Maisha na Huduma ya Yesu
Yesu Kibishanio
MUDA mfupi baada ya yeye kukaribishwa nyumbani mwa Simoni, yeye anaanza ziara ya pili ya kuhubiri Galilaya. Katika ziara yake iliyotangulia ya eneo hilo, walioambatana naye walikuwa wafuasi wake wa kwanza, Petro, Andrea, Yakobo na Yohana. Lakini sasa mitume wale 12 wanaambatana naye, na pia wanawake fulani. Hao ni kutia ndani Mariamu Magdalene, Susana, na Yoana, ambaye mume wake ni afisa wa Mfalme Herode.
Mwendo wa huduma ya Yesu unapoongezeka, ndivyo na mabishano yanayohusu utendaji wake. Mwanamume mmoja mwenye mashetani, ambaye pia ni kipofu na hawezi kusema, analetwa kwa Yesu. Yesu anapomponya, hivi kwamba anakuwa huru bila kuongozwa na mashetani na anaweza kusema na kuona pia, makutano wanaingiwa na furaha inayozidi. Wanaanza kusema: “Si huenda ikawa labda huyo ndiye Mwana wa Daudi?”
Makutano wanakusanyika kwa hesabu kubwa sana kuzunguka nyumba ile ambamo Yesu anakaa hivi kwamba yeye na wafuasi wake wanakuwa hawawezi hata kula mlo mmoja. Zaidi ya wale wanaofikiri kwamba labda yeye ndiye Mwana wa Daudi aliyeahidiwa, kuna waandishi na Mafarisayo ambao wamekuja umbali wote kutoka Yerusalemu ili wamwondolee sifa. Wakati watu wa ukoo wa Yesu wanaposikia juu ya ghasia inayomzunguka Yesu, wanakuja wamkamate. Kwa sababu gani?
Basi, ndugu za Yesu mwenyewe bado hawaamini mpaka sasa kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Pia, makelele mengi na ugomvi ambao yeye ametokeza hadharani ni tofauti kabisa na tabia ya Yesu waliyemjua alipokuwa akikua katika Nazareti. Basi wao wanaamini Yesu ana kasoro kubwa ya kiakili. “Yeye amerukwa na akili yake,” wao wanakata shauri, na kwa hiyo wanataka kumkamata na kumwondoa pale.
Hata hivyo, ushuhuda uko wazi kwamba Yesu aliponya mwanamume yule aliyekuwa na mashetani. Waandishi na Mafarisayo wanajua kwamba wao hawawezi kukana uhakika wa jambo hilo, pia uhakika wa miujiza mingine ya Yesu. Kwa hiyo ili wamwondolee Yesu sifa wanaambia watu wale: “Jamaa huyo hafukuzi mashetani ila kwa njia ya Beelzebubi, mtawala wa mashetani.”
Akijua kufikiri kwao, Yesu anawaita waandishi na Mafarisayo na kusema: “Kila ufalme uliogawanyika dhidi yao wenyewe unakuja kwenye ukiwa, na kila mji au nyumba iliyogawanyika dhidi yayo yenyewe haitasimama. Katika njia iyo hiyo, ikiwa Shetani anaondosha nje Shetani, yeye amekuwa amegawanyika dhidi yake mwenyewe; ni jinsi gani, basi, ufalme wake utasimama?”
Lo! njia hiyo ya kutoa sababu inakumba fikira zao kama nini! Kwa kuwa Mafarisayo wanadai kwamba watu kutoka kati yao wenyewe wametupa nje mashetani, Yesu anauliza pia: “Ikiwa mimi ninaondosha nje mashetani kwa njia ya Beelzebubi, ni kwa njia ya nani wana wenu wanayaondosha nje?” Ndiyo kusema, shtaka lao dhidi ya Yesu linapasa litumiwe kwa njia ile ile kuwahusu kama lilivyotumiwa kwake. Ndipo Yesu anapoonya hivi: “Lakini ikiwa ni kwa njia ya roho ya Mungu kwamba mimi ninaondosha nje mashetani, ufalme wa Mungu umewapita ninyi kikweli.”
Ili kutoa mfano kwamba kutupa kwake mashetani nje ni ushuhuda wa nguvu zake juu ya Shetani, Yesu anasema: “Ni jinsi gani mtu ye yote anaweza kuvamia nyumba ya mwanamume mwenye nguvu na kushika bidhaa zake zinazoweza kuhamishwa, isipokuwa kama kwanza yeye anafunga mwanamume mwenye nguvu huyo? Na ndipo yeye atateka nyara katika nyumba yake. Yeye asiye upande wangu yuko dhidi yangu, na yeye ambaye hakusanyi pamoja nami anatawanya.” Kwa wazi Mafarisayo wako dhidi ya Yesu, wakijionyesha kuwa ni mawakili wa Shetani. Wao wanatawanya Waisraeli watoke kwake.
Kwa hiyo, Yesu anaonya wapinzani hao wa Kishetani kwamba “kufuru dhidi ya roho halitasemehewa.” Yeye anaeleza: “Mtu awaye yote anayenena neno dhidi ya Mwana wa mtu, hilo atasamehewa; lakini mtu awaye yote anayenena dhidi ya roho takatifu, hilo hatasamehewa, la, si katika huu mfumo wa mambo wala katika ule utakaokuja.” Waandishi na Mafarisayo hao wametenda dhambi hiyo isiyosameheka kwa kumhesabia Shetani kwa nia mbovu sana jambo ambalo kwa wazi ni utendaji wa kimuujiza ya roho takatifu ya Mungu. Mathayo 12:22-32; Marko 3:19-30; Yohana 7:5, NW.
◆ Ziara ya pili ya Yesu ya Galilaya inatofautianaje na ile ya kwanza?
◆ Kwa sababu gani watu wa ukoo wa Yesu wanajaribu kumkamata Yesu?
◆ Mafarisayo wanajaribuje kuiondolea sifa miujiza ya Yesu, na Yesu anawakanushaje?
◆ Mafarisayo hao wana hatia ya nini, na kwa sababu gani?