Sura 12
Uislamu—Njia Inayoongoza kwa Mungu kwa Unyenyekevu
[Artwork—Arabic characters]
1, 2. (a) Ni maneno gani ya kufungua ya Qurani? (b) Ni kwa nini maneno hayo ni yenye maana kwa Waislamu? (c) Hapo awali Qurani iliandikwa katika lugha gani, na “Qurani” humaanisha nini?
“KWA jina la Mwenyezi Mungu Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo.” Sentensi hii yatafsiri maandishi ya Kiarabu, juu, kutoka Qurani. Yaendelea hivi: “Shukrani zote anastahiki Mwenyezi Mungu, Mola wa walimwengu wote. Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo. Mwenye kumiliki siku ya malipo. Wewe tu ndiye tunayekuabudu, na wewe tu ndiye tunayekuomba msaada. Tuongoze njia iliyonyoka. Njia ya wale uliowaneemesha; siyo (ya wale) waliokasirikiwa; wala (ya) wale waliopotea.”—Qurani, sura 1:1-7.a
2 Maneno hayo hufanyiza Al-Fãtihah (“Utangulizi”), sura ya kwanza, au mlango, ya kitabu kitakatifu cha Kiislamu, Qurani Tukufu. Kwa kuwa zaidi ya 1 katika 6 ya idadi ya watu wa ulimwengu ni Mwislamu nao Waislamu wa kidini hurudia aya hizo mara zaidi ya moja katika kila moja ya sala zao tano za kila siku, lazima hayo yawe ni miongoni mwa maneno yanayorudiwa zaidi duniani.
3. Uislamu umeenea pote kadiri gani leo?
3 Kulingana na chanzo kimoja, kuna Waislamu zaidi ya milioni 900 katika ulimwengu, hilo likifanya Uislamu kuwa dini ya pili tu katika hesabu kwa Kanisa Roma Katoliki. Labda hiyo ndiyo dini kubwa ya ulimwengu inayokua haraka zaidi, ikiwa na chama chenye kupanuka cha Uislamu katika Afrika na ulimwengu wa Magharibi.
4. (a) “Uislamu” humaanisha nini? (b) “Mwislamu” humaanisha nini?
4 Jina Uislamu ni lenye maana kwa Mwislamu, kwani humaanisha “unyenyekeo,” “kujitoa,” au “kujikabidhi” kwa Allah, na kulingana na mwanahistoria mmoja, “hueleza nia ya ndani zaidi ya wale ambao wametii kuhubiri kwa Muhammad.” “Mwislamu” humaanisha ‘mtu anayesilimu.’
5. (a) Waislamu huamini nini juu ya Uislamu? (b) Ni ulinganifu gani uliopo kati ya Biblia na Qurani?
5 Waislamu huamini kwamba imani yao ndiyo upeo wa mafunuo (wahyi) waliyopewa Waebrania waaminifu na Wakristo wa kale. Hata hivyo, kuhusu mambo fulani mafundisho yao yaachana na yale ya Biblia, hata ingawa hutaja Maandiko ya Kiebrania na ya Kigiriki katika Qurani.b (Ona kisanduku, ukurasa 285.) Ili kuelewa imani ya Kiislamu vizuri zaidi, twahitaji kujua ni jinsi gani, wapi, na ni lini dini hii ilianzishwa.
Kuitwa kwa Muhammad
6. (a) Wakati wa Muhammad kitovu cha ibada ya Kiarabu kilikuwa nini? (b) Ni pokeo gani lililokuwapo kuhusiana na Kaaba?
6 Muhammad alizaliwa katika Makka (Kiarabu, Makkah), Saudi Arabia wapata 570 W.K. Baba yake, ‛Abd Allah, alikufa kabla ya Muhammad kuzaliwa. Mama yake, Amina, alikufa alipokuwa na miaka sita hivi. Wakati huo Waarabu walizoea namna ya ibada ya Allah ambayo kitovu chayo kilikuwa katika bonde la Makka, kwenye mahali patakatifu pa Kaaba, jengo sahili lifananalo na mchemrabasawa ambako kipande cheusi cha kimwondo kiliheshimiwa sana. Kulingana na pokeo la Kiislamu, “Kaaba hapo awali lilijengwa na Adamu kulingana na kiolezo cha kimbingu na baada ya Gharika likajengwa upya na Ibrahimu na Ishmaeli.” (History of the Arabs, cha Philip K. Hitti) Likaja kuwa mahali patakatifu pa sanamu 360, moja kwa ajili ya kila siku ya mwaka wa mwezi.
7. Ni mazoea gani ya kidini yaliyomhangaisha Muhammad?
7 Muhammad alipokua, alishuku mazoea ya kidini ya siku zake. John Noss, katika kitabu chake Man’s Religions, hutoa taarifa hii: “[Muhammad] alihangaishwa na ugomvi usiokoma kwa ajili ya masilahi yaliyodhihirishwa ya dini na heshima miongoni mwa wakuu Waquraysh [Muhammad alikuwa wa kabila hilo]. Bado kutoridhishwa kwake na masalio ya kikale ya dini ya Kiarabu kulikuwa kukubwa zaidi, ibada ya vijimungu vingi vya sanamu na kuabudu vitu vya asili, ukosefu wa adili kwenye mikusanyo na karamu za kidini, kunywa, kucheza kamari, na kucheza dansi zilizokuwa mtindo, na kuzika wakiwa hai binti wachanga wasiotakwa ambako kulizoewa si katika Makka tu bali kotekote Uarabuni.”—Sura 6:137.
8. Kuitwa kwa Muhammad awe nabii kulitukia chini ya hali gani?
8 Kuitwa kwa Muhammad awe nabii kulitukia alipokuwa na miaka 40. Yeye alikuwa na desturi ya kwenda peke yake kwenye pango la mlimani lililokuwa karibu, ambalo liliitwa Ghar Hira, ili atafakari, naye alidai kwamba ilikuwa wakati wa mojawapo pindi hizo alipopokea wito awe nabii. Pokeo la Kiislamu husimulia kwamba alipokuwa angali hapo, malaika fulani, baadaye akatambulishwa kuwa Gabrieli, alimwamuru akariri katika jina la Allah. Muhammad alikosa kuitikia, kwa hiyo malaika huyo ‘akamshika akamminya kwa nguvu hata akaona taabu.’ Ndipo malaika huyo akarudia kutoa amri hiyo. Kwa mara nyingine, Muhammad akakosa kuitikia, basi malaika huyo ‘akamsonga’ tena. Hilo lilitukia safari tatu kabla ya Muhammad kuanza kukariri yale yaliyokuja kuonwa kuwa mfululizo wa kwanza wa mafunuo ambayo yakawa Qurani. Pokeo jingine husimulia kwamba upulizio wa kimungu ulifunuliwa kwa Muhammad kama mlio wa kengele.—The Book of Revelation kutoka Sahih Al-Bukhari.
Ufunuo wa Qurani
9. Husemekana ufunuo wa kwanza wa Muhammad ulikuwa gani? (Linganisha Ufunuo 22:18, 19.)
9 Ni nini unaosemekana kuwa ulikuwa ufunuo wa kwanza kupokewa na Muhammad? Mamlaka za Kiislamu kwa ujumla hukubaliana kwamba zilikuwa ni aya tano za kwanza za sura 96, yenye kichwa Al-‘Alaq, “Pande la Damu,” ambazo husomwa hivi:
“Kwa jina la Mwenyezi Mungu, Mwenye kuneemesha neema
kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo.
Soma kwa jina la Mola wako Aliyeumba.
Amemuumba mwanaadamu kwa pande la damu.
Soma na Mola wako ni Karimu sana
Ambaye Amemfundisha (Binadamu ilimu zote hizi)
kwa wasita (msaada) wa kalamu (zilizoandika vitabu,
watu wakapata ilimu);
Amemfundisha mwanaadamu (chungu ya)
mambo aliyokuwa hayajui.”—SASA
10-12. Qurani ilihifadhiwaje?
10 Kulingana na chanzo cha Kiarabu The Book of Revelation, Muhammad alijibu, “Mimi sijui kusoma.” Kwa hiyo, akalazimika kuyatia katika kumbukumbu yake mafunuo hayo ili aweze kuyarudia na kuyakariri. Waarabu walikuwa stadi wa kutumia kumbukumbu, na ilikuwa hali moja na Muhammad. Ilichukua muda gani apokee ujumbe kamili wa Qurani? Kwa ujumla huaminiwa kwamba mafunuo hayo yalikuja wakati wa kipindi cha miaka 20 mpaka 23 hivi, kuanzia kama 610 W.K. mpaka kifo chake katika 632 W.K.
11 Vyanzo vya Kiislamu hueleza kwamba baada ya kupokea kila ufunuo, Muhammad mara moja aliukariri kwa wale waliotukia kuwa karibu. Hao nao wakautia ufunuo huo katika kumbukumbu zao na kwa kukariri wakauendeleza. Kwa kuwa utengenezaji wa karatasi haukujulikana na Waarabu, Muhammad aliandikisha mafunuo hayo kupitia kwa waandishi juu ya vifaa vya kikale vilivyopatikana wakati huo, kama vile makombe ya mikono ya ngamia, majani ya mitende, mbao, na ngozi. Hata hivyo, haikuwa mpaka baada ya kifo cha nabii huyo ndipo Qurani ikachukua umbo layo la ki-siku-hizi, chini ya uelekezo wa waandamizi na wenzi wa Muhammad. Hiyo ilikuwa wakati wa utawala wa makhalifa, au viongozi wa Kiislamu watatu wa kwanza.
12 Mtafsiri Muhammad Pickthal aandika hivi: “Sura zote za Qurani, zilikuwa zimetunzwa katika maandishi kabla ya kifo cha Nabii huyo, na Waislamu wengi walikuwa wametia Qurani yote katika kumbukumbu. Lakini sura zilizoandikwa zilitawanywa miongoni mwa watu; na wakati, katika pigano moja . . . idadi kubwa ya wale waliojua Qurani yote kwa moyo walipouawa, mkusanyo wa Qurani yote ulifanyizwa na kuandikwa.”
13. (a) Ni vipi vyanzo vitatu vya fundisho na mwongozo wa Kiislamu? (b) Wasomi fulani wa Kiislamu huonaje tafsiri ya Qurani?
13 Maisha ya Kiislamu huongozwa na mamlaka tatu—Qurani, Hadithi, na Sharia. (Ona kisanduku, ukurasa 291.) Waislamu huamini kwamba Qurani katika Kiarabu ndiyo namna ya ufunuo iliyotakata, kwa kuwa, husema, ndiyo lugha iliyotumiwa na Mungu katika kunena kupitia Gabrieli. Sura 43:3 hutoa taarifa hii: “Tumeifanya (kitabu hiki) kiwe kisomo (kilichoteremka) kwa (lugha ya) Kiarabu ili mfahamu.” Kwa hiyo, tafsiri yoyote huonwa tu kuwa kutohoa kunakohusisha kupoteza utakato. Kwa kweli, wasomi fulani Waislamu hukataa kutafsiri Qurani. Maoni yao ni kwamba “kutafsiri nyakati zote ni kusaliti,” na kwa hiyo, “daima Waislamu wamekataa na nyakati nyingine kuzuia jaribio lolote la kuitafsiri katika lugha nyingine,” atoa taarifa Dakt. J. A. Williams, mhadhiri juu ya historia ya Kiislamu.
Mpanuko wa Uislamu
14. Ni tukio gani lililofanyiza badiliko kubwa katika historia ya mapema ya Kiislamu?
14 Muhammad alianzisha imani mpya yake chini ya upinzani mkubwa. Watu wa Makka, hata wa kabila lake mwenyewe, walimkataa. Baada ya miaka 13 ya mnyanyaso na chuki, alihamisha kitovu chake cha utendaji upande wa kaskazini kule Yathribu, ambalo ndipo likajulikana kuwa al-Madīnah (Madina) jiji la nabii. Mhamo huo, au hijrah, katika 622 W.K. ulifanyiza badiliko kubwa katika historia ya Kiislamu, na tarehe hiyo ilichukuliwa baadaye kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu.c
15. Makka likawaje kitovu kikuu cha Uislamu katika kuhiji?
15 Hatimaye, Muhammad alifaulu kupata utawala wakati Makka liliposalimu amri yake katika Januari 630 W.K. (8 A.H.) naye akawa mtawala walo. Akiwa na hatamu za uongozi wa nchi na wa dini mikononi mwake, aliweza kufagilia mbali mifano ya ibada ya sanamu kutoka Kaaba na kupaimarisha kuwa makao makuu ya kuhiji Makka ambako kwaendelea mpaka wa leo.—Ona kurasa 289, 303.
16. Uislamu ulienea umbali gani?
16 Katika muda wa makumi machache ya miaka baada ya kifo cha Muhammad katika 632 W.K., Uislamu ulikuwa umeenea mbali kufikia Afghanistan na hata Tunisia katika Afrika Kaskazini. Kufikia mapema karne ya nane, imani ya Qurani ilikuwa imepenya mpaka Hispania na ilikuwa kwenye mpaka wa Ufaransa. Ni kama alivyotoa taarifa Profesa Ninian Smart katika kitabu chake Background to the Long Search: “Ikiangaliwa kwa maoni ya kibinadamu, yaliyotimizwa na nabii wa Kiarabu aliyeishi katika karne ya sita na saba baada ya Kristo yastaajabisha. Kibinadamu, ustaarabu mpya ulimiminika kutoka kwake. Lakini bila shaka kwa Mwislamu kazi hiyo ilikuwa ya kimungu na yaliyotimizwa ni ya Allah.”
Kifo cha Muhammad Chaongoza Kwenye Mgawanyiko
17. Ni tatizo gani kuu lililokabili Uislamu alipokufa Muhammad?
17 Kifo cha nabii huyo kilitokeza hali ya hatari. Yeye alikufa bila ya kuwa na uzao wowote wa kiume na bila ya mwandamizi aliyewekwa kiwazi. Ni kama anavyotoa taarifa Philip Hitti: “Basi ukhalifa [cheo cha khalifa] ndilo tatizo la kale zaidi ambalo Uislamu ulipaswa kukabili. Ungali suala lenye kuchacha. . . . Kwa maneno ya mwanahistoria Mwislamu al-Shahrastani [1086-1153]: ‘Hakujapata kuwako suala la Kiislamu lililotokeza umwagaji-damu mwingi zaidi ya lile la ukhalifa (imāmah).’” Tatizo hilo lilitatuliwaje kule nyuma katika 632 W.K.? “Abu-Bakr . . . aliteuliwa (Juni 8, 632) kuwa mwandamizi wa Muhammad kupitia uchaguzi wa namna fulani ambao katika huo viongozi waliokuwa kwenye jiji kuu, al-Madīnah, walishiriki.”—History of the Arabs.
18, 19. Ni madai gani yanayogawanya Waislamu wa Sunni na wa Shi‛ia?
18 Mwandamizi wa nabii huyo angekuwa mtawala, khalifah. Hata hivyo, suala la waandamizi wa kweli wa Muhammad likawa kisabibishi cha migawanyiko kati ya washiriki wa Islamu. Waislamu wa Sunni hukubali kanuni ya kuchaguliwa kwenye cheo badala ya uhusiano wa damu kutoka kwa nabii. Kwa hiyo wanaamini kwamba makhalifa watatu wa kwanza, Abu Bakr (baba-mkwe wa Muhammad), ‛Umar (mshauri wa nabii huyo), na ‛Uthman (mwana-mkwe wa nabii huyo), ndio waliokuwa waandamizi halali wa Muhammad.
19 Dai hilo hubishwa na Waislamu Washi‛ia, wanaosema kwamba uongozi wa kweli huja kupitia uhusiano wa damu ya nabii huyo na kupitia binamu yake na mwana-mkwe, ‛Ali ibn Abi Talib, imām wa kwanza (kiongozi na mwandamizi), aliyeoa Fatima binti mpendwa zaidi wa Muhammad. Ndoa yao ilitokeza wajukuu wa Muhammad Hasan na Husayn. Washi‛ia pia hudai “kwamba tangu mwanzo Allah na Nabii Wake walikuwa wameteua waziwazi ‛Ali kuwa mwandamizi halali pekee lakini kwamba makhalifa watatu wa kwanza walimfanyia hila ya kupoteza wadhifa uliokuwa haki yake.” (History of the Arabs) Bila shaka, Waislamu Wasunni huliona hilo kwa njia tofauti.
20. Ni nini kilichompata ‛Ali mwana-mkwe wa Muhammad?
20 Ni nini kilichompata ‛Ali? Wakati wa utawala wake akiwa khalifa wa nne (656-661 W.K.), kung’ang’ania uongozi kulitokea kati yake na liwali wa Shamu, Mu‛awiyah. Walipigana, na ndipo ili waepushe umwagaji-damu zaidi wa Kiislamu, wakaacha mzozo wao usuluhishwe kwa kuzungumza. Kukubali kwa ‛Ali suluhisho kulidhoofisha hoja yake na kumtenganisha na wafuasi wake wengi, kutia ndani Khawarij (Wajiondoaji), ambao wakawa maadui wake hatari. Katika mwaka 661 W.K., ‛Ali aliuawa kwa upanga uliotiwa sumu na mfuasi shupavu fulani Mkhariji. Vikundi hivyo viwili (Wasuni na Washi‛ia) vilikuwa vyapingana. Hapo ndipo lile tawi la Uislamu wa Sunni likachagua kiongozi kutoka kwa Waumayyad, wakuu matajiri wa Makka, wasiokuwa wa familia ya nabii huyo.
21. Ni nini maoni ya Washi‛ia juu ya waandamizi wa Muhammad?
21 Washi‛ia humwona Hasan, mzaliwa wa kwanza wa ‛Ali, mjukuu wa nabii huyo, kuwa ndiye aliyekuwa mwandamizi wa kweli. Hata hivyo, yeye alijiuzulu na kuuawa kimakusudi. Nduguye Husayn akawa imam mpya, lakini naye pia akauawa na majeshi ya Umayyad mnamo Oktoba 10, 680 W.K. Kifo chake au kufia imani, kama wanavyokiona Washi‛ia, kimeathiri sana Shī‛at ‛Alī, chama cha ‛Ali, mpaka wa leo. Wao huamini kwamba ‛Ali alikuwa mwandamizi wa kweli wa Muhammad na “imam [kiongozi] wa kwanza aliyehifadhiwa kimungu asipatwe na kosa na dhambi.” ‛Ali na waandamizi wake walionwa na Washi‛ia kuwa walimu maasumu (wasiokosea) wenye “karama ya kimungu ya kutokuwa na kasoro.” Kisehemu kikubwa zaidi cha Washi‛ia huamini kwamba kumekuwako imām wa kweli 12 tu, na wa mwisho wao, Muhammad al-Muntazar, alitoweka (878 W.K.) “katika pango la msikiti mkubwa kule Samarra bila ya kuacha mzao yeyote.” Hivyo “yeye akawa imam ‘aliyesitiriwa (mustatir)’ au ‘anayetazamiwa (muntazar).’ . . . Baadaye atatokea akiwa Mahdi (mwenye kuongozwa kimungu) ili arejeshe Uislamu wa kweli, na kushinda ulimwengu wote na kuleta mileani fupi kabla ya mwisho wa mambo yote.”—History of the Arabs.
22. Washi‛ia huadhimishaje kufia imani kwa Husayn?
22 Kila mwaka, Washi‛ia huadhimisha kufia imani kwa Imam Husayn. Huwa na andamamo ambalo katika hilo wengine hujikata wenyewe kwa visu na panga na kujitesa kwa njia nyinginezo. Katika nyakati za kisasa, habari za Waislamu Washi‛ia zimeenezwa sana kwa sababu ya ushupavu wao wa kidini kwa minajili ya Kiislamu. Hata hivyo, wao huwakilisha asilimia kama 20 tu ya Waislamu wa ulimwengu, walio wengi wakiwa ni Waislamu wa Sunni. Lakini sasa, acheni tugeukie baadhi ya mafundisho ya Uislamu tuone jinsi imani ya Kiislamu ilivyo na matokeo juu ya mwenendo wa kila siku wa Waislamu.
Mungu Ni Mkuu Zaidi, Si Yesu
23, 24. Muhammad na Waislamu walikuwa na maoni gani kuelekea Dini ya Kiyahudi na Ukristo?
23 Dini tatu kubwa za ulimwengu zinazoamini Mungu mmoja ni Dini ya Kiyahudi, Ukristo, na Uislamu. Lakini kufikia wakati aliotokea Muhammad kuelekea mwisho wa karne ya sita W.K., dini mbili za kwanza, kulingana na yeye, zilikuwa zimekengeuka kutoka kwenye njia ya ukweli. Kwa kweli, kulingana na wafafanuzi fulani wa Kiislamu, Qurani hudokeza kukataa Wayahudi na Wakristo inapotoa taarifa hii: “Siyo (ya wale) waliokasirikiwa, wala (ya) wale waliopotea.” (Sura 1:7) Hiyo ni nini?
24 Kitabu kimoja cha ufafanuzi wa Qurani chatoa taarifa hii: “Watu waliopewa Kitabu walikosea: Mayahudi kwa kuvunja Agano lao, na kusingizia uwongo Mariamu na Yesu . . . na Wakristo kumkweza Yesu aliye Mtume apate kulingana na Mungu” kupitia kwa fundisho la Utatu.—Sura 4:153-176, AYA.
25. Ni ulinganifu gani tunaopata katika Qurani na Biblia?
25 Kwa ufupi, fundisho kuu la Uislamu ni lile linalojulikana kuwa shahādah, au ungamo la imani, ambalo kila Mwislamu alijua kwa moyo: “La ilāh illa Allāh; Muḥammad rasūl Allāh” (Hakuna mungu isipokuwa Allah; Muhammad ni mjumbe wa Allah). Hilo lakubaliana na usemi wa Qurani, “Mungu wenu ni Mungu mmoja tu; hakuna anayestahiki kuabudiwa ila Yeye ambaye ni Mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na Mwenye kuneemesha neema ndogo ndogo.” (Sura 2:163) Wazo hilo lilielezwa miaka 2,000 mapema kwa mwito wa kale kwa Israeli: “Sikiza, Ee Israeli; BWANA [Yehova, NW], Mungu wetu, BWANA [Yehova, NW] ndiye mmoja. (Kumbukumbu la Torati 6:4) Yesu alirudia amri hiyo ya kwanza kabisa, ambayo imeandikwa kwenye Marko 12:29, karibu miaka 600 kabla ya Muhammad, na hakuna popote ambapo Yesu alidai kuwa Mungu wala anayelingana Naye.—Marko 13:32; Yohana 14:28; 1 Wakorintho 15:28.
26. (a) Waislamu wana maoni gani kuelekea Utatu? (b) Je! Utatu ni wa Kibiblia?
26 Kuhusu umaalumu wa Mungu, Qurani hutoa taarifa hii: “Basi mwaminini Mwenyezi Mungu na Mitume yake; wala msiseme ‘watatu . . . ’ Jizuieni (na itikadi hiyo); itakuwa bora kwenu. Bila shaka Mwenyezi Mungu ni Mungu Mmoja tu.” (Sura 4:171) Hata hivyo, twapaswa kuangalia kwamba Ukristo wa kweli haufundishi Utatu. Hilo ni fundisho lenye chanzo cha kipagani lililoanzishwa na waasi-imani wa Jumuiya ya Wakristo baada ya kifo cha Kristo na mitume wake.—Ona Sura 11.d
Nafsi, Ufufuo, Paradiso, na Moto wa Helo
27. Qurani husema nini juu ya nafsi na juu ya ufufuo? (Linganisha Mambo ya Walawi 24:17, 18; Mhubiri 9:5, 10; Yohana 5:28, 29.)
27 Uislamu hufundisha kwamba binadamu ana nafsi (roho) inayoendelea kuishi katika maisha ya baadaye. Qurani hutoa taarifa hii: “Mwenyezi Mungu hutakabadhi roho [nafsi] wakati wa mauti yao. Na zile (roho) [nafsi] zisizokufa (bado, pia Mwenyezi Mungu anazitakabadhi) katika usingizi wao. Basi huzizuia zile alizozikidhia mauti, (alizozihukumia kufa).” (Sura 39:42) Wakati uo huo, sura ya 75 yote yazungumza juu ya “Qiyāmat, au Kiama”, au “Ufufuo.” Kwa sehemu inasema hivi: “Naapa kwa siku ya Kiama . . . Anadhani mtu ya kuwa sisi hatutaikusanya mifupa yake? . . . Anauliza: (kwa shere) ‘Itakuwa lini hiyo siku ya Kiama?’ . . . Je! Hakuwa Huyo [Allah] ni Muweza wa kuhuisha wafu?”—Sura 75:1, 3, 6, 40.
28. Qurani husema nini juu ya moto wa helo? (Tofautisha na Ayubu 14:13; Yeremia 19:5; 32:35; Matendo 2:25-27; Warumi 6:7, 23.)
28 Kulingana na Qurani, nafsi yaweza kupatwa na hali tofauti-tofauti, ambazo zaweza kuwa ama bustani-paradiso ya kimbingu au adhabu ya helo ya moto. Kama ambavyo Qurani inavyotoa taarifa hii: “Wanauliza (kwa mchezo, wanasema): ‘Ni lini (kuja kwake hiyo) Siku ya Hukumu?’ Hiyo siku watakayoadhibiwa Motoni. (Waambiwe): ‘Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyokuwa mkiyahimiza.” (Sura 51:12-14) “Wanayo adhabu katika maisha ya dunia; na bila shaka adhabu ya Akhera ni ngumu zaidi wala hawatakuwa na mlinzi kwa Mwenyezi Mungu.” (Sura 13:34) Swali hili laulizwa: “Na ni jambo gani litakalokujulisha (hata ukaujua) ni nini hiyo (Hawiya)? Ni Moto uwakao kwa ukali (kweli kweli).” (Sura 101:10, 11) Tokeo hilo lenye maafa laelezwa kirefu hivi: “Hakika wale waliozikataa Aya zetu, tutawaingiza katika Moto. Kila ngozi zao zitakapowiva, tutawabadilishia ngozi nyingine badala ya zile; ili wawe wanaonja (uchungu wa) adhabu (maisha). Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu (na) Mwenye hikima.” (Sura 4:56) Usimulizi zaidi watoa taarifa hii: “Kwa hakika Jahanamu inawangoja . . . Wakae humo dahari nyingi (karne baada ya karne). Hawataonja humo baridi (wala usingizi) wala kinywaji Ila maji yachemkayo sana na usaha.”—Sura 78:21, 23-25.
29. Tofautisha mafundisho ya Kiislamu na ya Biblia juu ya nafsi na yatakayoipata?
29 Waislamu huamini kwamba nafsi ya mfu huenda Barzakh, au “Kiambaza,” “mahali au hali ambayo watu watakuwamo baada ya kifo na kabla ya Hukumu.” (Sura 23:99, 100, AYA, kielezi-chini) Nafsi ina fahamu humo ikipatwa na kinachoitwa “Kurudiwa kwa Kaburi” ikiwa mtu huyo alikuwa mwovu, au akiona furaha ikiwa alikuwa mwaminifu. Lakini waaminifu pia lazima wapatwe na mateso fulani kwa sababu ya dhambi zao chache walipokuwa wangali hai. Siku ya hukumu, kila mtu hukabili tokeo lake la milele, ambalo hukomesha hali hiyo ya katikati.e
30. Waadilifu waahidiwa nini kulingana na Qurani? (Linganisha na Isaya 65:17, 21-25; Luka 23:43; Ufunuo 21:1-5.)
30 Kinyume cha hilo, waadilifu waahidiwa bustani-paradiso za kimbingu: “Na wale walioamini na kufanya vitendo vizuri, tutawaingiza katika Mabustani yapitayo mito mbele yake kwa kukaa humo milele.” (Sura 4:57) “‘Kwa yakini watu wa Peponi leo wamo katika shughuli (zao); wamefurahi:’ Wao na wake zao wamo katika vivuli, wameegemea juu ya viti vya fahari.” (Sura 36:55, 56) “Na hakika tuliandika katika Zaburi baada ya (kuandika katika) Allawhul Mahfudh ya kwamba ardhi (hii) watairithi waja wangu walio wema.” Kielezi-chini (AYA) cha sura hii hurejeza msomaji kwenye Zaburi 25:13 na 37:11, 29, na pia katika maneno ya Yesu kwenye Mathayo 5:5. (Sura 21:105) Mrejezo kwa wake sasa watufanya tugeukie swali jingine.
Ndoa ya Mke Mmoja au Ndoa ya Wake Wengi
31. Qurani husema nini juu ya ndoa ya wake wengi? (Linganisha na 1 Wakorintho 7:2; 1 Timotheo 3:2, 12.)
31 Je! kuoa wake wengi ndiyo kawaida ya Waislamu? Ingawa Qurani yaruhusu kuoa wake wengi, Waislamu wengi wana mke mmoja tu. Kwa sababu ya wajane wengi walioachwa baada ya vita vyenye gharama kubwa, Qurani iliruhusu kuoa wake wengi: “Na kama mkiogopa kutowafanyia uadilifu mayatima (basi ogopeni vile vile kutowafanyia uadilifu wanawake). Basi oeni mnaowapenda katika wanawake, (maadamu mtawafanyia insafu) Wawili au watatu au wane (tu). Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu, basi (oeni) mmoja tu, au (wawekeni masuria) wale ambao mikono yenu ya kiume imewamiliki.” (Sura 4:3) Wasifu wa Muhammad ulioandikwa na Ibn-Hisham hutaja kwamba Muhammad alioa Khadijah, mjane mwenye mali, aliyemzidi umri kwa miaka 15. Baada ya kifo chake alioa wanawake wengi. Alipokufa yeye aliacha wajane tisa.
32. Mut‛ah ni nini?
32 Namna nyingine ya ndoa katika Uislamu huitwa mut‛ah. Huelezwa kuwa “mkataba maalumu unaofanywa kati ya mwanamume na mwanamke kupitia posa na kukubali ndoa kwa kipindi fulani na kukiwa na mahari iliyowekwa barabara kama vile mkataba wa ndoa ya kudumu.” (Islamuna, cha Mustafa al-Rafi‛i) Wasunni huiita ndoa ya anasa, na Washi‛ia, ndoa ya kukomeshwa katika kipindi barabara cha wakati. Chanzo icho hicho hutoa taarifa hii: “Watoto [wa ndoa hizo] ni halali na wana haki zile zile kama watoto wa ndoa ya kudumu.” Yaonekana namna hii ya ndoa ya muda ilizoewa katika siku ya Muhammad, na yeye aliiruhusu iendelee. Wasunni husisitiza kwamba ilikatazwa baadaye, hali Waimami, kikundi kikubwa zaidi cha Washi‛ia, huamini kwamba ingali yatumika. Kwa kweli, wengi huzoea hiyo, hasa mwanamume anapokuwa mbali na mke wake kwa kipindi kirefu cha wakati.
Uislamu na Maisha ya Kila Siku
33. Ni zipi zilizo Nguzo Tano za Mwadhimisho na za Imani?
33 Uislamu wahusisha wajibu tano za msingi na imani tano za msingi. (Ona visanduku, kurasa 296, 303.) Mojawapo wajibu hizo ni kwamba Waislamu wenye kushika dini sana hugeuka kuelekea Makka mara tano kwa siku katika kusali (salāt). Katika sabato ya Kiislamu (Ijumaa), wanaume humiminika kwenye msikiti wakasali wanaposikia mbiu yenye kuita-ita ya mwadhini kutoka kinara cha msikiti. Siku hizi misikiti mingi hupiga sahani badala ya sauti ya moja kwa moja ya mtu kupiga mbiu hiyo.
34. Msikiti ni nini, nao hutumiwaje?
34 Msikiti (Kiarabu, masjid) ndipo mahali pa ibada pa Kiislamu, palipoelezwa na Mfalme Fahd Bin Abdul Aziz wa Saudi Arabia kuwa “jiwe la pembeni la mwito kwa Mungu.” Yeye alieleza msikiti kuwa “mahali pa sala, kujifunza, utendaji wa kisheria na kihukumu, pa kuomba uelekezo, kuhubiri, pa mwongozo, elimu na matayarisho . . . . Msikiti ndio moyo wa jamii ya Kiislamu.” Sehemu hizo za ibada sasa zapatikana ulimwenguni pote. Mojawapo unaojulikana zaidi katika historia ni Mezquita (Msikiti) wa Córdoba, Hispania, ambao kwa karne nyingi ulikuwa ndio mkubwa zaidi ulimwenguni. Kisehemu chao cha kati sasa chakaliwa na kathedro ya Katoliki.
Mgongano Pamoja na, na Ndani ya Jumuiya ya Wakristo
35. Katika nyakati zilizopita, ni hali gani iliyokuwapo kati ya Uislamu na Ukatoliki?
35 Kuanza na karne ya saba, Uislamu ulisambaa kuelekea magharibi kuingia Afrika Kaskazini, kuelekea mashariki kuingia Pakistan, India, na Bangladesh, na chini kuingia Indonesia. (Ona ramani, karatasi ya mwisho mbele.) Ulipokuwa ukifanya hivyo, uliingia katika mgongano na Kanisa Katoliki la kijeshi, ambalo lilipanga Krusedi ili kutwaa tena Bara Takatifu kutoka kwa Waislamu. Katika 1492 Malkia Isabella na Mfalme Ferdinand wa Hispania walikamilisha utekaji upya wa Kikatoliki wa Hispania. Waislamu na Wayahudi walilazimika kuongoka au kufukuzwa Hispania. Uvumiliano uliokuwa umekuwapo chini ya utawala wa Uislamu katika Hispania sasa ukatoweka chini ya uvutano wa Mahakama ya Kuhukumia Wazushi ya Kidini ya Katoliki. Hata hivyo, Uislamu uliendelea na katika karne ya 20 umevuvumuka tena na kukua sana.
36. Ni matukio gani yaliyokuwa yakiendelea katika Kanisa Katoliki huku Uislamu ukipanuka?
36 Uislamu ulipokuwa ukipanuka, Kanisa Katoliki lilikuwa likipatwa na msukosuko, likijaribu kudumisha umoja kati ya washiriki walo. Lakini mavutano mawili yenye nguvu yalikuwa yakikaribia kulipuka, na yangevunja-vunja hata zaidi ile hali ya muungano ya kanisa hilo. Mavutano hayo yalikuwa ni matbaa ya kuchapa na Biblia katika lugha ya watu. Sura yetu ifuatayo itazungumza kuvunjika-vunjika zaidi kwa Jumuiya ya Wakristo chini ya mavutano hayo na mengineyo.
[Maelezo ya Chini]
a “Qurani” (ambayo maana yake ni “Kukariri”) ndio mwendelezo unaopendelewa na waandikaji Waislamu na ndio tutakaotumia humu. Inapasa kuangaliwa kwamba Kiarabu ndiyo lugha ya awali ya Qurani, na tafsiri ya Kiswahili haikubaliwi kila mahali. Katika manukuu namba ya kwanza yawakilisha sura, na ya pili namba ya aya.
b Waislamu huamini kwamba Biblia ina mafunuo ya Mungu lakini kwamba baadhi yayo yalifanywa kuwa ya bandia baadaye.
c Kwa hiyo, mwaka wa Kiislamu hupewa kuwa A.H. (Kilatini, Anno Hegirae, mwaka wa mkimbio) badala ya A.D. (Anno Domini, mwaka wa Bwana) au W.K. (Wakati wa Kawaida).
d Kwa habari zaidi juu ya Utatu na Biblia, ona broshua Je! Uamini Utatu? iliyotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1990.
e Kuhusu habari ya nafsi na moto wa helo, linganisha maandishi haya ya Biblia: Mwanzo 2:7, UV; Ezekieli 18:4, ZSB; Matendo 3:23, NW. Ona Kutoa Sababu kwa Kutumia Maandiko, kurasa 232-236; 205-212, kilichotangazwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc., 1989.
[Sanduku katika ukurasa wa 285]
Qurani na Biblia
“Amekuteremshia Kitabu kwa haki, kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake. Na aliteremsha Taurati na Injili Zamani — ziwe uwongozi kwa watu. Na akateremsha vitabu vyengine vya kupambanua baina ya haki na batili.”—Sura 3:3, 4.
“Karibu masimulizi yote ya kihistoria ya Qurani yana ulingani wayo wa kibiblia . . . Kati ya watu wa Agano la Kale, Adamu, Nuhu, Ibrahimu (wanaotajwa karibu mara sabini katika sura ishirini na tano tofauti-tofauti na jina lake likiwa kichwa cha sura 14), Ishmaeli, Lutu, Yusufu (ambaye sura ya 12 imewekwa wakfu kwake), Musa (ambaye jina lake hutokea katika sura thelathini na nne tofauti-tofauti), Sauli, Daudi, Sulemani, Eliya, Ayubu na Yona (ambaye sura ya 10 ina jina lake) ni maarufu. Hadithi ya uumbaji na kuanguka kwa Adamu yatajwa mara tano, furiko mara nane na Sodoma mara nane. Kwa kweli Qurani huonyesha ulinganifu zaidi na Pentateuki zaidi ya sehemu nyingine yoyote ya Biblia. . . .
“Miongoni mwa watu wa Agano Jipya Zekaria, Yohana Mbatizaji, Yesu (‛Īsa) na Mariamu ndio pekee wanaokaziwa. . . .
“Uchunguzi wa kulinganisha wa . . . masimulizi ya qikurani na kibiblia . . . hufunua hakuna utegemeano wowote wa kimaneno ya kinywa [hakuna manukuu ya moja kwa moja].”—History of the Arabs.
[Sanduku katika ukurasa wa 291]
Vyanzo Vitatu vya Fundisho na Mwongozo
Qurani Tukufu, inayosemekana alifunuliwa Muhammad na malaika Gabrieli. Maana na maneno ya Qurani katika Kiarabu huonwa kuwa yamepuliziwa na Mungu.
Hadithi, au Sunnah, “vitendo, semi na kibali cha kimya (taqrīr) cha Nabii . . . viliwekwa wakati wa karne ya pili [A.H.] kwa namna ya hadithi zilizoandikwa. Kwa hiyo, hadithi ni maandishi ya kitendo au semi za Nabii.” Yaweza pia kutumiwa kuhusu vitendo au semi za yeyote wa “Wenzi [wa Muhammad] au Waandamizi wao.” Katika hadithi, ni maana tu inayoonwa kuwa imepuliziwa na Mungu.—History of the Arabs.
Sharia, au sheria ya kidini, yenye kutegemea kanuni za Qurani, huongoza maisha yote ya Mwislamu katika mambo ya kidini, kisiasa, na kijamii. “Vitendo vyote vya binadamu vyaainishwa chini ya vifungu vitano halali: (1) kinachoonwa kuwa wajibu kamili (fard) [kuhusisha thawabu kwa ajili ya kutenda au adhabu kwa ajili ya kukosa kutenda]; (2) vitendo vya kusifiwa au vyenye ustahili (mustahabb) [kuhusisha thawabu lakini hamna adhabu kwa kukosa kufanya]; (3) vitendo vinavyoruhusika (jā‛iz, mubāh), ambavyo kihalali havidhuru; (4) vitendo vya makuruhu (makrũh), ambavyo havikubaliki lakini si vya kuadhibika; (5) vitendo haramu (harām), ambavyo kuvifanya kwataka adhabu.”—History of the Arabs.
[Sanduku katika ukurasa wa 296]
Nguzo Tano za Imani
1. Imani katika Mungu mmoja, Allah (Sura 23:116, 117)
2. Imani katika malaika (Sura 2:177)
3. Imani katika manabii wengi lakini ujumbe mmoja. Adamu alikuwa nabii wa kwanza. Wengine wamekuwa ni kutia na Ibrahimu, Musa, Yesu, na “Muhuri wa Manabii,” Muhammad (Sura 4:136; 33:40)
4. Imani katika siku ya hukumu (Sura 15:35, 36)
5. Imani katika ujuaji yote wa Mungu, maarifa ya kimbele, na uamuo wa matukio yote. Hata hivyo, binadamu ana uhuru wa kuchagua katika vitendo vyake. [Faraka za Kiislamu zimegawanyika juu ya suala hilo la hiari] (Sura 9:51)
[Sanduku katika ukurasa wa 303]
Nguzo Tano za Mwadhimisho
1. Rudia kanuni ya imani (shahādah): “Hakuna mungu ila Allah; Muhammad ni mjumbe wa Allah” (Sura 33:40)
2. Sala (s̩alāt) kuelekea Makka mara tano kwa siku (Sura 2:144)
3. Zaka (zakāh), daraka la kutoa asilimia fulani ya mapato ya mtu na thamani ya mali fulani (Sura 24:56)
4. Kufunga (s̩awm), hasa wakati wa sherehe ya mwezi mzima ya Ramadhani (Sura 2:183-185)
5. Kuhiji (ḥajj). Mara moja maishani, kila Mwislamu wa kiume lazima afunge safari ya kwenda Makka. Maradhi na umaskini tu ndivyo udhuru halali (Sura 3:97)
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 304, 305]
Imani ya Baha‛i—Kutafuta Umoja wa Ulimwengu
1 Imani ya Baha‛i si faraka la Uislamu bali imetokana na dini ya Babi, kikundi kimoja katika Uajemi (leo Iran) kilichojitenga na tawi la Shi‛ia la Uislamu katika 1844. Kiongozi wa Wababi alikuwa Mirza ‛Ali Mohammad wa Shiraz, aliyejitangaza mwenyewe kuwa Bab (“Lango”) na imām-mahdī (“kiongozi mwenye kuongozwa ifaavyo”) kutoka nasaba ya Muhammad. Alinyongwa na mamlaka ya Uajemi katika 1850. Katika 1863 Mirza Hoseyn Ali Nuri, mshiriki mashuhuri wa kikundi cha Babi, “alijijulisha rasmi mwenyewe kuwa ‘Yeye ambaye Mungu atadhihirisha,’ ambaye Bab alikuwa ametabiri.” Pia alitwaa jina Baha’ Ullah (“Utukufu wa Mungu”) akaunda dini mpya, imani ya Baha’i.
2 Baha’ Ullah alipelekwa uhamishoni kutoka Uajemi na hatimaye akafungwa gerezani katika Acco (leo Acre, Israel). Huko aliandika maandishi yake makuu, al-Kitāb al-Aqdas (Kitabu Kilicho Kitakatifu Zaidi), akasitawisha fundisho la imani ya Baha’i kuwa fundisho lenye mambo mengi. Baha’ Ullah alipokufa, uongozi wa dini yake changa ulienda kwa ‛Abd ol-Baha’ mwana wake, kisha kwa Shoghi Effendi Rabbani, kilembwe chake, na katika 1963 kwa baraza teule la usimamizi lijulikanalo kuwa Nyumba ya Haki Katika Ulimwengu Wote Mzima.
3 Wabaha’i huamini kwamba Mungu amejifunua mwenyewe kwa binadamu kupitia “Madhihirisho ya Kimungu,” kutia Ibrahimu, Musa, Krishna, Zoroasta, Buddha, Yesu, Muhammad, Bab, na Baha’ Ullah. Huamini kwamba wajumbe hao walitokezwa ili waongoze ainabinadamu kupitia hatua ya mageuzi ambayo katika hiyo kutokea kwa Bab kulianzisha muhula mpya kwa ainabinadamu. Wabaha’i husema kwamba mpaka wa leo ujumbe wake ndio ufunuo kamili zaidi wa mapenzi ya Mungu na kwamba ndicho chombo kikuu kilichotolewa na Mungu kitakachofanya umoja wa ulimwengu uwezekane.—1 Timotheo 2:5, 6.
4 Mojawapo maagizo ya msingi ya Wabaha’i ni “kwamba dini zote kubwa za ulimwengu zina chanzo cha kimungu, kwamba kanuni zazo za msingi zapatana kabisa.” Hizo “zatofautiana tu katika sehemu zisizo za muhimu za mafundisho yazo.”—2 Wakorintho 6:14-18; 1 Yohana 5:19, 20.
5 Imani za Kibaha’i ni kutia ndani umoja wa Mungu, kutoweza kufa kwa nafsi, na mageuzi (kibayolojia, kiroho, na kijamii) ya ainabinadamu. Kwa upande mwingine, hukataa wazo la walio wengi la malaika. Pia hukataa Utatu, fundisho la kuzaliwa upya katika umbo jingine la Uhindu, na kuanguka kwa binadamu kutoka ukamilifu na ukombozi uliofuata kupitia damu ya Yesu Kristo.—Warumi 5:12; Mathayo 20:28.
6 Udugu wa binadamu na usawa wa wanawake ni sehemu kubwa za imani ya Kibaha’i. W97abaha’i huzoea ndoa ya mke mmoja. Angalau mara moja kwa siku, husali mojawapo sala tatu zilizofunuliwa na Baha’ Ullah. Huzoea kufunga tangu kuchomoza kwa jua mpaka kushuka kwa jua wakati wa siku 19 za mwezi ‛Ala wa Kibaha’i, ambao huwa katika Machi. (Kalenda ya Kibaha’i ina miezi 19, kila mmoja ukiwa na siku 19, kukiwako siku kadhaa za mpenyezo.)
7 Imani ya Kibaha’i haina desturi nyingi za kisherehe zilizowekwa, wala haina makasisi. Wowote wanaodai imani katika Baha’ Ullah na kukubali mafundisho yake waweza kuandikishwa kuwa washiriki. Wao hukutana kwa ajili ya ibada wakati wa siku ya kwanza ya kila mwezi wa Kibaha’i.
8 Wabaha’i hujiona wenyewe kuwa na utume wa kushinda kiroho sayari. Hujaribu kueneza imani yao kupitia maongezi, kielelezo, ushiriki katika kazi za jumuiya, na kampeni za kueneza habari. Wao huamini utii kamili wa sheria za nchi ambamo wanaishi, na ingawa wao hupiga kura, hujiepusha kushiriki katika siasa. Wao hupendelea kazi isiyo ya kupigana katika majeshi yenye kutumia silaha inapowezekana lakini wao hawakatai kwa kidhamiri.
9 Ukiwa ni dini ya umisionari, Ubaha’i umepata ukuzi wa haraka wakati wa miaka michache iliyopita. Wabaha’i hukadiria kwamba kuna waumini karibu 5,000,000 ulimwenguni pote, ingawa hesabu kamili ya watu wazima waliojiandikisha katika imani hiyo kwa wakati huu ni juu kidogo ya 2,300,000.
1, 2. Imani ya Kibaha’i ilianzishwaje?
3-7. (a) Ni nini baadhi za imani za Kibaha’i? (b) Imani za Kibaha’i zatofautianaje na mafundisho ya Biblia?
8, 9. Utume wa Kibaha’i ni nini?
[Picha]
Kihekalu cha Kibaha’i kwenye makao makuu ya ulimwengu katika Haifa, Israel
[Picha katika ukurasa wa 286]
Pokeo la Uislamu husema kwamba Muhammad alipaa mbinguni kutoka mwamba huu katika Kuba la Mwamba, Yerusalemu
[Picha katika ukurasa wa 289]
Wahiji Waislamu kule Makka hutembea mara saba kuzunguka Kaaba na kugusa au kubusu Jiwe Jeusi, kushoto chini
[Picha katika ukurasa wa 290]
Kiarabu ndicho lugha inayotakwa kwa ajili ya kusoma Qurani
[Picha katika ukurasa wa 298]
Kisaa kushoto juu:Kuba la Mwamba, Yerusalemu; misikiti katika Iran, Afrika Kusini, na Uturuki
[Picha katika ukurasa wa 303]
Mezquita wa Córdoba wakati mmoja ulikuwa msikiti mkubwa zaidi katika ulimwengu (kathedro ya Katoliki sasa hukalia katikati)