Je! Wewe Humfuata Yehova Kikamili?
“WENYE haki ni wajasiri kama simba.” (Mithali 28:1) Wanazoea imani, wanategemea Neno la Mungu kwa uhakika, na kwenda mbele kwa ujasiri katika utumishi wa Yehova dhidi ya hatari yoyote.
Waisraeli walipokuwa Sinai baada ya Mungu kuwakomboa kutoka katika utumwa wa Kimisri katika karne ya 16 K.W.K., wanaume wawili hasa walionyesha kwamba walikuwa wajasiri kama simba. Walionyesha pia uaminifu kwa Yehova chini ya hali mbaya. Mmoja wao alikuwa Yoshua wa kabila la Efraimu, aliyekuwa mtumishi wa Musa na aliyewekwa baadaye kuwa mwandamizi wake. (Kutoka 33:11; Hesabu 13:8, 16; Kumbukumbu la Torati 34:9; Yoshua 1:1, 2) Yule mwingine alikuwa Kalebu, mwana wa Yefune wa kabila la Yuda.—Hesabu 13:6; 32:12.
Kalebu alifanya mapenzi ya Yehova kwa uaminifu-mshikamanifu na kwa bidii. Maisha yake marefu ya utumishi mwaminifu kwa Mungu yalimwezesha kusema kwamba alikuwa ‘amemfuata Yehova kikamili.’ (Yoshua 14:8) “Nilikuwa mwaminifu-mshikamanifu kabisa kwa BWANA, Mungu wangu,” yasema The New American Bible. Kalebu “alitii kwa uaminifu,” au “alitekeleza kwa uaminifu-mshikamanifu kusudi la,” Yehova Mungu. (Today’s English Version; The New English Bible) Kwa njia nyingine yaweza kusemwa kwamba, Kalebu alijulisha hivi: “Mimi . . . nilimfuata BWANA Mungu wangu kwa moyo wote.” (New International Version) Namna gani wewe? Je! wewe humfuata Yehova kikamili?
Kuipeleleza Nchi
Ebu jiwazie ukiwa miongoni mwa Waisraeli muda mfupi baada ya Yehova kuwaweka huru kutoka katika utumwa wa Wamisri. Ona vile nabii Musa anavyofuata kwa uaminifu maagizo yaliyopewa na Mungu. Naam, na ona uhakika wa Kalebu kwamba Yehova yuko pamoja na watu Wake.
Huu ni mwaka wa pili baada ya kule Kutoka katika Misri, na Waisraeli wamepiga kambi kwenye Kadesh-barnea katika jangwa la Parani. Wametua kwenye mpaka wa Bara Lililoahidiwa. Kwa amri ya Mungu, Musa yuko karibu kuwatuma wapelelezi 12 kuingia Kanaani. Yeye asema hivi: “Pandeni sasa katika Negebu mkapande mlimani, mkaitazame nchi, ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi; na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome; nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi.”
Wale watu 12 wanaanza safari yao ya hatari. Safari yao inachukua siku 40. Huko Hebroni wanaona watu wakubwa sana. Katika bonde la Eshkoli, wanaona uwezo wa kuzaa wa nchi na wanaamua kurudi na baadhi ya matunda yalo. Kishada kimoja cha zabibu ni kizito sana hivi kwamba ni lazima kichukuliwe kwa mti kati ya watu wawili!—Hesabu 13:21-25.
Wakirudi kwenye kambi ya Waisraeli, wapelelezi hao wanaripoti hivi: “Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake. Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko. Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.” (Hesabu 13:26-29) Wapelelezi kumi hawako tayari kuyakubali maagizo ya Mungu na kupiga hatua kuingia Bara Lililoahidiwa.
‘Yehova Yu Pamoja Nasi’
Hata hivyo, akiwa na imani katika Yehova Mungu, yule mpelelezi asiye na hofu Kalebu ahimiza hivi: “Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.” Lakini wale wapelelezi kumi hawakubali, wakisema kwamba wakaaji wa Kanaani ni wenye nguvu zaidi ya Waisraeli. Wale wapelelezi wenye hofu kuu na wasio na imani wanajiona kuwa mapanzi kwa kulinganishwa.—Hesabu 13:30-33.
“BWANA [Yehova, NW] yu pamoja nasi; msiwaogope,” Kalebu na Yoshua wanahimiza. Watu wanakataa kuyasikia maneno yao. Watu wanapoanza kusema juu ya kuwapiga kwa mawe, Mungu aingilia na kutamka hukumu juu ya walalamikaji hao: “Hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni. Lakini watoto wenu . . . ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa. . . . Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini, . . . hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani. Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini, kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu.”—Hesabu 14:9, 30-34.
Bado Mwaminifu Miaka Kadhaa Baadaye
Muda wa miaka 40 wapita, na kizazi kizima cha walalamikaji wanakufa. Lakini Kalebu na Yoshua bado ni waaminifu kwa Mungu. Kwenye nyanda za Moabu, Musa na Kuhani Mkuu Eleazari wamewahesabu watu wenye umri wa kijeshi wa miaka 20 na zaidi. Mungu ataja mtu mmoja kutoka katika kila kabila la Israeli ili akabidhiwe ugawanyaji wa Bara Lililoahidiwa. Kalebu, Yoshua, na Eleazari wamo miongoni mwao. (Hesabu 34:17-29) Ingawa sasa ana miaka 79, Kalebu angali mwenye nguvu, ni mwaminifu-mshikamanifu, na mwenye moyo mkuu.
Musa na Haruni walipowahesabu watu Sinai muda mfupi kabla ya wao kukataa kwa hofu kuingia nchi ya Kanaani, wanajeshi wa Israeli walikuwa 603,550. Baada ya miongo minne jangwani, kulikuwako jeshi ndogo zaidi la watu 601,730. (Hesabu 1:44-46; 26:51) Hata hivyo, Yoshua akiwaongoza na Kalebu mwaminifu akiwa miongoni mwao, Waisraeli waliingia Bara Lililoahidiwa wakapata ushindi mmoja baada ya mwingine. Kama vile Yoshua na Kalebu walivyokuwa wametazamia sikuzote, Yehova alikuwa akiwashindia watu wake mapigano.
Wakivuka Mto Yordani pamoja na wanajeshi wa Israeli, Yoshua na Kalebu wazee-wazee wanachukua daraka lao katika mapigano yanayofuata. Hata hivyo, baada ya miaka sita ya vita, sehemu kubwa ya nchi ingali yakaliwa na watu. Yehova atawaondoa wakaaji hao lakini sasa aamuru kwamba nchi igawanywe kupitia kura miongoni mwa makabila ya Israeli.—Yoshua 13:1-7.
Alimfuata Yehova Kikamili
Akiwa mwanajeshi stadi wa mapigano mengi, Kalebu asimama mbele ya Yoshua na kusema hivi: “Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa BWANA [Yehova, NW] aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu. Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata BWANA [Yehova, NW], Mungu wako, kwa utimilifu [kikamili, NW].” (Yoshua 14:6-8) Naam, Kalebu amemfuata Yehova kikamili, akifanya mapenzi ya Mungu kwa uaminifu-mshikamanifu.
“Kisha,” Kalebu aongeza, “Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata BWANA [Yehova, NW], Mungu wako, kwa utimilifu [kikamili, NW]. Sasa basi, angalia, yeye BWANA [Yehova, NW] ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo BWANA [Yehova, NW] alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu. Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita, na kwa kutoka nje na kuingia ndani. Basi sasa unipe mlima huu, ambao BWANA [Yehova, NW] alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; humkini yeye BWANA [Yehova, NW] atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama BWANA [Yehova, NW] alivyonena.” Sasa Kalebu apata Hebroni ukiwa urithi.—Yoshua 14:9-15.
Kalebu mzee-mzee amepokea mojawapo migawo migumu zaidi—mkoa uliojaa watu wakubwa isivyo kawaida. Lakini hilo si jambo gumu sana kwa mpiga-vita huyo mwenye miaka 85. Baadaye wale wadhalimu wanaokaa Hebroni wanaangamizwa. Othnieli, mwana wa ndugu mchanga zaidi wa Kalebu na mwamuzi katika Israeli, ateka nyara Debiri. Baadaye majiji yote mawili yanakaliwa na Walawi, na Hebroni laja kuwa jiji la makimbilio kwa mwuaji asiyekusudia.—Yoshua 15:13-19; 21:3, 11-16; Waamuzi 1:9-15, 20.
Mfuate Yehova Kikamili Sikuzote
Kalebu na Yoshua walikuwa wanadamu wasiokamilika. Hata hivyo, walifanya mapenzi ya Yehova kwa uaminifu. Uaminifu wao haukupungua muda wa ile miaka 40 ya ugumu jangwani iliyokuwa tokeo la kushindwa kwa Israeli kumtii Mungu. Vivyo hivyo, Watumishi wa Yehova wa ki-siku-hizi hawaruhusu chochote kizuie utumishi wao kwa sifa ya Mungu. Wakijua kwamba kuna vita kati ya tengenezo la Mungu na lile la Shetani Ibilisi, wako thabiti, wakijaribu daima kumpendeza Baba yao wa kimbingu katika mambo yote.
Kwa kielelezo, watu wengi wa Yehova wamejasiri kutendwa kikatili na hata kifo ili kuadhimisha Mlo wa Jioni wa Bwana, au Ukumbusho wa kifo cha Yesu. (1 Wakorintho 11:23-26) Kwa habari hiyo mwanamke mmoja Mkristo aliyefungwa katika kambi ya mateso ya Nazi wakati wa Vita ya Ulimwengu 2 aliripoti hivi:
“Kila mtu aliambiwa awe katika chumba cha kufulia nguo saa tano jioni. Saa tano barabara za jioni zilipofika tulikusanywa pamoja, tukiwa 105. Tulisimama karibu pamoja katika mviringo, [katikati yetu] kukiwa na kiti cha kuwekea miguu chenye kitambaa cheupe kilichokuwa na mifano. Mshumaa ulinurisha chumba hicho, kwa kuwa taa za umeme zingaliweza kutusababisha tupatikane. Tulihisi kama wale Wakristo wa kale wakiwa ndani ya mapango yao ya kuwazikia watu. Ilikuwa karamu yenye uzito. Tulizisema tena nadhiri zetu kwa Baba yetu za kutumia nguvu zetu zote kwa ajili ya utetezi wa jina lake takatifu, kusimama kwa uaminifu kwa ajili ya Theokrasi.”
Yajapokuwa majaribu yetu tukiwa watumishi wa Yehova wanaonyanyaswa, tunaweza kutegemea nguvu ya kupewa na Mungu kumtumikia kwa moyo mkuu na kuleta heshima kwa jina lake takatifu. (Wafilipi 4:13) Tunapojitahidi kumpendeza Yehova, tutafaidika tukimkumbuka Kalebu. Kielelezo chake katika kumfuata Yehova kikamili kulimvutia sana kijana mmoja aliyeingia kazi ya kuhubiri wakati wote huko nyuma katika 1921. Yeye aliandika hivi:
“Ingawa kuwa painia kulimaanisha kuacha nyuma kazi yangu yenye ustarehe kwenye kiwanda cha uchapishaji cha ki-siku-hizi katika Coventry [Uingereza], sikuwa na majuto. Kujiweka wakfu kwangu kulikuwa kumesuluhisha jambo hilo tayari; maisha yangu yalikuwa yamewekwa wakfu kwa Mungu. Nilimkumbuka Kalebu, aliyeingia lile Bara Lililoahidiwa pamoja na Yoshua na ambaye ilisemwa juu yake kwamba, ‘Alimfuata Yehova kikamili.’ (Yos. 14:8) Hilo lilionekana kwangu kuwa mtazamo unaotamanika. Nilijua kwamba kumtumikia Mungu ‘kikamili’ kungefanya maisha yangu yaliyowekwa wakfu yawe ya maana zaidi; kungenipa fursa zaidi ya kutokeza matunda yanayotia alama Mkristo.”
Kwa hakika Kalebu alibarikiwa kwa ajili ya kumfuata Yehova kwa uaminifu-mshikamanifu kikamili, akijaribu sikuzote kufanya mapenzi ya kimungu. Kama yeye, wengine wamepata shangwe kubwa na baraka nyingi katika utumishi wa Mungu. Hilo na liwe ono lako ukiwa mtu ambaye humfuata Yehova daima kikamili.
[Picha katika ukurasa wa 26]
Kalebu na Yoshua walikuwa waaminifu kwa Yehova chini ya jaribu. Je! wewe ni mwaminifu?