Tauni ya Karne ya 14 Msiba wa Ulaya ya Enzi za Kati
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Ufaransa
Ulikuwa mwaka wa 1347. Tauni hiyo ilikuwa imeangamiza wengi katika Mashariki ya Mbali. Sasa ilikuwa imepenya viunga vya mashariki mwa Ulaya.
WAMONGOL walizingira kituo cha kibiashara cha Kaffa kilichoimarishwa katika Genoa, sasa chaitwa Feodosiya, huko Crimea. Wamongol walikomesha mashambulizi kwa sababu walikuwa wameangamizwa sana na maradhi hayo yasiyojulikana. Lakini walifyatua risasi kiholelaholela walipokuwa wakitoroka. Wakitumia manati kubwa, walivurumisha miili yenye joto ya watu waliokufa kwa tauni juu ya kuta za jiji. Walinzi wachache wa Genoa walipopanda manchani zao na kutoroka mji uliokumbwa na tauni, walieneza maradhi hayo kwa kila bandari waliyozuru.
Baada ya miezi michache Ulaya yote ilikumbwa na vifo. Msiba huo ulienea upesi katika Afrika Kaskazini, Italia, Hispania, Uingereza, Ufaransa, Austria, Hungaria, Uswisi, Ujerumani, Skandinavia, na katika Baltiki. Kwa muda wa miaka miwili hivi, zaidi ya robo ya watu wote wa Ulaya, watu milioni 25, walikufa kutokana na kile ambacho kimeitwa “msiba mkuu zaidi wa kinyama uliowahi kuikumba jamii ya kibinadamu.”—Tauni ya Karne ya 14.a
Mambo Yaliyochangia Kuenea kwa Msiba
Msiba wa Tauni ya Karne ya 14 ulihusisha mengi zaidi ya maradhi tu. Mambo kadhaa yalichangia msiba huo, mojawapo likiwa ni mhemko wa kidini. Mfano mmoja ni fundisho la purgatori. “Mwishoni mwa karne ya 13, itikadi ya purgatori ilisambaa kote,” asema mwanahistoria Mfaransa Jacques le Goff. Mapema katika karne ya 14, Dante alichapisha kichapo kilichopendwa sana cha The Divine Comedy, kikiwa na michoro yenye maelezo juu ya helo na purgatori. Kwa hiyo, watu walifuata maoni ya kidini ya kuwa na mwelekeo wa kushangaza wa kutojali tauni hiyo, huku wakiiona kuwa adhabu kutoka kwa Mungu mwenyewe. Kama tutakavyoona, maoni hayo ya kutazamia mabaya yalichangia sana kuenea kwa maradhi hayo. “Hali hiyo ilifanya tauni hiyo ienee sana,” chasema kitabu The Black Death, cha Philip Ziegler.
Halafu pia, kulikuwa na tatizo la muda mrefu la kuharibika kwa mazao katika Ulaya. Kama tokeo, idadi kubwa ya watu wa bara hilo walipatwa na utapiamlo—walikuwa dhaifu sana kuweza kukinza maradhi.
Tauni Yaenea
Kulingana na daktari wa Papa Clement wa Sita, Guy de Chauliac, Ulaya ilikuwa imekumbwa na aina mbili za tauni: ya nimonia na yenye mitoki. Alieleza kinaganaga maradhi hayo alipoandika hivi: “Tauni ya nimonia ilidumu kwa miezi miwili, dalili zilitia ndani homa na kukohoa damu mfululizo, na mgonjwa alikufa baada ya siku tatu. Tauni yenye mitoki ilidumu kwa kipindi kilichosalia, dalili zake pia zilitia ndani homa isiyokoma, usaha na majipu makubwa ngozini, hasa kwapani na kinenani. Mgonjwa alikufa baada ya siku tano.” Madaktari walishindwa kudhibiti kuenea kwa tauni hiyo.
Watu wengi walikimbia kwa woga—huku wakiacha maelfu walioambukizwa. Kwa kweli, matajiri wenye cheo na wataalamu walikuwa miongoni mwa waliokimbia kwanza. Ingawaje viongozi fulani wa kidini walikimbia pia, vikundi vingi vya wanadini walijificha katika makao ya watawa, huku wakitumaini kwamba wataepuka maambukizo.
Kukiwa na rabsharabsha hiyo, papa aliutangaza mwaka wa 1350 kuwa Mwaka Mtakatifu. Mahujaji ambao wangeenda Roma wangeruhusiwa kuingia moja kwa moja kwenye paradiso bila kupitia purgatori! Mamia ya maelfu ya mahujaji walitii mwito huo—wakasambaza tauni waliposafiri.
Jitihada Zisizofua Dafu
Jitihada za kudhibiti Tauni ya Karne ya 14 hazikufua dafu kwa kuwa hakuna mtu aliyejua jinsi ambavyo iliambukizwa. Wengi waling’amua kwamba kugusana na mtu aliyeambukizwa—au hata kugusa nguo zake—kulikuwa hatari. Wengine hata walihofu kutazamwa na mtu aliyeambukizwa! Hata hivyo, wakazi wa Florence, Italia, waliona paka na mbwa wao kuwa waenezaji wa tauni hiyo. Walichinja wanyama hao pasipo kujua kwamba kwa kufanya hivyo walikuwa wakimruhusu mnyama aliyeeneza maambukizo hayo azaane kwa wingi yaani panya.
Watu walipozidi kufa, wengine walimgeukia Mungu ili kupata msaada. Wanaume na wanawake walitoa mali zao zote kwa kanisa, wakitumaini kwamba Mungu atawalinda kutokana na maradhi—au angalau angewapa thawabu ya uhai wa kimbingu endapo wangekufa. Jambo hilo lilitajirisha sana kanisa. Hirizi za bahati njema, mifano ya Kristo, na talasimu zilionwa na wengi kuwa kinga. Wengine waligeukia ushirikina, mizungu, na dawa bandia ili kupata tiba. Ilisemekana kwamba marashi, siki, na mikorogo ya pekee vilidhibiti maradhi hayo. Utoaji-damu kwa ajili ya tiba ulipendwa sana pia. Kitivo cha kitiba cha kitaaluma katika Chuo Kikuu cha Paris hata kilidokeza kwamba tauni hiyo ilisababishwa na mfuatano wa sayari! Hata hivyo, maelezo na “tiba” bandia hazikukomesha kwa vyovyote kuenea kwa tauni hiyo yenye kufisha.
Athari Zenye Kudumu
Baada ya miaka mitano ilionekana kana kwamba Tauni ya Karne ya 14 ilikuwa imefikia kikomo hatimaye. Lakini kabla ya mwisho wa karne, tauni hiyo ilizuka tena angalau mara nne. Athari za Tauni ya Karne ya 14 zimelinganishwa na athari za Vita ya Ulimwengu ya Kwanza. “Wanahistoria wa kisasa wanakubaliana kabisa kwamba kuzuka kwa tauni yenye kuambukiza kuliathiri sana uchumi na jamii baada ya mwaka wa 1348,” chasema kitabu cha mwaka wa 1996 The Black Death in England. Tauni hiyo iliangamiza idadi kubwa ya watu, na maeneo mengine yalirudia hali yake baada ya karne nyingi. Kukiwa na wafanyakazi wachache, mshahara uliongezeka. Wamiliki-ardhi waliokuwa na ufanisi awali walifilisika, na mfumo wa kikabaila—sehemu muhimu ya Enzi za Kati—uliporomoka kabisa.
Kwa hiyo, Tauni hiyo ilitokeza mabadiliko ya kisiasa, kidini, na kijamii. Kabla ya tauni hiyo, lugha ya Kifaransa ilizungumzwa kwa kawaida na watu walioelimika huko Uingereza. Hata hivyo, kufa kwa walimu wengi sana wa Kifaransa, kulifanya lugha ya Kiingereza izungumzwe zaidi ya Kifaransa huko Uingereza. Kulikuwa na mabadiliko ya kidini pia. Kama mwanahistoria Mfaransa Jacqueline Brossollet anavyosema, kwa sababu ya uhaba wa watu waliotaka ukasisi, “kwa kawaida Kanisa liliwaandikisha watu wasio na ujuzi, na wasiojali.” Brossollet asisitiza kwamba “kupungua kwa vituo vya [kidini] vya elimu na imani kulikuwa mojawapo ya mambo yaliyoleta Marekebisho Makubwa ya Kidini.”
Bila shaka Tauni ya Karne ya 14 iliathiri sana sanaa, huku kifo kikiwa kichwa cha kawaida katika sanaa. Ile dansi mashuhuri ya kifo, yenye mifano ya viunzi na maiti, ikawa istiari ya kawaida ya uwezo wa kifo. Watu wengi waliookoka tauni waliishi maisha ya ufasiki kwa kuwa walikosa tumaini la wakati ujao. Kwa hiyo maadili yakazorota sana ajabu. Kwa habari ya kanisa, kwa sababu ya kushindwa kuzuia Tauni ya Karne ya 14, “watu wa enzi za kati walihisi kwamba Kanisa lao lilikuwa limewatahayarisha.” (The Black Death) Wanahistoria fulani wanasema pia kwamba mabadiliko ya kijamii yaliyotukia baada ya Tauni ya Karne ya 14 yaliendeleza ubinafsi na ujasiri na yaliboresha hali ya kijamii na kiuchumi—misingi ya ubepari.
Tauni ya Karne ya 14 ilichochea pia serikali ziimarishe mifumo ya kudhibiti usafi wa afya. Jiji la Venice lilichukua hatua ya kusafisha barabara zake baada ya tauni hiyo kukoma. Mfalme John wa Pili wa Ufaransa, aliyeitwa Mwema, hali kadhalika aliamuru usafishaji wa barabara ikiwa njia ya kuepuka tisho la ugonjwa wa mlipuko. Mfalme huyo alichukua hatua hiyo baada ya kupata habari za mfalme wa kale wa Ugiriki aliyeokoa Athene kutokana na tauni kwa kusafisha barabara. Barabara nyingi za enzi za kati, zilizokuwa mifereji tu ya maji machafu, hatimaye zilisafishwa.
Je, Ni Jambo la Kale?
Hata hivyo, ulipofika mwaka wa 1894 mtaalamu Mfaransa wa bakteria Alexandre Yersin aligundua basila iliyosababisha Tauni ya Karne ya 14. Iliitwa Yersinia pestis kutokana na jina lake. Miaka minne baadaye mwanamume mwingine Mfaransa, Paul-Louis Simond, aligundua fungu la kiroboto (anayebebwa na panya) katika uambukizaji wa maradhi hayo. Punde si punde chanjo isiyo na matokeo sana ilivumbuliwa.
Je, tauni hiyo ni jambo la kale? Hata kidogo. Wakati wa majira ya baridi kali ya mwaka wa 1910, watu wapatao 50,000 walikufa kutokana na tauni hiyo huko Manchuria. Na kila mwaka Shirika la Afya Ulimwenguni hurekodi maelfu ya visa vipya—idadi hiyo inazidi kuongezeka. Aina mpya ya maradhi hayo imegunduliwa pia—ni maradhi sugu. Naam, viwango vya msingi vya usafi visipozingatiwa, tauni hiyo itabaki tisho kwa wanadamu. Kitabu Pourquoi la peste? Le rat, la puce et le bubon (Mbona Kuwe na Tauni? Panya, Kiroboto, na Mtoki), kilichohaririwa na Jacqueline Brossollet na Henri Mollaret, kinakata kauli kwamba “mbali na kuwa maradhi ya Ulaya ya kale katika Enzi za Kati, . . . inasikitisha kuwa, huenda tauni hiyo ikawa maradhi ya wakati ujao.”
[Maelezo ya Chini]
a Watu walioishi wakati huo waliiita ugonjwa mkubwa wa kuambukiza au ugonjwa wa mlipuko.
[Blabu katika ukurasa wa 23]
Wanaume na wanawake walitoa mali zao zote kwa kanisa, wakitumaini kwamba Mungu atawalinda kutokana na maradhi
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 24]
Madhehebu ya Flagellants
Watu wengine walioona tauni hiyo kuwa adhabu kutoka kwa Mungu, walijaribu kutuliza hasira ya Mungu kwa kujipiga mijeledi. Udugu wa Flagellants, shirika lenye washiriki wapatao 800,000, lilipendwa sana wakati wa Tauni ya Karne ya 14. Sheria za madhehebu hayo zilikataza kuzungumza na wanawake, kufua au kubadili mavazi. Kujipiga mijeledi hadharani kulifanywa mara mbili kwa siku.
“Kujipiga mijeledi kulikuwa mojawapo ya njia chache zilizokuwapo za kutuliza hofu iliyowakumba watu,” chasema kitabu Medieval Heresy. Madhehebu ya Flagellants yalijulikana pia kwa sababu ya kushutumu uongozi wa makasisi na kudharau zoea lenye kunufaisha kanisa la kuachilia makosa. Si ajabu kwamba papa alishutumu madhehebu hayo mnamo mwaka wa 1349. Hata hivyo, madhehebu hayo yalididimia baada ya kukoma kwa Tauni ya Karne ya 14.
[Picha]
“Flagellants” walijaribu kumtuliza Mungu
[Hisani]
© Bibliothèque Royale de Belgique, Bruxelles
[Picha katika ukurasa wa 25]
Tauni hiyo huko Marseilles, Ufaransa
[Hisani]
© Cliché Bibliothèque Nationale de France, Paris
[Picha katika ukurasa wa 25]
Alexandre Yersin aligundua basila iliyosababisha tauni hiyo
[Hisani]
Culver Pictures