Kuutazama Ulimwengu
◼ ‘Ni wazi’ kwamba joto linaongezeka duniani, na ‘inaelekea sana’ kuwa shughuli za wanadamu ndizo zimesababisha hali hiyo.—KAMATI YA SERIKALI MBALIMBALI KUHUSU MABADILIKO YA HALI YA HEWA (IPCC), USWISI.
◼ Nchini Ujerumani, kuna watu kati ya milioni 1.4 na milioni 1.9 ambao wana “uraibu wa kutumia dawa za kawaida.” Tatizo hilo limesambaa kama tu tatizo la kutegemea kileo.—TAGESSCHAU, UJERUMANI.
◼ Nchini Uingereza, ni rahisi sana kwa watoto walio na umri wa chini ya mwaka mmoja kuuawa.—THE TIMES, UINGEREZA.
◼ Sehemu fulani za mpaka kati ya Marekani na Kanada zimeota mimea mingi hivi kwamba maofisa “wanakuwa na wakati mgumu kuupata mpaka huo.” “Ikiwa huwezi kuupata, basi huwezi kuudhibiti,” anasema Dennis Schornack wa Shirika la Kimataifa Linaloshughulikia Mipaka.—ASSOCIATED PRESS, MAREKANI.
Mwili Umeumbwa Ili Ujitibu
“Kiasili mwili wetu una uwezo wa kujitibu dhidi ya asilimia 60 hadi 70 ya magonjwa yote,” anasema Profesa Gustav Dobos, daktari mkuu katika Hospitali ya Miners, huko Essen, Ujerumani. Mwili unatengeneza dawa 30 hadi 40 hivi ili utibu magonjwa, dawa hizo zinatia ndani cortisone na dawa nyingine zinazozuia vijiwe vya figo. Watafiti wameelewa baadhi ya njia ambazo mwili hutumia kujitibu, lakini kuna mambo mengi ambayo bado hawaelewi. Kulingana na gazeti Vital, wanasayansi wamegundua kwamba “kuna mwingiliano tata kati ya homoni, chembe zinazopitisha habari, na chembe zinazoangamiza chembe nyingine,” wanasayansi hao wanasema kwamba “hata hisia zinachangia kutibu mwili.” Hata hivyo, gazeti hilo linaendelea kusema kwamba mfadhaiko na matatizo ya kibinafsi yanaweza “kupunguza nguvu za mfumo wa kinga mwilini kwa miezi mingi.”
Utajiri wa Ulimwengu Umegawanywaje?
“Asilimia 1 ya watu matajiri zaidi ulimwenguni wanamiliki asilimia 40 ya utajiri ulio kwenye sayari hii,” linasema gazeti la London Guardian. “Wale wanaoshughulikia huduma za kifedha na Intaneti ni kati ya watu matajiri zaidi,” linasema gazeti hilo. Utafiti mmoja uliofanywa na Umoja wa Mataifa ulionyesha kwamba asilimia 37 ya watu matajiri zaidi wanaishi Marekani, asilimia 27 Japani na asilimia 6 wanaishi Uingereza. Asilimia 50 ya watu maskini duniani wanamiliki chini ya asilimia 1 ya utajiri duniani. Kulingana na Duncan Green, ambaye ni mkuu wa utafiti katika Oxfam nchini Uingereza, “kiwango hicho cha ukosefu wa usawa kinashtua. . . . Haiwezekani kutoa sababu nzuri ya watu wachache kuwa na utajiri mwingi hivyo huku watu milioni 800 wanalala njaa kila siku.”
Ukosefu wa Usawa wa Kijinsia Nchini China
Mnamo 2005, kulikuwa na wavulana 118 kati ya wasichana 100 waliozaliwa. Katika maeneo fulani “namba hiyo imefikia wavulana 130 kati ya wasichana 100,” linasema gazeti China Daily. Sababu ya ukosefu huo wa usawa ni utoaji mimba baada ya kupima na kutambua jinsia ya mtoto. Maofisa wanakiri kwamba jambo hilo limetokea kwa sababu ya sera za China kuhusu kuzuia mimba zinazowaruhusu wenzi wa ndoa wanaokaa majijini wawe na mtoto mmoja tu. Gazeti hilo linasema: “Kufikia mwaka wa 2020, wanaume ambao wamefikia umri wa kuoa watakuwa milioni 30 zaidi ya wanawake,” na ukosefu huo wa usawa “utafanya jamii isiwe imara.”