Abrahamu—Kazikwa Hapa, na Bado yu Hai?
Kwa karne nyingi, Wayahudi, Waislamu, na Wakristo wamefunga safari ya kwenda mahali hapa.
Waweza kupazuru katika jiji la kale la Hebroni, kusini mwa Yerusalemu. Jengo hilo laitwa Haram el-Khalil na Kaburi la Wazee wa Ukoo. Ndiyo, hapa pakubaliwa na wengi kuwa mahali pa maziko pa wazee wa ukoo Abrahamu, Isaka, na Yakobo, kutia na wake zao Sara, Rebeka, na Lea.
Kumbuka yaliyo katika Biblia kwamba baada ya kifo cha mke wake mpendwa, Sara, Abrahamu alinunua pango na ardhi fulani katika Makpela, karibu na Hebroni kuwa mahali pa kuzikia. (Mwanzo 23:2-20) Baadaye, Abrahamu pia alizikwa hapo, kutia na washiriki wengine wa familia. Karne nyingi baadaye, karibu na mahali pa kuzikia watu pa kale, Herode Mkuu alijenga jengo lenye kuvutia ambalo baadaye lilirekebishwa na kupanuliwa na mataifa yaliyoshinda eneo hilo, wakionyesha itikadi zao wenyewe za kidini.
Unapoingia, waona minara sita (nguzo au kaburi tupu). Sehemu ya ndani yaonyesha ile ya Isaka, mwana wa Abrahamu. Karibu nayo kuna mashimo yanayopita sakafuni, ambayo yametumiwa ili kufikia vitu vilivyomo chini. Wachunguzi wamepata vyumba ambavyo huenda vilikuwa na mifupa mingi ya kale.
Vipi juu ya Abrahamu? Ikiwa alizikwa katika pango ambalo sasa liko chini ya mahali hapo, yeye amekuwa mfu kwa muda mrefu, sivyo? Wageni wengi wangekubali hilo. Lakini nabii aliye mkuu zaidi ya Abrahamu alisema kwamba, katika maana fulani, Abrahamu bado aishi. Jinsi gani? Nalo laweza kuwa na maana gani juu ya imani yako?
Tafadhali soma makala “Wapendwa Wako Waliokufa—Wao Wako Wapi?” (Ukurasa 3) Inaonyesha yale ambayo nabii huyo mkuu alisema juu ya Abrahamu kuwa hai, habari ambayo yaweza kuwa ya thamani kuu kwako na kwa familia yako.