Kumwacha Mungu Awe Mwenye Enzi Kuu wa Maisha Zetu
“Enzi kuu ya ulimwengu imepelekwa kwa Bwana wetu na Kristo wake, naye atatawala milele na milele.”—Ufu. 11:15, An American Translation.
1, 2. Je! ni jambo la maana kweli kujua aliye mwenye enzi kuu wa maisha zetu, na twawezaje kutoa mfano wa jambo hili?
JE! NI jambo la maana sana kujua aliye mwenye enzi kuu wa maisha zetu? Ndiyo! Bila shaka katika nchi yo yote ambamo mtawala ana mamlaka kamili, ni jambo la maana kujua bila kujali kama watu wana mwenye enzi kuu mzuri au mwenye enzi kuu mbaya.
2 Kwa jina hili “mwenye enzi kuu” anamaanishwa mfalme au mtawala wa kisiasa aliye na mamlaka kuu kuliko zote na mwenye cheo kikuu zaidi na uwezo mkuu zaidi wa kutoa amri kuliko wengine wote katika nchi. Mfalme au mtawala huyo anazo nguvu zote. Utawala wake wahusu maisha za raia zake wote, kwamba ni kwa mema au kwa mabaya. Mfalme mwenye hekima wa nyakati za kale alieleza shauri hili katika njia hii: “Wenye haki wakiwa na amri, watu hufurahi; bali mwovu atawalapo, watu huugua.”—Mit. 29:2.
3. Ni majeshi gani mawili yenye nguvu kuu mno leo yanayojaribu kutawala nafsi za watu wote duniani?
3 Leo nyakati ni zenye hatari sana. Hatuwezi kuliepa ulizo juu ya mwenye enzi kuu wa maisha zetu. Kwa juujuu, yaonekana kama majeshi makuu mawili ya kisiasa yanashindana vikali kwa ajili ya utawala, enzi kuu, juu ya maisha za watu wote wa dunia. Hata mataifa yale yanayojidai kuwa yasiyochukua upande wo wote katika siasa yanalazimishwa kuweka ulinzi wenye nguvu yasije yakashambuliwa na kushindwa na moja au mengine ya majeshi haya ya kisiasa yenye nguvu kuu mno. Miungano ya mataifa inajipanga kila upande bila kulegea washindanie kutawala nafsi za wanadamu. Upande mwingine ni wa kutawala kwa sharti, kuamuru kabisa watu katika mambo yao ya faragha na ya hadhara. Hata dini inaweza kutawaliwa na kuamriwa na wanasiasa, jambo hilo likiruhusiwa. Upande mwingine waruhusu kuwe na uhuru wa kadiri katika maisha za kipekee na shughuli za raia. Hata hivyo unadai kutawala kabisa maisha za watu wakati faida za utawala wa kisiasa zinapokaribia sana hatari na kuhitaji zilindwe juu ya shambulio kali.
4. Ni shindano gani linalokaribia upeo sasa ambalo ni kubwa zaidi kuliko lile lililo kati ya ukomunisti na demokrasi?
4 Walakini, kuna shindano ambalo ni kubwa mno kuliko shindano la kisiasa lililotangulia kutajwa, la kutawala maisha za wanadamu wote. Shindano kati ya ukomunisti wa mataifa yote na ubepari (utawala wa rasilmali) ni lenye kuenea dunia yote. Shindano lililo kubwa zaidi lahusu ulimwengu mzima (universe). Ni kati ya nguvu kuu mbili za adili, moja ni kwa ajili ya mema na nyingine kwa ajili ya mabaya. Shindano hili limekuwa likiendelea sasa kwa muda wa karibu miaka elfu sita ya historia ya kibinadamu. Karibuni litafikia upeo. Nguvu mbili zinazoshindana ni za watu wenye akili. Hivyo si nguvu mbili zisizo na akili, kama vile nguvu za sumaku au uvutano, zinazotenda kwa mema na kwa mabaya bila tabia ya utu, bila uongozi wenye akili unaoziendesha. Kwa hiyo, ubaya uko kwa sababu watu hufanya mabaya, nao wema uko kwa sababu watu hufanya mema. Kuna chanzo cha kiutu kwa utendaji wa mema. Vilevile, kuna chanzo cha kiutu kwa utendaji wa mabaya. Sheria njema hutokana na Mtu mwema; sheria mbaya hutokana na Mtu mbaya.
5. Nguvu mbili hizi zinalinganishwa na nini, na kwa sababu gani?
5 Nguvu mbili zenye kushindana zinalinganishwa na nuru na giza. Nguvu ya mema hulinganishwa na nuru, kwa kuwa matendo ya wema hufanywa katika nuru, mtendaji wayo asione haya wala kuogopa. Nguvu ya mabaya yalinganishwa na giza, kwa vile matendo ya ubaya hufanywa katika giza, mtendaji wayo akijua kwamba anatenda kosa bila kutaka kuadhibiwa. Anapotenda matendo mabaya yanayofanywa katika giza ili kuepuka kuonwa, mtendaji wayo huchukia nuru pamoja na nguvu yake ya kufunua mambo wazi. Ni kama alivyosema mwandikaji ambaye maneno yake husomwa na kutumiwa mahali pote: “Watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi.”— Yohana 3:19-21.
6. Matendo yanayohusiana na giza na yale yanayohusiana na nuru yanatofautishwaje katika Warumi 13:12-14?
6 Akionyesha zaidi tofauti kati ya yale yanayohusiana na nuru, mwandikaji mwingine mashuhuri wa karne ya kwanza W.K. aliwaambia watu waliopenda kutenda mema hivi: “Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia; basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru. Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. . . . msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake.”—Rum. 13:12-14.
7. (a) Ni mamlaka gani iliyoshinda usiku wa kusalitiwa kwa Yesu? (b) Ni nani aliyekuwa anapendezwa zaidi kusababisha uhalifu uliotokea siku ya Kupitwa ya mwaka wa 33 W.K.?
7 Mwanzishi wa Ukristo aliposalitiwa na mmoja wa mitume wake mwenyewe kumi na wawili, mhaini Yuda Iskariote, aliliambia hivi kundi la watu wenye silaha waliokuja usiku wamkamate kwa siri: “Hii ndiyo saa yenu, na mamlaka ya giza.” (Luka 22:53) Mamlaka hiyo ya giza ilishinda usiku huo wenye msiba, lakini wajumbe wa kibinadamu ndio waliotumika kuyatimiza matendo ya giza yaliyofanya uhalifu ulio mkubwa kuliko uhalifu wote katika historia ya kibinadamu utendwe alasiri iliyofuata, siku ya Kupitwa ya mwaka wa 33 W.K. Tena, alikuwako mtu fulani aliye juu zaidi na mwenye nguvu zaidi aliyependezwa zaidi kufanya uhalifu huo kuliko walivyokuwa wahalifu wa kibinadamu. Alikuwako mtu mwenye akili asiyeonekana aliye juu zaidi aliyekuwa akiwaongoza wafanye uhalifu huu. Mtu huyo mwenye kupita uwezo wa kibinadamu ndiye aliyetumia kwa faida yake nafasi iliyopatikana akatia katika moyo wa Yuda Iskariote wazo baya la kumsaliti Bwana wake asiye na hatia. Habari yasema hivi kwa maneno hakika: “Shetani akamwingia Yuda, aitwaye Iskariote, naye ni mmoja wa wale [mitume] Thenashara. Akaondoka, akaenda akasema na wakuu wa makuhani na majemadari, jinsi atakavyoweza kumtia mikononi mwao.” (Luka 22:3, 4) Katika chakula cha jioni cha Kupitwa, wakati Yesu Kristo alipoonyesha ambaye angekuwa msaliti wake kumpa tonge la chakula, kama habari inavyotuambia, “baada ya hilo tonge Shetani alimwingia. . . . Basi huyo, akiisha kulipokea lile tonge, akatoka mara hiyo. Nako kulikuwa ni usiku.”—Yohana 13:27-30.
8. Yesu alionyeshaje aliyekuwa mwanzishi wa uhalifu huo je! huyo alishinda?
8 Baada ya haya, wakati Yesu alipokuwa peke yake pamoja na mitume waaminifu kumi na mmoja, alionyesha hasa aliye mwanzishi wa uhalifu wote uliokuwa ukitendeka, kwa kuwaambia hivi: “Tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano.” (Luka 22:31) Kwa sababu hiyo, mitume kumi na mmoja hawa walitawanyika kwa muda kama ngano zilizopepetwa, hata kumwacha Yesu Kiongozi wao. Lakini Shetani Ibilisi hakushinda, maana mitume hawa walikutana tena wakafanya kazi pamoja kama kikundi chenye umoja chini ya ukichwa wa Kiongozi wao aliyefufuliwa. Hata mtume Simoni Petro, aliyemkana Yesu mara tatu usiku huo wa Kupitwa, alikuwa katika kikundi hicho.—Luka 22:47-62; Mt. 26:31, 35; Marko 14:50-52.
MWENYE ENZI KUU MWOVU
9. Yesu alionyeshaje kwamba kulikuwa na mtu mwenye akili aliye na uwezo kupita wa kibinadamu aliyefanya Wayahudi wakusudie kumwua?
9 Hakuna shaka! Wakati huo katika karne ya Wakati wetu wa Kawaida alikuwako mtu mwenye akili aliye na uwezo kupita wa kibinadamu aliyekuwa haonekani kwa macho ya kibinadamu aliyefaulu kuongoza matendo ya wajumbe wake wa kibinadamu wafanye matendo ya giza la kiadili. Huyo alikuwa Shetani Ibilisi. Kwani, hata Yesu Kristo aliwaambia wananchi wenzake waliokuwa wakitumiwa na mwovu huyo hivi: “Kama mngekuwa watoto wa Ibrahimu, mngezitenda kazi zake Ibrahimu. Lakini sasa mnatafuta kuniua mimi. . . . Ibrahimu hakufanya hivyo. Ninyi mnazitenda kazi za baba yenu. . . . Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo” uongo.—Yohana 8:39-44.
10. Yesu alisema nini juu ya “ibada” ya upuzi kwa Mungu, lakini ni kanuni gani inayotumika hapa?
10 Mpaka leo hii Wayahudi wa asili, waliotahiriwa wanapatwa na matokeo yenye kuhuzunisha kutokana na matendo ya giza yaliyofanywa katika taifa lao miaka mia kumi na tisa iliyopita. Hii yaonyesha yanayoweza kulipata taifa zima linalokuja chini ya uongozi wa Shetani Ibilisi, mtu mwenye akili yule asiyeonekana mwenye kupita uwezo wa kibinadamu. Yesu Kristo alimwita Mwovu huyu “mkuu wa ulimwengu huu,” nalo taifa la Yesu mwenyewe lilimtii huyo kama “mkuu” wao, mwenye enzi kuu wao, badala ya kumtii Mungu ambaye walidai kumwabudu katika hekalu la Yerusalemu. Yesu Kristo aliwaambia mitume wake waaminifu hivi: “Saa yaja atakopodhania kila mtu awauaye ya kuwa anamtolea Mungu ibada.” (Yohana 12:31; 16:2) Lakini si hivyo! Mwanadini aliyepotezwa anayefanya uovu huo kwa hakika anamtumikia Shetani Ibilisi, Adui ya Mungu. Kanuni inayotumika hapa yaelezwa kwa usahihi katika maneno haya: “Kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii.”—Rum. 6:16.
11. Paulo aliandika nini juu ya kushindana mweleka kwa Wakristo, akituonya juu ya kuwako kwa watawala wengine waovu zaidi ya wale walio na mwili na damu?
11 Leo ni wakati unaowapasa watu wajue kwamba wako watawala wengine wa ulimwengu zaidi ya wale wanaoonekana wenye damu na mwili duniani. Akituonya juu ya hilo, mtume Paulo, aliyeteswa na wale waliodhani kwamba walikuwa wakimtolea Mungu ibada, aliwaambia waamini wenzake katika mji wa kipagani wa Efeso, Asia Ndogo: “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme [Enzi, Jerusalem Bible] na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili [Nguvu zinazoanzisha giza katika ulimwengu huu, Je], juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho [Jeshi la kiroho la uovu katika mbingu, Je].”—Efe. 6:11, 12.
12. “Roho wakuu wa ulimwengu huu wenye giza” wako chini ya nani, na kuwa kwetu katika ulimwengu huu kunatufanya tujiulize ulizo gani?
12 Ni nani leo, katika nusu ya mwisho ya karne hii ya 20, atakayepinga kwamba giza hilo la kiadili—yaani, kazi na matendo ya aina mbaya—halitawali dunia? Ijapokuwa watu wengi wenye hekima ya ulimwengu, wasadikio vitu vinavyoonekana tu wakane, uhakika wadumu, na kuna ushuhuda wa kuonyesha, kwamba wako “wakuu wa giza hili,” au, kama An American Translation inavyotafsiri andiko hili la Biblia ya Kigiriki, “roho wakuu wa ulimwengu huu wenye giza.” Lote hili “jeshi la kiroho la uovu katika mbingu” zisizoonekana liko chini ya enzi kuu ya Shetani Ibilisi, ‘“yule mwovu.” (Efe. 6:16; Mt. 13:19) Sote na tuufikie uhakika bila kuepa. Humaanisha jambo fulani la kipekee sana kwetu. Ni jambo gani? Basi, sisi sote bila kuepa tumo “ulimwenguni.” (Yohana 17:11) Hivyo tunapata matokeo ya nyakati zote zenye taabu ambazo katika hizo ulimwengu wa wanadamu umekuwa ukipita, hasa tangu mwaka wa 1914, na hili latufahamisha hali mbaya tulimo. Hivyo, ulizo ambalo hakuna mtu wa kwetu aweza kuliepa ni hili: Kwa kuwa Shetani Ibilisi ndiye “mkuu wa ulimwengu huu” tulimo—je! kwa sababu hiyo yeye ndiye mwenye enzi kuu wa maisha zetu?
13. Bado ulimwengu uko wapi kuhusiana na yule mwovu, na kwa hiyo inafaa tujiulize maulizo gani?
13 Ulizo hili la kipekee lastahili tulifikirie kwa uzito na kwa unyofu. Hali ya mambo ya ulimwengu leo haikubadilika kuliko ilivyokuwa karne kumi na tisa zilizopita wakati mwandikaji wa mwisho wa Biblia aliposema: “Ulimwengu mzima uko katika nguvu ya yule mwovu.” (1 Yohana 5:19, NW) Hivyo twaweza kujiuliza mmoja mmoja, Je! ni kutia na mimi? Je! mimi pia niko katika nguvu ya Ibilisi, yule mwovu, mwenye enzi kuu wa ulimwengu huu? Haitabadili mambo yetu kuchukizwa na ulizo hilo na kusema, ‘Ulizo hilo ni lenye kuchukiza mno nisiweze kulifikiria, hasa, ni lenye matusi mno nisiweze kuliangalia, kwa heshima yangu mwenyewe.’ Bila shaka hatutaki tujipumbaze wenyewe, sivyo? Hata hivyo twaweza kufanya hivyo. Mwandikaji wa Biblia alikuwa akitabiri matukio ya wakati wetu wenyewe aliposimulia kushushwa kwa yule Mwovu na majeshi yake ya kiroho, akisema:
14, 15. Ibilisi anadanganya nani, na mara ya kwanza atakapozuiwa asifanye hivyo ni lini?
14 “Yule joka akatupwa, yule mkubwa, nyoka wa zamani, aitwaye Ibilisi na Shetani, audanganyaye ulimwengu wote; akatupwa hata nchi, na malaika zake wakatupwa pamoja naye. Nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema, . . . Ole wa nchi na bahari! kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.”—Ufu. 12:9-12.
15 Mdanganyifu Mkubwa huyo hapendezwi na ye yote duniani. Bado yuko huru katika ujirani wa dunia yetu ambako ametupwa. Hatazuiwa asiudanganye ulimwengu wote mpaka baada ya “vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi” penye Har–Magedoni inayoendelea kukaribia. Ndipo, kwanza, yeye pamoja na malaika zake wa kishetani ‘atakapotupwa katika kuzimu, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu ya kutawala kwa Yesu Kristo itimie.’ (Ufu. 16:14, 16; 20:1-3) Wakati huo wa kumwondoa Shetani Ibilisi na mashetani wake kutoka ujirani wa dunia yetu na kuwatenga katika shimo refu sana haujaja, na mambo jinsi yalivyo duniani leo huonyesha kwamba haujaja. Hivyo, kila mtu bado anaweza kudanganywa na mwenye enzi kuu wa Kiibilisi wa ulimwengu huu. Ikiwa kwa kujitumaini twadai kwamba hatudanganywi na yeye ambaye ulimwengu mzima uko katika nguvu yake, basi je! twajikuta tukifaulu tunaposhindana mweleka na majeshi ya uovu yenye kupita uwezo wa kibinadamu? Ama tunadanganywa ama tunashindana mweleka; ni jambo mojawapo.
16. Tukijifanya sehemu ya ulimwengu huu tutakuwa hatushindani mweleka na nani, na kwa sababu gani jitihada za kuutengeneza ulimwengu hazitafaulu?
16 Basi, waacheni wote wale wanaosisitiza sana kwamba Shetani Ibilisi siye mwenye enzi kuu wa maisha zao wajiulize kwa unyofu, Je! mimi ninashinda ninapopigana mweleka na “falme” katika tengenezo lisiloonekana lenye kupita uwezo wa kibinadamu la Ibilisi, na mamlaka zilizomo, na “watawala wa ulimwengu wa giza hili,” na “majeshi ya roho yenye uovu katika mahali pa kimbinguni”? (Efe. 6:12, The Bible in Living English’, New World Translation) Ulimwengu wa wanadamu unaodanganywa haufanyi hivyo, nasi tukijifanya sehemu ya ulimwengu huu, basi hata sisi hatushindi, hata tuwe tunajaribuje kuutengeneza ulimwengu huu kisiasa, kidini, kijamii, kimwili. Kwa kujaribu kulifanya tengenezo lionekanalo la Ibilisi kuwa zuri zaidi duniani watu wanajaribu kuliendeleza zaidi na kulifanya liwe lenye kuvutia zaidi na lenye kuvumilika tu. Jitihada hizo za kutengeneza hazitaleta kamwe mileani ya amani, ufanisi na furaha kwa wanadamu wote. Ulimwengu au jamii hii ya wanadamu chini ya mpango wake wa sasa haikukusudiwa itengenezwe katika dunia yote. Imekusudiwa uharibifu, na “mkuu wa ulimwengu huu” hawezi kuzuia hili!
KUAMUA JUU YA ALIYE MWENYE ENZI KUU WETU
17, 18. Ikiwa Ibilisi siye mwenye enzi kuu wetu, ni nani anayebaki kuwa ndiye, naye asema nini juu ya kuwako kwake?
17 Kwa sababu hatuwezi kutoka katika ulimwengu huu bali lazima tuwe ndani yake, je! tutamwacha Shetani Ibilisi, chanzo cha uovu, awe mwenye enzi kuu wa maisha zetu? Ikiwa hatutaki hili litukie, basi tunabaki na nani wa kuchagua kama mwenye enzi kuu wa maisha zetu? Ni Yeye ambaye Shetani Ibilisi ni Adui yake mkuu. Huyu ndiye Mungu wa kweli aliye hai. (Yer. 10:10) Ndiye Biblia Takatifu husema jina lake ni Yehova. (Zab. 83:18) Yeye si kanuni ya kuwazika, roho yenye umajimaji, isiyo mtu, isiyo na umbo inayoenea ulimwengu wote na vitu vyote vigusikavyo vilivyomo tu. Yeye ni mtu, kama Shetani Ibilisi alivyo mtu. Hutumia usemi juu yake unaoonyesha kwamba ana mwili, umbo lakini ambalo hatuwezi kuwazia. Tofauti na Shetani Ibilisi, ambaye ni mungu wa kujifanya, Yehova ndiye Mungu wa kwanza, Mungu asiyeumbwa na viumbe vilivyoko, Mungu aliyekuwa peke yake kabla ya viumbe vyote. Kwa kujitofautisha na miungu ya mataifa inayofanywa na wanadamu, kwa kufaa anasema hivi juu yake mwenyewe:
18 “Kabla yangu hakuumbwa Mungu awaye yote, wala baada yangu mimi hatakuwapo mwingine. Mimi, naam, mimi, ni [Yehova], zaidi yangu mimi hapana mwokozi.”—Isa. 43:10, 11.
19, 20. Kwa sababu gani Yehova Mungu ndiye Chanzo cha kila kitu chema, Naye alimwumba mwanadamu wa kwanza kwa mfano wa nani?
19 Yeye ndiye Mtu mwenye akili aliye chanzo cha kila kitu chema. Ni kwa sababu Yeye mwenyewe ni mwema kabisa. Yeye Ndiye aliyeumba dunia yetu na mbingu na vitu vyote vilivyomo. Ndiye aliyemweka mwanadamu duniani, akimfanya awe kama Yeye ambaye ni mwema kabisa. Kitabu cha kwanza cha Biblia Takatifu chatuambia hivi: “Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. , . .
20 “Mungu akaona kila kitu alichokifanya, na tazama, ni chema sana. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya sita.”—Mwa. 1:27-31.
21. Mungu aliacha uumbaji ukiwa katika hali gani, naye hakufikiria kuumba nini?
21 Mungu alipoona kwamba kila kitu alichokuwa ameumba kilikuwa “chema sana,” alikiacha kiendelee kuwa chema akapumzika kwa kazi zake za uumbaji wa dunia yetu na mwanadamu juu yake. Yeye hakusema hivi: ‘Kwa kila kitu lazima kuweko kinyume chake, kibaya. Basi yanipasa niumbe kilicho kibaya. Mimi ni Mungu mwema, basi yanipasa niumbe kinyume changu, mungu mwovu. Yanipasa niweke kanuni yenye uovu itende. Yanipasa niwape wanadamu nia ya kufanya mabaya.’
22. Ni mfano gani wa mitume unaotolewa kuonyesha kwamba Mungu hawezi kuwa chanzo cha mema na chanzo cha mabaya ya adili?
22 La! Mungu hakuwazia filosofia hiyo mbaya. Hangeweza kuwa chanzo cha mema na chanzo cha mabaya, kama vile chemchemi isivyoweza kuwa chanzo cha maji matamu na chanzo cha maji ya chumvi wakati ule ule. (Yak. 3:12) Hawezi kuwa nuru na giza wakati ule ule. Mtume Paulo aliuliza ulizo lenye kuhusu sana hivi: “Pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?” (2 Kor. 6:14) Kuonyesha mfano jinsi Mungu wa kweli alivyo mwenye kutakata, mwangavu, safi na mwenye kutoa nuru, mtume Yohana aliandika hivi: “Mungu ni nuru, wala giza lo lote hamna ndani yake. Tukisema ya kwamba twashirikiana naye, tena tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatuifanyi iliyo kweli; bali tukienenda nuruni, kama yeye alivyo katika nuru, twashirikiana sisi kwa sisi.”—1 Yohana 1:5-7.
23, 24. (a) Ni kwa njia gani Mungu ndiye “Baba wa mianga” ya kimbinguni? (b) Kama vile katika siku ya kwanza ya uumbaji, ni kwa njia gani Mungu alifanya nuru ya kiroho iangaze siku za mitume?
23 Yehova ndiye Mungu atoaye mwangaza kwa faida ya viumbe vyake, kwamba ni mbinguni au duniani. Jinsi amri yake ilivyokuwa ya maana siku ya kwanza ya juma ya uumbaji wa Mungu: “Iwe nuru”! Kwa sababu aliumba vitu vyenye kutoa nuru katika mbingu vitoe nuru kwa viumbe duniani, ameitwa “Baba wa mianga” ya kimbinguni. Nuru ya asili ya mchana ni mojawapo la mambo mema kutoka kwake, kama ilivyoandikwa: “Kila kutoa kuliko kwema, na kila kitolewacho kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kwa Baba wa mianga; kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeuka-geuka.”—Mwa. 1:3, 14-18; Yak. 1:17.
24 Jinsi maneno ya mtume Paulo yalivyo na ufasaha juu ya uwezo wa Mungu wa kutoa nuru: “Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.” (2 Kor. 4:6) Kulingana na ushuhuda huu, hakuna mtu awezaye kusema kwa kweli kwamba Yehova, Mungu wa Biblia, anasadiki giza la kutojua kitu na la mafundisho ya uongo. Yatupasa tuseme pamoja na mtume Yohana “Mungu ni nuru” na, akiwa hivyo, Yeye ndiye Mtoaji-nuru mkuu zaidi aliyeko. Ukristo, ule wa kweli si ule unaodaiwa na makanisa ya Jumuiya ya Wakristo, ndio nuru kubwa zaidi kuliko zote iliyopelekwa kwa wanadamu. Kama nuru, unatoa uhai, unatoa uhuru!
25. Tukimwacha Mungu huyu wa nuru awe Enzi Kuu wa maisha zetu, maisha zetu zitaangaziwaje nuru?
25 Je! Mungu huyu wa nuru ndiye Mtu wa kiroho tunayetaka awe Mwenye Enzi Kuu wa maisha zetu? Tukimfanya hivyo, basi maisha zetu lazima ziangaziwe nuru ya kweli, nuru inayotuweka huru, tuwe na mwendo na matendo ya akili ya mambo yaliyo mema, na kuangaziwa nuru inayotuonyesha njia ya uzima wa milele kupatana na Mwenye Enzi Kuu wa ulimwengu wote.
[Picha katika ukurasa wa 200]
Yuda Iskariote aliruhusu Shetani Ibilisi awe mwenye enzi kuu wake, hata akamsaliti Yesu Kristo kwa sababu hiyo