Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 11/22 kur. 15-18
  • Ziwa Viktoria—Ziwa Kuu la Afrika

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ziwa Viktoria—Ziwa Kuu la Afrika
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Chanzo cha Naili
  • Maisha Kwenye Ziwa
  • Viumbe vya Ziwa
  • Ziwa Lenye Matatizo
  • Baikal—Ziwa Kubwa Zaidi Ulimwenguni
    Amkeni!—2007
  • Je, Kweli Kuna Ziwa Lenye Rangi ya Waridi?
    Amkeni!—2005
  • “Ziwa la Moto” na Kusudi Lake
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1974
  • Visiwa Vinavyoelea vya Ziwa Titicaca
    Amkeni!—1994
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 11/22 kur. 15-18

Ziwa Viktoria—Ziwa Kuu la Afrika

Na mleta-habari wa Amkeni! katika Kenya

MNAMO mwaka wa 1858, Mwingereza mmoja alipitia pori ambalo bado halikuwa limevumbuliwa ndani kabisa ya Afrika. Akisafiri pamoja na wapagazi Waafrika wachache tu na kulemewa na ugonjwa, uchovu, na wasiwasi, aliwahimiza watu wake waendelee kuchapa miguu. John Hanning Speke alikuwa akitafuta kitu kikubwa sana ambacho hakikuwa rahisi kupatikana—chanzo cha Naili.

Akichochewa na hadithi kuhusu ziwa kubwa ambalo Waarabu wenye kufanya biashara ya utumwa waliliita Ukerewe, Speke aling’ang’ana kuvuka pori ambalo lilionekana kana kwamba hallishi. Hatimaye, baada ya kutembea kwa siku 25, kikundi hicho kidogo cha wasafiri kilithawabishwa na mwono wa ajabu. Mbele yao, kufikia upeo wa macho, waliona ziwa kubwa sana la maji safi. Baadaye Speke aliandika: “Nikawa sina shaka yoyote kwamba ziwa hili ndilo chanzo cha ule mto wa ajabu, chanzo ambacho kimezungumziwa sana, na ambacho wavumbuzi wengi wamekitafuta.” Akaupa uvumbuzi wake jina la malkia aliyekuwa akitawala Uingereza wakati huo—Viktoria.

Chanzo cha Naili

Leo, ziwa hilo ambalo lingali linaitwa Viktoria ni mashuhuri kwa kuwa namba mbili kwa ukubwa kati ya maziwa yote yenye maji safi ulimwenguni—ni Ziwa Superior pekee, katika Amerika Kaskazini, lililo kubwa zaidi. Uso shwari wa Ziwa Viktoria umeenea kwa kilometa za mraba 69,484 na wafanana na kioo kikubwa sana chenye kumetameta katika jua la ikweta. Ziwa hili limevukwa na ikweta kwenye mwisho wake wa kaskazini, na liko katikati ya sehemu ya mashariki na magharibi ya Bonde Kuu la Ufa, likiwa hasa nchini Tanzania na Uganda na kwenye mpaka wa Kenya.

Mto mkuu unaoingia kwenye ziwa hilo ni Kagera nchini Tanzania, ambao hupata maji yake kutoka kwenye milima ya Rwanda. Lakini, mengi ya maji yaingiayo ndani ya Viktoria hutokana na mvua ambayo hunyesha kwenye bara lenye kulizunguka, ambalo limeenea kwa zaidi ya kilometa za mraba 200,000. Mto mmoja tu unaotoa maji nje ya ziwa upo Jinja, nchini Uganda. Mahali hapo, maji huelekea kaskazini kwa kasi na kuanzisha Naili Nyeupe. Ingawa Ziwa Viktoria si chanzo pekee cha Mto Naili, hilo lina maji mengi sana nalo daima lina maji safi na kutegemeza uhai kotekote hadi Misri.

Maisha Kwenye Ziwa

Mtumbwi mmoja, wenye tanga nyeupe mithili ya ubawa wa kipepeo uliosimama wima, waabiri kwenye ziwa. Mtumbwi huo wapeperushwa na pepo zitokazo kwenye bara linalozunguka na kupelekwa kuelekea katikati ya ziwa. Kufikia adhuhuri pepo zabadili njia na kuurudisha huo mtumbwi mahali ambapo ulitoka. Jambo hilo limerudiwa-rudiwa kwa maelfu ya miaka na wavuvi wa ziwa hilo.

Vijiji vilivyoezekwa nyasi zenye rangi ya hudhurungi vimezunguka Ziwa Viktoria. Samaki ndio chakula kikuu cha wanavijiji wa jamii ya Niloti, nao hutegemea ziwa kwa riziki yao ya kila siku. Siku ya mvuvi huanza alfajiri. Watu huondoa maji kutoka kwenye mitumbwi yao yenye kuvuja na kuanza safari ya kuingia kwenye ziwa lenye ukungu. Wakiimba pamoja, wao hupiga makasia hadi maji yenye kina sana na kusimamisha tanga zenye viraka-viraka. Wanawake hutazama kutoka kwenye ufuo mitumbwi hiyo ipoteapo kwenye upeo. Punde si punde, wao huenda zao, kwa kuwa wana kazi chungu nzima za kufanya.

Watoto wanapocheza-cheza majini katika sehemu zenye maji machache, wanawake wafua nguo na kuteka maji ya kunywa kwenye ziwa. Hatimaye, wao humaliza kazi yao kwenye ufuo. Wanawake hurudi nyumbani polepole wakiwa wamebeba kichwani mitungi ya maji kwa makini sana, wamefunga watoto mgongoni, mikono yote miwili ikiwa imebeba nguo zilizofuliwa. Huko, wao hulima mashamba yao madogo-madogo ya mahindi na maharagwe, huokota kuni, na kukandika nyumba zao za udongo kwa mchanganyiko wa samadi na majivu. Mbele zaidi kwenye ufuo, wanawake wanafuma kwa ustadi kamba thabiti za mkonge na vikapu maridadi. Mlio wa shoka wasikika wanaume fulani wanapokata gogo kubwa ili kutengeneza mtumbwi.

Mchana uanzapo kuisha, wanawake waanza tena kutazama ziwa hili kubwa lenye maji safi. Kuonekana kwa ncha za tanga nyeupe kwenye upeo ni ishara ya kwamba wanaume wanarudi. Wao watazamia kwa hamu kurudi huko, wakitaka kuwaona waume zao na samaki watakaoleta.

Kandokando ya ziwa na visiwa, jumuiya hizi ndogo-ndogo hupokea wageni ambao huleta ujumbe wa amani. Kwa miguu na kwenye mitumbwi, kila kijiji hufikiwa. Watu hao ni wanyenyekevu na husikiliza kwa urahisi. Wao hasa husisimuka kusoma fasihi ya Biblia iliyochapishwa katika lugha zao wenyewe za Niloti na za Kibantu.

Viumbe vya Ziwa

Ziwa Viktoria lina zaidi ya aina za samaki 400, na baadhi yao hawapatikani mahali pengine popote ulimwenguni. Aina iliyo ya kawaida sana ni jamii ya perege, au ngege. Samaki hao wadogo wenye rangi-rangi wana majina yenye kuwafafanua kama vile flameback, pink flush, na Kisumu frogmouth. Aina fulani za perege wana njia za ajabu za kuwalinda watoto wao. Wakati wa hatari, mama hufumbua kinywa na watoto wake wachanga huingia ndani kwa ajili ya ulinzi. Baada ya hatari, yeye huwatema tena, nao huendelea na shughuli zao za kawaida.

Ziwa Viktoria ni makao ya ndege wa maji wa aina mbalimbali. Kibisi, mnandi, na mbizi hupiga mbizi ndani ya maji na kudunga samaki kwa ustadi kwa midomo yao mikali. Taji, kulasitara, korongo, na domokijiko hutembea-tembea kwenye maji machache, wakitua bila kumaliza hatua, wakisubiri samaki yeyote asiyetahadhari aje karibu. Juu, kundi la mwari wapaa wakionekana kana kwamba wana tumbo kubwa. Wanapoogelea katika vikundi, wao huzingira makundi ya samaki kisha wao huwachota kwa midomo yao mikubwa inayofanana na vikapu. Bingwa wa anga ni yowe, mwenye mabawa yenye nguvu. Akiondoka kwenye tawi la mti juu ya maji, yeye huelekea chini kwa nguvu, upepo ukitoa sauti nyembamba kwenye mabawa yake, na bila kufanya jitihada kubwa anyakua samaki kutoka kwenye uso wa ziwa. Mnaana wenye rangi nyangavu hujenga viota katika vichaka vinene vya mafunjo ambavyo vimeingia ndani ya ziwa, na mlio wa huzuni wa hondohondo waweza kusikika juu kwenye ufuo katika misitu ya michongoma.

Wakati wa asubuhi na wa jioni, mlio mzito wa viboko waweza kusikika mbali sana kwenye ziwa tulivu. Kufikia mchana wao hulala kwenye ufuo, wakifanana na majabali laini yanayochomoza kwenye maji machache. Watu wa ziwa hujihadhari nyakati zote na mamba. Wachache wa wanyama hao wenye kuogofya wangali wanaishi katika sehemu zenye upweke za Ziwa Viktoria, ingawa wengi wao wameangamizwa na wanadamu.

Ziwa Lenye Matatizo

Idadi ya watu wa Afrika imeongezeka sana tangu siku ambazo John Speke alipoona Viktoria kwa mara ya kwanza. Kwenye ukingo wa ziwa hilo mnaishi watu wapatao milioni 30 ambao sasa hutegemea maji yake safi kwa ajili ya riziki. Katika nyakati zilizopita wavuvi wa eneo hili walitegemea njia za zamani za uvuvi. Wakiwa na vikapu vya kuvulia samaki, wavu wa mafunjo, ndoana, na mikuki, wao walivua kiasi tu walichohitaji. Leo, kwa kuwa boti kubwa za kuvua samaki na nyavu kubwa zimevumbuliwa ambazo huenea maeneo makubwa sana na kuvua tani nyingi za samaki katika maji yenye kina, kuvua samaki kupita kiasi kunahatarisha ikolojia ya ziwa hilo.

Samaki mmoja kutoka nchi za kigeni aliingizwa kwenye ziwa hilo naye akavuruga ikolojia na uvuvi katika ziwa hilo. Matatizo mengine zaidi yanayokumba ziwa hili ni gugu-maji, ambalo huelea na kutokeza ua maridadi la zambarau. Gugu hilo lilitoka Amerika Kusini, na linakua haraka sana hivi kwamba limeziba sehemu kubwa za ufuo wa ziwa na vilevile mito inayoingia kwenye ziwa, likifanya ufuo na gati zisifikiwe na mashua za mizigo, feri za abiria, na mitumbwi ya wavuvi. Ukataji wa miti katika maeneo yanayoleta maji kwenye ziwa, takataka, na ukuzi wa viwanda zimefanya wakati ujao wa ziwa hilo uwe hatarini.

Je, Ziwa Viktoria litaokoka? Hilo ndilo swali ambalo linajadiliwa, na hakuna mtu ajuaye kwa hakika jinsi matatizo yake mengi yatakavyotatuliwa. Lakini, Ziwa Viktoria ni kitu cha asili ambacho kitaendelea kuwapo kwenye dunia muda mrefu baada ya Ufalme wa Mungu kuondoa wale “wanaoiangamiza dunia.” (Ufunuo 11:18) Kisha, wanadamu wataweza kutafakari daima umaridadi wa ziwa hili kubwa la Afrika.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18]

Samaki Anayeliangamiza Ziwa Hilo

Ana mafuta mengi, ni mlafi, anazaa sana, na kukua kufikia urefu wa futi sita. Huyo ni nani? Yeye ni Lates niloticus! Samaki huyu mkubwa na mroho ambaye kwa kawaida anaitwa sangara, au mbuta, aliyeingizwa kwenye Ziwa Viktoria katika miaka ya 1950, ameangamiza ikolojia ya ziwa hilo. Kwa miaka 40 tu tangu aletwe, ameangamiza karibu nusu ya aina 400 za samaki wenyeji wa ziwa hilo. Maangamizi haya yametisha chakula cha mamilioni ya watu ambao hutegemea perege wadogo na samaki wengine wenyeji ili kulisha familia zao. Samaki hao wadogo pia huchangia afya ya ziwa. Baadhi yao hula konokono ambao husababisha maradhi hatari ya kichocho, kwa njia hiyo wakisaidia kudhibiti ugonjwa huo. Wengine hula mwani na mimea mingine ya ziwa ambayo sasa inamea kwa fujo. Ukuzi huo usiodhibitiwa umepunguza oksijeni kwenye maji kwa sababu ya mimea inayooza. Kwa sababu kuna samaki wachache tu wa kuondoa takataka hizo, “maeneo mafu” yametokea, ambamo maji hayana oksijeni, na kuua hata samaki wengi zaidi. Kwa sababu ya uhaba wa samaki wa kula, sangara huyo asiyeshiba sasa amegundua chakula kipya—watoto wake! Samaki anayeliangamiza ziwa sasa yuko katika hatari ya kujiangamiza!

[Ramani katika ukurasa wa 15]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

UGANDA

KENYA

TANZANIA

ZIWA VIKTORIA

[Picha katika ukurasa wa 15]

Kutoa ushahidi kwenye fuo za Ziwa Viktoria

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mnaana

[Picha katika ukurasa wa 16]

Mwari

[Picha katika ukurasa wa 17]

Yangeyange

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Mamba

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Kulasitara amesimama juu ya kiboko

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki