Uadilifu Si kwa Mapokeo ya Mdomo
“Haki yenu [uadilifu wenu, NW] isipozidi hiyo haki ya [uadilifu wa, NW] waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”—MATHAYO 5:20.
1, 2. Kulitukia nini kabla tu Yesu hajatoa Mahubiri yake juu ya Mlima?
YESU alikuwa amekaa mlimani usiku kucha. Mbingu zenye nyota zilitandaa juu ya kichwa chake. Wanyama wadogo wa kiusiku walichakacha katika vichaka. Upande wa mashariki maji ya Bahari ya Galilaya yaliugonga-gonga ufuo kwa uanana. Lakini ingeweza kuwa kwamba Yesu alikuwa akiyafikiria kidogo tu mazingira hayo yenye amani na upendezi wenye kutuliza hisia. Alikuwa amekaa usiku kucha akisali kwa Baba yake wa kimbingu, Yehova. Alihitaji mwongozo wa Baba yake. Siku iliyoko mbele ilikuwa ya umaana mkubwa sana.
2 Katika mashariki anga lilichomoza nuru. Nyuni walianza kuwayawaya, wakilia chiriri-chiriri kwa sauti laini. Maua-mwitu yaliyumba-yumba kwa uanana katika ubaridi ule. Mionzi ya kwanza ya jua ilipochomoza kwenye upeo wa macho, Yesu aliwaita wanafunzi wake akachagua 12 kati yao wawe mitume wake. Halafu, akiwa pamoja na hao wote, akaanza kuteremka chini kando ya mlima. Tayari umati wa watu ungeweza kuonwa ukimiminika kuingia kutoka Galilaya, Tiro na Sidoni, Yudea na Yerusalemu. Walikuja ili waponywe magonjwa yao. Nguvu kutoka kwa Yehova zilikuwa zikimtoka Yesu wakati watu wengi walipokuwa wakimgusa na kuponywa. Walikuwa pia wamekuja kusikia maneno yake yaliyokuwa kama marhamu yenye kuponya nafsi zao zilizofadhaika.—Mathayo 4:25; Luka 6:12-19.
3. Kwa nini wanafunzi na umati wa watu walikuwa wakitazamia kwa hamu Yesu alipoanza kusema?
3 Katika vipindi vyao vya mafundisho vilivyokuwa na urasmi mwingi zaidi, marabi walikuwa na desturi ya kuketi, na katika asubuhi hii hususa ya msimu wa masika ya 31 W.K., Yesu alifanya hivyo, yaonekana akiwa kwenye usawa ulioinuka juu zaidi upande wa kilima. Wanafunzi wake na umati wa watu walipoona hilo, waling’amua kwamba jambo maalumu lilikuwa mwendoni, hivyo basi wakakusanyika kumzunguka kwa kutarajia. Alipoanza kusema, walikuwa wakitazamia maneno yake kwa hamu; alipomaliza muda fulani baadaye, walibaki wakiwa wamestaajabia waliyoyasikia. Acheni tuone sababu.—Mathayo 7:28.
Aina Mbili za Uadilifu
4. (a) Ni aina gani mbili za uadilifu zilizohusika? (b) Lilikuwa nini kusudi la mapokeo ya mdomo, na je! lilitimizwa?
4 Katika Mahubiri yake juu ya Mlima, yaliyoripotiwa kwenye Mathayo 5:1–7:29 na kwenye Luka 6:17-49 pia, Yesu alitofautisha wazi sana jamii mbili: waandishi na Mafarisayo na watu wa kawaida waliowaonea. Alisema juu ya aina mbili za uadilifu, ule wa kinafiki wa Mafarisayo na uadilifu wa kweli wa Mungu. (Mathayo 5:6, 20) Uadilifu wa kujihesabia binafsi wa Kifarisayo ulikuwa na mizizi katika mapokeo ya mdomo. Yalikuwa yameanzishwa katika karne ya pili K.W.K. ili yawe “ua wa kuizungukia Sheria” ili kuilinda na mipenyo ya Uheleni (utamaduni wa Kigiriki). Yalikuwa yamekuja kuonwa kuwa sehemu ya ile Sheria. Kwa uhakika, waandishi hata waliyakadiria mapokeo ya mdomo kuwa bora kuliko ile Sheria iliyoandikwa. Mishnah husema: “Ufuatiliaji mkubwa zaidi wa sheria wahusu kushika maneno ya Waandishi [mapokeo yao ya mdomo] kuliko kushika maneno ya Sheria iliyoandikwa.” Kwa sababu hiyo, badala ya kuwa “ua wa kuizungukia Sheria” ili kuilinda, mapokeo yao yaliidhoofisha Sheria na kuibatilisha, kama Yesu alivyosema: “Mwaikataa [kwa werevu, NW] amri ya Mungu mpate kuyashika mapokeo yenu.”—Marko 7:5-9; Mathayo 15:1-9.
5. (a) Ilikuwa nini hali ya watu wa kawaida waliokuja kumsikia Yesu, nao walionwaje na waandishi na Mafarisayo? (b) Ni nini kilichofanya mapokeo ya mdomo yawe mzigo mzito sana juu ya mabega ya wanaume wenye kufanya kazi?
5 Watu wa kawaida waliosongamana wakamsikie Yesu walikuwa mafukara kiroho, wakiwa “hoi na wenye wasiwasi kama kondoo wasio na mchungaji.” (Mathayo 9:36, HNWW) Waandishi na Mafarisayo waliwabeza kwa majivuno, wakawaita ‘am-ha·’aʹrets (watu wa bara), na kuwadharau kuwa watenda dhambi wakosa-maarifa waliolaaniwa, wasiostahili ufufuo kwa sababu hawakushika mapokeo ya mdomo. Kufikia wakati wa Yesu mapokeo hayo yalikuwa yamekuwa mengi sana yakiwa na vuruguvurugu ya kuonea watu kwa kupekua-pekua vijikosa vidogo mno vya kuvunja sheria—yakiwa yamejawa sana na sherehe za kiibada zenye kula wakati sana—hivi kwamba hakuna mfanya kazi yeyote angeweza kamwe kuyashika. Si ajabu Yesu aliyashutumu mapokeo hayo kuwa ‘mizigo mizito iliyotwikwa mabegani mwa watu.’—Mathayo 23:4; Yohana 7:45-49.
6. Matamko ya Yesu ya ufunguzi yalikuwa na nini cha kugutusha sana, nayo yalionyesha badiliko gani kwa wanafunzi wake na kwa waandishi na Mafarisayo?
6 Hivyo basi Yesu alipoketia upande wa kilima, waliokaribia kumsikiliza walikuwa wanafunzi wake na umati wa watu walioachwa wafe njaa kiroho. Ni lazima hawa wawe waligutushwa na matamko yake ya ufunguzi. ‘Wenye furaha ni walio maskini, wenye furaha ni walio na njaa, wenye furaha ni wale wanaolia machozi, wenye furaha ni wale wachukiwao.’ Lakini nani awezaye kuwa mwe-nye furaha akiwa maskini, mwenye njaa, mwenye kulia machozi, na mwenye kuchukiwa? Na ole zikajulishwa rasmi kwa ajili ya wale waliokuwa matajiri, wenye kula vizuri, wenye kucheka, na wale walioonewa fahari! (Luka 6:20-26) Kwa maneno machache tu, Yesu aligeuza desturi zote za kukadiria ubora wa mambo na viwango vya kibinadamu vilivyokubaliwa. Ulikuwa mgeuzo wa vyeo wenye kutazamisha, kupatana na maneno ya Yesu ya baadaye: “Kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.”—Luka 18:9-14.
7. Maneno ya Yesu ya ufunguzi ni lazima yawe yalikuwa na tokeo gani juu ya umati wenye kumsikiliza Yesu ulioachwa ufe njaa kiroho?
7 Kwa utofautisho na waandishi na Mafarisayo wenye kinaya, wale wenye kumjia Yesu asubuhi hii hususa walijua kwamba hali yao ilikuwa ya kuhuzunisha kiroho. Maneno yake ya ufunguzi ni lazima yawe yaliwajaza tumaini: “Wenye furaha ni wale wajuao uhitaji wao wa kiroho, kwa kuwa ufalme wa mbingu ni wao.” Na ni lazima roho yao iwe ilichangamka kama nini alipoongezea hivi: “Wenye furaha ni wale wanaoona njaa na kuona kiu ya uadilifu, kwa kuwa watajazwa”! (Mathayo 5:3, 6, NW; Yohana 6:35; Ufunuo 7:16, 17, UV) Kujazwa uadilifu, ndiyo, lakini si ule unamna-namna wa Kifarisayo.
Haitoshi Kuwa
‘Waadilifu Mbele ya Wanadamu’
8. Kwa nini watu fulani wangeshangaa ni jinsi gani uadilifu wao ungeweza kuwa mwingi kuliko ule wa waandishi na Mafarisayo, hata hivyo kwa nini ingekuwa lazima uwe hivyo?
8 “Haki yenu [uadilifu wenu, NW] isipozidi hiyo haki [uadilifu, NW] ya waandishi na Mafarisayo,” akasema Yesu, “hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.” (Mathayo 5:17-20; ona Marko 2:23-28; 3:1-6; 7:1-13.) Ni lazima watu fulani wawe waliwaza hivi: ‘Eti waadilifu kuliko Mafarisayo? Wao hufunga na kusali na kutoa zaka na sadaka za kusaidia maskini na kutumia maisha zao wakijifunza Sheria. Uadilifu wetu wawezaje kuja kuzidi ule wao?’ Lakini ilikuwa ni lazima uwe mwingi zaidi. Huenda ikawa Mafarisayo walistahiwa sana na wanadamu, lakini si na Mungu. Katika pindi nyingine Yesu alisema hivi kwa Mafarisayo hawa: “Ninyi ndinyi mnaojidai haki [uadilifu, NW] mbele ya wanadamu, lakini Mungu awajua mioyo yenu; kwa kuwa lililotukuka kwa wanadamu huwa chukizo mbele za Mungu.”—Luka 16:15.
9-11. (a) Ni njia gani moja ambayo waandishi na Mafarisayo walifikiri wangepokea msimamo wa uadilifu mbele za Mungu? (b) Ni kwa njia gani ya pili walitarajia kupata uadilifu? (c) Ni njia gani ya tatu waliyotegemea, na mtume Paulo alisema nini cha kuonyesha kwamba hiyo ingekuwa kazi bure tu?
9 Marabi walikuwa wametunga sheria zao wenyewe za kupata uadilifu. Moja ilikuwa kustahili kwa sababu ya kuwa na asili ya Abrahamu: “Wanafunzi wa Abrahamu baba yetu wauonea shangwe ulimwengu huu na kurithi ulimwengu utakaokuja.” (Mishnah) Yawezekana kwamba ilikuwa ili kukinza pokeo hili ambalo Yohana Mbatizaji aliwaonya Mafarisayo waliomjia yeye: “Zaeni matunda yanayofaa na toba: musifiki[r]i kusema ndani yenu, Tuna Abrahamu, ndiye baba yetu [kana kwamba hiyo ilitosha].”—Mathayo 3:7-9, ZSB; ona pia Yohana 8:33, 39.
10 Njia ya pili ya kupata uadilifu, wao wakasema, ilikuwa kwa kutoa sadaka za kusaidia maskini. Vitabu viwili vya Kiapokrifa vilivyoandikwa na Wayahudi wacha Mungu katika karne ya pili K.W.K. huonyesha maoni hayo ya kimapokeo. Taarifa moja huonekana katika Tobiti: “Kutoa sadaka za kusaidia maskini huokoa mtu na kifo na kulipia kila dhambi.” (12:9, The New American Bible) Kitabu cha Siraki (Eklesiastikasi) huafikiana na hilo: “Maji hufyonza moto unaowaka miali, na sadaka huwa upatanisho kwa ajili ya dhambi.”—3:29, NAB.
11 Njia ya tatu walivyotafuta uadilifu ilikuwa kwa kazi za Sheria. Mapokeo yao ya mdomo yalifundisha kwamba ikiwa kadiri kubwa ya matendo ya binadamu yalikuwa mema, yeye angeokolewa. Hukumu “ni kulingana na kazi zilizo nyingi zaidi kama ni njema au ni za uovu.” (Mishnah) Ili wasimame hukumuni kwa njia yenye kupendeleka, hangaikio lao lilikuwa “kupata mastahili ambayo yangeuzi-di uzito wa madhambi.” Ikiwa kazi njema za binadamu zilizidi kazi zake mbaya kwa kazi moja, yeye angeokolewa—kana kwamba Mungu alihukumu kwa kuweka hesabu ya vitendo vyao vidogo-vidogo! (Mathayo 23:23, 24) Akitoa maoni sahihi, Paulo aliandika hivi: “Hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki [mwadilifu, NW] mbele zake [Mungu] kwa matendo ya sheria.” (Warumi 3:20) Kwa uhakika, ni lazima uadilifu wa Kikristo uwe mwingi kuliko ule wa waandishi na Mafarisayo!
‘Mlisikia Kwamba Ilinenwa’
12. (a) Yesu alifanya badiliko gani la kuiacha njia yake ya kawaida ya kutoa utangulizi wenye kurejezea Maandiko ya Kiebrania katika Mahubiri yake juu ya Mlima, na kwa nini? (b) Twajifunza nini kutokana na utumizi wa sita wa usemi “Imesemwa”?
12 Yesu aliponukuu kutokana na Maandiko ya Kiebrania hapo kwanza, alisema hivi: “Imeandikwa.” (Mathayo 4:4, 7, 10) Lakini mara sita katika yale Mahubiri juu ya Mlima, alifanya utangulizi wa zile zilizosikika kama taarifa za kutoka kwenye Maandiko ya Kiebrania kwa maneno haya: “Ilisemwa.” (Mathayo 5:21, 27, 31, 33, 38, 43, NW) Kwa nini? Kwa sababu alikuwa akirejezea Maandiko kama yalivyofasiriwa kulingana na mapokeo ya Kifarisayo yaliyopinganisha amri za Mungu. (Kumbukumbu 4:2; Mathayo 15:3) Hilo laonyeshwa wazi katika rejezo la Yesu la sita lililo la mwisho katika mfululizo huu: “Mmesikia [mlisikia, NW] kwamba imenenwa [ilisemwa, NW], Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako.” Lakini hakuna sheria yoyote ya Kimusa iliyosema, “Umchukie adui yako.” Waandishi na Mafarisayo ndio waliosema hivyo. Hiyo ilikuwa ndiyo fasiri yao ya Sheria ya kupenda jirani yako—jirani yako Myahudi, hakuna wengine.
13. Yesu aonyaje hata dhidi ya mwanzo wa mwenendo ambao ungeweza kuongoza kwenye uuaji halisi?
13 Sasa fikiria ya kwanza ya mfululizo huu wa taarifa sita. Yesu alijulisha rasmi hivi: “Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usiue; na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila amwoneaye [aendeleaye kumwonea, NW] ndugu yake hasira itampasa hukumu.” (Mathayo 5:21, 22) Kasirani katika moyo yaweza kuongoza kwenye matusi na kutoka hapo iongoze kwenye hukumu za laana, na hatimaye huenda ikaongoza kwenye kitendo chenyewe cha kuua. Kasirani yenye kukuzwa kwa muda mrefu moyoni yaweza kuwa hatari: “Kila amchukiaye ndugu yake ni mwuaji.”—1 Yohana 3:15.
14. Yesu atushaurije hata tusianze kuteremkia ile barabara iongozayo kwenye uzinzi?
14 Ndipo Yesu akasema hivi: “Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye [aendeleaye kutazama, NW] mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” (Mathayo 5:27, 28) Je! wewe hutafanya uzinzi? Basi hata usianze kuteremkia barabara hiyo kwa kukaribisha mawazo ya jambo hilo. Linda moyo wako, ambapo ndipo chanzo cha mambo hayo. (Mithali 4:23; Mathayo 15:18, 19) Yakobo 1:14, 15 yaonya hivi: “Kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.” Nyakati fulani watu husema: ‘Usianze usichoweza kumaliza.” Lakini katika kisa hiki twapaswa kusema: ‘Usianze usichoweza kuacha.’ Watu fulani ambao wamekuwa waaminifu hata walipotishwa kuuawa mbele ya kikosi cha wafyatuaji bunduki wameanza kuhisi upenzi kwa ule mtego wenye ushawishi wa kukosa adili katika ngono.
15. Msimamo wa Yesu juu ya talaka ulitofautianaje kabisa na ule uliosimuliwa katika mapokeo ya mdomo ya Wayahudi?
15 Sasa twaja kwenye taarifa ya tatu ya Yesu. Alisema hivi: “Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye [akimtaliki, NW] mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa [aliyetalikiwa, NW, yaani, aliyetalikiwa kwa sababu zisizo ukosefu wa adili katika ngono], azini.” (Mathayo 5:31, 32) Wayahudi fulani wali-shughulika na wake zao kwa hila na wakawataliki kwa visababu hafifu kabisa. (Malaki 2:13-16; Mathayo 19:3-9) Mapokeo ya mdomo yaliruhusu mwanamume kutaliki mke wake “hata ikiwa alimharibia mapishi” au “ikiwa alipata mwingine mrembo kuliko yeye.”—Mishnah.
16. Ni zoea gani la Kiyahudi lililofanya kuapa viapo kukose maana, na Yesu alichukua msimamo gani?
16 Kwa kufuata ukanda ule ule Yesu aliendelea hivi: “Tena mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, Usizuri [usiape bila kufanya, NW] . . . lakini mimi nawaambia, Usiape kabisa.” Kufikia wakati huu Wayahudi walikuwa wakivunja heshima ya kiapo wakawa wakiapa-apa viapo vingi juu ya vijambo visivyo vya maana bila kuvifanya. Lakini Yesu alisema: “Usiape kabisa . . . Bali maneno yenu yawe Ndiyo, ndiyo; Siyo, siyo.” Kanuni yake ilikuwa sahili: Sema ukweli nyakati zote, bila kulazimika kuhakikisha neno lako kwa kiapo. Acha viapo vibakie kwa mambo yaliyo muhimu.—Mathayo 5:33-37; linganisha 23:16-22.
17. Yesu alifundisha kufuata njia gani bora kuliko “jicho kwa jicho, na jino kwa jino”?
17 Ndipo Yesu akasema: “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino; lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.” (Mathayo 5:38-42) Hapa Yesu harejezei pigo lenye madhumuni ya kuumiza bali kofi la madharau kwa kutumia upande wa nyuma wa mkono. Wewe mwenyewe usijishushie hadhi kwa kurudisha madharau. Kataa kurudisha ovu kwa ovu. Bali, rudisha wema na hivyo “uushinde ubaya kwa wema.”—Warumi 12:17-21.
18. (a) Wayahudi walibadilishaje sheria juu ya kupenda jirani yako, lakini Yesu alikinzaje hilo? (b) Jibu la Yesu lilikuwa nini kwa mwanasheria fulani aliyetaka kuweka mipaka ya utumizi wa “jirani”?
18 Katika kielelezo cha sita kilicho cha mwisho, Yesu alionyesha wazi jinsi Sheria ya Kimusa ilivyodhoofishwa na pokeo la kirabi: “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako; lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi.” (Mathayo 5:43, 44) Sheria ya Kimusa iliyoandikwa haiweki mipaka juu ya upendo: “Umpende jirani yako kama nafsi yako.” (Walawi 19:18) Mafarisayo ndio waliosita kufuata amri hii, na ili waiepuke waliliwekea mipaka neno “jirani” likahusu wale tu walioyashika mapokeo. Basi ikawa kwamba baadaye Yesu alipokumbusha mwanasheria fulani juu ya amri ya ‘kupenda jirani yako kama nafsi yako mwenyewe,’ mwanamume huyo alipiga chenga hivi: “Na jirani yangu ni nani?” Yesu alijibu kwa kielezi cha Msamaria mwema—jifanye jirani kwa yule akuhitajiye.—Luka 10:25-37.
19. Yesu alipendekeza tufuate tendo gani la Yehova kuelekea waovu?
19 Akiendelea na mahubiri yake, Yesu alipiga mbiu kwamba ‘Mungu alionyesha upendo kwa waovu. Alisababisha jua liwaangazie na mvua iwanyeshee. Hakuna jambo lolote la ajabu katika kupenda wale wakupendao. Waovu hufanya hivyo. Hakuna sababu ya kuthawabishwa kwa jambo hilo. Jithibitisheni kuwa wana wa Mungu. Mwigeni. Jifanye uwe jirani wa wote na umpende jirani yako. Na hivyo mwe “wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu.”’ (Mathayo 5:45-48) Lo, ni wito wa ushindani kama nini kuishi kwa kutimiza kiwango hicho! Nacho chaonyesha upungufu mkubwa kama nini wa uadilifu wa waandishi na Mafarisayo!
20. Badala ya kuiweka kando Sheria ya Kimusa, Yesu aliongezeaje upana na kina cha uzito wayo na kuiweka kwenye kiwango cha juu hata zaidi?
20 Hivyo basi Yesu aliporejezea sehemu za Sheria na kuongezea, “Lakini mimi nawaambia,” hakuwa akiiweka kando Sheria ya Kimusa na kuweka kitu kingine mahali payo. Sivyo, bali alikuwa akiongeza kina na upana wa kani yayo kwa kuonyesha roho iliyokuwa kusudi la kuwako kwayo. Sheria ya juu zaidi ya udugu yahukumu uhasama wenye kuendelea kuwa ni uuaji. Sheria ya juu zaidi ya utakato yashutumu fikira ya kuendelea na nyege za tamaa mbaya kuwa uzinzi. Sheria ya juu zaidi ya ndoa yakataa kutaliki bila sababu ya maana kuwa ni mwendo unaoongoza kwenye kufunga upya ndoa za uzinzi. Sheria ya juu zaidi ya ukweli yaonyesha kuwa si lazima kuapa-apa. Sheria ya juu zaidi ya upole yaweka kando kulipa kisasi. Sheria ya juu zaidi ya upendo yataka upendo wa kimungu usio na mipaka.
21. Maonyo ya Yesu yalifunua nini juu ya uadilifu wa kujihesabia binafsi wa marabi, na umati wa watu ungejifunza nini zaidi?
21 Ni lazima maonyo hayo ya upole yasiyopata kusikiwa yawe yalikuwa na uzito wa kina kirefu yaliposikiwa na wenye kuyasikia kwa mara ya kwanza! Yaliuonyesha uadilifu wa kujihesabia binafsi uliotokana na kutumikia mapokeo ya kirabi kuwa wa bure kama nini! Lakini Yesu alipoendelea na Mahubiri yake juu ya Mlima, umati wa watu wenye kuona njaa na kiu ya uadilifu wa Mungu wangejifunza kihususa jinsi ya kuufikia, kama ionyeshavyo makala inayofuata.
Maswali ya Kupitia
◻ Kwa nini Wayahudi walifanyiza mapokeo yao ya mdomo?
◻ Yesu alifanya mgeuzo gani wa kutazamisha kuhusu waandishi na Mafarisayo na watu wa kawaida?
◻ Waandishi na Mafarisayo walitarajia kupataje msimamo wa uadilifu pamoja na Mungu?
◻ Yesu alionyesha nini kuwa ndiyo njia ya kuepuka uasherati na uzinzi?
◻ Kwa kuonyesha roho iliyokuwa kusudi la kuwako kwa Sheria ya Kimusa, Yesu alithibitisha viwango gani vya juu zaidi?