Asali—Zawadi ya Nyuki kwa Wanadamu
Na mwandishi wa Amkeni! nchini Mexico
ALIPOFIKA mahali palipokuwa na sega la asali lililokuwa likidondoka asali mwituni, askari Mwisraeli aliyekuwa amechoka alichovya fimbo yake ndani na kula asali hiyo. Mara moja, “macho yake yakaanza kung’aa” na akapata nguvu tena. (1 Samweli 14:25-30) Simulizi hilo la Biblia linaonyesha njia moja ambayo asali humnufaisha mwanadamu. Inaweza kumpa mtu nguvu mara moja kwani karibu asilimia 82 yake ni wanga. Kwa kupendeza, inasemekana kwamba gramu 30 tu za asali zinaweza kumpa nyuki nguvu za kuuzunguka ulimwengu!
Je, nyuki hutengeneza asali kwa manufaa ya mwanadamu tu? La, asali ni chakula chao. Bumba la nyuki lenye ukubwa wa kawaida linahitaji kati ya kilo 10 hadi 15 za asali ili nyuki waendelee kuwa hai wakati wa majira ya baridi kali. Lakini katika majira mazuri, nyuki hao wanaweza kutokeza kilogramu 25 hivi za asali, kukiwa na kiasi cha ziada kinachoweza kutumiwa na wanadamu na pia wanyama kama vile dubu na rakuni.
Nyuki hutengenezaje asali? Nyuki hukusanya nekta kutoka kwenye maua kwa kuifyonza kwa ndimi zao zilizo kama mrija. Wao huibeba hadi kwenye mzinga katika mojawapo ya matumbo yao. Nyuki wengine huichukua na “kuitafuna” kwa nusu saa hivi na kuichanganya na vimeng’enya vinavyotoka kwenye tezi zilizo kinywani mwao. Kisha wao huitia ndani ya sega lenye pembe sita lililotengenezwa kwa nta ya nyuki na kuipepea kwa mabawa yao ili kuondoa maji.a Baada ya kiasi cha maji kupunguzwa kwa asilimia 18, sega hufunikwa kwa tabaka nyembamba ya nta. Asali iliyofunikwa inaweza kudumu milele. Inaripotiwa kwamba asali inayoweza kuliwa imepatikana katika makaburi ya Mafarao ambayo yamekuwapo kwa miaka 3,000 hivi.
Manufaa ya Asali kwa Afya
Zaidi ya kuwa tu chakula kinachofaa, asali ni mojawapo ya dawa za zamani zaidi zinazotumika, kwani ina vitamini B nyingi, madini kadhaa, na vitu vyenye uwezo wa kuzuia utendaji wa oksijeni.b Dakt. May Berenbaum, mtaalamu wa wadudu katika Chuo Kikuu cha Illinois, Marekani, anasema: “Asali imetumiwa kwa karne nyingi kutibu matatizo mengi ya afya kama vile vidonda, kuungua, watoto wa jicho, vidonda vya ngozi na majeraha ya kukwaruzwa.”
Likieleza kuhusu upendezi wa hivi karibuni kuhusu manufaa za asali kwa afya, Shirika la Habari la CNN linaripoti hivi: “Asali iliacha kupakwa kwenye vidonda wakati dawa za kuua viini vya ugonjwa zilipovumbuliwa wakati wa Vita vya Pili vya Ulimwengu. Lakini utafiti mpya na kutokea kwa bakteria zisizoweza kuuawa na dawa hizo umefanya asali ianze kutumiwa tena.” Kwa mfano, sehemu moja ya utafiti huo inahusu kutibu majeraha ya kuungua. Ilionekana kwamba wagonjwa walipona haraka na kuhisi maumivu machache na kuwa na makovu machache walipotibiwa kwa asali.
Uchunguzi unaonyesha kwamba kwa sababu ya kimeng’enya fulani kinachoongezwa kwenye nekta na nyuki, asali ina uwezo wa kupigana na bakteria na viini. Kimeng’enya hicho hutokeza haidrojeni peroksaidi, ambayo huua bakteria hatari.c Isitoshe, inapopakwa juu ya kidonda, asali hupunguza mwasho na kuchochea ukuzi wa tishu zinazofaa. Hivyo, mtaalamu wa biolojia na kemia Dakt. Peter Molan wa New Zealand anasema: “Wataalamu wa matibabu wanaiona asali kuwa dawa nzuri, inayofaa kwa matibabu.” Kwa kweli, Shirika la Matibabu la Australia limeidhinisha asali kuwa dawa, na asali huuzwa kama dawa ya kutibu vidonda katika nchi hiyo.
Ni vyakula gani vingine vitamu ambavyo hujenga mwili na vinavyoweza kutumiwa kama dawa? Si ajabu kwamba zamani sheria zilipitishwa ili kulinda nyuki na wafugaji wa nyuki! Ilikuwa kosa kukata miti au kuharibu mizinga yenye nyuki, na mtu angeweza kuadhibiwa kwa kutozwa faini kubwa au hata kuuawa. Kwa kweli, asali ni zawadi nzuri kwa mwanadamu ambayo humletea Muumba sifa.
[Maelezo ya Chini]
a Nta ambayo nyuki hutumia kutengeneza sega la asali hutengenezwa kwenye tezi za pekee katika mwili wa nyuki. Vyumba vyenye pembe sita vya sega huwezesha kuta zake, zilizo na unene wa thuluthi moja ya milimeta, kutegemeza uzito ambao umezidi uzito wa sega kwa mara 30. Kwa hiyo, sega ni ubuni wa ajabu.
b Watoto wachanga hawapaswi kula asali kwa sababu wanaweza kupatwa na ugonjwa unaodhoofisha misuli ambao husababishwa na bakteria zenye sumu katika watoto wachanga.
c Kwa kuwa kimeng’enya hicho huharibiwa na joto na nuru, asali ambayo haijaondolewa vijidudu hutumiwa kama dawa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 16]
Kupika kwa Asali
Asali ni tamu zaidi kuliko sukari. Kwa hiyo, unapotumia asali, tumia tu nusu hadi robo tatu ya kiasi ambacho ungetumia ikiwa ungetumia sukari. Pia kwa kuwa asilimia 18 hivi ya asali ni maji, punguza vitu vyenye umajimaji katika vitu unavyotumia kupika. Ikiwa hakuna vitu vyenye umajimaji, ongeza vijiko viwili vikubwa vya unga kwa kila kikombe cha asali. Unapooka, ongeza pia nusu kijiko kidogo cha magadi kwa kila kikombe cha asali na upunguze kiasi cha joto la kiokeo chako kwa nyuzi 15 Selsiasi.
[Hisani]
National Honey Board
[Picha katika ukurasa wa 16]
Nyuki anayetafuta nekta
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Sega la asali
[Picha katika ukurasa wa 17]
Bumba la nyuki wa asali
[Picha katika ukurasa wa 17]
Mfugaji wa nyuki akikagua ubao wa mzinga