“Usiwaache Kunguni Wakuume!”
KUFIKIA katikati ya karne ya 20, ilionekana kwamba wanadamu wamefaulu kuwadhibiti kunguni. Watu fulani walifahamu kunguni kupitia tu wimbo wa zamani wa Kiingereza ulioimbwa na watoto wa shule za nasari (au chekechea) uliosema: “Usiwaache kunguni wakuume.” Hata hivyo, katika miaka ya 1970, nchi nyingi ziliamua kupiga marufuku matumizi ya dawa ya DDT—iliyokuwa dawa kuu ya kuua kunguni—kwa kuwa ilikuwa yenye sumu na iliharibu mazingira.
Hata hivyo, kemikali nyingine zilipotumiwa ilionekana kwamba kunguni walikuwa sugu na hazikuwaua. Pia watu walianza kusafiri mara nyingi zaidi na bila kujua walihama pamoja nao. Matokeo yakawaje? Ripoti moja ya mwaka wa 2012 kuhusu kuwadhibiti wadudu hao inasema: “Katika miaka 12 ambayo imepita kunguni wameanza kuonekana tena nchini Marekani, Kanada, Mashariki ya Kati, nchi kadhaa za Ulaya, Australia, na katika sehemu fulani za Afrika.”
Huko Moscow, Urusi, katika mwaka mmoja hivi karibuni, ripoti za kutokea kwa kunguni ziliongezeka mara kumi kuliko ilivyokuwa hapo awali. Wakati huohuo, upande ule mwingine wa ulimwengu, huko Australia, kumekuwa na ongezeko la asilimia 5,000 la kunguni tangu mwaka wa 1999!
Watu fulani hubeba kunguni bila kujua wanapoenda dukani, kwenye kumbi za sinema, au hotelini. “Upende usipende utabeba kunguni,” anasema meneja fulani wa hoteli nchini Marekani. “Maadamu hoteli inapata wateja lazima kunguni wataendelea kuwapo.” Kwa nini ni vigumu kiasi hicho kuwamaliza kunguni? Unaweza kujilindaje? Kunguni wanapovamia nyumba yako, unaweza kuchukua hatua gani zinazofaa ili kuwaondoa na kuwazuia wasirudi tena?
Wadudu Wasiokufa kwa Urahisi
Kwa kuwa wadudu hao ni wadogo kama mbegu ya tofaa na wana mwili bapa, kunguni wanaweza kujificha mahali popote pale. Wanaweza kujificha katika godoro lako, fanicha zako, sehemu ya ukutani ya kuunganishia vitu vya umeme, au hata kwenye simu yako. Kwa kawaida kunguni hupenda kujificha mita tatu hadi sita kutoka kwenye vitanda na maeneo ya kuketi. Kwa nini? Ili wawe karibu na chakula chao, yaani, wewe!a
Mara nyingi, kunguni huwauma watu wanapolala. Hata hivyo, watu wengi hawahisi wanapoumwa kwa sababu mdudu huyo humdunga mtu kitu kinachogandisha kinachomwezesha kuendelea kula kwa dakika kumi hivi bila kukatizwa. Na ingawa kunguni wanaweza kula kila juma, imesemekana kwamba wanaweza kuendelea kuishi bila kula kwa miezi mingi.
Tofauti na mbu na wadudu wengine, inaonekana kwamba kunguni hawaenezi magonjwa ya kuambukiza. Hata hivyo, wanapomuuma mtu wanatokeza mwasho na baadaye sehemu hiyo inavimba, na watu wengi huathiriwa kihisia. Watu walioumwa na kunguni wanaweza kupoteza usingizi, kuaibika, na hata kufikiri kwamba kunguni amewauma muda mrefu baada ya wadudu hao kutoweka. Jarida moja nchini Sierra Leone linasema kuwa kunguni “ni wasumbufu sana na wanawakosesha watu usingizi” na linaonya kuhusu “aibu inayohusianishwa na kunguni.”
Kuwadhibiti Kunguni
Kunguni wanaweza kumsumbua mtu yeyote. Ni rahisi kuwadhibiti ukitambua mapema kwamba wapo. Kwa hiyo, jifunze kutambua ishara za kwamba wapo nyumbani na unaposafiri. Chunguza fanicha zako na vitu vingine vya mbao pamoja na mizigo, uone ikiwa kuna mayai madogo yanayofanana na mbegu ndogo nyeusi au alama za damu. Tumia tochi unapowatafuta kunguni ili uweze kuwaona.
Usiruhusu kunguni wawe na sehemu nyingi za kujificha. Ziba nyufa zote ukutani na kwenye viunzi vya milango. Ingawa kunguni hawaletwi na uchafu, itakuwa rahisi zaidi kuwatambua na kuwadhibiti ikiwa unasafisha nyumba kwa ukawaida na kupunguza vitu vilivyorundamana. Ukiwa hotelini, unaweza kupunguza uwezekano wa kubeba kunguni kwa kuepuka kuweka masanduku yako sakafuni na kitandani.
Kunguni Wanapovamia Nyumba Yako
Ukipata kunguni nyumbani au hotelini, huenda ukawa na wasiwasi au hata ukaaibika. Dave na mke wake waliumwa na kunguni walipokuwa likizoni. Dave anasema: “Tuliaibika sana. Tulijiuliza tutawaambia nini watu wa familia na marafiki tutakapofika nyumbani? Je, wakati wowote wanapojikuna au kupatwa na mwasho wa ngozi wangejiambia ni kwa sababu walitutembelea?” Hata ingawa ni kawaida kuwa na maoni kama hayo, usiache aibu ikuzuie kutafuta msaada. Wizara ya Afya ya Mwili na Akili ya New York City inatoa uhakikisho huu: “Ni vigumu, lakini inawezekana kuwaangamiza kunguni.”
Chunguza uone kama kuna kunguni kisha uchukue hatua za kuwazuia wasijifiche nyumbani kwako
Hata hivyo, usifikiri kwamba ni rahisi kuwamaliza kunguni. Kunguni wakivamia nyumba yako, unaweza kupata msaada kutoka kwa mtaalamu wa kuwadhibiti wadudu wasumbufu. Ingawa kemikali zilizotajwa awali hazitumiwi tena, wataalamu hao hutumia mbinu kadhaa zinazofaa ili kuwaangamiza kunguni. Dini M. Miller, mtaalamu wa wadudu anasema hivi pia: “Kuwadhibiti kunguni kunahitaji ushirikiano mkubwa sana kati ya wakaaji wa nyumba, wamiliki wa nyumba yenyewe, na kampuni ya kuwadhibiti wadudu wasumbufu.” Kwa kufuata mwelekezo wa mtaalamu na kuchukua tahadhari zinazohitajika, unaweza kutimiza sehemu yako na ‘kutowaacha kunguni wakuume’!
a Wataalamu wa wadudu wanasema kwamba kunguni hula damu ya wanadamu na wanyama wengine kutia ndani wanyama-vipenzi.