Uvutio wa Santeria
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO
SANTERIA imekuwa dini maarufu nchini Kuba kwa miaka mingi. Hata hivyo, hatua kwa hatua dini hii imeingizwa katika nchi nyingine. Kwa mfano, katika mojawapo ya masoko makubwa huko Mexico City kuna maduka yanayouza vifaa vya dini vya Santeria peke yake, kama vile misalaba, mishumaa, hirizi, na sanamu. Mengi ya maduka hayo yanaitwa botanica, nayo yanapatikana katika majiji mengine makubwa ya Amerika. Katika New York City maduka hayo hutangazwa katika kurasa za biashara za kitabu cha simu mara nyingi kuliko maduka mengine ya kidini.
Watu wengi huvutiwa na usirisiri na hali isiyo ya kawaida ya Santeria. Mazoea ya Santeria yanapatikana katika baadhi ya muziki na fasihi ya Kilatini. Santeria inaelekea kuwa ya kilimwengu na kitamaduni zaidi kuliko ya kidini, nayo imepenya katika sherehe za utamaduni na muziki wa Kiafrika na visiwa vya Karibea.
Mwanzo Katika Afrika ya Kale
Mapokeo na mazoea mengi ya Santeria yafanana na ya dini ya kale ya Kiafrika ya kabila la Yoruba huko Nigeria. Wayoruba walipopelekwa visiwa vya Karibea wakiwa watumwa mnamo miaka ya 1770 hadi 1840, waliingiza dini yao huko. Kule Amerika, Waafrika hao waliokuwa watumwa walilazimishwa kukubali Ukatoliki, lakini walikataa kuacha mapokeo yao kabisa. Kwa hiyo wakaanzisha ibada mpya iliyokuwa na mazoea yaliyochanganywa kutoka katika dini zote mbili.
Walipojitahidi kuabudu kulingana na itikadi zao za kale, watumwa hao waliwapa watakatifu wa Kikatoliki majina mawili, hivyo kila mtakatifu wa Kikatoliki alilingana na mungu wa Kiafrika aliyekuwa na sifa na nguvu hususa. Kwa hiyo, miungu ya kiume na ya kike ya Kiafrika, iliyoitwa orisha, ilipata majina na maumbile ya watakatifu wa Kikatoliki. Hata hivyo, desturi, mapokeo na itikadi za dini hiyo zilidumu sawa na jinsi zilivyokuwa barani Afrika. Kasisi mmoja wa Santeria nchini Kuba anaeleza hivi: “Mchanganyiko huo wa dini unatuwezesha kuabudu mungu wa Kikatoliki madhabahuni, lakini twatambua mungu wa Kiafrika anayewakilishwa.”
Dini kama vile za uchawi, Obeah, na macumba pia zimefanyizwa na visehemu vya liturujia, sakaramenti, na vifaa vitakatifu vya Kanisa Katoliki ambavyo vimechanganywa na mazoea ya uchawi ya Kiafrika. Kwa kuwa tangu mwanzo Kanisa Katoliki la Amerika ya Kusini lilipinga dini za Kiafrika, ibada ya dini ya Santeria ilifanywa kisirisiri kwa muda mrefu. Hatimaye, Kanisa Katoliki likakubali mchanganyiko huo wa dini miongoni mwa watumwa.
Mazoea ya Santeria
Ibada hiyo ina mazoea gani? Wasanteria huabudu mungu mkuu mmoja, na kikundi cha miungu ya Wayoruba, waitwao orisha. Mapenzi ya orisha hufasiriwa na mapadre wa Santeria kupitia uaguzi. Yasemekana kwamba mara kwa mara waabudu hupagawa na orisha ili shauri la orisha litolewe kupitia waabudu hao. Wafuasi waweza kusihi orisha kupitia maombi, muziki, tabia nzuri, na kwa kuitolea sadaka. Madhabahu ni muhimu katika ibada hiyo; wasanteria wana madhabahu nyumbani mwao, nao huweka maua, kileo kiitwacho rum, keki, na sigara juu ya madhabahu hayo ili kuifurahisha miungu na kupata msaada.
Katika makala moja ya gazeti la New York Times, Lizette Alvarez alieleza hivi juu ya mafundisho ya Santeria: “Dini hiyo inakazia mambo ya maisha tuliyo nayo sasa badala ya maisha ya baada ya kifo, nayo hukazia nguvu za asili. Kila mungu huwakilisha jambo fulani la asili, kama radi, na sifa moja ya kibinadamu, kama nguvu.” Mapadre wa Santeria husaidia watu kutatua matatizo ya kila siku kwa kutafuta shauri kutoka kwa orisha. Hao si mapadre wa Kanisa Katoliki, nazo desturi zao za ibada hufanywa katika nyumba za watu wala si katika hekalu.
Watu wanaohitaji msaada wa kihisia-moyo na kiuchumi wanavutiwa hasa na Santeria kwa kuwa washiriki wa dini hiyo ni kama familia nao wana umoja fulani. Wanaopendezwa hasa ni maskini na watu wanaohamia nchi yenye dini ya Santeria. Wafuasi ni washiriki wa jumuiya yenye msanteria wa kiume ama wa kike aliye kama baba ama mama wa ubatizo, mshauri, na padre kwa jumuiya hiyo. Washiriki wapya huingizwa na padre kupitia sherehe yenye muziki, dansi, na kutolewa kwa dhabihu za wanyama. Dhabihu za wanyama hutolewa pia ili kusherehekea kuzaliwa kwa mtoto, ndoa, na wakati mtu afapo. Kuku, mbuzi, njiwa, hua, na kasa ni baadhi ya wanyama ambao hutumiwa kwa kusudi hilo.
Muziki wa Santeria
Muziki ni sehemu muhimu katika ibada ya Santeria. Muziki huchezwa wakati wa bembé, ambazo ni sherehe za kupiga ngoma kuomba miungu. Midundo hususa hupigwa kumwita mungu fulani. Mdundo wa ngoma huvuma sana hivi kwamba wasikika mbali sana.
Ala za muziki kama ngoma, au marimba, zimetumiwa katika ibada huko Afrika Magharibi kwa karne nyingi. Hivyo ndivyo ala hizo zilivyotumiwa watumwa walipozileta Amerika. Nchini Brazili, utando wa ngoma takatifu hutengenezwa kwa ngozi za wanyama ambao wametolewa dhabihu kidesturi, kisha ala mpya hubatizwa kidesturi kwa maji “matakatifu” kutoka katika Kanisa Katoliki. Katika utamaduni wa Karibea na Afrika nchini Haiti, baadhi ya ngoma huwakilisha mungu fulani.
Si jambo geni kupata diski zenye muziki mtakatifu wa Santeria madukani, ambazo zinaonyesha yaliyomo waziwazi. Ngoma hasa ndizo hutumiwa, nayo majina ya baadhi ya nyimbo hizo ni majina ama ya miungu ya Santeria ama ya desturi ya dini hiyo. Polepole, midundo hiyo imeingizwa katika baadhi ya muziki wa Kilatini. Baadhi ya nyimbo za Kilatini zina maneno ya Santeria.
Maoni ya Biblia
Dini ya Santeria ina uhusiano wa karibu na uwasiliani-roho, ambao ni aina ya ibada inayokatazwa katika Biblia. (Mambo ya Walawi 19:31) Neno la Mungu lataja “zoea la uwasiliani-roho” pamoja na “kazi za mwili” zinazomzuia mtu asiweze kuurithi Ufalme wa Mungu. (Wagalatia 5:19-21) Wale watakao kupata upendeleo wa Mungu wanaamriwa katika Maandiko ‘kuikimbia ibada ya sanamu’ na ‘kumwabudu Baba kwa roho na kweli.’—1 Wakorintho 10:14; Yohana 4:23, 24.
Wakristo wapaswa kutambua kwamba mazoea na muziki wa Santeria zinazidi kuwa za kilimwengu. Tafrija mbalimbali na baadhi ya desturi ya utamaduni wa Amerika-Latini zimechanganywa na mazoea ya Santeria. Hizo zinapendwa na wengi nazo zinaonwa kuwa hazina madhara yoyote. Hata hivyo, Wakristo washauriwa kuepuka chochote kile kisichopatana na kanuni za Biblia hata ingawa chapendwa na wengi, na hata ingawa hakionekani kuwa chenye kudhuru.—2 Wakorintho 6:14-18.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]
MANENO YANAYOTUMIWA KATIKA DINI YA SANTERIA
Babalú-aye: Mungu mponyaji anayeabudiwa kama “Mtakatifu” Lazaro.
Changó: Mungu wa moto, ngurumo, na radi naye ni mlinda-mizinga, anayeabudiwa kama “Mtakatifu” Barbara katika Kanisa Katoliki.
Ifa Corpus: Mfumo wa sheria ulioandikwa kwa alama 256 zinazowakilisha mapokeo ya Santeria.
Ikole orun: “Mbingu” ambamo wanadamu wote watakwenda wafapo. Hata hivyo, watu wabaya wataishi katika moto wa mateso duniani na kuteswa katika ikole orun.
Obatalá: Mungu aliyeumba uhai na ufahamu wa kibinadamu kutoka kwa dunia yenyewe.
Ochún: Mungu wa kike wa mito, upendo, ndoa, fedha, shangwe, na utele, yeye pia ni Virgen de la Caridad, mtakatifu-mlinzi wa Kuba.
Oggún: Mungu-mlinzi wa wachimba-migodi na wafanyakazi, anayeabudiwa kama “Mtakatifu” Petro.
Oloddumare: Mungu mkuu kabisa, aliyeumba ulimwengu wote.
Orumila: Mungu aamuaye wakati ujao wa kila mtu mmoja-mmoja.
Yemayá, au Xemayá: Mungu wa kike wa bahari na wa uwezo wa kuzaa, anayejulikana kama Bikira Maria, au Virgen de Regla wa Kuba.
[Picha katika ukurasa wa 24]
Vifaa vya Santeria katika duka la “botanica”