Sura 41
Yesu Kibishanio
MUDA mfupi baada ya yeye kukirimiwa nyumbani mwa Simoni, Yesu anaanza ziara ya pili ya kuhubiri Galilaya. Katika ziara yake iliyotangulia ya eneo hilo, walioambatana naye walikuwa wafuasi wake wa kwanza, Petro, Andrea, Yakobo na Yohana. Lakini sasa mitume wale 12, na pia wanawake fulani, wanaambatana naye. Hao ni kutia ndani Mariamu Magdalene, Susana, na Yoana, ambaye mume wake ni ofisa wa Mfalme Herode.
Mwendo wa huduma ya Yesu unapoongezeka, ndivyo na mabishano yanayohusu utendaji wake. Mwanamume mmoja mwenye roho mwovu, ambaye pia ni kipofu na hawezi kusema, analetwa kwa Yesu. Yesu anapomponya, hivi kwamba anakuwa huru na udhibiti wa roho mwovu na anaweza kusema na kuona pia, umati unazidiwa na furaha. Unaanza kusema: “Si huenda pengine huyu akawa ndiye Mwana wa Daudi?”
Umati unakusanyika kwa hesabu kubwa sana kuzunguka nyumba ile ambamo Yesu anakaa hivi kwamba yeye na wafuasi wake wanakuwa hawawezi hata kula mlo mmoja. Kuongezea wale wanaofikiri kwamba labda yeye ndiye “Mwana wa Daudi” aliyeahidiwa, kuna waandishi na Mafarisayo ambao wamekuja umbali wote kutoka Yerusalemu ili wamwondolee sifa. Wakati watu wa ukoo wa Yesu wanaposikia juu ya ghasia inayomzunguka Yesu, wanakuja wamkamate. Kwa sababu gani?
Basi, hata ndugu za Yesu mwenyewe bado hawaamini mpaka sasa kwamba yeye ni Mwana wa Mungu. Pia, makelele mengi na ugomvi ambao yeye ametokeza hadharani ni tofauti kabisa na tabia ya Yesu waliyemjua alipokuwa akikua katika Nazareti. Basi, wao wanaamini Yesu ana kasoro kubwa ya kiakili. “Yeye amerukwa na akili yake,” wao wanakata shauri, na kwa hiyo wanataka kumkamata na kumwondoa pale.
Hata hivyo, uthibitisho uko wazi kwamba Yesu aliponya mwanamume yule aliyekuwa na roho mwovu. Waandishi na Mafarisayo wanajua kwamba wao hawawezi kukana uhakika wa jambo hilo. Kwa hiyo, ili wamwondolee Yesu sifa wanaambia watu wale: “Jamaa huyu hafukuzi roho waovu ila kwa njia ya Beelzebubu, mtawala wa roho waovu.”
Akijua kufikiri kwao, Yesu awaita waandishi na Mafarisayo na kusema: “Kila ufalme uliogawanyika dhidi yao wenyewe unakuja kwenye ukiwa, na kila jiji au nyumba iliyogawanyika dhidi yayo yenyewe haitasimama. Katika njia iyo hiyo, ikiwa Shetani anafukuza Shetani, yeye amekuwa amegawanyika dhidi yake mwenyewe; basi, ufalme wake utasimamaje?”
Lo! njia hiyo ya kutoa sababu nzuri inakumba kama nini! Kwa kuwa Mafarisayo wanadai kwamba watu kutoka kati yao wenyewe wamefukuza roho waovu, Yesu anauliza pia: “Ikiwa mimi nafukuza roho waovu kwa njia ya Beelzebubu, ni kwa njia ya nani wana wenu wanawafukuza?” Ndiyo kusema, shtaka lao dhidi ya Yesu linapasa litumiwe kwa njia ile ile kuwahusu kama lilivyotumiwa kwake. Ndipo Yesu anapoonya hivi: “Lakini ikiwa ni kwa njia ya roho ya Mungu kwamba mimi nafukuza roho waovu, ufalme wa Mungu umewapita nyinyi kweli kweli.”
Ili kutoa kielezi kwamba kufukuza kwake roho waovu ni uthibitisho wa nguvu zake juu ya Shetani, Yesu anasema: “Mtu yeyote anawezaje kuvamia nyumba ya mwanamume mwenye nguvu na kushika bidhaa zake zinazoweza kuhamishwa, isipokuwa kama kwanza yeye anafunga mwanamume huyo mwenye nguvu? Na ndipo yeye atateka nyara nyumba yake. Yeye asiye upande wangu yuko dhidi yangu, na yeye ambaye hakusanyi pamoja nami anatawanya.” Kwa wazi Mafarisayo wako dhidi ya Yesu, wakijionyesha kuwa ni mawakili wa Shetani. Wao wanatawanya Waisraeli watoke kwake.
Kwa hiyo, Yesu anaonya wapinzani hao wa kishetani kwamba “kufuru dhidi ya roho halitasamehewa.” Yeye anaeleza: “Mtu awaye yote anayenena neno dhidi ya Mwana wa binadamu, hilo atasamehewa; lakini mtu awaye yote anayenena dhidi ya roho takatifu, hilo hatasamehewa, la, si katika huu mfumo wa mambo wala katika ule utakaokuja.” Waandishi na Mafarisayo hao wametenda dhambi hiyo isiyosameheka kwa kumhesabia Shetani kwa njia mbovu sana jambo ambalo kwa wazi ni utendaji wa kimuujiza wa roho takatifu ya Mungu. Mathayo 12:22-32; Marko 3:19-30; Yohana 7:5, NW.
▪ Ziara ya pili ya Yesu ya Galilaya inatofautianaje na ile ya kwanza?
▪ Kwa nini watu wa ukoo wa Yesu wanajaribu kumkamata?
▪ Mafarisayo wanajaribuje kuiondolea sifa miujiza ya Yesu, na Yesu anawakanushaje?
▪ Mafarisayo hao wana hatia ya nini, na kwa nini?