamba hilo litokeapo, uso wa dunia huakisi nuru ya jua zaidi kurudi kwenye angahewa. Tokeo: Angahewa yapata kuwa yenye joto zaidi, mawingu hutawanyika, na mvua hupunguka.
Bara kame laweza pia kufanya mvua ipunguke kwa sababu sehemu kubwa ya mvua inayonyesha kwenye misitu ni maji ambayo kwanza yalivukizika kutoka kwenye mimea yenyewe—kutoka kwenye majani ya miti na vichaka. Yaani, mimea hutenda kama sifongo kubwa ambayo hufyonza na kushikilia mvua. Ukiondoa miti na vichaka, ni maji machache yatakayovukizika na kufanyiza mawingu ya mvua.
Kadiri ambavyo matendo ya binadamu yanaathiri mvua bado ni jambo linalojadiliwa; utafiti zaidi wabaki kufanywa. Lakini hili ni hakika: Upungufu wa maji umeenea sana. Tayari, upungufu watisha uchumi na hali ya afya katika nchi 80, yaonya Benki ya Ulimwengu. Na tayari, asilimia 40 ya wakazi wa dunia—zaidi ya watu bilioni mbili—hawana maji safi au hawana njia za kuondoa uchafu.
Yanapokabiliwa na upungufu wa maji, kwa kawaida mataifa tajiri hufaulu kuepuka matatizo makubwa. Hayo hujenga mabwawa, hutumia tekinolojia iliyo ghali ili kurejesha maji yake, au hata kutoa chumvi katika maji ya bahari. Mataifa maskini hayawezi kufanya hivyo. Mara nyingi yanalazimika kuchagua ama kupima maji safi, jambo liwezalo kuzuia maendeleo na kupunguza utokezaji wa chakula, au kutumia tena maji yasiyotiwa dawa, jambo ambalo hueneza maradhi. Uhitaji wa maji uongezekapo kila mahali, wakati ujao waonekana kuwa wenye upungufu mkubwa sana wa maji.
Mwongo wa Tumaini
Siku ya Novemba 10, 1980, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilisema kwa uhakika juu ya “Mwongo [uliokuwa ukija] wa Kupatikana Kimataifa kwa Maji ya Kunywa na Usafi wa Kutunza Afya.” Baraza hilo lilisema kwamba mradi ulikuwa kuandaa, kufikia mwaka wa 1990, maji safi kwa wote na usafi wa kutunza afya kwa watu wote waishio katika nchi zinazoendelea. Kufikia mwisho wa mwongo huo, dola bilioni 134 hivi zilikuwa zimetumiwa ili kuleta maji safi kwa zaidi ya watu bilioni moja na vifaa vya kuondoa maji machafu kwa zaidi ya watu milioni 750—matokeo yenye kuvutia sana.
Hata hivyo, maongezeko haya yalisawazishwa na ongezeko la watu milioni 800 katika nchi zinazoendelea. Hivyo, kufikia 1990, kulibaki zaidi ya watu bilioni moja ambao walikosa maji safi na vifaa vya kutosha vya usafi wa kutunza afya. Ilionekana kwamba hali hii ilikuwa ikionyesha kile ambacho malkia alimwambia Alice katika hadithi za watoto Through the Looking-Glass: “Waona, wapaswa kukimbia mbio kadiri uwezavyo, ili kudumisha hali yako ya wakati huu. Ikiwa wataka kufika mahali pengine, ni lazima ukimbie kasi kwa mara mbili zaidi kuliko ukimbiavyo!”
Tangu 1990, maendeleo ya jumla katika kuboresha hali ya wale wasio na maji na usafi wa kutunza afya, kulingana na WHO, ni “vichache sana.” Alipokuwa naibu-msimamizi wa utafiti kwenye Worldwatch Institute, Sandra Postel aliandika: “Yabaki kuwa kasoro kubwa sana ya maadili kwamba watu bilioni 1.2 hawawezi kunywa maji bila kujihatarisha kupatwa na maradhi au kifo. Sababu haihusiani hasa na uhaba wa maji au ukosefu wa tekinolojia bali ni ukosefu wa ujitoaji wa kijamii na wa kisiasa katika kutosheleza mahitaji ya msingi ya maskini. Itachukua dola zipatazo bilioni 36 zaidi kwa mwaka, sawa na asilimia 4 hivi ya matumizi ya kijeshi ulimwenguni, ili kuletea binadamu kile ambacho wengi wetu twakiona kuwa cha kawaida tu—maji safi ya kunywa na njia safi ya kuondoa uchafu.”
Idadi ya Watu Inayoongezeka, Ongezeko la Uhitaji
Usambazaji usio sawa wa maji unafanywa kuwa tata na tatizo la pili: Kadiri idadi za watu ziongezekavyo, ndivyo uhitaji wa maji uongezekavyo. Mvua ulimwenguni pote hubaki kwa kiwango kilekile, lakini idadi za watu huongezeka. Utumizi wa maji umerudufika angalau mara mbili karne hii, na wengine wakadiria kwamba waweza kurudufika tena kwa miaka 20 ijayo.
Bila shaka, idadi zinazoongezeka za watu huhitaji si maji zaidi ya kunywa tu bali pia chakula zaidi. Nao utokezaji wa chakula wahitaji kiwango kikubwa zaidi cha maji. Hata hivyo, ni lazima kilimo kishindane na uhitaji wa maji wa viwanda na wa watu mmoja-mmoja. Kadiri majiji na maeneo ya viwanda yazidivyo kupanuka, mara nyingi kilimo hushindwa. “Chakula kitatoka wapi?” auliza mtafiti mmoja. “Twaweza kutoshelezaje mahitaji ya watu bilioni 10 wakati tunashindwa kutosheleza mahitaji ya watu bilioni 5 na kwa hakika tukipokonya kilimo maji?”
Ongezeko kubwa la idadi ya watu latukia katika nchi zinazoendelea, ambapo mara nyingi kuna uhaba wa maji. Kwa kuhuzunisha, nchi hizo haziwezi kushughulikia matatizo ya maji kifedha na vilevile kiufundi.
Uchafuzi
Ongezea matatizo yaliyopo ya upungufu wa maji na mahitaji ya idadi ya watu inayoongezeka, lile tatizo la tatu: uchafuzi. Biblia husema juu ya “mto wa maji ya uhai,” lakini mito mingi leo ni mito ya kifo. (Ufunuo 22:1) Kulingana na kadirio moja, kiwango cha maji machafu—ya nyumbani na ya viwanda—yanayoingia katika mito ya ulimwengu kila mwaka hufikia kilometa 450 za kyubiki. Mito mingi na vijito vingi vimechafuliwa tangu mwanzo wake hadi mwisho wake.
Katika mataifa ya ulimwengu yanayoendelea, maji machafu yasiyotiwa dawa huchafua karibu kila mto mkubwa. Uchunguzi wa mito mikubwa 200 ya Urusi ulionyesha kwamba 8 kati ya 10 ilikuwa na viwango vya juu vilivyo hatari vya vitu vilivyo na bakteria na virusi. Mito hiyo na tabaka za maji za nchi zilizoendelea sana, ingawa hazijajaa maji machafu, mara nyingi zina kemikali zenye sumu, kutia ndani zile zitokazo katika mbolea za kilimo. Katika karibu sehemu zote za ulimwengu, nchi zilizo kando ya bahari hupiga pampu maji machafu yasiyotiwa dawa katika maji yasiyo na kina kwenye pwani zake, zikichafua vibaya sana fuo.
Hivyo, uchafuzi wa maji ni tatizo la tufeni pote. Kikijumlisha hali yote, kijitabu cha Audubon Society, Water: The Essential Resource hutaarifu hivi: “Thuluthi moja ya wanadamu husedeka daima katika ugonjwa au udhaifu kwa sababu ya maji yasiyo safi; thuluthi nyingine inatishwa na kule kutiwa majini kwa vitu vya kemikali ambavyo athari yake ya muda mrefu haijulikani.”
Maji Yasiyofaa, Afya Mbaya
Dede, aliyetajwa mapema, aliposema kwamba “njaa ya maji inatuua,” alikuwa akisema kitamathali. Hata hivyo, ukosefu wa maji safi na yaliyo matamu huua, kihalisi. Kwake yeye na kwa mamilioni ya watu kama yeye, hakuna namna ila kutumia maji ya vijito na mito, ambavyo mara nyingi ni kama tu mitaro ya maji machafu. Si ajabu kwamba, kulingana na WHO, mtoto mmoja hufa kwa sababu ya maradhi yanayohusiana na maji kwa kila sekunde nane!
Katika nchi zinazoendelea, kulingana na gazeti World Watch, asilimia 80 ya maradhi yote huenezwa kwa sababu ya kutumia maji yasiyo safi. Vijiumbe vya kuleta maradhi katika maji na uchafuzi huua watu milioni 25 kila mwaka.
Maradhi yenye kuua yahusianayo na maji—kutia ndani maradhi fulani ya kuhara, kipindupindu, na homa ya matumbo—huua watu wengi katika maeneo ya Kitropiki. Hata hivyo, maradhi yasababishwayo na maji hayako tu katika nchi zinazoendelea. Mwaka wa 1993, nchini Marekani, watu 400,000 walikuwa wagonjwa katika Milwaukee, Wisconsin, baada ya kunywa maji ya mfereji yaliyokuwa na kijiumbe-maradhi ambacho hakikuweza kuuawa na klorini. Katika mwaka huohuo, vijiumbe-maradhi vilivyo hatari viliingia katika mifumo ya maji ya majiji mengine Marekani—Washington, D.C.; New York City; na Cabool, Missouri—vikilazimisha wakazi wachemshe maji yaliyotoka miferejini.
Kushiriki Maji ya Mito
Matatizo yanayohusiana ya upungufu wa maji, uhitaji wa ongezeko la idadi za watu, na uchafuzi unaotokeza afya mbaya yote ni mambo yanayoweza kusababisha mkazo na mzozo. Kwa vyovyote, maji si anasa. Mwanasiasa fulani aliyekuwa akipambana na shida ya maji Hispania alisema hivi: “Si tena pambano la kiuchumi, bali ni pigano la kusalimika.”
Kisababishi kikubwa cha mkazo ni kushiriki maji ya mito. Kulingana na Peter Gleick, mtafiti nchini Marekani, asilimia 40 ya watu huishi katika mabonde 250 ya mito ambayo maji yake yanashindaniwa na zaidi ya taifa moja. Mito Brahmaputra, Indus, Mekong, Niger, Naili, na Tigris kila mmoja hupitia nchi nyingi—nchi zinazotaka kutoa maji mengi kadiri iwezekanavyo kutoka mito hiyo. Tayari, kumekuwa na mabishano.
Kadiri uhitaji wa maji uzidivyo kuongezeka, mikazo kama hiyo itaongezeka. Naibu-msimamizi wa Maendeleo Yasiyodhuru Mazingira ya Benki ya Ulimwengu atabiri hivi: “Vita vingi katika karne hii vilikuwa juu ya mafuta, lakini vita vya karne ifuatayo vitakuwa juu ya maji.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
Molekuli Mwendoni
Ebu tufuate safari za molekuli moja ya maji katika safari yake isiyokoma. Mfululizo wa picha zilizoambatanishwa, zenye nambari kulingana na maandishi, huonyesha mojawapo tu ya njia nyingi sana ambazo molekuli moja ya maji yaweza kufuata na kurudi mahali ilipotoka.—Ayubu 36:26; Mhubiri 1:7.
Tutaanza na molekuli iliyo kwenye uso wa bahari-kuu.(1) Maji yavukizwapo na nguvu za jua, hiyo molekuli hupaa hadi maelfu kadhaa ya futi juu ya dunia.(2) Sasa, hiyo hujiunga na molekuli nyinginezo za maji ili kufanyiza tone dogo sana la maji. Tone hilo husafiri kwa upepo kwa mamia ya kilometa. Baada ya muda, tone hilo huvukizika, na molekuli hiyo hupaa tena hadi, hatimaye, ijiungapo na tone la mvua ambalo ni kubwa vya kutosha kuanguka ardhini.(3) Tone hilo la mvua huanguka upande wa milimani pamoja na mabilioni mengineyo ya matone ya mvua; maji hayo huteremka kuingia katika kijito.(4)
Kisha dia hunywa maji kutoka kwenye kijito hicho, akiimeza molekuli tunayozungumzia.(5) Saa nyingi baadaye dia huyo hukojoa, na molekuli hiyo huingia ardhini ambapo huchukuliwa na mizizi ya mti fulani.(6) Kutoka hapo, molekuli hiyo husafiri juu mtini na hatimaye huvukizika kutoka katika jani moja kuingia hewani.(7) Kama awali, hiyo hupaa ili kusaidia kufanyiza tone jingine dogo sana. Tone hilo hupaa na upepo hadi lijiungapo na wingu zito jeusi la mvua.(8) Molekuli hiyo yaanguka tena pamoja na mvua, lakini wakati huu yafikia mto ambao huipeleka baharini.(9) Huko, yaweza kukaa maelfu ya miaka kabla ya kufika usoni pa bahari, kuvukizika, na kubebwa hewani tena.(10)
Duru hiyo haikomi kamwe: Maji huvukizika kutoka baharini, husafiri juu ya bara, hunyesha yakiwa mvua, na kurudi baharini. Kwa kufanya hivyo, maji hutegemeza uhai wote ulio duniani.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 9]
Kile Ambacho Kimependekezwa
Kujenga viwanda vya kuondoa chumvi. Hivi huondoa chumvi kutoka katika maji ya bahari. Hilo kwa kawaida hufanywa kwa kupiga pampu maji ndani ya vyumba vyenye msongo wa chini, ambapo maji huchemshwa. Maji huvukizika na kuelekezwa kwingine, yakiacha chembechembe za chumvi. Ni utaratibu wenye kugharimu sana, usioweza kufikiwa na nchi nyingi zinazoendelea.
Kuyeyusha vilima vya barafu. Wanasayansi fulani huamini kwamba vilima vya barafu vilivyo vikubwa sana, ambavyo vina maji safi na matamu, vyaweza kuburutwa kutoka Antaktika na meli kubwa za kuburuta ili viyeyushwe na kuandaa maji kwa nchi kame zilizo katika Kizio cha Kusini. Tatizo moja ni: Nusu hivi ya kila kilima cha barafu kitayeyuka baharini kabla ya kufika mahali kinapopelekwa.
Kuteka maji ya miamba-maji. Miamba-maji ni miamba iliyo chini sana ardhini yenye maji. Maji yaweza kupigwa pampu, hata katika jangwa kavu zaidi kutoka katika miamba hiyo. Lakini kuteka maji haya ni ghali na hushusha tabaka ya maji. Tatizo jingine ni: Miamba-maji mingi hurudia hali yake polepole—na mingine hairudii kabisa hali yake.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 8]
Picha: Mora, Godo-Foto
[Picha katika ukurasa wa 5]
Kupata maji kwaweza kuchukua muda wa saa nne kila siku
[Picha katika ukurasa wa 8]
Kilometa zipatazo 450 za kyubiki za maji machafu huingia mitoni kila mwaka