Miguu Yake Ilikuwa Wapi?
“MTESWAJI Apopotolewa Msalabani, Masalio Yaliyofukuliwa Yaonyesha.” Je! wewe uliona kichwa kikuu cha habari kama hicho katika Januari 1971? Labda, kwa kuwa kulikuwa na makala nyingi za magazetini kuhusu “ushuhuda” fulani mpya juu ya kifo msalabani.
Baada ya kichwa kilicho juu, makala hiyo ilianza hivi: “Yerusalemu, Jan. 3 (Reuter)—wachimbuzi Waisraeli, wakiwa wamefukua ushuhuda wa habari za kwanza wa kusulubiwa, walisema leo kwamba ingeonyesha kwamba huenda Yesu Kristo akawa alisulubiwa katika kikao tofauti na kile kinachoonyeshwa katika msalaba wa kimapokeo.”
Je! ushuhuda huu mpya ulifunua jinsi Wayahudi katika wakati wa Yesu walivyouawa kwenye msalaba au mti? Wachimbuzi waliamua nini kuhusu kikao cha mwili wa mteswaji huyo? Je! hili lilihusiana na kifo cha Yesu? Huenda ukauliza, ushuhuda huo ulikuwa thabiti kadiri gani?
Msumari Katika Visigino
Huko nyuma katika 1968 mapango fulani ya kuzikia yaligunduliwa bila kutazamiwa karibu na Yerusalemu. Humo ndani, miongoni mwa mifupa iliyokuwa imezikwa tena, kulikuwamo kile kilichoonekana kuwa uvumbuzi wenye kutokeza—mifupa ya kisigino ikiwa imetobolewa kwa msumari wenye kutu. Dakt. Nico Haas, mtaalamu wa anatomia na anthropolojia wa Shule ya Tiba ya Kiebrania ya Chuo Kikuu cha Hadassah, aliongoza uchunguzi wa mifupa ii hii. Jarida linaloheshimiwa Israel Exploration Journal (1970, Buku 20, kurasa 38-50) lilichapisha maneno mkataa yake, yaliyoongoza kwenye makala fulani za magazetini zenye kushangaza. Maneno mkataa hayo yalikuwa yapi?
Yeye aliripoti kwamba kilichogunduliwa kilikuwa si kingine ila masalio ya mwanamume aliyeuawa msalabani katika karne ya kwanza. Kwa msingi, ilionekana kwamba visigino viwili vya mteswaji huyo vilipigiliwa msumari pamoja kwenye mti ulio wima, lakini msumari huo ulijikunja kwenye ncha ulipogonga fundo katika mbao hiyo. Baada ya mteswaji huyo kufa, watu wa ukoo walikuwa na tatizo kuuondoa msumari huo, kwa hiyo uliachwa katika visigino vyake alipozikwa. Kwa kuwa msumari mmoja ulikuwa umetoboa mifupa ya visigino vyote viwili na kwa kuwa ilionekana kwamba mifupa ya miguu ilikuwa imekatwa kwa mkingamo, Dakt. Haas aliripoti kwamba yaelekea mteswaji huyo aliuawa katika kikao kinachoonyeshwa hapa chini. (Dakt. Haas anahisi pia kwamba kwaruzo lililokuwa katika mfupa wa mkono linaonyesha kwamba mikono ya mwanamume huyo ilipigiliwa kwa msumari kwenye mti uliokingama.) Huenda ukawa umeona mchoro kama huo katika gazeti au makala ya gazeti. Watu wengi walisisimuka juu ya madokezo hayo kuhusu jinsi alivyokufa Yesu.
Ingawaje, utafanya vema kuuliza tena hivi: “Ushuhuda huo ulikuwa wenye kutegemeka, na je! ulifungamana kweli kweli na jinsi alivyokufa Yesu?
Kukadiria Tena Vile Visigino
Katika miaka michache iliyofuata, wanachuo fulani wenye kujulikana, kama Profesa Yigal Yadin, walianza kutilia shaka maneno mkataa ambayo Haas alikuwa amefikia. Mwishowe, jarida Israel Exploration Journal (1985, Buku 35, kurasa 22-7) lilichapisha “Kukadiriwa Tena” na mtaalamu wa anthropolojia Joseph Zias (Idara ya Vitu vya Kale na Nyumba za Kuhifadhia Sanaa ya Israeli) na Eliezer Sekeles (Shule ya Tiba ya Kiebrania ya Chuo Kikuu cha Hadassah). Wao walikuwa wamechunguza ushuhuda wa kwanza, picha, mifano, na rediografu za mifupa. Huenda ukashangazwa na mengine ya mavumbuzi yao:
Ule msumari ulikuwa mfupi kuliko alivyoripoti Haas na hivyo haungeweza kuwa mrefu vya kutosha kutoboa mifupa ya visigino viwili pamoja na ile mbao. Vipande vya mfupa vilikuwa vimetambuliwa kimakosa. Hakukuwa na mfupa kutoka katika kisigino cha pili; ule msumari ulitoboa kisigino kimoja tu. Vipande fulani vya mfupa vilitoka kwa mtu mwingine tofauti kabisa. Mfupa wa mkono uliokwaruzwa, ‘haukuwa ushuhuda wenye kusadikisha’ wa kupigiliwa kwa msumari kwenye mti uliokingama; ‘kwa kweli, alama mbili zinazofanana na hiyo zilionekana kwenye mfupa wa mguu; hakuna yo yote yazo inayohusianishwa na kusubuliwa.’
Uchanganuzi huu mpya uliongoza kwenye maneno mkataa yapi? “Miundo yote miwili ule wa kwanza na wa mwisho uliofanyizwa tena [na Haas] ya kusulubishwa haiwezekani kiufundi na kianatomia wakati mmoja anapofikiria ule ushuhuda mpya . . . Sisi hatukuona ushuhuda wa mfupa wa kisigino cha kushoto na tulikadiria kwamba ule msumari ulitosha kupigilia mfupa wa kisigino kimoja tu . . . Ukosefu wa jeraha lenye maumivu kwenye kigasha na kiganja cha mkono unaelekea kudokeza kwamba mikono ya mhukumiwa huyo ilikuwa imefungwa badala ya kupigiliwa misumari.” Unaona katika ukurasa huu namna Zias na Sekeles wanawazia kikao cha mwanamume huyo kilivyokuwa alipokuwa akiuawa.
Namna Gani Kuhusu Yesu?
Kwa hiyo, jambo hilo linaonyesha nini kuhusu alivyouawa Yesu? Kwa kweli, halionyeshi mengi hata kidogo! Kwa mfano, kama tulivyozungumzia katika ukurasa 23 yaelekekea zaidi sana kwamba Yesu aliuawa juu ya mti ulio wima bila mti ulioukingama. Hakuna mwanadamu leo anayeweza kujua kwa uhakika hata ni misumari mingapi iliyotumiwa kwa habari ya Yesu. The International Standard Bible Encyclopedia (1979, Buku. 1, ukurasa 826) kinatoa maelezo haya: “Hesabu kamili ya misumari iliyotumiwa . . . imekuwa jambo la makisio mengi. Katika picha za kwanza za kusulubiwa miguu ya Yesu inaonyeshwa ikiwa imepigiliwa misumari mmoja mbali na mwingine, lakini katika picha za baadaye imepitana na imepigiliwa kwa ule ulio wima kwa msumari mmoja.”
Tunajua kwamba mikono Yake haikufungwa tu, kwa kuwa Tomaso alisema hivi baadaye: “Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, . . . “(Yohana 20:25) Hilo lingeweza kumaanisha kwamba kila mkono ulitobolewa kwa msumari, au wingi wa “misumari” ungeweza kuelekeza kwenye makovu ya msumari katika ‘mikono yake na miguu yake.’ (Ona Luka 24:39.) Hatuwezi kujua barabara mahali ambapo misumari ilimtoboa, ingawa kwa wazi ni katika sehemu ya mikono yake. Masimulizi ya Kimaandiko hayatoi habari kamili, wala hayahitaji kufanya hivyo. Na ikiwa wanachuo ambao wamechunguza moja kwa moja mifupa iliyopatikana karibu na Yerusalemu katika 1968 hawawezi kuwa na uhakika kuhusu kikao cha maiti hiyo, hakika hilo halithibitishi kikao cha Yesu.
Hivyo sisi tunatambua kwamba picha za kifo cha Yesu katika vichapo vyetu, kama mnavyoona katika ukurasa 24, ni sanaa tu yenye akili ya tamasha hiyo, si maneno kamili ya kianatomia. Picha hizo hazihitaji kuonyesha maoni yenye kubadilika na kuhitilafiana ya wanachuo, na kwa wazi michoro hiyo inaepuka mifano ya kidini inayotokana na upagani wa kale.