Ungamo La Dhambi—Je! Kuna Kasoro?
“UNGAMO ni utakaso wa kiroho, njia ya kuanza tena, njia ya kufutilia mbali makosa yote ya zamani. Mimi hupenda kwenda kwenye Ungamo, kuambia padri dhambi zangu, ili nipate msamaha wake na ustarehe wa raha nyingi ifuatayo.” Ndivyo asemavyo Mkatoliki mmoja mwenye kujitoa sana.—Bless Me, Father, for I Have Sinned (Nibariki, Baba, Maana Nimetenda Dhambi).
Kulingana na New Catholic Encyclopedia, “ni padri peke yake ambaye Kristo alimpa au akamkabidhi mamlaka ya kufunga na kufungua, ya kusamehe na kubakiza” dhambi. Kazi iyo hiyo ya marejezo yasema kwamba ungamo la kawaida hukusudiwa “kurudisha utakatifu wa uhai uliopotezwa na dhambi mbaya sana na . . . kutakasa dhamiri ya mtu.” Hata hivyo, hali ya kiadili katika mabara mengi yaonyesha kwamba ungamo la kawaida halisababishi wengi walizoealo ‘kugeuka mbali kutoka lililo baya, na kutenda lililo jema.’ (Zaburi 34:14) Hivyo je! kuna kasoro?
Je! Ni Desturi ya Ibada Tu?
Huenda ungamo likaanza likiwa desturi ya ibada tu. Katika Ailandi, ungamo la kwanza huja kabla tu ya Ushirika wa kwanza. Na je! inashangaza hata kidogo kwamba msichana wa miaka saba angefikiri zaidi juu ya vazi dogo sana la bibi-arusi ambalo yeye angevaa kuliko kufikiri juu ya ‘kurudisha utakatifu wa uhai uliopotezwa na dhambi mbaya sana’?
“Jambo lililonisisimua sana lilikuwa lile vazi, zaidi ya kupata pesa kutoka kwa watu wa ukoo wangu,” asema wazi Ramona, ambaye alifanya ungamo lake la kwanza akiwa na miaka saba. “Miongoni mwa wasichana wote niliojua,” yeye aendelea kusema, “hakukuwa na hisia ya kiroho. Hakuna yeyote kati yetu ambaye hata alifikiria Mungu wakati huo.”
Kwa uhakika, kulazimisha watoto wachanga kuungama dhambi kwa ukawaida kwaweza kuongoza kwenye utamkaji wa maneno ya kidesturi tu. “Mimi nilitumia mistari ile ile tena na tena,” asema Michael, ambaye pia alianza lile zoea la ungamo akiwa na miaka saba.
Maelezo ya Wakatoliki fulani walionakiliwa katika kitabu Bless Me, Father, for I Have Sinned (Nibariki, Baba, Maana Nimetenda Dhambi) yaonyesha kwamba ungamo halikuwa na maana kubwa ya kiroho kwao hata baada ya wao kuongezeka umri. “Ungamo hukufundisha kusema uwongo, kwa sababu kuna mambo fulani usiyoweza kamwe kupata ujasiri wa kumwambia padri,” akasema wazi mtu mmoja. Ukosefu wa upatani miongoni mwa mapadri ungeweza kutumiwa kufanyia kitubio cha kadiri ndogo. Wengine wao walitafuta mwungamishaji “mzuri” ili wapate shauri walilotaka kusikia. “Baada ya kutafuta-tafuta kwa miezi mitatu, nilimpata mwungamishaji wangu. Mimi humwona kila mwezi, uso kwa uso katika chumba cha upatanisho, naye ni mzuri wee,” asema mwanamke kijana mmoja. “Ikiwa ulitumia akili, ulipata padri asiyesikiliza mambo ambaye hakujua Kiingereza chochote isipokuwa yale maneno ya ‘Mbarikiwa Maria mara tatu,’” akasema Mkatoliki mwingine.
Basi, kwa wazi, kuna kasoro kuhusiana na ungamo lizoewalo na watu fulani. Lakini Biblia yaonyesha kwamba kuna uhitaji wa kuungama dhambi, kwa maana yasema hivi: “Hakuna afichaye dhambi zake atakayefanikiwa, awaye yote aziungamaye na kuzikataa atapata rehema.”—Mithali 28:13, The New Jerusalem Bible.
Je! hii yamaanisha kwamba Mkristo apaswa kuungama dhambi zake zote? Ikiwa ndivyo, kwa nani? Makala ifuatayo itachunguza maswali haya.